Simulizi ya kipelelezi: Document number 72 (Nyaraka namba 72)

STORY: DOCUMENT NUMBER 72
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
EPISODE 35

"Watu wengi wanaiongelea Ikulu kirahisi sana wakihisi pengine ni kazi ndogo kukaa ndani ya hili jengo ila kiuhalisia unatakiwa kuwa na moyo mgumu sana ili kuweza kufanikiwa kuingia ndani ya hili eneo hususani kama hauna historia kubwa sana kwenye maisha yako ambayo inaendana na mambo ya siasa. Ndiyo sababu huwa nashangaa sana pale mtu anapotokea tu mtaani na kuhitaji kukutoa kirahisi kwenye sehemu hii ambayo anakuwa hajui ni kwa namna gani umefanikiwa kuingia na ni gharama kiasi gani umezitumia kufikia sehemu ya kupendwa na watu wengi ndani ya nchi"

"Mimi huenda sikutakiwa kuwa hapa leo kutokana na historia yangu ambayo haijawahi kuwa nzuri licha ya mimi leo kuwa kiongozi mkubwa, huenda mpaka leo nilitakiwa niwe natumikishwa na watu huko kijijini kwetu ambako mimi nimezaliwa, ila cha ajabu mimi ndiye ninaye watumikisha leo nitakavyo hahahaha"

"Mimi ni mnyiha kwa kabila, ni mnyiha kabisa kwa asili na Kinyiha ndiyo lugha mama yangu. Nimezaliwa ndani ya kata ya Idiwili katika kijiji cha Idiwili. Hii ni moja ya kata zinazo patikana wilaya ya Mbozi, ndani ya mkoa wa Songwe ambao zamani ulifahamika kama Mbeya. Kijiji chetu kilikuwa ni maarufu sana kwa biashara ya minaada ya uuzaji wa ng'ombe ambapo kila siku za minaada ungeweza kutaona magari makubwa yakiwa yanapakia ng'ombe wengi kuelekea maeneo mbali mbali ndani ya nchi huku wengine wakiwasafirisha kwenda nje ya nchi, kadri walivyo ona kwamba inawafaa kwa biashara yao wao"

"Mimi nimezaliwa kwenye familia ambayo naweza kusema ni ya kimaskini sana, maisha hayakuwa mazuri ya kusema nitaishi na kupata kila kitu hapana bali yalikuwa maisha ya uhakika wa kula kile kilicho patikana kwa jitihada za baba yangu mzazi. Kwa maisha ambayo tulikuwa nayo nyumbani, baba yangu aliona kwamba njia pekee ya kuja kuikomboa familia yetu kutoka kwenye yale maisha ni kuweza kunisomesha mimi kwa bidii sana hivyo nikawa nimeanzishwa shule ndani ya shule ya msingi Idiwili"

"Tangu nikiwa mdogo sana baba yangu alikuwa akinisisitiza sana kuhusu umuhimu wa elimu, alinihakikishia kwamba elimu inaweza kunisafirisha eneo lolote lile ambalo mimi ningelihitaji duniani hivyo nisimuache elimu aende zake, maneno ya baba yangu nikayaweka akilini kwa usahihi. Baba yangu aliniambia kwamba nifanye kila nalo liweza ila tu nihakikishe kwamba familia yangu haiji kuishi kwenye umaskini kama vile ambavyo familia yake tunaishi, hilo nikaliweka kabisa ndani ya moyo wangu ili nisije nikalisahau hata siku moja"

"Kutokana na maisha kuwa ya hali ya chini ndani ya kile kijiji, baba yangu akaanza kujihusisha na shughuli za uvuvi ambapo kila wiki ilikuwa ni lazima aende ziwa Tanganyika huko na aliporudi basi walau tulipata bahati ya kuweza kula vizuri maisha yakawa yanakuwa mazuri pale anapoondoka na kurudi na kitu ambacho kilimsaidia sana baba kwenye upambanaji ni kwamba alibahatika kupata mwanamke bora sana ambaye alikuwa ni mama yangu mzazi"

"Ugumu wa maisha uliwafanya wazazi wangu waweze kuchelewa sana kunitafutia mdogo wangu huenda ndiyo ilikuwa sababu yangu nyingine ya kuwa mpweke sana kwa maana sikuwa nimezoeana na mtu mwingine yeyote yule zaidi ya mama yangu ambaye muda mwingi nilikuwa naye hivyo akawa ndiye rafiki yangu mkubwa sana. Alikuwa anapenda sana kunisimulia hadithi za kale na namna walivyokutana na baba yangu basi nikawa nina furaha sana."

"Tangu naanza kujitambua sikuwahi kuona ndugu yeyote yule pale nyumbani wala kusikia kama tulikuwa na ndugu mahali, ndipo siku moja nikaamua kumuuliza mama yangu. Alisikitika huku akisema kwamba baba yangu mpaka umri huo alikuwa hajawahi kumjua baba yake kwani mama yake alikuwa mtu wa kusafiri sana kwenye mikoa mbali mbali na aliporudi alirudi akiwa na mimba hivyo akawa anahangaika mpaka nilipozaliwa"

"Baba yangu aliishi maisha ya mtaani sana mpaka alipofikia umri wa kuoa ambapo alimpata mama na kumuoa ambapo alidai kwamba familia ya mama ikawa ndiyo familia yake pekee. Baba yake na mama yangu yaani babu yangu alikuwa ni mfugaji wa ng'ombe pale kijijini hivyo ikamfanya kuwa maarufu sana ila umaarufu huo ndio ulio mfanya mama yangu akabaki kuwa yatima."

