MLANGO WA 77 "DOOR77" Sehemu 03
Mtunzi; Robert Heriel
Whatsapp 0693322300
Sehemu 03
ILIPOISHIA
“ Imaculata?” Peter Mirambo akajikuta anang’aka. Lakini kabla Tarikh hajaongea chochote Mlango ukafunguliwa wakaingia wanaume wawili waliovalia suti zilizowakaa vyema, Peter Mirambo akasalimiana nao, kisha mwanaume mmoja akamwambia Peter Mirambo amfuate ofisini. Wakati Peter bado akiwa hajaelewa vizuri nini kinaendelea akashangaa moja ya watu wale waliokuja akitoa bastola na kumpiga yule kijana risasi ya kichwa, Tarikh akadondoka chini wakati Peter akiwa anajaribu kumzuia yule mwanaume asimpige Risasi lakini alikuwa amechelewa.
ENDELEA
Peter akawa anajaribu kumnyanyua Tarikh kuona kama atakuwa hai lakini alikuwa keshapoteza maisha. Kwa hasira akamfuata yule mwanaume aliyempiga Tarikh risasi kisha akampiga ngumi ya uso, yule mwanaume akadondoka chini, akamfuata pale chini kisha akamkunja shati kwenye kifua na kumnyanyua juu kwa nguvu.
“ Kwa nini umemuua? Nakuuliza why did you kill him?” Peter akafoka huku akiutazama uso uliokuwa unavuja damu puani wa yule mwanaume. Yule mwanaume wa pili akamshika Peter na kuwaamulia. Kisha akamruhusu yule mwanaume aliyemuua Tarikh kuondoka. Ingawaje Peter alikuwa anahangaika kutaka kumzuia yule mwanaume asiondoke lakini haikuwezekana.
“ Noo! Kwa nini umemruhusu huyo muuaji aondoke, ni nani?” Peter Mirambo akamgeukia Bekha ambaye ndiye alikuwa ameingia na yule mwanaume.
“ Tulia! Punguza hasira Peter.” Bekha akasema,
“ Yule mwanaume ni nani nimekuuliza? Mimi ndiye nimekabidhiwa hii operesheni, watu wote waliochini yangu katika hii kazi ninawajua na wote waliuawa jana tulipokuwa kwenye misheni isipokuwa Mimi na wewe, huyu jamaa uliyekuja naye sio miongoni mwa ambao nilikabidhiwa. Tafadhali Bekha” Peter Akasema.
“ Alikuja. Baada ya kunisalimu akatoa simu yake mfukoni kisha akapiga namba Fulani, haikuita sana ikapokelewa, hapohapo akanikabidhi pasipo kusema chochote, nikaiweka sikioni, kisha nikasikia sauti ya upande wa pili ambayo bila ya kunisalimia ikaniambia kuwa nimpeleke huyo mwanaume kwenye chumba cha mahojiano. Kisha simu ikakata” Bekha akasema,
“ Hivyo tuu! Alikuwa ni nani aliyekuwa akiongea?”
“ Alikuwa ni CDF Haidari Mwera” Bekha akajibu.
“ Lakini hii inawezekanaje? Na kwa nini huyu mwanaume amuue huyu shahidi haramia?” Peter akauliza kwa sauti ya chini huku akimtazama Bekha.
“ Hata mimi nimeshangaa kitendo kilichotokea”
Peter akatembea mpaka alipoufikia mlango, akaufungua kisha akatoka akimuacha Bekha akiwa anazungumza. Moja kwa moja akaenda kwenye vyumba ambavyo wale Maharamia waliwekwa kwani kila haramia aliwekwa kwenye chumba chake. Peter alipigwa butwaa mara alipoona maiti ya haramia mwingine ikiwa imelala sakafuni ikiwa inajeraha la risasi kichwani. Hakutaka kupoteza muda akasonga kwenye chumba kilichokuwa kinafuata, nako akakutana na hali ileile. Hapo akazidi kuchanganyikiwa, akasonga kwenye chumba cha mwisho cha tatu, huko akakutana na hali tofauti kidogo. Haramia huyu alipigwa risasi ya tumbo na kifua. Naye alikuwa amekufa.
