Simulizi ya Kijasusi: Noti Bandia

Simulizi ya Kijasusi: Noti Bandia

SEHEMU YA 21

kuashiria kuwa tumeruhusiwa kupita. Gari hilo pia likafuata taratibu kama tulivyofanya nalo likapita. Ilikuwa BMW nyeusi, ndani kulikuwa na vijana wawili, ambao hata hivyo sikuweza kuwaona vizuri.

Haraka nilifungua mkoba wangu nikatoa lens yangu ndogo ambayo hunisaidia kuona vitu vya mbali. Kulikuwa na vijana wanne, kila mmoja alionekana kuwa majukumu yake kama wenyewe walivyokuwa wamepangiana. "Ingia kituo cha mafuta", nilimwambia dereva wa gari hii akanishangaa.

"Gari yangu ina mafuta ya kutosha, sisi huwa tunajaza full kwa ajili ya kuepuka usumbufu kwa abiria wetu, ni agizo la uwanja, kwa hilo usihofu", alisema.

"Nataka kuingia Super Market kidogo", nilidanganya.

"Hapa wanafunga saa nne usiku, sasa ni saa tano na nusu, labda tujaribu Super Market ya Uchumi", alishauri kijana huyu aliyekuwa akiendesha Toyota Carina muundo wa TI.

Mbele yetu nikaliona gari lingine aina ile ile ya BMW, rangi ya blue, nilipovuta lens yangu kulikuwa na vijana wawili nao wakiwa tayari kutimiza kazi waliyotumwa. Nilijilaumu kwa kutokuweka tahadhari, lakini kwa vile nilikuwa nimegundua hali hii mapema nikajiweka tayari kwa lolote ambalo lingetokea.

Mara ujumbe mfupi ukaingia kwenye simu yangu, 'KUWA MAKINI BOSI, NYOKA MWENYE SUMU KALI ANATEMBEA KARIBU NA MIGUU YAKO, AKIKUNG'ATA UMEKWISHA'. Wakati tunavuka kwenye taa za kuongoza magari za uwanja wa ndege. Gari lililokuwa mbele yangu lilipungua mwendo ili kuruhusu gari letu lianze kupita kwenye taa hizi.

Ghafla nilisikia kelele za risasi, wakati huo nilikuwa tayari nimejitupa nje na kuliacha gari likiseleleka kuelekea mtaroni. Mara lilitokea Lori lililobeba takataka na kuigonga BMW iliyopunguza mwendo ili kuturuhusu sisi tupite, Vijana wawili waliovalia mavazi yaliyoficha nyuso zao waliruka kutoka kwenye lori na kurusha risasi kuyashambulia magari hayo.

Ilikuwa asubuhi ya misukosuko, vurugu na jitimai, wakazi wa Jiji la Dar es Salaam walikimbia bila mpangilio. Kila mmoja akijaribu kuitetea roho yake, wakati askari kutoka Kikosi Maalum cha Polisi wa Kutuliza Ghasia walipokuwa wakitekeleza moja ya majuku yao ya kuzuia fujo katikati ya Jiji.
 
SEHEMU YA 22

Wakitumia magari yao ya kazi aina ya Landrover Defender TDI za jeshi la polisi Tanzania, zikiwa na rangi ya blue, bunduki maalum za kurushia mabomu ya moshi zikiwa mikononi mwao. Askari hawa walipita mitaani kifua mbele, wakirusha mabomu ya machozi huku na huku ili kutimiza wajibu wao huo.


Magari haya yaligawanyika katika pande mbili mengine yalielekea upande wa Mnazi Mmoja. Mengine yakaelekea upande wa Ilala, ili kuwakabili vyema wananchi hawa waliodaiwa kukaidi agizo la serikali lililowakataza kufanyabiashara katikati ya jiji. Askari hawa waliendelea kurusha mabomu kila mahali palipoonekana kuwa na mkusanyiko wa watu kuanzia wawili.
Hali hii ilionekana sawa na mchezo wa kuigiza. Sikufurahishwa na kitendo hiki cha askari kurusha mabomu bila mpangilio, wananchi sasa walikimbia huku na huku mfano wa Pundamilia waishio kwenye mbuga za wanyama za Serengeti, wanapofukuzwa na mnyama mwenye njaa kali Simba.
Hata hivyo kulikuwa na ukaidi wa wazi kutoka kwa raia hawa, ambao walionekana wazi kukaidi amri hii iliyotolewa na polisi kupitia chombo maalum cha kukuza sauti. "Amri ya Jeshi la Polisi, mnatakiwa kutawanyika haraka, vinginevyo tutatumia nguvu kuwatawanya", sauti ilisikika kutoka katika chombo hicho maalum.
Wakati huo mimi nilikuwa nimesimama kwenye ukuta wa Shule ya Msingi Uhuru, karibu na makutano ya Barabara ya Uhuru na Msimbazi, nikifuatilia kwa karibu kasheshe hilo, ambalo kwa kiasi fulani lilibadili sura nzuri ya Jiji la Dar es Salaam, hali ya utulivu ikatoweka na hofu ikachukua sehemu yake. Kumbukumbu za mauaji yaliyosababisha kuwa na wakimbizi wengi katika nchi za Congo, Rwanda na Burundi ikanirudia kichwani.
"Hali hii ikiachwa iendelee hivi kama ilivyo sasa, itatuletea matatizo siku za usoni", nilijisemea moyoni. Nilikumbuka somo la usalama wa ndani, nilifundishwa somo hili na Luteni John John, wakati huo nikiwa mwanafunzi huko Monduli, mkoani Arusha, kuwa askari wanapashwa kufuata taratibu zilizowekwa wakati wa kukabiliana na hali kama hii, kukaidi amri halali.
Kila mahali ambapo askari hao waliona kuna mkusanyiko wa watu, walisogea
 
SEHEMU YA 23

na kurusha kombora, hali ilikuwa mbaya, karibu kila upande kilio kikubwa kilikuwa ni kuwashwa macho, kutokana na moshi huo kuwaingia machoni. Ili hali hii isikupate lazima ufumbe macho, jambo ambalo ni vigumu kukwepa.
Mimi pia nilikumbwa na kadhia hii, baada ya bomu lililorushwa kuanguka na kulipuka karibu kabisa na mahali nilipokuwa nimesimama. Kutokana na uzoefu wangu katika majanga kama haya, nilifanikiwa kutoka eneo hilo haraka bila kupatwa na madhara makubwa. Kila kikubwa cha watu ilikuwa ni kuwashwa macho, wengine walikimbilia maji ili kusafisha nyuso zao, lakini wakabaki kutetea kile walichoona kinafaa.
Kiasi nilibaini kuwa askari hawa hawakuwa makini katika kutekeleza majukumu yao, nilibaini kuwa iwapo wananchi hawa wakipata silaha zenye ubora kama walizonazo wao huenda wangesalimu amri kutokana na mpangilio wao kuwa mbovu, "Mmmh mfano hali hii ingetokea katika nchi za wenzetu na askari hawa wakafanya mchezo kama hivi, itakuwaje?" nilijiuliza.
"Mabomu haya yanayorushwa hovyo, hivi askari hawa hawaoni kuwa wanaitia hasara serikali", alisema mama mmoja wa makamo alisimama karibu yangu akiyahaha kuyasafisha macho yake.
"Hakuna hasara mama, mabomu haya yamenunuliwa na serikali kwa kazi hii, lakini hayakupaswa kutumika sasa, sioni sababu ya tembo kupigana na sungura, polisi wanatumia nguvu kubwa kupambana na adui ambaye hana silaha yoyote ya hatari, nikisema silaha nina maana hata wembe sidhani kama wamebeba hawa", nilisema.
"Kwanini wasitumie silaha kama hizi kukomesha matukio ya ujambazi yaliyokithiri nchini, au kuwakamata maharamia wanaosumbua wanachi katika maeneo ya mipaka na sehemu ya bahari, ambako kila siku tunasikia meli zinatekwa", alishauri mama huyu.
"Kuhusu suala la ujamnazi ni kweli silaha hizi zingesaidia sana mama, lakini hili na kukabiliana na maharamia wanaoteka meli hapa, polisi hawahusiki, hilo ni jukumu la wanajeshi, majukumu ya polisi ni kukabiliana na raia wakorofi, kama hawa waliogoma kutia amri ya serikali", nilimwambia mama huyu akaonekana kutabasamu.
"Nimejifunza kitu kutoka kwako kijana wangu, kumbe mipakani ni jukumu la
 
SEHEMU YA 24

wanajeshi? Nimeelewa sasa mwanangu", aliongeza mama huyu aliyekuwa na rafidhi ya mkoa wa Mtwara.
Pamoja na rafidhi yake kuwa ya kimakonde, alionekana mama mwenye busara nyingi, baada ya kumtafakari nikabaini kuwa huenda ni mmoja wa viongozi wa taasisi za wanawake ama mjasiriamali. "Kuwasumbua wananchi kwa kuwapiga mabomu kama hivi wewe kwa mtazamo wako unaona sawa?", aliniuliza.
"Si sawa kabisa, lakini pia lazima uangalia chanzo nini? Serikali imetenga bajeti ya kuagiza silaha kama hizi, kwa ajili ya kazi kama hii, lakini busara ilihitajika kwanza, sijui kama wamefuata njia hizo, pengine inatafutwa sababu ili kupunguza masalia ya silaha hizo", nilimwambia akanikazia macho halafu akacheka.
"Kuwachokoza wananchi ili uwarushie mabomu?, hilo umejaribu kuweka chumvi, sijui, labda kwenye Serikali za Kidikteta", alisema tukacheka huku nikimuaga baada ya hali ya vurugu kutulia kidogo.
Gari langu dogo aina ya VW Golf, lenye muundo wa polisi ambalo wengi hawalijui, nililiegesha ndani ya uzio wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, nilifanya hivyo kuepuka hali hii, ambayo baadhi ya watu huitumia kuwaibia wengine kwa mgongo wa watu wenye msimamo mkali.
Kilichonifikisha katika eneo hili ni kamba maalum niliyokuwa nikihitaji kuinunua, kamba hii ilikuwa na maana kubwa katika kazi zangu za hatari. Nilikuja kuinunua kamba hii baada ya kutokea shambulizi la kushitukiza wakati niliposhuka Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere. Sikujua walionishambulia walikusudia nini. Lakini pia taarifa ya kuteketea kwa jengo la ofisi zetu iliyotolewa na Kanali Emilly, ambayo si kweli iliniongezea tahadhari.
Nilijikuta nikitafakari hili na lile, nikiwaza na kuwazua, nilibaini kuwa kuna tukio la hatari limetokea hivyo, Kanali Emilly alinihitaji haraka ofisi kwake, akalazimika kugeuza lugha, kuwa ofisi zetu tunateketea kwa moto. Hata nilipofuatilia tukio hilo kwenye vyombo vya habari, taarifa hiyo haikuwepo. Hata nilipoongea na Peter Twite, ilionekana hakuna tukio la kuungua jengo la ofisi zetu barabara ya Azikiwe.
Baada ya kupata kitendea kazi kilichonileta eneo hili. Yaani, kamba nyembamba lakini madhubuti kwa ajili ya mambo yangu, nilijiondoa taratibu, nikatembea kwa tahadhari kubwa kuelekea lilipo gari langu, kila mtu karibu yangu alionekana kuwa adui yangu, waswahili wanasema uking'atwa na nyota, ukiguswa na ujani unashtuka, ndiyo hali niliyokuwa nayo, nililikagua gari hilo vizuri, baada ya kujiridhisha nikaingia na kuliodoka taratibu kuelekea Posta, ofisini kwa Kanali Emilly.
 
SEHEMU YA 25

Niliendesha gari taratibu kuelekea kwenye ofisi zetu zilizoko Barabara ya Azikiwe. Kichwa changu kilishika hili na lile, nilijiuliza maswali mengi ambayo hata hivyo nilikosa maelezo yake. Nilijilaumu kwa kutozima simu yangu ya mkononi nilipokuwa kijijini kwetu Nyamuswa, ningefanya hivyo, pengine sasa ningekuwa nafaidi samaki, kuku wa kienyeji na maziwa ya mtindi.

Kutoka Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, nilipokuwa nimeegesha gari, nilipita kwenye Barabara za Shauri Moyo na Uhuru nikaibukia kwenye taa za kuongoza magari za Karume, ambapo nilisimama kusubiri ruhusa ya taa hizi. Nilipoingia kwenye Barabara ya Rashid Kawawa, niliongeza mwendo kidogo ili kuwafanya madereva wa magari ya nyuma yangu yasipate usumbufu. Nilipolipita eneo la Msimbazi Centre, niliiacha barabara hii nikaingia kulia halafu kulia tena nikaupita Uwanja wa mpira wa Kaunda, unaomilikiwa na Klabu ya Yanga ya Dar es Salaam.

Shambulizi la usiku uwanja wa ndege liliniongezea hofu na umakini katika kufanya maamuzi, nilijiweka tayari kwa lolote, kila mtu alionekana kuwa adui yangu, nilijiuliza maswali mengi, ningekuwa wapi muda huu iwapo shambulizi lile lingefanikiwa, sikujua sababu za watu hao kufanya shambulizi hilo lililolenga kuniondolea maisha, moyo wangu haukuwa na amani tena, nililitilia shaka kila gari lililoonekana kuwa nyuma au mbele yangu.

Ilikuwa vigumu sana kwa mtu asiye na uwezo wa ziada kama wangu kulibaini gari ninaloendesha, nililazimika kutumia gari hii Toyota Brevis ya rafiki yangu Tigani, ili kukwepa shambulizi lingine, japokuwa dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia hakuna jambo la siri, lolote laweza kutokea.

Shambulizi hilo lilinithibitishia kuwa watu hawa hawana mchezo na wamejipanga vizuri katika mipango yao ya kazi, nilimtafuta Luteni Fred Libaba kwenye simu yake, baada ya kumpata nilimuuliza mahali alipo akanijulisha kuwa yuko Wizara ya Mambo ya Nje kwa kazi maalum nikamtaka asirudi ofisini mpaka nitakapomjulisha ili baadaye tuonane juu kwa juu nje ya ofisi.
**********************

Wakati huo, kikao cha dharura kilifanyika nyumbani kwa mzungu Carlos Dimera. Kikosi maalumu cha matapeli wa kisasa kabisa kikiongozwa na mzungu huyu kilikutana kwa siri kujadili hatua za kuchukua baada ya shambulizi la kumuua Teacher kutofanikiwa.

"Nani aliongoza mpango wa mashambulizi ya usiku kule uwanja wa ndege?" akiwa amechukizwa sana Carlos Dimera aliuliza baada ya wajumbe wote muhimu kufika kwenye kikao hiki.

Tofauti na kikao cha awali kilichofanyika juzi, ambapo Carlos alifanya mazungumza na washiriki pande mbili, kila upande aliupangia majukumu yake, safari hii aliwakutanisha wote, kilikuwa kikao cha pamoja, kikiwahusisha wataalam wa wizi madini feki, watakatishaji wa noti bandia na wasafirishaji wa dawa za kulevya.

"Bosi Carlos... Vijana walijipanga vizuri mno, tulikuwa na asilimia zaidi ya mia kumaliza kazi hii, kwa hili tusitafute mchawi, lazima ufahamu katika mawindo, kuna kuwindwa pia, ndicho kilichotokea usiku. Lakini tukuhakikishie kuwa kutenda kosa siyo kosa, kosa ni kulirudia hilo kosa, leo itakuwa mwisho wa maisha ya Teacher, popote atakapoonekana amekwisha", alisema Nombo.

"Sitaki kusikiliza hadithi za Abunuasi hapa, natoa nafasi ya mwisho, kama Nombo alivyosema kazi hii iishe leo mapema ili tupate uhuru wa kufanya mambo yetu, tukionana kesho tusizungumzie habari ya Teacher tena, nimetenga kiasi cha pesa kwa ajili ya sherehe kubwa, mkimaliza kazi hii vizuri tukutane tupongezane kwa kazi nzuri", Carlos Dimeta alieleza.

"Pamoja na kikao hiki cha dharura, Nyati, Simba na Chui wako katika mawindo, tunawasiliana kila baada ya dakika tano au kumi, kama unavyowajua vijana hawa bosi, jua la kesho Teacher hawezi kuliona kabisa, hasa nikimfikiria Nyati alivyo Teacher amekwisha", alieleza Jackina.

Je nini kiliendelea?
usikose sehemu zifuatazo

ITAENDELEA




BURE SERIES
 
SEHEMU YA 26 & 27

Baada ya mpango huu kuwekwa sawa, mjadala mwingine ulianza, walibuni mbinu nyingi za kuchukua pesa kwa wafanyabiashara matajiri na baadhi ya wastaafu walioorodheshwa bila kusababisha madhara. Mbinu hii ilipangwa na Carlos mwenyewe, mzungu huyu alikuwa na mbinu nyingi na kuwafanya washiriki wa mtandao huu kutegemea zaidi mawazo yake.

Pamoja na kumiliki pesa nyingi, ambazo walifanikiwa kuziiba kwenye mabenki kadhaa ya Dar es Salaam. Pia waliweza kusafiri ndani na nje ya nchi wakitumia hati bandia na mbinu hizi na zile kujipatia pesa.

Carlos Dimera alikuwa karibu na baadhi ya viongozi wa serikali. Nchini Tanzania, alikuja nchini kwa mgongo wa mwekezaji aliyekuja kujenga kiwanda cha kutengeneza tembe maalumu za kope za urembo wa akina dada. Kutokana na ukarimu wake alifahamiana na kila mtu. Machoni mzungu huyu alionekana kama rafiki wa kila mtu, lakini moyoni alikuwa adui mkubwa wa maendeleo ya taifa.

Kumbukumbu zilionyesha kuwa mzungu Carlos Dimera alikuwa amefukuzwa kutoka katika baadhi nchi za Afrika ambako alibainika kufadhili vikundi vya wahalifu. Nchi ya mwisho kutimuliwa ilikuwa Rwanda, ambako aliishi kwa zaidi ya miaka mitatu, akitokea Kampala, nchini Uganda baada ya kutiliwa shaka. Alipoingia Dar es Salaam Tanzania hakuwa mgeni katika nchi ya Afrika Mashariki, kwani alimudu kuongea kwa ufasaha lugha ya kiswahili hivyo haraka aliweza kuunda mtandao wake na kuanza kazi rasmi.

Maofisa kadhaa wa idara za serikali, waliokuwa na dhamana ya kusimamia pesa za umma waliibiwa kwa mbinu hizi na zile, baadhi waliona aibu kuripoti taarifa hizo polisi wakihofia kufukuzwa kazi wengine wakijipeleka polisi wenyewe wakidanganya wamevamiwa na majambazi.

Baada ya kuingia Jijini Dar es Salaam, haraka Carlos aliweza kujenga hekalu au jumba kubwa la kisasa kando ya bahari na kuiomba serikali imruhusu kuweka walinzi wake binafsi, baada ya kupata kibali, aliweka ulinzi mkali kuzunguka jumba hili, akiwatumia askari wa kukodi kutoka kitengo maalum cha ujasusi cha Havana, nchini Cuba.

Vinywaji na vyakula vya aina mbalimbali vililetwa, wajumbe walikula, wakanywa na kusaza, wakiifurahia faida ya kazi yao, kila mmoja alionekana mwenye furaha kupita kiasi, wakimuomba mungu awasaidie kufanikisha jukumu lililokuwa mbele yao.

Pamoja na wajumbe hawa, Carlos Dimera, alikuwa na vijana wengine watatu ambao huonekana kwa nadra sana. hawa waliokuwa wamehitimu vizuri mafunzo ya ujasusi sehemu mbalimbali duniani, vijana hawa pia aliwatumia kwa nadra sana, hususan pale Simba, Chui na Nyati wanapokuwa wameshindwa kutimiza moja ya majukumu yao. Simba, Chui na Nyati walikuwa mfano wa mbwa mwitu, kazi yao kubwa ilikuwa kuteka au kuua watu pale wanapoagizwa kufanya vile.

Kufukuzwa kwa Carlos katika baadhi ya nchi hizo haikumfanya kuvunja mitandao yake huko, kazi ziliendelea kama kawaida kwani ndiye aliyeanzisha utapeli wa noti za bandia, pia ndiye muasisi wa kutegesha vyura, mijusi na wadudu kwenye baadhi ya ofisi za serikali na hivyo kuwafanya watumishi wa ofisi hizo, Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Wizara na Wakurugenzi kuzikimbia ofisi zao wakiamini kurogwa na wakati huo huo vijana wa Carlos Dimera wanageuka kuwa waganga hodari wa tiba na kufanikiwa kujipatia mapesa mengi kutoka kwa vigogo hao.

"Bosi, nakuhakikishia vijana wako tayari kwa kazi, tumefanya mengi kupitia ubunifu wa kichwa chako, ili tusonge mbele lazima mtu afe, mtu huyo anajiita Kapteni Teacher, kama alipona katika shambulizi la jana, leo hawezi kuchomoka, vijana wameapa", alisema Hawa kwa kujiamini.

Mwana mama huyu alikuwa katili na kipenzi cha Carlos Dimera, alikuwa na sifa kadhaa za kumfanya awe kipenzi cha mzungu huyu, moja ya sifa hizo ni ukatili pia alikuwa na uwezo wa kubadili jambo, akalisimamia kwa nguvu zake zote hata likawa sheria au kanuni.

"Sikilizeni, nimepata ujumbe wa maandishi kutoka kwa wanaspoti wetu, kama mtakumbuka wiki iliyopita tuliweza kuchukua kiasi kikubwa cha pesa kwa watu wawili, mmoja ni Waziri mstaafu huko Mikocheni, mwingine ni mfanyabiashara wa Sinza". Carlos Dimera aliwaeleza.
 
SEHEMU YA 28 & 29



"Naam bosi, kilikuwa kibarua kigumu mno, lakini tuliweza kufanikiwa, kuna nini bosi?" alihoji Jackina aliyekuwa kiongozi wa operesheni hiyo.

"Wahusika wametoa taarifa polisi. Lakini sina tatizo na jeshi la polisi, hawa ni watu wetu wanachukua mshahara hapa, mbaya ni kwamba malalamiko yamepelekwa idara ya usalama inayosimamiwa na wanajeshi, Hawa amesema tuna watu wetu huko lakini haitoshi, wanajeshi ni kigeugeu. Jaribio la jana lilikusudia kumuua Teacher na kutoa onyo, baada ya jaribio hilo kushindwa naamini adui yetu atajipanga vizuri zaidi, akionekana popote ua kwanza", alisema Carlos Dimera.

Baada ya kutafakari kwa sekunde kadhaa, Jakina akasimama, "Taarifa kutoka kwa wana mtandao wetu ni kwamba idara hii inawategemea sana maofisa wake wawili. Huyu Kapteni Teacher na mwingine anaitwa Fred, huyu ni afisa wa cheo cha Luteni.

"Safi sana Jackina, ndiyo sababu nakuamini sana, naamini kazi yako itafanyika vizuri, ukitoka hapa pita kwa mhasibu akuongezee nguvu, ikiwezekana Teacher na huyu Fred wasilione jua la kesho. Lakini jitahidi kuwahadharisha vijana wako wasiende kichwa kichwa kwa watu kama hawa", Carlos Dimera alishauri.

"Kuhusu hilo ondoa shaka bosi, hivi tunavyoongea vijana wako nyuma yake, tumewahadharisha wasiwe na papara, kazi hizi hazitaki papara, subiri wakati ufike, utasikia", alisema Jackina kwa kujiamini.

"Naamini kuwa wote mmeinjoy vizuri, haya ndiyo maisha, nani kati yenu atapenda kurudi kijijini, aanze maisha ya kijijini, unaamka alfajiri na jembe mkononi, mazao baada ya miezi sita, unavuna, bado kuna usumbufu kibao, ikiwemo kukopwa mazao na usilipwe kwa wakati au hata usilipwe kabisa", alihoji Nombo.

Baada ya kupanga mipango ikapangika, kikao kilivunjwa, huku Carlos akisisitiza kupewa taarifa ya kifo cha Teacher mapema iwezekanavyo.

Ofisi zetu ziko ghorofa ya juu katika jengo la Benjamin Wiliam Mkapa. Baada ya kuegesha gari kwenye maegesho ya Hotel JB Belmont, nilikwea ngazi mbili tatu nikaitafuta lifti iliyonipeleka juu kabisa. Shambulizi la usiku lilinifanya niliweka ulinzi wa kutosha kuzunguka eneo la ofisi zetu.

Kazi yangu ya kwanza niliyofanya usiku baada ya kutuliza akili yangu ni kuwasiliana na Sajenti Julius Nyawaminza, huyu ni Komandoo aliyebobea, akilitumikia jeshi katika vikosi vya Zanzibar. Nilimwagiza kufika haraka Dar es Salaam, kwa vile Unguja ni karibu alifika Jijini asubuhi na kujiweka kwenye pointi niliyompangia awe.

Kwa kuwa vijana wetu wa Dar es Salaam wanafahamika kwa kiasi fulani, nilipanga kuwatumia kwa kazi zingine, hivyo niliwasiliana pia na Luteni, Claud Mwita kutoka vikosi vya Komandoo mkoani Morogoro, ambaye pia aliweza kufika kwa wakati, akafanya kile alichoelekezwa kufanya.

Nilichelewa kwa dakika kadhaa kufika ofisini kwa Kanali Emilly kama ambavyo tulikuwa tumeafikiana, kuchelewa kwangu kulitokana na mipango ya hapa na pale, maana mtu akikuanza utani lazima ujiandae kutaniana naye, lakini pia akikuanza uchokozi muonyeshe kuwa amepita njia mbaya.

Mapokezi nilipokelewa na Linnah David, Katibu Muhtasi wa Kanali Emilly, "Ulikuwa wapi Teacher? Mzee anakusubiri kwa shauku kubwa, amesema ukitia pua tu, usisimame, moja kwa moja ingia ofisini kwake", Linnah alitania.

"Vipi hali yako Linnah, sikukuacha ofisini, nilisikia wewe pia umepata likizo kulikoni? Au ndiyo umeitwa haraka kama mimi?", nilimuuliza akatabasamu.

"Nitakwambia ukitoka kwa bosi", alisema Linnah huku akinihimiza kuingia ndani ya ofisi ya Kanali Emilly.

Mapigo ya moyo wangu yalianza kunienda mbio, sikujua kilichotokea hata nikaitwa haraka kiasi hiki, taratibu niligonga mlango wa ofisi ya bosi, baada ya kusubiri kwa sekunde kadhaa nilitasua kitasa cha mlango na kuingia ndani. Kanali Emilly aliponiona haraka alisimama na kunielekeza sehemu ya kuketi. Nilishangazwa na hatua hii, kunielekeza mahali pa kukaa karibu kabisa na yeye tofauti kabisa na kawaida yake.

Kanali Emilly alikuwa mzee wa makamo, lakini mwenye busara na nguvu nyingi, hakuwa mwepesi wa kushindwa jambo. Baada ya kupeana mikono na mimi kuketi mahali aliponielekeza, aliinua simu yake ya mezani akamwagiza Linnah atuletee vinywaji. Kabla ya kukata simu, Kanali Emilly alimtaka Linnah kuongeza vinywaji kwa ajili ya wageni wanaokuja. Mimi nikabaki kimya.
 
SEHEMU YA 30 & 31




"Karibu sana Teacher, pole kwa kukatisha likizo yako fupi, nimekuita kwa sababu kuna tatizo limetusibu, tutakuwa na wageni hapa ofisini muda si mrefu, wanakuja kuongea na sisi, tutawasikiliza, tutashauriana nini cha kufanya", alisema Kanali Emilly, aliinua tena simu yake ya mezani akaongea na watu ambao mimi sikuwajua, akawajulisha kuwa mimi nimefika hivyo waje ofisini kwake.

"Kuna tatizo gani bosi, maana sielewi kinachoendelea?" nilimuuliza Kanali Emilly.

"Kuna tatizo kidogo limetoke. Nikaitwa haraka nyumba kubwa, kutakiwa kurudi kwako haraka ni agizo la Rais. Wakati tunawasubiri hawa ndugu zetu, nitakudokeza kidogo kilichotokea", alifungua droo ya meza yake, akatoa bahasha kubwa iliyojaa mapesa, pia akatoa kiboksi kilichojaa makaratasi yaliyoandaliwa kama pesa, akanipatia.

"Hizi ni pesa zangu?", nilimuuliza Kanali Emilly akache

"Ziangalie kwanza Teacher, halafu nitakueleza sababu".

Zilikuwa pesa nyingi zinazotumika katika mataifa mbalimbali duniani. Zilikuwepo noti za shilingi elfu kumi za kitanzania, nilizipitia noti hizi moja baada ya nyingine, sikuona tofauti. Niliendelea kuziangalia noti hizi kwa umakini mkubwa, zilikuwepo noti za Saandaang Piso zinazotumika Jamhuri ya watu wa Philipines, Diez ya Uruguay, Paundi ya Misri, Birr ya Ethiopia, Yen ya Japan na Won ya Korea Kusini.

Niliendelea kuzipitia pesa hizi kwa umakini sana, Kanali Emilly alikaa kimya akiniangalia, sikufahamu lengo la mzee huyu kunipatia pesa hizi niziangalie tu. Niliendelea na zoezi la kuzikagua noti hizi, Rupiah ya Indonesia, Rupee ya Pakistan, Rand ya South Afrika, Afghan ya Afghanistan, Rouble ya Belerus na Peso ya Cuba.

Kulikuwa na idadi kubwa ya noti, ni vizuri nikutajie aina zote za noti zilizoko mbele yetu ili uweze kunielewa vizuri, kabla mzee hajasema jambo.

Aina nyingine ya pesa sikuwahi kuziona kabisa, kama Rouble ya Russia, Litu ya Luthuania, shilingi ya Kenya, Franc ya Afrika ya Kati, Real ya Brazil, Drams ya Armenia, Lira ya Uturuki, Krone ya Denmark na Riyal ya Saudi Arabia. Zingine ni Paund ya Sudan, Lei ya Romani, Dong ya Vietnam, Dollah ya New Zealand, Peso ya Argentina, Dinar ya Libya, Hryvmy ya Ukraine, Sum ya Uzbekistan, Kwacha ya Zambia, Franc ya Kongo, Franc ya Chad, Dinar ya Algeria, Rouble ya India, Franc ya Cameroun, Mark ya Ujeruman na Dollar ya Marekani.

Baada ya kuzipitia pesa hizi, nikazirejesha mikononi mwa Kanali Emilly, ambaye alizijaza kwenye bahasha kubwa, akaniangalia kwa sekunde mbili tatu, alipoona nimekaa kimya nikimwangalia akatoa bahasha nyingine iliyojazwa makaratasi yaliyokatwa kwa mpangilio mzuri mfano wa pesa. Karatasi hizi zilifungwa kwa mafungu sawa na noti, zikitofautiana kwa ukubwa wa aina ya pesa husika.

Niliendelea kuumiza kichwa changu, nilijiuliza sababu ya Kanali Emilly kuleta pesa hizi mbele yangu, kilichoanza kunizindua ni haya makaratasi yaliyokatwa mfano wa pesa, mawazo yangu hayakunipeleka mbali, nikahisi kuwa huenda karatasi hizi zimekamatwa kwa matapeli waliotapakaa kila kono ya miji ya Afrika Mashariki na duniani, wakiwaibia watu kila siku.

"Naam kamanda wangu, nifahamishe sasa. Kuna habari gani mkuu?", nilimuuliza baada ya kumaliza kazi ya kuzipitia karatasi alizokuwa amenipatia. "Hizi noti na karatasi nahisi zimekamatwa kwa matapeli", niliongeza.

"Afadhali tungekuwa tumewakamata, Teacher hili ni tukio linalotia huruma sana, huwezi kuamini nikikueleza kile kilichofanyika, watu wameuza majumba, magari na wengine wamefirisika kabisa kutokana na pesa na karatasi hizi ulizoziona", Kanali Emilly alieleza.

"Ehee?", nilihoji huku nikikiweka tayari kumsikiliza. Mara simu ikaita, akainua mkonga wa simu na kuiweka katika sikio lake la kushoto, baada ya muda alisema, "Waruhusu wapite tafadhali", akaweka simu chini.

"Teacher, kabla sijakueleza hali halisi ya tukio hili, bahati nzuri wahusika wamefika, utawasikiliza kwa makini, wataeleza kilichowasibu, sidhani kama tutashindwa kuwasaidia katika hili", alisema Kanali Emilly.

"Itategemea na kazi yenyewe bosi, kama ujuavyo hii ni dunia, hata uwe mjuzi wa kuogelea kiasi gani, iko siku maji yatakuzidi ujanja, unaweza kuingia mpaka kimo fulani ukashindwa kuendelea, lolote laweza kutokea", nilimwambia. Sikuona vizuri kumsimulia kuhusu tukio la usiku, hivyo nilimezea.
 
SEHEMU YA 32 & 33



Mlango wa ofisi uligongwa, Linnah akaingia akifuatiwa na watu wawili waliotakata vizuri, ukiwaangalia huhitaji kuuliza, moja kwa moja niliamini kuwa watu hawa ni vigogo kutoka serikalini ama matajiri wenye mapesa yao.

Sajenti Julius Nyawaminza aliwasili bandarini, Dar es Salaam kwa Meli ya Kilimanjaro II majira ya saa moja na dakika ishirini asubuhi akitokea Visiwani Zanzibar. Baada ya kuwasili Dar es Salaam, kutoka bandarini, Nyawaminza alitembea kwa miguu yake hadi eneo la Posta mpya kama alivyokuwa ameelekezwa.
Kijana huyu alikuwa na shauku ya kufanya kazi aliyokuja kuifanya Dar es Salaam, alifikiria mambo mengi aliyozungumza na Teacher usiku, akajiona mwenye bahati kipindi hiki kuitwa kufanya kazi katika mazingira aliyokuwa akiyasubiri kwa siku nyingi.
Baada ya kuhitimu kozi mbalimbali za kijeshi ndani na nje ya nchi, Sajenti Julius Nyawaminza alipangiwa kazi katika vikosi vya Zanzibar. Akiwa Visiwani Zanzibar, alifanya mazoezi yake ya kawaida kila siku akisubiri hali mbaya itokee. Yeyote angemuona barabarani kwa bahati mbaya asingeamini kuwa kijana huyu ni moto wa kuotea mbali, kama huamini mtafute umchokoze ili uamini haya niyasemayo..
Begani, Nyawaminza alining'iniza mkoba wake mdogo wenye vifaa vyake kadhaa vya kazi. Alipofika eneo la Posta mpya alinunua gazeti la michezo, akaketi kwenye mojawapo wa vibanda vya abiria wanaosubiri usafiri vilivyoko mbele ya jengo la Benjamini Wiliam Mkapa na Benki ya CRDB.
Luteni Claud Mwita, kutoka mkoani Morogoro, naye pia alikuwa amewasili katika eneo hilo, yeye alitumia usafiri wa bodaboda kutoka Ubungo, alifanya hivyo kutokana na hali ya barabara za Dar es Salaam asubuhi kuwa na msongamano wa magari mengi, hususan wakati wa kuelekea katikati ya Jiji.
Kama alivyofanya Sajenti Julius Nyawaminza, Claud Mwita alitafuta gazeti ya michezo, baada ya kupitia vichwa vya habari vya gazeti hili, akatafuta uelekeo akaweka makazi yake ya muda akisubiri taarifa kutoka kwa Teacher.
Pamoja na kusoma magazeti, vijana hawa walifika hapa kwa kazi maalum, kuangalia aina ya watu wanaofika eneo hilo na muda wa kukaa kusubiri usafiri wa daladala ama taksi zilizoegeshwa katika eneo hilo. Kila mmoja kwa wakati wake alituma ujumbe mfupi wa maneno kumfahamisha Teacher kuwa tayari amefika na yuko kwenye pointi ya kazi.
Nao Simba, Nyati na Chui kama wanavyofahamika, walifika eneo hilo mapema zaidi, hawa waligawana njia za kuingia na kutoka katika jengo hilo, Simba akiulinda mlango mkuu wa mbele unaoangalia kituo cha daladala, Nyati akajiweka upande wa kuingia na kutoka magari, Chui akaimalisha ulinzi kwenye mlango mdogo unaotokea sehemu ya maduka kama unatokea barabara ya Jamhuri.

Teacher aliingia ofisini kwa Kanali Emilly na kuonyeshwa karatasi zilizoandaliwa mfano wa noti, lakini zilikuwa bandia.
"Karibuni", Kanali Beny Emilly alisimama kuwakaribisha wageni hawa. Kwa sheria za kijeshi ilinilazimu mimi pia kusimama ili kumuunga mkono bosi wangu. Baada ya wageni hawa kushikana mikono na mzee huyu, wakanishika mkono.
"Karibuni, karibuni sana, mnaweza kuketi", Kanali Emilly alirudia kusema huku akiwaonyesha sehemu za kuketi.
"Shukrani sana", walisema wageni hawa kwa pamoja huku wakiketi taratibu kwenye viti vilivyokuwa mbele yangu. Kutokana na uzoefu wangu wa kazi nikabaini kuwa wageni hawa walikuwa na tatizo zito linalosumbua nafsi zao.
"Karibuni tena ndugu zangu, karibuni sana hapa ofisini kwangu, huyu kijana ndiye Teacher ambaye niliwafahamisha amesafiri, nikaona ni vizuri tumsubiri awepo ili tuzungumze wote kuona namna ya kusaidia jambo hili", Kanali Emilly alisema akiwaangalia wageni hawa.
Halafu akanigeukia, "Teacher, hawa ni wageni wetu, nimefarijika kukuona umerejea wakati muafaka kabisa, dunia ya sasa hakuna siri, jana niliitwa Ikulu kwa mheshimiwa Rais, nimeulizwa maswali mengi ambayo nimekosa majibu, nikaamini kuwa ukirudi tutajadiliana na majibu yatapatikana, ndivyo ninavyoamini", alisema huku nikimwangalia kwa makini.
Aliinua simu yake ya mezani akampigia Katibu Mahsusi wake Linnah, akamwambia atuletee vinywaji juisi, soda, maji na sambusa. Haikupita hata dakika tano, vinywaji vililetwa, tukaanza kunywa huku kila mmoja akiliweka tayari koo lake kwa mazungumzo.
"Mko tayari kwa mazungumzo yaliyowaleta, ni muda muafaka sasa kuzungumza?", Kanali Emilly aliwauliza watu hawa.
 
SEHEMU YA 34 & 35


"Naam, tunaweza kuanza mazungumzo yetu", alisema mmoja wa watu hawa huku akimwangalia mwenzake usoni, mfano wa mtu anayeomba ridhaa ama kibali kwa ajili ya kuanza kutoa maelezo.
"Itapendeza kama mtaeleza kuanzia mwanzo ili tuwe pamoja na Teacher katika mazungumzo haya", Kanali Emilly aliwaeleza watu hawa, halafu akanigeukia mimi", "Teacher jana nilikutana na watu hawa, walinisimulia kwa undani kuhusu jambo hili lakini itapendeza zaidi wakirudia mbele yako ili upate picha kamili" aliniambia.
"Kijana au Teacher kama mzee wetu anavyokuita. Naamini utaelewa vizuri nikianza kwa kujitambulisha, sisi ni nani tunatoka wapi na tumefika hapa kwa sababu gani?".
"Naam", nilijibu kwa mkato.
"Asante. Mimi binafsi naitwa Enock Nyanda, mkaazi wa Msasani ni mfanyabiashara maarufu hapa Jijini Dar es salaam", alisema huku akiniangalia, nikamuonyesha ishara aendelee.
"Huyu mwenzangu anaitwa mzee Sadik Tagazi, makazi yake pia ni Msasani, ni mfanyabiashara wa siku nyingi... Kijana wangu, naamini nitaeleweka vizuri kwako nikisema wazi kuwa tamaa ya kupata mali nyingi imeniponza mimi, imemponza hata huyu mzee mwenzangu, tumeingizwa mjini, nimeibiwa kiasi kikubwa cha pesa, huyu mzee mwenzangu pia amefanyiwa hivyo hivyo, tumeumizwa", alisema huku machozi yakianza kumtoka, jambo ambalo kwa kiasi fulani liliushitua sana moyo wangu.
"Ehee, ilikuwaje mpaka mkaibiwa kiasi kikubwa cha pesa kama ulivyosema", nilihoji huku akili yangu ikibadilika, maana tukio hili ni moja ya matukio ya kawaida ambayo huwatokea watu kila siku, mawazo yangu yakarejea shambulizi la usiku, nikajiuliza ni wizi huu wa pesa uliosababisha nishambuliwe na kuponea chupuchupu.
"Labda, niseme wazi kuwa watu hawa wametumika teknolojia ya kisasa sana, naamini kwa teknolojia hii hata nani angeibiwa, mimi ni mtu makini sana, lakini huwezi amini nimeibiwa kirahisi mno", anaeleza mzee Sadik ambaye kwa muda mrefu alikuwa kimya.
"Ni teknolojia ipi hiyo, mbona mnazunguka tu hamsemi wazi?", niliwauliza.
"Nimewapa nafasi ya kuzungumza, ndiyo maana nikasema uwanja ni wenu, tusipoteze muda, cha msingi elezeni nini kilitokea mpaka mkaibiwa, jambo hili ni kweli linaweza kumpata kila mtu, lakini mengine ni uzembe wa mtu", alisema Kanali Emilly kwa hasira.
"Si kusudi letu kupoteza muda, tunataka kueleza jambo hili kwa kinagaubaga zaidi ili muone jinsi ya kutusaidia pia kuwanusuru ndugu wengine wanaokusudiwa kuibiwa kama sisi, nashauri mwenzangu aanze maana yeye ana taarifa nzuri na muhimu zaidi", alisema mzee Enock.
"Leo ni tarehe ngapi", alihoji mzee Sadik.
"Leo... Jumatatu ya Machi 21, unataka kusema nini?", Kanali Emilly alieleza na kuhoji.
"Ehee ni jambo zito lakini nitafanyaje, Machi 13, mwaka huu watu wawili nadhifu sana walifika ofisini kwangu... Nitaeleza kwa kifupi, utaniuliza maswali itakapobidi", alisema mzee Sadik. "Baada ya watu hawa kufika ofisini kwangu, tulianzia mbali sana, niliamini ni watu safi, tena waungwana sana, wakajitambulisha kuwa wanafanya kazi katika ubalozi mmoja nchini Tanzania, baada ya kujitambulisha walitoa karatasi fulani kuwa hizo ni dola za Kimarekani ambazo hazijasafishwa", alinyamaza kidogo ili kumeza mate.
Linnah aliingia ofisini kwa Kanali Emilly akiwa amebeba faili kubwa, aliliweka sehemu ya mafaili yanayoingia halafu akaniangalia na kufinya jicho lake, nikatabasamu akatoka.
"Ehee, leta habari, baada ya kuonyeshwa karatasi hizo ambazo walidai ni dola wewe kama wewe uliamini kuwa ni dola?", nilimuuliza. Alionekana kupagawa, kiasi fulani alionekana mwenye aibu kiasi.
"Teacher, ukweli ni kwamba hawa jamaa zetu wameibiwa lakini inashangaza jinsi wanavyoona abu kueleza ukweli kuhusu tukio hili, kwa uzoefu wangu, baada ya kukutana nao na kuzungumza nao jana, nimeamini kuwa hawapendi jambo hili litoke nje, yaani kwenye vyombo vya habari, hilo tumelizingatia, sasa watueleze kwa undani jambo hili lilivyotokea", Kanali Emilly alieleza.
"Kama ulivyosema, itakuwa fedheha iwapo tukio hili litarushwa kwenye vyombo vya habari, vinginevyo hakuna tunachoficha, ndio maana nikasema tumeibiwa, wezi wametumia teknolojia ya kisasa kabisa, hata hivyo mimi na mwenzangu tunakiri kuwa tamaa ya kupata utajiri zaidi imetuponza. Kama ambavyo nilivyotangulia kusema, watu hawa walijitambulisha kuwa wanatoka
 
SEHEMU YA 35 & 37

ubalozi wa Marekani na walifika kwangu wakidai kuwa wanatafuta mtu mwaminifu ili wamkabidhi hizo dola azisimamie wakati wa kusafishwa, na kwamba mtu waliyemuona ni mimi", alisema mzee Sadik.
"Uliwauliza, walikufahamu vipi?", nilimuuliza.
"Naam, niliwauliza wamenifahamu vipi, pia niliwauliza wanajuaje kuwa mimi ni mwaminifu katika masuala ya pesa, mmoja wao alisema amepata kusikia sifa zangu na ndiye aliyependekeza waje kwangu, mara moka nikayaamini maneno yake", alisema mzee Sadik.
Nikajiweka vizuri kwenye kiti ili niweze kusikia habari hii, maana kwa kiasi fulani ilianza kuusisimua mwili wangu, "Baada ya hapo nini kiliendelea?".
"Baada ya kuongea mambo kadhaa na watu hawa, nikiuliza maswali nao wakijibu, hatmaye walinidokeza kuwa baada ya tukio la wizi wa dola milioni mbili za Kimarekeni, lililotokea Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, usafirishaji wa dola, paundi na pesa zingine zinazoingizwa nchini Tanzania ulibadilishwa, sasa zinaingia kama karatasi halafu zinasafishwa kwa dawa maalumu ili zianze kutumika kama dola", alinyamaza kidogo ili kupisha swali, alipoona nimekaa kimya akaendelea.
"Nilihoji pia, ili kujuwa kama ni tukio hilo la wizi tu lililopelekea pesa zote zinazoingizwa nchini Tanzania kuchafuliwa, pia nilitaka kujuwa hali hiyo ni kwa Tanzania peke yake, watu hao ambao walikuwa wakiongea taratibu kwa kujiamini sana, walisema uhalifu umeongezeka sana duniani hivyo mamlaka za fedha zimeona hiyo ndiyo njia salama zaidi ya kusafirisha pesa", alieleza.
Aisee ni stori tamu sana, endelea nakusikiliza", nilisema huku Kanali Emilly akitabasamu.
"Baada ya majadiliano ya muda mrefu, maofisa hawa waliodai kuwa wanatoka Ubalozi, walitoa mfano wa karatasi kadhaa zikiwa na rangi nyeusi, wakadai kuwa hizo ni dola orijino ambazo huletwa nchini na baadaye kusafishwa kwa dawa maalumu ambayo walisema pamoja na kupatikana kwake kuwa vigumu, wao wanajua mahali pa kuipata na kazi hiyo ikafanyika vizuri. Una swali?", aliuliza huku akiniangalia usoni, macho yetu yalipokutana, alionekana wazi kuwa mwenye aibu.
"Teacher, karatasi anazoeleza mzee Sadik nimekuonyesha kabla hatujaanza mazungumzo", alisema Kanali Emilly nikatikisa kichwa kukubaliana naye.
"Sasa ilikuwaje ukaamini kuwa hizi karatasi ni dola?", nilimuuliza baada ya kusimama, nikazichukua zile karatasi alizonionyesha Kanali Emilly, nikamuonyesha, maana maelezo haya yaliniingia vizuri, nikasahau kama nilikuwa likizo.
"Lo, sijui shetani gani aliniingia, mwanzo sikuwaanini kabisa, nilipanga kupiga simu kuwajulisha polisi kuhusu watu hawa ili wakamatwe, lakini baadaye nilishawishika kuwaomba vitambulisho vyao, hakika vilikuwa vitambulisho vya ubalozi wa Marekani, nikaanza kuyaamini maneno yao, nikaingia kwenye mtego baada ya mmoja wa maofisa hawa kutoa dawa na kusafisha karatasi kadhaa ambazo ziligeuka kuwa dola halali kwa matumizi. Hakika nilianza kusadiki, baada ya kudai kuwa dawa waliyonayo ni kidogo haiwezi kusafisha zaidi ya karatasi ishirini", alinyamaza kidogo akachukua glasi yake ya juisi akanywa kiasi huku midomo yake ikimcheza mfano wa mtu aliyekutana na baridi kali.
"Teacher, nakuhakikishia kuwa, kazi ya kusafisha karatasi hizo na kuwa dola ilifanyika mbele ya macho yangu, nilifuatilia tukio hilo kwa umakini wa hali ya juu. Karatasi kumi ziliingizwa kwenye dawa nikiona, baada ya sekunde kadhaa zikatolewa zikiwa tayari zimebadilika na kuwa dola mia mia za Kimarekani, wakati huo boksi kadhaa zilikuwa kando zikiwa zimesheheni karatasi hizo, hakika nikauona utajiri mkubwa mbele yangu, nikajua sasa nimeukata", alisema mzee Sadik, alinyamaza kupisha kama kuna mtu mwenye swali, alipoona kimya akaeleza.
Baada ya karatasi hizo kusafishwa na kila moja ilikuwa dola mia za Kimarekani kuonekana, walinikabidhi, halafu wakaanza kusafisha karatasi ambazo walidai ni paundi za Uingereza ambazo pia zilipotakata zilikuwa paundi mia kila moja. Wakadai dawa hiyo imeisha nguvu, wanatafuta watu wa kusaidia ili karatasi hizo zisafishwe na kuwa dola. Wakanipatia dola zilizosafishwa ili niende sehemu ya kubadilishia pesa kuthibitishe kama ni dola halali, nikafanya hivyo, hakika zilikuwa dola halali kabisa, nikajiona mwenye bahati kuonana na watu hawa".
"Aisee, kweli hapo hakuna ujanja, lazima utaibiwa tu", nilimwambia akacheka kidogo huku akisisitiza kuwa huo ni wizi ambao si rahisi mtu kukwepa, labda uwe fukara. Na jamaa hawa hawamfuati mtu asiye na kitu.
 
SEHEMU YA 38 & 39


"Tamaa ya kupata pesa nyingi imeniponza", alisema akitoa kitambaa cha jasho mfukoni akafuta machozi yaliyokuwa yakimtoka.
"Karatasi walizokuja nazo ofisini kwako na kudai kuwa ni dola ambazo hazijasafishwa, waliziacha kwako?". niliuliza.

"Yes, waliziacha karatasi hizo kwangu huku wakisisitiza kuwa nisitoe taarifa hii kwa mtu yeyote, wakadai kuwa wangerudi kesho yake mapema kuangalia kama nimebadili dola, ili tuangalie uwezekano wa kupata pesa za kununua dawa kwa ajili ya kusafisha karatasi zilizobaki, ambazo walidai iwapo zitasafishwa zote ni zaidi ya shilingi bilioni tano za Tanzania, nilifurahi sana", alisema mzee huyu.
"Kama ndivyo, mbona wewe umefaidika", nilimwambia.
"Hapana, nimeumia sana Teacher, waliporudi mara ya pili walinieleza kuwa karatasi hizo zina thamani kubwa sana, ni mapesa ya kigeni yanayosubiri kusafishwa, kwa hiyo waliniomba mimi kama mwenyeji wao niwatafutie mtu mwenye pesa ili tununue dawa na kusafisha karatasi hizo, ambazo wao walidai kuwa waliziiba ubalozini", anabainisha.
"Ndipo wewe ulipotoa pesa?", nilimuuliza.
"Hapana, kwa vile walinieleza kuwa dawa ya kusafisha karatasi hizi inauzwa kwa bei mbaya, nilimfuata mzee mwenzangu, Enock Nyanda, baada ya kumshawishi alikubali tushirikiane kutoa pesa ili dawa ipatikane, ndipo kazi ya kutafuta dawa ilipoanza".
"Hapo ndiyo patamu sasa, ehee?", niliteka masikio.
Baada ya utaratibu wa pesa kupatikana, maofiosa hawa kutoka ubalozi walituambia kuwa, sehemu ambayo tunaweza kupata dawa ni kwenye maabara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Walishauri kuwasiliana na Profesa waliyedai kuwa anahusika na maabara ya chuo, baada ya kuwasiliana naye kwa simu yake ya mkononi, alitupangia muda ya kwenda kumuona", alitulia kidogo, akaonesha hasira iliyokuwa katika nafsi yake, halafu akacheka.
""Watu hawa walijipanga vizuri", nilijisemea.
"Hakika, kwa mchezo huu walijipanga vizuri kuhakikisha wanafanikiwa", alirukia Kanali Emilly.
"Inaonyesha hivyo. Maana siku iliyofuata tulifika eneo la chuo kikuu, tukakutana na Profesa mmoja anaitwa Davis Magajimbo, kwa vile alikuwa ametuelekeza sehemu ya kumuona, Baada ya kumfahamisha kuwa tunahitaji dawa ya kusafisha dola, alitueleza kuwa dawa hiyo inauzwa bei mbaya na ili kuipata lazima zipatikane shilingi milioni mia moja za kitanzania", alisema, baada ya kutafakari kidogo akaendelea.
Kutokana na thamani ya dola na wingi wa karatasi zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya kusafishwa, tulikubali kutoa kiasi hicho cha pesa kwa Profesa, ambaye alitukabidhi dawa huku akidai kuwa dawa hii ni nyingi sana, akashauri kama ikibaki tutaitumia wakati mwingine. Haraka tuliwasiliana na maofisa wa ubalozi kuwajulisha kuwa dawa imepatikana, nao hawakuchelewa kufika".
"Walipofika ikawaje?", niliuliza.
"Kufika kwa maofisa hawa kulitupa faraja, walishauri dawa hiyo ihifadhiwe vizuri kwenye jokofu, ili kazi ya kusafisha dola kwa vile ni nzito ifanyike kesho yake mapema alfajiri, kwa madai kuwa kuna kazi nyingine wanaifanya wakati huo ili kesho yake wasiwe na ratiba nyingine", alisema mzee Enock ambaye alikuwa kimya kwa muda mrefu.
"Ah, jambo hili lilipangwa kwa ustadi wa hali ya juu, tulihifadhi dawa hii vizuri kama watu hawa walivyoagiza, siku ya pili walifika mapema alfajiri kama walivyoahidi, walinihimiza nitoe dawa ili kazi ya kusafisha dola ianze", alipofika hapo machozi yakaanza kumwagika.
"Usilie tafadhali, hii ni hali halisi ya dunia, unaweza kulala masikini ukaamka tajiri, ama ukalala tajiri ukaamka masikini, yote ni mipango ya Mungu", niliwaambia ili kuwatia moyo