"Wakati huo mama anaishi na baba eneo jingine, siku moja familia yake ilivamiwa na watu ambao walikuwa na shida ya ile mifugo ya baba yake, walifanikiwa kuichukua mifugo na kuua familia nzima, yaani palibakia patupu. Hivyo naye akaungana na baba kuwa wakiwa kwa pamoja na kwa bahati iliyokuwa mbaya sana wote walikuwa wakiitegemea mifugo ya babu yangu ili kuishi yale maisha ya kawaida ambayo waliyazoea"

"Hali hiyo ilipelekea maisha kuwa magumu sana kwa upande wao kwani mtu ambaye walikuwa wanamtegemea alipotea ghafla sana huku hata mifugo ambayo ingewapa msaada mkubwa nayo ikabebwa, hali hiyo iliwafanya wapoteze tumaini la maisha na kukata tamaa mpaka pale nilipo zaliwa mimi. Mama yangu aliniambia kwamba kuzaliwa kwangu ni kama kuliibua tumaini jipya lililokuwa limepotea ndani yao na wakapata nguvu mpya ya kuanza kuyapambania upya maisha ili mtoto wao niishi na nifurahie kuwa na wazazi bora duniani. Ina maana kama sio mimi huenda mpaka wakati huo wasingekuwa hai."

"Hadithi ya mama iliniuma sana hivyo nikaapa kwamba ni lazima mimi nije kuwa mtu mkubwa sana hapo baadae kwa gharama yoyote ile. Maisha ya baba yangu kwenda ziwani yaliendelea, maisha ambayo yalileta unafuu wa maisha pale nyumbani na kwa wakati huo nilikuwa naujua ukweli kwamba sikuwa na ndugu yeyote wa kumtegemea kwa kudhani labda uwepo wake ungeleta ulaini kwenye maisha yangu, ilitakiwa kuwa mimi na maisha, maisha na mimi tu basi, hiyo ikanifanya niwe mwanafunzi niliyekuwa nasoma kwa hasira sana nikiwa bado mdogo mno. Hali hiyo ikanifanya niwe na uwezo mkubwa kichwani nikiwa bado mtoto mdogo"

"Upendo mkubwa wa wazazi wangu na maisha yaliyo anza kubadilika taratibu yakanifanya niwe na furaha isiyo na kipimo hasa baada ya kugundua kwamba mama yangu alikuwa mjamzito. Nilifurahi sana kuona kwamba muda mfupi tu ujao naenda kuwa na mtu ambaye angeniita kaka, hivyo nilijiandaa vyema kumpokea bwana mdogo ambaye nilikuwa nina uhakika kwamba nitampenda sana huenda hata zaidi ya ninavyo jipenda mimi mwenyewe"

"Taratibu nilianza kuwa mtu mwenye furaha sana ila furaha yangu ilikamilishwa na tabasamu ambalo nilianza kuliona kwenye uso wa mama yangu kila ilipo itwa leo, tulishia kuwa na kicheko kabla ya siku moja kupata taarifa, taarifa ambayo ilikuwa mbaya sana, taarifa iliyo nifanya kwa mara ya kwanza mimi kuwa na chuki sana na wanadamu kwa yale ambayo yalikuja kunikuta, hahahahaha eti wale wale wananiita raisi leo"

"Ni siku moja ya juma ambayo kama kawaida ilikuwa ni lazima baba yangu aende ziwani. Ziwani ambako mimi nilijua kwamba baba yangu huwa anaenda kununua samaki kisha angeingia mtaani kuwauza na kupata ujira wake ila mawazo yangu hayakuwahi kuwa sahihi kwani baba yangu alikuwa ni zaidi ya hapo. Sikuwahi kujua kwamba baba alikuwa anaingia mwenyewe ziwani na kwenda kuvua kwa mikono yake, nilikuja kujua nikiwa nimechelewa sana na ndiyo siku ambayo heshima yangu kwa mzee yule iliongezeka zaidi ya mara kumi, alikuwa anafanya kila kitu ili kuhakikisha familia inakuwa ina furaha. Baba yangu alikuwa mwanaume wa shoka haswa"

"Siku ile anaondoka, nakumbuka aliniaga usiku wake kwa maana kesho nisingekutana naye kwa sababu alikuwa anawahi sana kuondoka kabla ya mimi kuamka na hata wakati ningerudi shule basi nisingemkuta mpaka mwisho wa juma ambapo ndipo angerudi. Nilifurahi kwa sababu nilijua baba anaenda kupambana ili mwanae nipate angalau mahitaji ya mhimu ila sikujua kwamba ndiyo siku ya mwisho kumuona baba, yale maneno yake ya busara ambayo aliniambia kwamba napaswa kumsikiliza mama yangu, alikuwa ananiaga baba yangu na huenda alijua kwamba hatarudi tena kwenye maisha yangu. Kuna muda huwa natamani nimlaumu kwanini asingeniambia ili nimzuie kwenye ile safari yake? Ila kila nikikumbuka maisha yanapangwa na kila mtu atakufa huwa najikuta naishiwa nguvu kabisa naamua kuwa mpole"

"Zilipita siku mbili tu tangu baba yangu aweze kuondoka ndipo ilikuja taarifa mbaya zaidi mimi kuwahi kuisikia kwenye masikio yangu. Wakati narudi shule nilikuta mama yangu amezimia huku baadhi ya wanawake wakiwa wanampepea na tumbo lake. Kabla sijakaa sawa kuna jirani yetu akaniita pembeni na kuniambia kwamba baba yangu amezama ndani ya ziwa na amekufa hivyo mimi natakiwa kuwa mfariji wa mama yangu kwa maana mwili wa baba yangu ungeletwa kesho kwa ajili ya kufanyiwa mazishi."