“ Hii inamaanisha jambo gani? Inawezekana vipi?” Peter alikuwa akijiuliza huku akiwa anakagua maiti ya haramia wa tatu. Hakuna cha ziada, akatoka na moja kwa moja akaelekea mapokezi ambapo alimkuta yule Mwanamke aliyevalia kijeshi aliyewaletea kifungua kinywa. Yule mwanamke aliona uso wa Peter ukiwa umebadilika na hiyo ilimaanisha kuna tatizo. Akauliza:
“ Vipi Peter kuna tatizo?” Kabla Peter hajajibu, wote wakatazama lilipodirisha ambalo lilionyesha kwa nje, hapo waliona geti linafunguliwa na punde wakaona Gari la CDF Haidari Mwera likiingia. Baada ya gari kuegeshwa akashuka CDF akiwa yupo ndani ya gwanda la kijeshi kama ilivyodesturi yake. Baada ya walinzi wa nje kumpa heshima, akasonga kuingia ndani. Peter hakujua ni kwa nini mapigo yake ya moyo yalikuwa yakienda mbio. Alikuwa na wasiwasi. “ Kuna jambo haliendi sawa hapa. Sasa kama CDF ndio kamuamuru yule mwanaume awaue, kilichomleta yeye sasa hivi ni kitu gani?” Peter akawaza huku akitazama mlango wa mapokezi ukifunguliwa na punde CDF akatokea akiwa anamkabili. Peter Mirambo akatoa heshima ya kijeshi, na yule mwanamke wa kijeshi naye akatoa.
“ vipi kazi inaendeleaje?” CDF akauliza huku akimtazama Peter Mirambo, hapo Peter akawa haelewi ajibu nini. Kabla hajajibu, mawazo yake yakakatishwa na sauti ya cdf;
“ Wako wapi hao vijana mliowakamata?” Kufikia hapo Peter nguvu zikawa zimemuisha, mapigo ya moyo yalifufuka na mwili ulianza kupata moto. “ kwa mara ya kwanza ninaenda kushindwa vibaya, nimezidiwa mbinu” Peter akawaza,
“ Wako wapi?” Akauliza tena, mara hii akiwa anamtazama Peter kwa udadisi, aligundua kuna jambo halipo sawa kwa jinsi uso wa Peter ulivyokuwa.
“ Mkuu..!”
“ Sitaki kusikia excuse yoyote, maneno kinyume na nilichokutuma hapa hayaitajiki” Cdf akamkatisha Peter. Punde Bekha akatokea, akatoa heshima ya kijeshi kisha akawa anawatazama kwa zamu Cdf pamoja na Peter.
“ Mkuu uliongea na Bekha” Peter akasema, hapo CDF akamgeukia Bekha, akamtazama kwa sekunde kadhaa kisha akamgeukia Peter, akasema;
“ Kuhusu nini?”
“ Mkuu si uliongea na mimi Kupitia yule mwanaume uliyekuwa umemtuma, tukazungumza kwenye simu, ukaniambia nimpeleke yule mwanaume kwenye chumba cha mahojiano” Bekha akasema,
“ Mimi!”
Hapo ukimya ukatokea, wote tulikuwa tukimtazama Bekha tusijue kama tunapaswa kumuamini au laa. CDF kakataa kuwa hakuongea na Bekha. Sasa nani mkweli na nani muongo. Kama tukimuamini Bekha basi tungemfanya Cdf kuwa muongo, na kama tukimuamini cdf basi Bekha angekuwa muongo.
“Bekha! Uliongea na mimi leo? Embu onyesha simu yako najua kwa level yako huwezi kuzungumza na simu pasipo kuweka rekodi” cdf akasema.
“ Mkuu! Nilitumia simu ya yule mwanaume ambaye alijitambulisha kuwa ulimtuma”
“ Alisema anaitwa nani”
“ Hakujitambulisha jina lake. Yeye baada ya kunisalimu akatoa simu kutoka mfukoni mwake akabonyeza na kupiga simu, ilipoita akanikabidhi, kisha nikaongea na wewe” Bekha akasema,
“ Kwa hiyo ulishindwa hata kutazama kwenye kioo cha simu aliyokupa kuona namba au jina la mtu utakayeenda kuongea naye?”
