STORY: DOCUMENT NUMBER 72
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
EPISODE 37
Alfajiri na mapema kabisa siku moja Calvinjr alikuwa anaelekea nyumbani kwa mama yake kuweza kumtambulisha mpenzi wake huyo ambaye miezi kadhaa alitoka kumvesha Pete Ikulu, ni kwa muda mrefu sana mama yao amekuwa akiwataka watoto hao wawili ambao alikuwa nao wampatie wajukuu wa kucheza naye ila wamekuwa wakimkwepa kwepa sana hatimaye mwanae wa kiume alikuwa anaenda kumpatia heshima kubwa sana ambayo hakuwa ameitarajia kabisa kuipata.
Licha ya Calvinjr kwenda kumtambulisha mtoto wa waziri mkuu kama mchumba wake ila pia alihitaji kuwepo na kikao cha familia pia ambapo walitakiwa kuongea wakiwa pamoja hivyo dada yake ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kabisa kufika hapo kwao ili kusaidiana na mama yake kwenye maandalizi kwa maana waliambiwa kwamba kuna mgeni anafika muda sio mrefu.
Calvinjr wakati anaingia ndani ya geti la nyumbani kwao baada ya kushuka kwenye gari na mapenzi wake alipishana na mwanaume mmoja ambaye alikuwa kwenye suti ya bei ghali akiwa na kofia kubwa kichwani kwake. Mwanaume huyo uso wake haukuwa sawa kama zilivyo nyuso za watu wengine, uso wake ulikuwa na alama kubwa ya kutisha kuonyesha kwamba kuna kitu chenye ncha kali sana kiliwahi kumpitia ambacho kiliuharibu kabisa mwonekano wake huo.
Mwanaume huyo alimsogelea Calvinjr pale alipokuwepo akiwa anamwangalia kwa umakini sana kwenye uso wake.
"Umekua sana Calvinjr" aliongea huku akiwa anampa mkono. Calvinjr alibaki ameduwaa kwa maana hakuwa na kumbukumbu kama kwenye maisha yake aliwahi kukutana na mtu wa namna hiyo, ila hakuwa na namna akaamua kuupokea mkono huo ambao ulikuwa umekomaa isivyokuwa kawaida, hakuonekana kuwa mtu wa kawaida. Mwanaume huyo baada ya kumpatia salamu hiyo alianza kuelekea getini. Kupitia kusalimiana na mtu huyo Calvinjr alifanikiwa kuona kitu kimoja kwenye mwili wake, wakati anampa mkono suti ilijivuta na alama ya "Nge" ikaonekana kwenye mkono wa mtu huyo.
Aliangalia getini, mlinzi alikuwepo hivyo akawa na uhakika kwamba nyumbani palikuwa na amani akaamua kumuacha mtu huyo aende ila alitamani sana kujua taarifa zake, akatabasamu na kumbusu mpenzi wake na kuingia naye ndani kwa mikogo. Mama yake na Calvinjr ndiye alikuwa mtu wa kwanza kwenda kumpokea mrembo huyo kwa furaha, mama huyo alishangilia isivyokuwa kawaida kwa maana jambo hilo amelisubiria kwa muda mrefu sana hatimaye leo MUNGU alikuwa ameyajibu maombi yake.
Ulifika wakati wa chakula, hakutana kukaa mbali na mkwewe akiwa anamsisitiza kwamba anatakiwa kula ili awe na afya nzuri kwa sababu watoto ili wazaliwe wakiwa sawa mama anatakiwa kuwa na afya njema. Ulifuata utambulisho ambapo mama huyo alimpa sana pole binti huyo kuweza kumpoteza baba yake mzazi na sasa alikuwa rasmi amekaribishwa kwenye hiyo familia muda wowote ambao angehitaji kufika hapo palikuwa ni kama kwake.
Baada ya chakula kuisha Calvinjr aliwaita wote mezani ili wake kikao kama alivyokuwa amewaambia mwanzo.
"Mama nashukuru sana kwa mapokezi yako mazuri kwa mkweo, ni matumaini yangu wote mmefurahi sana na rasmi muda sio mrefu anaenda kuwa mke wangu kabisa wa ndoa. Lakini pia hapa kuna jambo moja la mhimu sana ambalo unatakiwa kulijua ikiwepo kutoa baraka zako ila kabla ya kulisema jambo hilo naomba kumfahamu yule mtu ambaye nimepishana naye asubuhi hapa maana anaonekana mwamba ananifahamu sana ila mimi sijawahi kumuona hata siku moja"
"Mhhhh Calvinjr mwanangu, yule ni moja ya watu ambao tuliwahi kuwa na urafiki nao miaka ya nyuma huko hivyo familia yangu anaijua vizuri sana ila kwa bahati mbaya usingeweza kumjua kwa sababu muda mwingi ameutumia kuishi kwenye nchi za watu huko. Leo alitamani sana kukaa na nyie hapa awafahamu vizuri ila kwa bahati mbaya akawa amepokea simu kwamba anahitajika mahali ndiyo maana amefika na kuondoka haraka sana ila kuna siku mtakutana naye tena" Calvinjr hakutaka kuuliza sana mbele ya mgeni ila aliona kabisa mama yake anamdanganya, macho ya mama huyo yalionyesha wazi kwamba mwanamke huyo hakuwa akiongea ukweli wowote ndani yake.