"Nakumbuka vizuri sana kwa wakati ule nilikuwa nipo darasa la nne tu ila kiakili nilikuwa najielewa vizuri. Nililia sana siku ile, huenda ningesema kwamba nalia kwa sababu uchungu wa kumpoteza baba yangu tu ila kwa baadae nilikuja kugundua kwamba ilikuwa ni zaidi ya hapo baada ya kumuona mama yangu akiwa anateseka na lile tumbo lake ambalo lilikuwa limesha anza kuwa kubwa. Mama yangu alikuwa anazimia kila wakati, hata pale tulipo maliza mazishi na kila mtu akawa ametawanyika, kazi yangu kubwa ikawa ni kuwa karibu na mama yangu kwa maana hali yake ilianza kuwa mbaya sana."

"Alikuwa mtu wa majonzi wakati wote kwa kumpoteza mumewe kipenzi. Kwa sababu mama yangu aliishi na watu vizuri nilianza kuomba msaada kwa majirani ili waweze kunisaidia angalau mama yangu aweze kutibiwa vizuri na apone na ule ujauzito wake ila kilicho tokea watu wale walianza kunikejeli na kudai mama yangu alijiona ameyapatia maisha baada ya mumewe kuanza kumtunza, wakadai kwamba mama yangu acha akione cha moto kwa maana alijiona yeye ndo anajua kupendwa sana. Kwenye kuhangaika kwa watu wale ndipo nikaja kugundua kwamba hata kufa kwa baba yangu haikuwa bahati mbaya bali ni wenzake walimfanyia hila baada ya kumuona kila akienda huko angerudi na samaki wengi sana na kupata ujira mzuri kuliko wao, hivyo wakaona wamuulie huko huko na kumuacha katikati ya ziwa huko bila msaada mpaka pale alipo anza kutafutwa na kukutwa akiwa amekufa"

"Niliwachukia sana binadamu ila sikuwa na namna. Hali ya mama ilitufanya tuuze maeneo kidogo yaliyokuwepo, kutokana na bei za vijijini haikusaidia kitu mpaka siku ambayo niliona mama yangu anakufa kwenye mikono yangu mwenyewe huku nikiwa sina namna ya kumsaidia. Halafu tumboni alikuwa amembeba mdogo wangu ambaye nilikuwa namsubiria kwa hamu sana. Pale ndipo nilipokuja kuwakoma wanadamu kwa waliyokuja kunifanyia"

"Bosi, chakula kipo tayari na mzigo ambao uliuagiza tayari umeletwa" mheshimiwa raisi Theobald Mnyika akiwa kwenye hayo mawazo mazito ambayo yalimrudisha kwenye historia ya nyuma kabisa ya maisha yake. Alikatishwa na sauti ya mlinzi wake ambaye alikuwa anamkumbusha kwamba chakula Chake kilikuwa tayari lakini hata mzigo wake ulikuwa umefika.

Kuna lipi lipo nyuma ya historia ya mheshimiwa raisi? Anahitaji kutuambia nini mpaka kuwe na ulazima wa kuijua historia yake?

Episode ya 35 inafika mwisho.

Febiani Babuya.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
STORY: DOCUMENT NUMBER 72
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
EPISODE 36

Siku zilienda kwa kasi mno isivyokuwa kawaida. Calvin alipata mwaliko ndani ya Ikulu kwa mara ya kwanza. Mwaliko ambao uliambatana na ahadi ya mheshimiwa raisi, mualiko huo ulikuwa ni maalumu lakini lia ulikuwa sawa sawa na ujio wa wageni mbali mbali kutoka mataifa mbali mbali kwa ajili ya kuja kutoa pole zao kutokana na lile tukio ambalo lilikuwa limeikumba nchi ya Tanzania.

Calvinjr mwaliko wake ulikuwa unawahusu yeye na Sarafina, mapenzi yao yalikuwa yapo wazi kwa sasa na raisi huyo alikuwa anahitaji kuwaona watu hao wawili wakivalishana Pete nia yake ikiwa ni kama kutumiza ahadi yake ya kuhakikisha mtoto wa rafiki yake waziri mkuu anakuwa sawa licha ya yale ambayo yalikuwa yamemkuta.

Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza Calvinjr kufika ndani ya eneo hilo akiwa ameongozana na mpenzi wake Sarafina William, sasa alielewa kwamba ni kwanini watu wengi huwa wanaing'ang'ania hiyo sehemu, ni pazuri isivyokuwa kawaida. Tafrija ndogo ilikuwa ikiendelea na wageni mbali mbali walikuwa kwenye sherehe hiyo mwanaume akiendelea kufurahia mazingira taratibu mpaka pale alipo muona bosi wake ila walifanya kama vile hawakuwahi kuonana kabisa kwenye maisha yao yote wakapishana kana kwamba hawajuani kwa lolote.