“ Mkuu hapo ndipo nilikosea, yaani simu ilipopokelewa moja kwa moja niliposikia sauti yako sikuwa na haja ya kuangalia namba na jina Mkuu” Bekha akasema akiwa anawasiwasi mwingi.
“ Kwa hiyo wako wapi? Au ndio wamechukuliwa na huyo mtu?” Cdf akauliza, hapo tukawa tunatazamana na Bekha. Wakati huo yule Mwanamke mwanajeshi aliyevaa kijeshi akiwa ameshika kitabu cha wageni. CDF akaondoka na kuelekea moja kwa moja kwenye chumba cha mahojiano pamoja na vile vyumba walivyokuwa wamewekwa wale maharamia. Baada ya kitambo kidogo akarudi akiwa amefura kwa hasira.
“ Mmekuwaje wajinga kiasi hicho? Mpaka mnaruhusu uzembe kama huu watu kama ninyi ambao tunawategemea. Kwa hiyo hakuna hata mmoja aliyebakia. Yaani hii imewezekanaje wezekanaje?”
“ Hamkufanikiwa kumhoji yeyote kati yao?” Cdf akauliza huku akitutazama kwa macho ya hasira.
“ Ndio nilikuwa nimeanza kumhoji Tarikh”
“Tarikh ni nani?”
“Ni moja wa wale maharamia Mkuu”
“ Ennhee! Angalau umenipa moyo, nakujua Peter ulivyohodari na mahiri kwa kazi ya kuhoji. Naamini utanipa furaha” CDF akasema, wakati huu zile hasira zilikuwa zimepungua, uso wake ulikuwa angalau unatazamika.
“ Sikufanikiwa Mkuu, wakati ndio naanza kumhoji ndipo Bekha alipoingia na yule mwanaume, na alimuua palepale kabla hajafanya chochote”
“ Bekha! Unaona uzembe ulioufanya? Embu mkamateni Bekha mkamuweke sehemu maalumu kwa watu wa aina yake. Watu wazembe kama ninyi ndio mnaweza kuliuza taifa lenu kirahisi kama hivi” Cdf akasema na papohapo Bekha akakamatwa, Peter alitaka kuzuia lakini nafsi yake ikamuonya.
“ Siamini kama Bekha anaweza kuwa alinidanganya, lakini kama hakunidanganya ni nani aliyekuwa ameongea naye kwenye simu?” Peter akawa anawaza.
“Mkuu yule mwanaume aliandika jina lake hapa” Yule mwanamke mjeshi akasema akiwa amefungua kile kitabu cha wageni, akamkabidhi, Cdf akawa anasoma jina la yule mwanaume ambalo lilisomeka Dismas Sabuni Kazarage, mbele kulikuwa na namba ya simu na sahihi yake. “Embu ipigie hiyo namba” Cdf akasema, yule mwanamke mjeshi akachukua simu kisha akaipigia ile namba, akaweka sauti kwenye simu “Loud speaker” Ikaanza kuita, “Krii krii! Krii Krii! Krii krii! Kisha ikapokelewa. Sauti ya upande wa pili ilikuwa ya mwanamke.
“ Hello” Hapo Cdf, Peter na Yule mwanamke mjeshi wakatazamana, Cdf akamuashiria Mwanamke mjeshi aendelee kuongea, bado kwenye simu sauti ya mwanamke ilikuwa ikisema; Hellow!
“Hello! Habari?” Mwanamke mjeshi akaitikia,
“ Salama, naongea na nani?” Mwanamke wa kwenye simu akauliza,
“ Samahani nitakuwa nimekosea namba, lakini tunaweza kufahamiana?”
“ Sidhani, kwa kheri” mwanamke wa kwenye simu akasema na akawa kama anataka kukata simu lakini punde ikatokea sauti ya kiume ikisema “ mchezo ndio kwanza umeanza” alafu simu ikakatika. Jambo moja ambalo la kushangaza ni kuwa sauti ile ilimshtua sana Cdf ni kama alikuwa akiijua. Uso wa Cdf ulipoteza utulivu. Akaomba tena kile kitabu ili aingalie ile namba, akawa anaisoma kwa macho namba moja mpaka nyingine. Jambo hilo Peter aliligundua Kupitia kuisoma saikolojia ya Cdf akajikuta anamuuliza;
“ Unaifahamu hiyo namba Mkuu?”
