Simulizi ya kweli: Niliishi kuzimu siku saba

Simulizi ya kweli: Niliishi kuzimu siku saba

SEHEMU YA 56



Harakaharaka nikafungua mlango nikiwa ni kama siamini nilichokisikia, nikamkuta Shenaiza akihangaika kujigeuza, jambo ambalo hakuwa amelifanya kwa kipndi kirefu tangu akiwa kule hospitalini.
“Shenaiza! Shenaiza,” nilisema huku nikipiga magoti pembeni ya kitanda chake. Bado hakuwa amefumbua macho yake.
SASA ENDELEA...
Hata hivyo, japokuwa hakuwa amefumbua macho, niliona akiyapepesa kama anayetaka kuyafumbua, nikainua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu. Kumbukumbu za yote yaliyotokea kuanzia siku ya kwanza msichana huyo aliponipigia simu mpaka muda huo zilipita kwa kasi ndani ya kichwa changu.
Kila kitu kilikuwa kikitokea kwa kasi kubwa ambayo ungeweza kudhani ni ndoto ya kusisimua na muda si mrefu nitazinduka. Kwa kuwa Junaitha aliniambia nikamsubiri chumbani kwake, sikukaa muda mrefu ndani ya chumba hicho cha Shenaiza kwa sababu nilijua hawezi kufurahi akinikuta nikifanya tofauti na maagizo aliyonipa, nikambusu Shenaiza kwenye paji la uso kisha nikatoka na kuelekea chumbani kwa Junaitha.
Maisha aliyokuwa akiishi mwanamke huyu yalikuwa na tofauti kubwa kati ya nje na ndani. Wakati kwa nje ungeweza kudhani Junaitha ni mwanamke ‘mayai’ anayependa sterehe na anasa, ndani ya nafsi yake alikuwa mtu mwingine kabisa. Nikaingia ndani ya chumba chake kilichojaa vitu vingi vya kisasa, tena vyote vya thamani kubwa na kwenda kukaa kwenye sofa dogo lililokuwa pembeni ya kitanda.
Japokuwa kimwili nilikuwa hapo lakini kiakili nilikuwa mbali sana. Nilianza kujiuliza kwamba yale yote yaliyokuwa yananitokea, yalikuwa na maana gani hasa? Nilifikia hatua hiyo baada ya kuona ni kama naishi kwenye ‘script’ fulani ambayo tayari maisha yangu yameshapangwa kwamba ni lazima nipitie hatua moja hadi nyingine kuelekea nisikokujua.
Hata mtu mwingine yeyote angeweza kufikiria hivyo kwa sababu kabla ya mfululizo wa mambo yote hayo, nilikuwa nikiishi maisha ya kawaida kabisa, nikifanya kazi kwa bidii nikiwa na ndoto nyingi maishani. Nilikuwa nikiishi kama kijana wa kisasa anavyotakiwa kuishi lakini kila kitu kilibadilika baada ya kukutana na Shenaiza.
Yaani ni kama nilikuwa nimelala na asubuhi kulipopambazuka kila kitu maishani mwangu kilikuwa kimebadilika. Nilimfikiria Raya na jinsi tulivyokuwa tukiishi naye kabla mambo hayajaanza kwenda mrama, nikamfikiria Shamila nilivyokutana naye nikiwa hospitalini na jinsi alivyotokea kunipenda na yote yaliyotokea mpaka muda huo ambao sasa nilikuwa kwenye himaya ya Junaitha, mwanamke ambaye hata sijui nimuelezee vipi.
Nilizinduka kutoka kwenye lindi la mawazo baada ya kusikia mlango ukifunguliwa, Junaitha akaingia huku akionesha kuchoka sana, nikamuona akiufunga mlango kwa funguo kisha akanisogelea pale nilipokuwa nimekaa.
“Nimechoka sana mume wangu,” alisema na kunibusu mdomoni, nikabaki nimeduwaa. Niliduwaa kwanza kwa kitendo chake cha kuniita ‘mume wangu’ kwa sababu kiumri alikuwa sawa na mama yangu mdogo au shangazi yangu lakini pia alinibusu mdomoni, miongoni mwa mambo ambayo yalikuwa yakiufanya mwili wake uwe kama umepigwa na shoti ya umeme.
“Yaani wewe pamoja na yote haya tuliyoyafanya pamoja bado tu hunizoei?” alisema baada ya kugundua kwamba nilikuwa nimepigwa na butwaa, nikajichekesha na kuvunga. Kiukweli baada ya kuuona upande wa pili wa Junaitha, nilikuwa hata sielewi mwanamke huyo ni mtu wa aina gani.
Kuna wakati hata nilikuwa nahisi kwamba hata kitendo cha mimi kujikuta nikifanya mapenzi na mwanamke huyo kilikuwa cha hatari sana kwa sababu kumbe alikuwa na uwezo mkubwa mno wa nguvu zisizoonekana kwa macho.
Kumbukumbu za tukio lililotokea muda mfupi uliopita la kumkamata yule mwanamke kichawi na kufanikiwa kumleta mle ndani, huku pia tukifanikiwa kulikimbia joka kubwa la kutisha katika ule ulimwengu wa giza, ziliufanya moyo wangu uwe na hofu kubwa mno.
“Leo umenifurahisha sana kwa sababu tumefanya kazi mbili kubwa ambazo zinatumia nguvu kubwa lakini katika zote, wewe ndiyo umekuwa kama steringi, si unaona wenzako hakuna aliyezinduka hata mmoja wakati hakuna kazi yoyote ya maana waliyoifanya?” alisema Junaitha huku akifungua vifungo vya blauzi yake na kuanza kuivua.
Wala hakuwa na wasiwasi wowote au hakuhisi aibu yoyote licha ya mimi kuwepo pale, akaivua na kuitupia kwenye kapu la nguo chafu, akabaki kifua wazi.
“Mbona unaniangalia hivyo wakati mimi nakusemesha mambo ya maana,” alisema huku akiachia tabasamu baada ya kugundua kuwa akili na mwili wangu havikuwa kwenye ushirikiano mzuri.
“Unajua mimi nina dharau sana kwa wanaume lakini sijui kwa sababu gani wewe nimetokea kukuamini na kukupenda ndani ya muda mfupi namna hii,” alisema huku akianza kuvua za chini, akatoa zote akiwa hana hata chembe ya wasiwasi, eti mimi ndiyo nikawa na kazi ya kukwepesha macho yangu kwa aibu mpaka alipochukua upande wa khanga na kujifunga.
“Hizi nguo ukishaenda nazo kule kwenye ulimwengu mwingine hutakiwi kuzivaa tena mpaka zifuliwe kwa maji yenye udi, mdalasini na karafuu, hebu acha ushamba wako,” alisema huku akinipiga kimasihara begani, akanishika mkono na kunisimamisha, akaanza kufungua vifungo vya shati langu.
“Si unaona unaelekea kupona, hebu sogea hapa ujiangalie,” alisema huku akilitazama vizuri jeraha langu la kifuani, nikasogea kwenye kioo na kujitazama. Ni kweli nilikuwa nimeanza kupona haraka kuliko hata nilivyotegemea.
Jeraha ambalo nilikaa kwa muda mrefu hospitalini lakini likawa bado hata haliponi, leo ndani ya saa chache tu lilikuwa likielekea kupona! Ilikuwa ni zaidi ya maajabu kwangu.
“Na pale mguuni alipokujeruhi yule mshenzi panaendeleaje?” alisema, nikataka nipandishe suruali juu ili nimuoneshe lakini badala yake, alinipa taulo na kuniambia nivue tu suruali kwa sababu kuna dawa nyingine alikuwa anataka tuitumie ili kutoa nuksi zote tulizotoka nazo kule kwenye ulimwengu wa giza.
Kwa jinsi Junaitha alivyokuwa anajua kunibembeleza kama mtoto mdogo, nilijikuta nikiishiwa na ile hofu iliyokuwa ndani ya moyo wangu, nikawa nafanya kila kitu alichonigiza. Muda mfupi baadaye, nilibaki na taulo tu, na yeye alibaki na upande wa khanga.
Akatembea kimikogo huku mwili wake uliojengeka vizuri kikekike ukitingishika kwa namna ya kuvutia sana, akaenda kufungua droo iliyokuwa pembeni ya kitanda, akatoa vichupa viwili vilivyokuwa na vitu kama mafuta, akanisogelea.
“Hii dawa inabidi ukaogee na hii ntakupaka tena kwenye kidonda chako, sawa baba’angu,” alisema huku akiwa amenisogelea sana, tukajikuta tumekumbatiana tena, tukagusanisha ndimi zetu.
“Nataka suala la yote tunayofanya mimi na wewe liwe siri yetu, umenielewa mume wangu,” alirudia tena kutamka neno lile, safari hii kwa sauti iliyokuwa inasikika kwa mbali kama mtu anayejilazimisha kuzungumza, nikaitikia kwa kutingisha kichwa, akanishika mkono na kunipeleka kwenye bafu la ndani ambapo alinielekeza namna ya kuogea ile dawa.
Cha ajabu, japokuwa yale mafuta hayakuwa na rangi, nilipoyajaribu kunawia mikono tu kama alivyonielekeza mwenyewe, nilishangaa mwili wangu ukitoa uchafu mwingi mweusi kama maji yaliyochanganywa na mkaa, nikawa nashangaa kwa hofu.
“Ule ulimwengu mwingine una mambo mengi machafu sana, usipojisafisha kwa hii dawa vizuri mwili mzima, unaweza kujikuta unabadilika na kuwa kiumbe wa ajabu sana,” alisema na kunifanya nishtuke sana.
“Oga fastafasta nakusubiri,” alisema huku akitoka na kuniacha bafuni, nikafanya kama alivyoniambia ambapo nilijipaka ile dawa mwili mzima na kusogea kwenye bomba la mvua, nikafungulia maji ambayo uchafu mwingi ulikuwa ukitiririka kutoka mwilini mwangu. Nilikaa kwenye maji kwa zaidi ya dakika tatu ndiyo uchafu wote ukaisha, nikashangaa ule uchovu wote niliokuwa nao umeyeyuka kama barafu juani.
Nikajifuta kwa taulo na kutoka mpaka chumbani ambako nilimkuta Junaitha naye ameshaenda kuoga, nadhani alitumia bafu la chumba kingine maana vyumba vingi ndani ya nyumba hiyo vilikuwa ‘self contained’, akanipokea kwa mabusu motomoto na kunitaka nijilaze kidogo pale kitandani kwake ‘tupunguze uchovu’.
Hata sijui nini kilitokea lakini muda mfupi baadaye, wote tulikuwa kama tulivyoletwa duniani, tukaianza safari tamu kwenye ulimwengu wa huba, ambayo lazima niwe mkweli, iliukonga mno moyo wangu, nikajikuta nimepitiliza na kuuchapa usingizi mzito.
“Jamal! Jamal! Amka, kuna tatizo,” sauti ya Junaitha ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye usingizi fofofo, nikakurupuka nikiwana shauku kubwa ta kutaka kujua kumetokea nini tena.
Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 57



ILIPOISHIA:
“Jamal! Jamal! Amka, kuna tatizo,” sauti ya Junaitha ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye usingizi fofofo, nikakurupuka nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kumetokea nini tena.
SASA ENDELEA...
“Kuna nini tena?”
“Huyu mshenzi anataka kunizidi nguvu, amka ukanisaidie,” alisema Junaitha, huku kijasho chembamba kikimtoka. Harakaharaka nikakurupuka na kuvaa bukta na fulana, nikaongozana na Junaitha ambaye tayari alishatoka na kuanza kukimbilia kule kwenye chumba chake cha siri.
Tulipokaribia nilisikia sauti za kutisha mno, yule mwanamke tuliyemteka akawa ananguruma kama mnyama wa porini huku akikwangua mlango wa chuma kwa kucha zake ngumu, akitaka kutoka.
“Nisikilize! Jamal nisikilize,” alisema Junaitha ambaye alikwama ghafla pale mlangoni.
“Tukifungua mlango atatuzidi, inabidi tuingie kwa kutumia nguvu zetu tukapambane naye hukohuko ndani, amenitia meno, si unaona,” alisema Junaitha huku akinionesha alama ya meno mkononi mwake, huku damu nyeusi zikichuruzika.
Kumbe zile kelele ziliwashtua Raya, Firyaal na Shamila ambao kwa muda mrefu walikuwa wamelala fofofo kutokana na uchovu, nao wakawa wanakuja kwa kujikokota, kila mmoja akionesha kuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wake.
“Msije, nyie ishieni hapohapo,” alisema Junaitha kwa sauti ya juu, wote wakafunga breki na kuanza kututazama.
“Inabidi tupeane migongo na kuunganisha mikono ili tuingie kwa urahisi, haya sogea,” alisema. Bila kupoteza muda nilifanya kama alivyoniambia, tukashikana mikono kwa nguvu, mkono wake wa kulia ukaushika wangu wa kushoto na wangu ukamshika yeye kwa namna ya kubadilishana, kushoto na kulia.
Alinielekeza tufumbe macho, tulipofumbua tayari tulikuwa ndani ya chumba hicho cha siri ambacho sikuwahi kuingia hata siku moja, yule mwanamke akawa anaendelea kusumbua pale mlangoni bila kujua kwamba tayari tulikuwa nyuma yake.
“Kumbe ana kamba nyingine pale shingoni, inabidi ufanye kama tulivyofanya kule porini, kaikate kwa nguvu, usijali hata akikuumiza dawa ipo, ishinde hofu,” alisema Junaitha, nikawa namsogelea kwa kunyata, mara nikakanyaga kitu chini kilichofanya niteleze na akuanguka kama mzigo, puuh!