Calvinjr alienda kukaa na mpenzi wake huku mpenzi wake akiwa amesindikizwa na marafiki kadhaa ila baada ya dakika chache aliomba aelekezwe uani ni wapi. Mwanaume baada ya kuelekea huko uani akiwa anajiweka sawa alihisi kama hatua chache kutoka alipokuwa kuna mtu alikuwa anapewa onyo kali kwa kosa ambalo alikuwa amelifanya.
"We mpuuzi unajua ni gharama kiasi gani watu wanazitumia kufika hapa"
"Najua kiongozi, imetokea ni bahati mbaya sana baada ya kulewa nikaanza kuongea ukweli"
"Kwahiyo ukinywa bia mbili tu unaanza kuropoka?"
"Hapana mkuu ni bahati mbaya tu"
"Unatakiwa uende unakostahili mbwa wewe" mwanaume huyo ambaye alionekana kumgombeza mwenzake huyo alitoa bastola yake akaweka kifaa cha kuzuia sauti kisha akamfumua kijana huyo kichwani. Calvinjr alikuwa amejibanza sehemu akiwa anarekodi hilo tukio na simu yake iliyokuwa na uwezo mkubwa kisha akarudi ile sehemu ambayo alikuwa amekaa mwanzo huku akiwa anashangaa sana kivipi sehemu ambayo inasemekana kuwa ndiyo salama zaidi ndani ya nchi nako wanafanyia mauaji namna ile? Hilo jambo alilihifadhi kwenye nafsi yake.

Mheshimiwa raisi baada ya kumaliza kusalimiana na wageni wake alisimama ili kutoa maneno machache ambayo alihisi ulikuwa ni wakati wake sahihi kuweza kuyaongea.
"Ni matumaini yangu mpo wazima wa afya kabisa, leo ni moja ya siku nzuri ambazo tumepata bahati kama nchi ya kutembelewa na wageni kutoka pande mbali mbali za dunia wakija kutupa pole na kutuunga mkono mwamba tupo pamoja kwa kila hatua kwa tatizo ambalo lilitupata miezi kadhaa ambayo imekwisha kupita huko nyuma"

"Siku ya leo pia ni moja ya siku ambazo nina imani rafiki yangu waziri mkuu ambaye alitutoka atakuwa na furaha sana akiwa mahali anamwangalia binti yake alivyokuwa na furaha isiyokuwa na kifani. Ni baada ya binti huyo kufanikiwa kuipata sehemu ambayo ni furaha ya maisha yake kwa hapa duniani"

"Leo ni siku maalumu ambayo Sarafina William anavalishwa Pete yake na mchumba wake wa siku nyingi ambaye wanapendana sana,Mr Calvinjr. Hivyo nawaombeni sana popote mlipo muweze kusimama na kutupatia furaha ambayo bila shaka ni moja ya lengo kubwa sana la sisi kuwa hapa" hakukuwa na jambo lingine zaidi ya wachumba hao kusimama na kukamilisha kile ambacho kilikuwa kimewaleta hapo.

Zoezi hilo lilienda vizuri kabisa kama wao walivyokuwa wamelipanga na hatimaye likaisha salama. Baada ya tukio hilo kumalizima, Sarafina akiwa anapongezana na wageni waalikwa mbali mbali pamoja na marafiki zake, mheshimiwa raisi alihitaji kupata neno pamoja na Calvinjr kwa mara nyingine wakiwa wawili tu.
"Kijana wangu nadhani ni mara ya pili hii tunapata nafasi ya kuzungumza tena. Sitaki sana kuingilia mambo yako ila nahisi kama sijaona ndugu yeyote kutoka upande wa kwenu, kuna tatizo gani?" Swali lilikuwa lina maana kubwa kwa sababu kwa hali iliyokuwepo Calvinjr hakuwa na mtu hata mmoja ambaye alikuja kwa ajili yake kwenye siku ya mhimu kama hiyo ambayo alikuwa anamvalisha pete mpenzi wake

"Mheshimiwa upo sahihi sana, siku ya leo ni siku kubwa sana na huenda nilitakiwa kufanya hivyo kwa sababu nimepata heshima kubwa mno kutoka kwako. Sikutegemea kama unaweza ukanifanyia jambo kubwa kama hili la kumvalishua mpenzi wangu Pete ndani ya ikulu, naomba nikushukuru sana kwa hilo. Kuhusu upande wa ndugu zangu kuja, mimi sina ndugu wengi ninao wajua, wapo wawili tu mheshimiwa ambao ni mama yangu pamoja na dada yangu ila kwa bahati iliyokuwa mbaya mama yangu ni mgonjwa na dada yangu ndiye mtu pekee ambaye anakuwa anamuangalia mama pale ambapo mimi nakuwa mbali hiyo ndiyo sababu kubwa"

"Pole sana kijana wangu, huo ndio utu uzima. Kwa umri ulio fikia unatakiwa kuwa tayari kuyabeba majukumu ya aina yoyote yale ili tu kupata nafasi ya kuilinda na kuitunza familia yako. Niliamua kukualika hapa Ikulu ili uje uone namna nchi inavyo endeshwa kwani tayari unaelekea kuoa kwenye familia ya siasa"

"Yes, hilo nimeliona vizuri mheshimiwa. Ikulu ni moja kati ya sehemu bora sana kuishi. Mazingira yake, watu wake, namna mambo yanavyo endeshwa hapa ni tofauti kabisa na maisha ya huko nje yanavyo endeshwa"

"Hahahahaha ndiyo maana watu wengi sana wanahitaji kuingia hapa hata kwa kutoa maisha ya watu, hawajali kuua wala maisha ya watu maskini ila wanacho jali ni kufika hapa nilipo mimi, unahisi kwanini Calvinjr?"