“ Eeeh! Mmmh ndio, hapana ninamaanisha siifahamu” Cdf akawa anababaika wakati anajibu swali hilo jambo ambalo liliwatia wasiwasi Peter pamoja na Yule Mwanamke Mjeshi.
“ Inaonekana Cdf anaijua vizuri hiyo namba au anaijua sauti ya mzungumzaji wa kwenye simu au ile sauti ya kiume. Hapa kuna jambo” Peter akawaza.
“Ulichukua vitambulisho vyake wakati alipoingia?”
“ Hapana Mkuu, vitambulisho wanaachaga kule nje getini kwa Walinzi” Mwanamke Mjeshi akasema,
“ Sawasawa” Akatoka akiwaacha pale ndani, kisha wakawa wanamtazama akiwa nje Kupitia dirisha. Wakamuona akipanda kwenye gari lake kisha geti likafunguliwa akaondoka.
SURA YA PILI
“ Hamjambo watoto wazuri”
“ Hatujambo! Shikamoo! Tunaomba pesa ya kula Mjomba.” Watoto Chokoraa waliitikia na kumsalimia Tobias Marengo.
“ Msijali pesa nitawapa. Mnaziona hizi” akawaonyesha akiwa ndani ya gari, wale watoto chokoraa walipoona zile pesa wakapigana vikumbo wakigombea kuingia kwenye dirisha la gari. Tobias akazikwepesha na kuzificha.
“ Tulieni, nitawapa. Lakini kabla ya kuwapa niambieni yupo wapi Imaculata?” Tobias akasema. Wale watoto wakawa wanatazamana kila mmoja akiwa anajiuliza huyo Imaculata ni nani. Tobias aliweza kuzisoma vizuri nyuso za wale watoto na kugundua hawalifahamu jina hilo, “ Kale katoto kalinidanganya jina” Akawaza. “ pengine hapa sio Maskani moja” akawaza na kabla hajamaliza mtoto mmoja akasema,
“ Mjomba! Huyo unayemuuliza hana jina jingine?” Tobias akamtazama yule mtoto, kisha akatingisha kichwa kuashiria hana. “ Mjomba hapa kama unavyotuona wengine hatujuani majina, kuna makundi manne ambayo kila kundi lina watoto wa maskani moja, hivyo ni ngumu kujuana majina hapa. Labda utuambie huyo msichana anafananaje?”
“ Oooh! Mmesema hapa yapo makundi manne? Kuna kundi lolote ambalo leo halipo? ” Tobias akauliza,
“ Makundi mawili leo hayapo hapa, nafikiri yatakuwa maeneo ya Mwenge, au Maeneo ya Kariakoo kule” Yule mtoto Chokoraa akasema, maelezo yake yalimfanya Tobias atabasamu na kumsifu mtoto yule kimoyomoyo. Akatoa noti ya shilingi elfu kumi na kumpatia yule mtoto kisha akatoa nyingine na kumpa kiongozi wa kundi jingine la watoto chokoraa. Kisha akaondoka akichukua uelekeo wa barabara ya Bagamoyo kuikabili Mwenge. Kutokea Daraja la Salenda mpaka Mwenge sio mbali sana, ni mwendo wa dakika kumi na tano kwa mwendo wa kawaida kama hakuna foleni. Macho yake aliyaelekeza nje kutazama huku na huku kuona kama angemuona Imaculata, lakini hakuweza kumuona. Akafika Mwenge Mataa, akakatisha upande wa kushoto barabara ya Sam Nujoma akikabiliwa na Mlimani City. Akiwa amekata tamaa kabisa ghafla kwa mbali kwenye Mzunguko wa barabara ya Mlimani City alishtuka kumuona Imaculata akiwa na kundi la watoto chokoraa wenzake wakiwa wanatembea pembezoni mwa barabara jua kali likiwa linawachoma.