"Mama dada amepata kazi ndani ya nchi ya Rwanda, kazi hiyo inaenda kutusaidia kuimarisha kampuni yetu pamoja na makampuni mengine ambayo yanafanya kazi ndani ya nchi hiyo hivyo anatakiwa kusafiri na kwenda huko. Samahani sana kwa kuchelewesha taarifa hii kufika mwenye mkono wako kwa maana maombi yenyewe yamejibiwa jana tu" kauli ya Calvinjr ilimfanya mama huyo amgeukie mwanae huyo wa kike aliyekuwa anaitwa Tina, ambaye aliitikia kwa kutikisa kichwa.
"Yaani mwanangu mimi aende Rwanda? Kisa kazi au kuna lingine? Shida ni pesa? Anataka shingapi? Hiyo pesa nitampa mimi mwenyewe siwezi kuruhusu hilo jambo litokee. Watoto wenyewe ninao wawili tu, hapana kwakweli" mama huyo alipingana na hizo stori ambazo watoto wake walianza kumletea hapo na kuona kama wanamuumiza kichwa tu. Walimdanganya kwamba mwanamke huyo alikuwa anaenda kufanya kazi ya kampuni asijue kwamba wanae wote ni majasusi na huko ilikuwa inaenda kufanywa moja kati ya kazi ngumu isivyokuwa kawaida.
"Shida sio pesa mama, tunahitaji hii kampuni iwe zaidi ya hivi ilivyo leo. Kuna familia kubwa inakuja hapo baadae, watoto wanatakiwa kukuta mazingira rafiki kwao ambayo hayatawafanya waanze kuhangaika. Hizi nafasi ambazo tunazipata tunahitaji kuzitumia ili tupate watu wengi ambao watatusaidia hapo baadae hususani pale tutakapo hitajika kufungua fursa zingine kwenye nchi zingine kubwa. Nakuomba sana mama yangu uniruhusu nikafanye hii kazi" ilikiwa ni sauti ya Tina akiwa anamsisitiza mama yake aweze kumpa hicho kibali cha kwenda kuifanya hiyo kazi.
Mama huyo aliinuka na kwenda chumbani kwake, alitoka na kipande kidogo cha picha ambacho kilikuwa kimechakaa sana kwenye upande wa sura ya mtu ambaye alikuwa kwenye picha hiyo na kuifanya sura ya mtu huyo isionekane.
"Ni miaka zaidi ya ishirini sasa bila yeye kuwepo wala kuwaona nyie. Jambo pekee ambalo nilijiahidi mwenyewe ni kuhakikisha kwamba nawalinda kwa gharama yoyote ile ili hata yeye huko aliko aweze kufurahia wanae wawe na furaha. Sasa vipi tena mwanangu unataka kwenda mbali huko ambako bila shaka sitaweza kukulinda? Kwanini mwanangu?" mama huyo aliongea kwa uchungu sana akiwa analia, alikuwa anawapenda sana hao watoto na hakuwa tayari kuwaona wanapata matatizo ndiyo maana aliogopa sana kumruhusu mwanae huyo aweze kutoka ndani ya mipaka ya Tanzania tena akiwa mwenyewe kabisa.
Wanae pamoja na mkwewe walimkumbatia mama huyo kwa maana hakuwa na namna ya kuweza kuzuia, kisha dada mtu akatoka nje na kaka mtu ili kuweza kuongea kidogo.
"Sis una uhakika na hili?"
"Ndiyo, nina uhakika nalo, ni mwaka umeisha sasa tangu lile tukio liweze kutokea, kwa sasa tunatakiwa rasmi tukamalize kile ambacho tuliamua kukianza"
"Unajua mambo sio marahisi kama unavyo yahisi wewe" Calvinjr yeye mwenyewe alikuwa na wasiwasi sana kumruhusu dada yake kwenda pekeyake ndani ya taifa la Rwanda ila hakuwa na namna ya kufanya kwa sababu kazi ilikuwa inawataka wafanye hivyo. Hii ndiyo siku ambayo dada yake alimwelekeza mdogo wake kwamba hatakiwi kutumia sana hisia kwenye lile eneo ambalo linamtaka atumie zaidi akili, Calvinjr hakuwa na namna zaidi ya kumkubalia dada yake.
"Kitu cha msingi sana unapokuwa kule, zingatia mawasiliano. Hakikisha hauna mawasiliano ya mara kwa mara ambayo yatawafanya wakushtukie kabisa, yaani jifanye kama mtu ambaye hauna lolote unalo lijua kuhusu watu wengine ila kama ikitokea dharura, nadhani unajua namna ya kuwasiliana namimi" mdogo mtu alimsisitiza dada yake huku akiwa anamkumbatia, alijua huko aendako kuna mawili, kurudi au kuishia huko huko na asirudi tena.
Walimuaga mama yao na kuondoka huku Calvinjr akienda kwake na mpenzi wake na dada yake akielekea ndani ya taifa la Rwanda rasmi.
Mwanamke huyo baada ya wanae na mkwewe kuondoka, aliingia kwenye chumba chake ambapo aliingia kwenye ile sehemu yake ya siri na Kujifungia, aliziangalia kwa uchungu sana zile picha ambazo alizisambaza kwenye ukuta wake huku zote zikiwa zimekatwa upande wa kichwani, alikuwa akitoa chozi akiwa anaziangalia picha hizo. Aliingiza mkono kwenye droo moja na kuitoa picha ya mwanaume huyo ambayo ilikuwa kamili kabisa, aliiangalia mpaka chozi likadondokea kwenye picha hiyo.
"Mwanao amekua sasa, mwanao ameniletea mkwe leo. Leo ni moja ya siku za furaha sana kwangu ila pia ni moja ya siku ya uchungu sana kwangu. Natamani kama ungekuwa hapa leo na mimi tumfurahie mtoto wetu, natamani ungesimama kama baba ukayanena yaliyo mema kwa mwanao ila kitu cha kusikitisha ni kwamba hauwezi kuwa hapa kwa sababu huenda hata haujui kama nina damu yako"
"Nawaza siku mwanangu akija kujua ataniona mimi mama wa aina gani, nawaza atanichukuliaje? Nabaki naogopa sana. Ila sitaruhusu jambo lolote limkute mwanangu na sitaruhusu kamwe aje kujua kwamba wewe bado unaishi, huyu anatakiwa kujua kwamba wewe ulikufa miaka mingi sana, nitamlinda mwanangu kwa gharama yoyote na atakaye onyesha tu kujua hili jambo nipo radhi kumuua. Leo mwanangu wa kike ameondoka na kwenda mbali na mimi, nimechanganyikiwa hata sijui nifanye nini ila sitaruhusu na mwanangu wa kiume aende mbali, huyu ni wa kwangu mimi baba Calvinjr, sitaruhusu mtu yeyote amguse mwanangu" mwanamke huyo aliongea kwa sauti ya juu sana huku akiwa anaipiga piga hiyo picha ambayo haikueleweka ina uhusiano gani na hao watoto wake hasa mwanae wa kiume kwa maana alikuwa na uchungu sana anapokuwa anaiona picha hiyo.
Aliichukua simu yake nyeusi ambayo ilikuwa ndani ya droo hiyo na simu hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kuwasiliana na mtu mmoja tu, aliipiga ikapokelewa kwa haraka sana.
"Mwanangu wa kike anaenda Rwanda ,nahitaji alindwe na asije akapatwa na jambo lolote lile"
"Mama sidhani kama huo utakuwa ni uamuzi wenye busara" sauti nzito ila yenye heshima ilisikika upande wa pili ikiongea kwa utulivu.
"Miss anaishi maisha ya kawaida ambayo yanamfanya asiwe na maadui wala kushtukiwa na mtu yeyote yule, ila tukisema kwa sasa aanze kulindwa basi italeta mashaka sana na ataonekana kule ana agenda zake hivyo tunaweza kumuwekea hatari zaidi kuliko faida ambazo zitakuwepo. Kule ni nchi ya watu, akiingia kule serikali ya Rwanda inahusika kumlinda kwa asilimia miamoja kwani wanajua mtanzania akipata tatizo basi inaweza kupelekea mahusiano baina ya hizi nchi mbili kuvunjika" mwanaume huyo alitoa maelezo, wakati mama huyo akiwa anayafuta machozi yake.
"Unajua nitakacho kufanya kama mwanangu akipata tatizo lolote?"
"Ndiyo mama najua" aliikata simu na kutoka humo ndani, alifika mpaka nje ambapo alikutana na wanaume wawili waliokuwa kwenye suti, waliinamisha vichwa vyao baada ya mama huyo kufika, akaingia kwenye gari na kutoka na watu hao ambao bila shaka walionekana kuwa walinzi wake ambao hata wanae hawakuwa wakiwajua kabisa.
Unahisi kuna jambo gani haswa ambalo mama huyu analijua na hataki walimwengu walifahamu?
Episode ya 37 inafika mwisho.
Febiani Babuya.
Sent from my SM-A107F using
JamiiForums mobile app