"Huenda ni kwa sababu ya upekee wa hili eneo lakini pia muda mwingine huwa ni raha sana pale ambapo wewe ndiye unakuwa mtu unaye sikilizwa zaidi. Hiyo ndiyo sababu kubwa zaidi ambayo huenda huwa inawafanya watu wawe wanakesha ili kuweza kuingia ndani ya sehemu hii inayo onekana kuwa nzuri sana"
"Vipi wewe hautamani siku moja kuja kukalia kiti hiki na wewe ukawa ndiye mtu anaye sikilizwa zaidi ndani ya nchi hii?"
"Mheshimiwa nadhani sijakuelewa, unamaanisha nini kusema hivyo?"
"Namaanisha wewe hautaki kuwa raisi?"
"Hapana mheshimiwa sijawahi kufikiria kabisa mambo ya siasa na siyawezi kabisa ndiyo maana huwa nipo nayo mbali sana"
"Kwanini unahisi labda hauiwezi siasa?"
"Sina uhakika mheshimiwa ila nasikia kwamba siasa ina mambo mengi sana ya kutisha. Nasikia huku maisha unakuwa umeyashikilia kwenye mikono yako muda wowote kuna watu wanaweza kuondoka nayo lakini kinacho nitisha zaidi ni kwamba kuna muda nasikia inatakiwa uue hata wasio na hatia au kuwasingizia wanyonge kesi ili uwe salama. Kwani ni ya kweli haya mhesimiwa raisi?"

"Hahahaha, Calvinjr umesikia mengi sana kuhusu siasa, hayo ni maneno ya watu wa mtaani na mitandaoni lakini mengine yanatoka kwa watu ambao wapo kwenye siasa pia hususani wapinzani. Siasa kama ni mbaya kiasi hicho na wapinzani wanasema hivyo sasa haujiulizi wao bado wanatafuta nini kwenye siasa? Yaani mtu anakuchafua kwa jambo ambalo naye analihitaji kwa namna ile ile, hapo ndipo panaleta maswali mengi sana. Mengi yanayo zungumzwa yapo sahihi, unajua kwenye siasa mwenye nguvu kubwa ndiye anaye ishi au ndiye anayeshinda na mnyonge lazima ashindwe au aliwe. Ni kama mfumo wa wanyamapori, simba lazima amle swala ili aishi, kama akishindwa kufanya hivyo basi anatakiwa yeye kufa, je nani yupo tayari? Hapo ndipo siasa inapoanza kutisha kama una moyo mwepesi kwa sababu kuna muda inatakiwa uyafanye mambo ya kutisha ambayo huenda hata moyo wako haupo tayari kukumbana nayo ili uwe salama"

"Mheshimiwa kwamba na wewe umewahi kufanya hayo mambo labda?" Swali la Calvinjr lilimfanya raisi huyo amwangalie sana huyo kijana.

"Nikiwa na umri kama wako huo nilikuwa nimefanya kila jambo hapa duniani, liwe jema sana, baya sana na mpaka yale mambo ya kutisha. Unajua kwanini nilifanya hivyo? Kwa sababu ya maisha. Kuna muda maisha yanakufanya usiwe na chaguo la kufanya ila unaamua kufanya ili uweze kuishi pamoja na kuuepuka ulimwengu wa fedheha ambao unaendelea na dharau nyingi. Leo ambao walikuwa wananicheka na kuninyanyasa wananipigia magoti kila wakiniona na hivyo ndivyo wanaume wenye mamlaka wanavyo paswa kuwa bwanamdogo"

"Kwanini umeona ninafaa mpaka uniulize kama natamani kuwa raisi?"
"Hahaha, nina umri mara mbili yako na zaidi huenda. Naweza kumsoma mwanadamu kwa macho na namna uhalisia wake ulivyo. Wewe ni kijana mpole sana na upo smart sana ila kila nikikutazama kwenye macho yako naona kuna moto unawaka, inamaanisha ndani yako una roho nyingine tofauti na hii ambayo inaonekana kwa. Ninaweza kukufanya ukawa raisi kwa makubaliano" Calvinjr alihisi kama jambo hilo lilikuwa la utani ila aliona kama mzee huyo alikuwa anazidi kuwa siriasi sana.
"Mheshimiwa naomba nipe muda kuhusu hilo niweze kulifikiria kwa umakini ili nikupe jibu sahihi zaidi"
"Nina imani utafanya maamuzi ya kiume, naweza kukufanya ukawa mwanaume mwenye nguvu zaidi ndani ya nchi hii ukaishi unavyotaka wewe"
"Sawa mheshimiwa, ila kuna kitu kidogo nilikuwa naomba kuuliza"
"Nakusikiliza"
"Hivi mkuu mhusika wa ule mlipuko aliweza vipi kupatikana? Kwa maana mimi bado nina wasiwasi sana, naona ni muda mfupi ujao naenda kuoa isije kutokea tena tatizo lingine nikashindwa kuishi vyema na mke wangu" swali la Calvinjr kwa mara ya kwanza lilionekana kumshtua sana raisi huyo ila alivyo malizia mwishoni kuonyesha hofu mzee huyo alitabasamu.

"Haya ni mambo ya ndani sana kuhusu usalama wa nchi na siwezi kukwambia ila nataka uwe na amani na ujue ya kwamba hili jambo haliwezi kutokea tena kamwe kwa sababu limeisha. Unaweza ukaendelea na utaratibu mwingine mimi natoka kuongea na wageni wangu" Mzee huyo aliamua kuyafupisha maelezo hayo ambayo hakuoneka kuvutiwa nayo. Calvinjr kuuliza hilo swali kulikuwa na maana kubwa sana kwa upande wake ila bahati iliyokuwa mbaya alijibiwa kifupi fupi tu akashindwa kupata kile ambacho alikikusudia hivyo hakuwa na namna zaidi ya kuondoka.
"Sawa Mr president"

Episode ya 36 inafika mwisho.

Febiani Babuya.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
STORY: DOCUMENT NUMBER 72
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
EPISODE 37

Alfajiri na mapema kabisa siku moja Calvinjr alikuwa anaelekea nyumbani kwa mama yake kuweza kumtambulisha mpenzi wake huyo ambaye miezi kadhaa alitoka kumvesha Pete Ikulu, ni kwa muda mrefu sana mama yao amekuwa akiwataka watoto hao wawili ambao alikuwa nao wampatie wajukuu wa kucheza naye ila wamekuwa wakimkwepa kwepa sana hatimaye mwanae wa kiume alikuwa anaenda kumpatia heshima kubwa sana ambayo hakuwa ameitarajia kabisa kuipata.

Licha ya Calvinjr kwenda kumtambulisha mtoto wa waziri mkuu kama mchumba wake ila pia alihitaji kuwepo na kikao cha familia pia ambapo walitakiwa kuongea wakiwa pamoja hivyo dada yake ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kabisa kufika hapo kwao ili kusaidiana na mama yake kwenye maandalizi kwa maana waliambiwa kwamba kuna mgeni anafika muda sio mrefu.

Calvinjr wakati anaingia ndani ya geti la nyumbani kwao baada ya kushuka kwenye gari na mapenzi wake alipishana na mwanaume mmoja ambaye alikuwa kwenye suti ya bei ghali akiwa na kofia kubwa kichwani kwake. Mwanaume huyo uso wake haukuwa sawa kama zilivyo nyuso za watu wengine, uso wake ulikuwa na alama kubwa ya kutisha kuonyesha kwamba kuna kitu chenye ncha kali sana kiliwahi kumpitia ambacho kiliuharibu kabisa mwonekano wake huo.

Mwanaume huyo alimsogelea Calvinjr pale alipokuwepo akiwa anamwangalia kwa umakini sana kwenye uso wake.
"Umekua sana Calvinjr" aliongea huku akiwa anampa mkono. Calvinjr alibaki ameduwaa kwa maana hakuwa na kumbukumbu kama kwenye maisha yake aliwahi kukutana na mtu wa namna hiyo, ila hakuwa na namna akaamua kuupokea mkono huo ambao ulikuwa umekomaa isivyokuwa kawaida, hakuonekana kuwa mtu wa kawaida. Mwanaume huyo baada ya kumpatia salamu hiyo alianza kuelekea getini. Kupitia kusalimiana na mtu huyo Calvinjr alifanikiwa kuona kitu kimoja kwenye mwili wake, wakati anampa mkono suti ilijivuta na alama ya "Nge" ikaonekana kwenye mkono wa mtu huyo.

Aliangalia getini, mlinzi alikuwepo hivyo akawa na uhakika kwamba nyumbani palikuwa na amani akaamua kumuacha mtu huyo aende ila alitamani sana kujua taarifa zake, akatabasamu na kumbusu mpenzi wake na kuingia naye ndani kwa mikogo. Mama yake na Calvinjr ndiye alikuwa mtu wa kwanza kwenda kumpokea mrembo huyo kwa furaha, mama huyo alishangilia isivyokuwa kawaida kwa maana jambo hilo amelisubiria kwa muda mrefu sana hatimaye leo MUNGU alikuwa ameyajibu maombi yake.

Ulifika wakati wa chakula, hakutana kukaa mbali na mkwewe akiwa anamsisitiza kwamba anatakiwa kula ili awe na afya nzuri kwa sababu watoto ili wazaliwe wakiwa sawa mama anatakiwa kuwa na afya njema. Ulifuata utambulisho ambapo mama huyo alimpa sana pole binti huyo kuweza kumpoteza baba yake mzazi na sasa alikuwa rasmi amekaribishwa kwenye hiyo familia muda wowote ambao angehitaji kufika hapo palikuwa ni kama kwake.

Baada ya chakula kuisha Calvinjr aliwaita wote mezani ili wake kikao kama alivyokuwa amewaambia mwanzo.

"Mama nashukuru sana kwa mapokezi yako mazuri kwa mkweo, ni matumaini yangu wote mmefurahi sana na rasmi muda sio mrefu anaenda kuwa mke wangu kabisa wa ndoa. Lakini pia hapa kuna jambo moja la mhimu sana ambalo unatakiwa kulijua ikiwepo kutoa baraka zako ila kabla ya kulisema jambo hilo naomba kumfahamu yule mtu ambaye nimepishana naye asubuhi hapa maana anaonekana mwamba ananifahamu sana ila mimi sijawahi kumuona hata siku moja"

"Mhhhh Calvinjr mwanangu, yule ni moja ya watu ambao tuliwahi kuwa na urafiki nao miaka ya nyuma huko hivyo familia yangu anaijua vizuri sana ila kwa bahati mbaya usingeweza kumjua kwa sababu muda mwingi ameutumia kuishi kwenye nchi za watu huko. Leo alitamani sana kukaa na nyie hapa awafahamu vizuri ila kwa bahati mbaya akawa amepokea simu kwamba anahitajika mahali ndiyo maana amefika na kuondoka haraka sana ila kuna siku mtakutana naye tena" Calvinjr hakutaka kuuliza sana mbele ya mgeni ila aliona kabisa mama yake anamdanganya, macho ya mama huyo yalionyesha wazi kwamba mwanamke huyo hakuwa akiongea ukweli wowote ndani yake.