Tobias moyo wake ukiwa umelipuka kwa furaha akapunguza gari mwendo kabisa, akawa anaendesha polepole huku akiwamtathmini Imaculata na wenzake, tayari alikuwa ameshamaliza ile
Roundabout akasonga nao mpaka kilipokuwa kituo cha daladala cha Mlimani City kwa mbele. Hapo akasimamisha Gari lake pembeni ya barabara mbele yao. Kisha akashusha kioo cha dirisha la gari. Imaculata bila ya kuwa na hili wala lile walipolifikia lile gari, Imaculata alishtuliwa na sauti kutoka katika dirishani kwenye lile gari., Alipomtazama aliyeita alimkumbuka ni yuleyule Mjomba aliyempa pesa jana kule Salenda Darajani.
“ Shikamoo Mjomba”
“ Marhaba Imaculata, unanikumbuka?” Tobias alizungumza kwa sauti yenye upendeleo na ukarimu huku akiachia tabasamu .
“ Nakukumbuka Mjomba”
“ Kumbe mnafika mpaka huku, poleni sana wadogo zangu” Hapo kimya kidogo kikatokea, ni kama Imaculata na wenzake walikuwa wakijadili maneno “wadogo zangu” wakati wakimtazama umri wake unalingana na babu yao hivi.
“ Mnaelekea wapi sasa hivi?”
“ Sisi! Aanha! Tunaelekea nyumbani”
“ Nyumbani ni wapi? Ninaweza kuwapa Lifti mpaka nyumbani” Tobias akasema,
“ Hapana Mjomba, tunashukuru”
“ Dada acha tupande tuu mimi nimechoka kutembea” Mtoto mmoja chokoraa akamkatisha Imaculata.
“ Tupande tuu Dada” Mtoto mwingine akadakia. Hapo Imaculata hakuwa na chaguo zaidi ya kuwasikiliza wadogo zake. Wakapanda kwenye gari la Tobias na safari ikaanza.
“ Hamkuniambia nyumbani kwenu ni wapi?” Tobias akasema,
“ Ni pale kimara mwisho, Darajani.” Imaculata akasema,
“ Kwa nini wazazi wenu wamewaruhusu mje huku kuhangaika?” Tobias akasema huku akiwachungulia wale watoto chokoraa Kupitia kioo kilichokuwa juu ya gari.
“ Sisi hatuna waza..zi” Mtoto mmoja akaropoka lakini Imaculata akamkatisha “ Tunaishi na wazazi” Tobias akaelewa kuwa Imaculata anadanganya, na hata jina alilomtajia halikuwa jina la kweli. Lakini hakutaka kumbughuzi wala hakuwa na haraka ya kujua jina lake. Wakafika Kimara Korogwe, Tobias akasimamisha gari Mbele kidogo ya kituo cha Daladala kwenye barabara ya pembeni. Imaculata akashangaa ni kwa nini gari imesimama.
“ Chukueni hii pesa mkalete Dozeni ya chupa za maji na juisi. Shika na hii” Tobias akawapa elfu hamsini, alipotaka kushuka Imaculata Tobias akamzuia, akamwambia “ Wewe kaa tuu acha wadogo zako wakalete, wala sio nzito, mje na Biscut zenye chocolate” Imaculata hakuwa na jinsi zaidi ya kukubali matakawa ya Mzee Tobias Marengo.
“ Rudishia mlango vumbi linaingia” Tobias akasema, hapohapo Imaculata akafunga mlango, alipofunga tuu mlango, Tobias akawasha gari na kuondoka. Imaculata alikuwa akipiga kelele lakini hakukuwa na namna yoyote ya kupata msaada. Akageuka nyuma kuangalia Kupitia kwenye dirisha la nyuma la gari akawaona wadogo zake wakiwa wapo dukani wasijue kuwa dada yao ametekwa.
Itaendelea
1. Jipatie softcopy ya Kitabu cha Mlio Wa Risasi harusini Tsh 8,000/=
Hardcopy. Tsh 15,000/=
2. Kitabu cha Wakala wa Siri Tsh 15,000/=
3. Kitabu cha Kaburi la Mwanamuziki Tsh 15,000/=
0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel