Abdallahking
JF-Expert Member
- Mar 19, 2018
- 3,985
- 10,840
Simulizi : KIGUU NA NJIA
Mwandishi : BEN R. MTOBWA
Imeletwa kwenu na: BURE SERIES
SEHEMU YA 1
likuwa mara yangu ya kwanza kumuona baba akitokwa na machozi. Kwa kweli, ilikuwa mara yangu ya kwanza kumuona mwanamume yeyote mwenye
umri wa baba akilia, iwe sirini au hadharani. Kitendo cha mwanamume kutokwa na machozi, iwe kwasababu ya maumivu au majonzi, hakikupata kukubalika katika jamii yetu.
Nakumbuka nilipokuwa mtoto mdogo, wa miaka mitatu au minne hivi, nilipojikwaa na kuumia au kupigana na wenzangu nikalia. Baba alikuwa akinicharaza bakora huku akisema, “Mwanaume gani wewe unalia? Mwanaume halii!”
Babu yangu pia, mzee Karimanzila, aliwahi kunicheka sana kwa suala hilo la kulia. Siku hiyo mtego nilioutega mwituni ulikuwa umemnasa kanga mkubwa sana. Rafiki yangu mmoja tuliyekuwa naye porini aliniita kwa sauti kubwa kuniarifu juu ya kanga huyo. Lakini nilipofika kwenye mtego huo nilimkuta Katato, ambaye alituzidi sana kwa umri na umbile, akimfungua kanga huyo kwa madai kuwa ni mtego wake. Tulibishana naye sana. Kwa kunikomoa Katato alimwachia kanga wangu, ambaye aliruka na kutokomea zake mwituni. Nilijaribu kupigana naye lakini akanizidi nguvu na kunitia ngeu katika paji la uso. Nililia njia nzima hadi kijijini. Babu
aliposikia habari hizo aliniita na kunidhihaki kwa kusema, “Ukiona mwanaume analia ujue na roho ya kike. Angestahili kuvaa gauni badala ya kaptula.”
“Lakini yule alikuwa kanga wangu wa kwanza. Nimekwishanasa njiwa, hondohondo na kware. Leo