"Mama dada amepata kazi ndani ya nchi ya Rwanda, kazi hiyo inaenda kutusaidia kuimarisha kampuni yetu pamoja na makampuni mengine ambayo yanafanya kazi ndani ya nchi hiyo hivyo anatakiwa kusafiri na kwenda huko. Samahani sana kwa kuchelewesha taarifa hii kufika mwenye mkono wako kwa maana maombi yenyewe yamejibiwa jana tu" kauli ya Calvinjr ilimfanya mama huyo amgeukie mwanae huyo wa kike aliyekuwa anaitwa Tina, ambaye aliitikia kwa kutikisa kichwa.

"Yaani mwanangu mimi aende Rwanda? Kisa kazi au kuna lingine? Shida ni pesa? Anataka shingapi? Hiyo pesa nitampa mimi mwenyewe siwezi kuruhusu hilo jambo litokee. Watoto wenyewe ninao wawili tu, hapana kwakweli" mama huyo alipingana na hizo stori ambazo watoto wake walianza kumletea hapo na kuona kama wanamuumiza kichwa tu. Walimdanganya kwamba mwanamke huyo alikuwa anaenda kufanya kazi ya kampuni asijue kwamba wanae wote ni majasusi na huko ilikuwa inaenda kufanywa moja kati ya kazi ngumu isivyokuwa kawaida.

"Shida sio pesa mama, tunahitaji hii kampuni iwe zaidi ya hivi ilivyo leo. Kuna familia kubwa inakuja hapo baadae, watoto wanatakiwa kukuta mazingira rafiki kwao ambayo hayatawafanya waanze kuhangaika. Hizi nafasi ambazo tunazipata tunahitaji kuzitumia ili tupate watu wengi ambao watatusaidia hapo baadae hususani pale tutakapo hitajika kufungua fursa zingine kwenye nchi zingine kubwa. Nakuomba sana mama yangu uniruhusu nikafanye hii kazi" ilikiwa ni sauti ya Tina akiwa anamsisitiza mama yake aweze kumpa hicho kibali cha kwenda kuifanya hiyo kazi.

Mama huyo aliinuka na kwenda chumbani kwake, alitoka na kipande kidogo cha picha ambacho kilikuwa kimechakaa sana kwenye upande wa sura ya mtu ambaye alikuwa kwenye picha hiyo na kuifanya sura ya mtu huyo isionekane.

"Ni miaka zaidi ya ishirini sasa bila yeye kuwepo wala kuwaona nyie. Jambo pekee ambalo nilijiahidi mwenyewe ni kuhakikisha kwamba nawalinda kwa gharama yoyote ile ili hata yeye huko aliko aweze kufurahia wanae wawe na furaha. Sasa vipi tena mwanangu unataka kwenda mbali huko ambako bila shaka sitaweza kukulinda? Kwanini mwanangu?" mama huyo aliongea kwa uchungu sana akiwa analia, alikuwa anawapenda sana hao watoto na hakuwa tayari kuwaona wanapata matatizo ndiyo maana aliogopa sana kumruhusu mwanae huyo aweze kutoka ndani ya mipaka ya Tanzania tena akiwa mwenyewe kabisa.

Wanae pamoja na mkwewe walimkumbatia mama huyo kwa maana hakuwa na namna ya kuweza kuzuia, kisha dada mtu akatoka nje na kaka mtu ili kuweza kuongea kidogo.
"Sis una uhakika na hili?"

"Ndiyo, nina uhakika nalo, ni mwaka umeisha sasa tangu lile tukio liweze kutokea, kwa sasa tunatakiwa rasmi tukamalize kile ambacho tuliamua kukianza"

"Unajua mambo sio marahisi kama unavyo yahisi wewe" Calvinjr yeye mwenyewe alikuwa na wasiwasi sana kumruhusu dada yake kwenda pekeyake ndani ya taifa la Rwanda ila hakuwa na namna ya kufanya kwa sababu kazi ilikuwa inawataka wafanye hivyo. Hii ndiyo siku ambayo dada yake alimwelekeza mdogo wake kwamba hatakiwi kutumia sana hisia kwenye lile eneo ambalo linamtaka atumie zaidi akili, Calvinjr hakuwa na namna zaidi ya kumkubalia dada yake.

"Kitu cha msingi sana unapokuwa kule, zingatia mawasiliano. Hakikisha hauna mawasiliano ya mara kwa mara ambayo yatawafanya wakushtukie kabisa, yaani jifanye kama mtu ambaye hauna lolote unalo lijua kuhusu watu wengine ila kama ikitokea dharura, nadhani unajua namna ya kuwasiliana namimi" mdogo mtu alimsisitiza dada yake huku akiwa anamkumbatia, alijua huko aendako kuna mawili, kurudi au kuishia huko huko na asirudi tena.
Walimuaga mama yao na kuondoka huku Calvinjr akienda kwake na mpenzi wake na dada yake akielekea ndani ya taifa la Rwanda rasmi.