"Teacher, sasa tunawasaidiaje wazee hawa?", lilikuwa swali kutoka kwa Kanali Emilly. Kutokana na swali hili, nilitembea hatua tatu kutoka nilipokuwa nimesimama, halafu nikarejea tena kwenye kiti nilichokuwa nimeketi awali.

"Inategemea...", nilijibu kwa mkato,

Baada ya kutafakari kwa muda, huku tukiangaliana kama mabubu, nililazimika kumweleza Kanali Emilly kuhusu mkakati wangu wa kazi zilizokuwa mbele yangu.

"Afande..., kabla sikaingia kazini rasmi, naomba utambue kuwa kujiingiza katika jambo hili, ni sawa na kuanzisha vita, nasema hivi kwa sababu watu waliofanya uhalifu huu wana mtandao mkubwa mno. Hawa ndio wahusika wakubwa wa dawa za kulevya, ndio wahusika wa uhalifu wa kila aina. Swali langu ni kwamba, uko tayari kwa mapambano na watu hawa?", nilimuuliza.
 
SEHEMU YA 40 & 41


"Potelea mbali, lolote liwe, dunia itatukumbuka kwa hili, tukilimaliza salama tutashukru, tukiishia njiani naamini wapo watakaokuja kuliendeleza", Kanali Emilly alisema huku akisimama kuonyesha msisitizo. "Niko tayari kabisa".

Nililazimika kumweleza Kanali Emilly, kuhusu shambulizi la jana usiku uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, akaonekana kushangazwa, nami nikatumia nafasi hiyo kumweleza jinsi nilivyojipanga kukabiliana na watu hawa, maana walikuwa wamenianza.

"Afande, kutokana na umuhimu wa jambo hili, nimelazimika kuwaita vijana wetu wawili, Luteni Claud Mwita kutoka Morogoro na Sajenti Julius Nyawaminza kutoka Zanzibar, hawa ni makomandoo wenye uwezo mzuri, bahati nzuri wako karibu na eneo hili. Hapa ofisini nimeamua kuwatumia Luteni Fred Libaba na Sajenti Peter Twite tu, nina sababu za kufanya hivyo", nilidokeza.

"Sababu gani hiyo Teacher, wakati idara yetu hapa inao vijana wenye uwezo mzuri tu, wangeweza kukusaidia kwa karibu zaidi, jambo hili linahitaji ushirikiano wenu", alishauri.

"Afande, nimelazimika kufanya hivi kwa sababu, sielewi ilibainika vipi kuwa nimesafiri, ilifahamika vipi kuwa niko kwenye ndege nikirejea Dar es salaam, na sijui nini kilisababisha hata watu hawa wakanishambulia baada ya kutoka kwenye ndege, hilo linanitia shaka", nilimwambia. "Hawa vijana tutawashirikisha kwa kazi nyingine, kuhusu hii watuache kwanza. Kama utapenda operesheni hii iwe na mafanikio utaniwia radhi kwa hilo".

"Umesomeka, hakuna ubishi katika hilo. Kuna la ziada?".

"Hapana", nilimwambia, baada ya ukimya wa sekunde kadhaa nilimwambia kuhusu ujio wa shemeji yangu Mama Feka. "Afande, kama ulivyosikia nikiongea na simu, shemeji yangu tunayeshibana sana yuko njiani kuja Dar es Salaam, pamoja na kwamba anakuja kwenye mahafari ya chuo kikuu, kwa vyovyote vile atapenda kufikia kwangu, kama unavyojua familia yangu nimeihamisha kabisa ili sasa vita vianze, itakuwa vita ya kufa au kupona", nilisema kwa hasira.

"Sasa kuhusu huyu shemeji yako utafanyaje, maana nyumbani kwako sasa si sehemu salama kama ulivyosema?", alihoji Kanali Emilly.

"Nafikiria kumshirikisha katika vita hivi, maana ujio wake unaweza kuwa faida au hasara, lolote laweza kutokea", nilimwambia Kanali Emilly akaonekana kunishangaa.

"Kwanini umeamua kufanya hivyo Teacher?. Huyu shemeji yako ataweza kumudu hali ngumu ya vita ambavyo hatujui nani adui na rafiki?".

Nilitumia dakika mbili tatu kumweleza Kanali Emilly, kuhusu uhodari wa Mama Feka. Nilimweleza jinsi mama huyu alivyo na msimamo imara katika kutekeleza majukumu yake, nilieleza historia yake fupi, kuwa kabla ya kujiunga na chuo kikuu huria cha Tanzania, alifanya kazi kama mwalimu wa michezo katika shule kadhaa, lakini kabla ya hapo alikuwa ameshiriki mafunzo mbalimbali ya kijeshi kwa mjibu wa sheria.

"Kuhusu hilo nakuachia utaamua mwenyewe. sasa umepanga kumtumiaje huyo shemeji yako, au ni siri yako?".

"Hapana, ndiyo maana nikakushirikisha kuhusu jambo hili. Afande, Mama Feka ni mwanamke mrembo sana, ni mwanamke ambaye anaweza kumshawishi mwanaume yeyote akaingia katika himaya yake. Labda nikudokeze jambo moja".

"Itakuwa vizuri".

"Hapa Dar es Salaam, kuna mtandao wa uhalifu ukiongozwa na mzungu mmoja aitwae Carlos Dimera, kama unavyojua taratibu na sheria za nchi yetu huwezi kumkamata mtu bila kuwa na ushahidi wa kutosha. Taarifa nilizonazo ni kwamba huyu Carlos anapenda sana wanawake warembo, kwa Mama Feka ataingia, akiingia amekwisha", nilifafanua.

"Ni mpango mzuri Teacher, tufanye kila iwezekanavyo watu hawa wakamatwe na ushahidi, hii itasaidia kuwafikisha mahakamani, nikutakie kazi njema, tuwasiliane kila hatua utakayofikia, ukihitaji msaada wa aina yoyote usisite kunijulisha, kuanzia sasa ofisi hii itaacha mambo mengine yote ili tushughulikie jambo hili", Kanali Emilly alisema.

"Nikutakie kazi njema, tuombe mungu ndiye mwenye dhamana ya uhai wetu, lolote likitokea itakuwa kwa mapenzi yake, lakini pia tuko tayari kufa kutetea wengi", nilisema huku tukisimama. Tukashikana mikono.

Muda ulikuwa umeyoyoma sana, nilitoka ofisini kwa Kanali Emilly, huku mawazo mengi yakiwa yamenizonga juu ya jambo hili, nilijiuliza kuhusu mbinu walizotumia watu hawa, kiasi fulani nilijikuta nikicheka mwenyewe na kuwasifu kwa jinsi walivyoweza kufanikisha mpango wao wa wizi na kuwaacha wazee hao kwenye mataa. Nilifungua mlango nikatokea mapokezi. Linnah aliponiona akasimama.
 
Back
Top Bottom