Mwanamke huyo baada ya wanae na mkwewe kuondoka, aliingia kwenye chumba chake ambapo aliingia kwenye ile sehemu yake ya siri na Kujifungia, aliziangalia kwa uchungu sana zile picha ambazo alizisambaza kwenye ukuta wake huku zote zikiwa zimekatwa upande wa kichwani, alikuwa akitoa chozi akiwa anaziangalia picha hizo. Aliingiza mkono kwenye droo moja na kuitoa picha ya mwanaume huyo ambayo ilikuwa kamili kabisa, aliiangalia mpaka chozi likadondokea kwenye picha hiyo.

"Mwanao amekua sasa, mwanao ameniletea mkwe leo. Leo ni moja ya siku za furaha sana kwangu ila pia ni moja ya siku ya uchungu sana kwangu. Natamani kama ungekuwa hapa leo na mimi tumfurahie mtoto wetu, natamani ungesimama kama baba ukayanena yaliyo mema kwa mwanao ila kitu cha kusikitisha ni kwamba hauwezi kuwa hapa kwa sababu huenda hata haujui kama nina damu yako"

"Nawaza siku mwanangu akija kujua ataniona mimi mama wa aina gani, nawaza atanichukuliaje? Nabaki naogopa sana. Ila sitaruhusu jambo lolote limkute mwanangu na sitaruhusu kamwe aje kujua kwamba wewe bado unaishi, huyu anatakiwa kujua kwamba wewe ulikufa miaka mingi sana, nitamlinda mwanangu kwa gharama yoyote na atakaye onyesha tu kujua hili jambo nipo radhi kumuua. Leo mwanangu wa kike ameondoka na kwenda mbali na mimi, nimechanganyikiwa hata sijui nifanye nini ila sitaruhusu na mwanangu wa kiume aende mbali, huyu ni wa kwangu mimi baba Calvinjr, sitaruhusu mtu yeyote amguse mwanangu" mwanamke huyo aliongea kwa sauti ya juu sana huku akiwa anaipiga piga hiyo picha ambayo haikueleweka ina uhusiano gani na hao watoto wake hasa mwanae wa kiume kwa maana alikuwa na uchungu sana anapokuwa anaiona picha hiyo.

Aliichukua simu yake nyeusi ambayo ilikuwa ndani ya droo hiyo na simu hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kuwasiliana na mtu mmoja tu, aliipiga ikapokelewa kwa haraka sana.

"Mwanangu wa kike anaenda Rwanda ,nahitaji alindwe na asije akapatwa na jambo lolote lile"
"Mama sidhani kama huo utakuwa ni uamuzi wenye busara" sauti nzito ila yenye heshima ilisikika upande wa pili ikiongea kwa utulivu.

"Miss anaishi maisha ya kawaida ambayo yanamfanya asiwe na maadui wala kushtukiwa na mtu yeyote yule, ila tukisema kwa sasa aanze kulindwa basi italeta mashaka sana na ataonekana kule ana agenda zake hivyo tunaweza kumuwekea hatari zaidi kuliko faida ambazo zitakuwepo. Kule ni nchi ya watu, akiingia kule serikali ya Rwanda inahusika kumlinda kwa asilimia miamoja kwani wanajua mtanzania akipata tatizo basi inaweza kupelekea mahusiano baina ya hizi nchi mbili kuvunjika" mwanaume huyo alitoa maelezo, wakati mama huyo akiwa anayafuta machozi yake.

"Unajua nitakacho kufanya kama mwanangu akipata tatizo lolote?"

"Ndiyo mama najua" aliikata simu na kutoka humo ndani, alifika mpaka nje ambapo alikutana na wanaume wawili waliokuwa kwenye suti, waliinamisha vichwa vyao baada ya mama huyo kufika, akaingia kwenye gari na kutoka na watu hao ambao bila shaka walionekana kuwa walinzi wake ambao hata wanae hawakuwa wakiwajua kabisa.

Unahisi kuna jambo gani haswa ambalo mama huyu analijua na hataki walimwengu walifahamu?

Episode ya 37 inafika mwisho.

Febiani Babuya.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
Natka kufahamu mbinu maaalum yenye inatumika kutambua kama mwenzangu nachepuka 🙏
 
THE LAST DANCE....OFA

Wakati tunaisubiri JIJI LA KAMARI ambayo inatoka rasmi kesho......natoa ofa ya mzigo huu wote wa SAKATA LA UCHAGUZI-PESA KWENYE DAMU kwa shilingi 2500 tu.......hii inaisha asubuhi na mapema kabisa (Ni ofa ya masaa machache sana)....Ruka na ofa yako tukutane inbox....ikifika asubuhi ofa inakuwa imeisha[emoji996]

LIPIA KWA NAMBA

0621567672 (WHATSAPP)

0745982347

ZOTE JINA FEBIANI BABUYA.

BURUDIKA SASA KABLA MUDA HAUJAISHA.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
JIJI LA KAMARI (GAMBLING)

Kesho softcopy (nakala laini) itaachiwa rasmi kwa mfumo wa pdf.

Ni simulizi mpya ya kipelelezi ambayo ina visa vingi sana, story kali sana na mapigano yasiyo ya kawaida.

Bei yake ni shilingi 5000 tu.

Unaweza ukanicheki WhatsApp kwa namba hii[emoji116]

0621567672

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…