Kishindo cha kuanguka kwangu kilimshtua yule mwanamke ambaye sasa macho yake yalikuwa yamebadilika na kuwa ya kung’aa kama mnyama mkali wa porini anavyong’aa gizani.
Nilipotupia macho haraka kwenye kitu kilichofanya niteleze, nilishtuka mno baada ya kugundua kuwa ilikuwa ni mifupa ya fuvu la mtoto mdogo.
“Ishinde hofu, kamilisha kazi kwanza mengine baadaye,” alisema Junaitha, nilipogeuka kumtazama yule mwanamke, bado alikuwa amenikazia macho huku akiendelea kunitazama kwa ukali, udenda mwingi ukitoka na meno yake makali yakionekana.
Kwa ujasiri wa hali ya juu nilisimama, yule mwanamke naye akakaa mkao wa kutaka kushambuliana na mimi, tukawa tunatazamana. Kiukweli alikuwa akitisha sana lakini sauti ile ilisikika tena ndani ya moyo wangu kwamba natakiwa kuishinda hofu.
Kwa kasi ya ajabu nilimrukia yule mwanamke, kutokana na uzito wangu nikamzidi nguvu na kudondoka naye mpaka chini, akapiga kelele kwa nguvu zaidi kisha akanikamata mkono wa kushoto na kuning’ata kwa nguvu.
Kwa jinsi meno yake yalivyokuwa makali, nilihisi kama mkono wangu unakatika lakini nikapiga moyo konde na kumkamata shingoni, nikafanikiwa kukamata kamba nyingine ngumu na kuivuta kwa nguvu zangu zote, ikakatika na kumfanya yule mwanamke wa ajabu aishiwe nguvu, akadondoka kama mzigo na macho yake yakabadilika na kurudi kwenye hali ya kawaida.
“Unaniuaaa! Jamal unaniuaaa,” alisema huku akilitaja jina langu, nikashangaa sana amelifahamu vipi jina langu?” kabla sijajibu chochote, Junaitha alimrukia pale chini na kumkaba shingoni, akaanza kumzibua makofikwa hasira.
“Safari hii ukirudia tena nakuchinja kwa mikono yangu,” alisema Junaitha, tukasaidiana kumfunga tena kamba na safari hii, tulimfunga mikono kwa nyuma na kuunganisha na miguu, akawa analia kwa uchungu huku akisema tumsamehe kwani na yeye ana familia hivyo hayupo tayari kufa.
“Leo utasema kila kitu, wewe si unajifanya mshenzi,” alisema Junaitha na kabla ya yote, akamtaka kwanza mwanamke huyo amtibu jeraha alilomng’ata mkononi pamoja na lile alilokuwa amenijeruhi mimi kwenye mkono wangu wa kushoto.
Kama ilivyokuwa mwanzo, mwanamke huyo alitoa ulimi wake mrefu uliokuwa na mabakamabaka na kumlamba kwenye lile jereha, mvuke kama moshi ukatoka kisha taratibu likaanza kujifunga.
Na mimi nikasogea ambapo alifanya hivyohivyo lakini cha ajabu, mwanamke huyo alinitazama kwa namna ambayo sikuielewa, ni kama aliyekuwa anataka nitafute upenyo wa kuzungumza naye tukiwa wawili tu.
Kwa muda wote huo bado sikuwa nimepata nafasi ya kukichunguza vizuri kile chumba, ni mpaka jeraha langu lilipoanza kupunguza maumivu ndipo nilipopata akili ya kutaka kutazama vizuri kwanza lile fuvu lililosababisha nijikwae, kuteleza na kuanguka na vitu vingine vilivyokuwa ndani ya chumba hicho.
Cha ajabu, Junaitha aliniwahi na kuniziba macho, nikamsikia akitamka maneno fulani kisha kufumba na kufumbua, tukajikuta tumetoka nje ya chumba hicho kimazingara, tukaangukia palepale tulipokuwa tumekaa awali tukijadiliana namna ya kuingia.
“Vipi mbona sielewi?”
“Usiwe na haraka Jamal, naomba uniamini kwanza hayo mengine yote utayajua, tumalize kwanza kazi yetu,” alisema Junaitha kwa sauti ya chini, akiwa ni kama hataki akina Raya, Shamila na Firyaal ambao bado walikuwa wamesimama palepale, wasikie.
“Lakini...”
“Lakini nini Jamal? Unanipenda hunipendi?”
“Nakupenda.”
“Basi naomba unisikilize ninachokwambia,” alisema kwa sauti ya kunong’ona, nikawa sina ujanja. Nilimsikia yule mwanamke kule ndani ya chumba cha siri akiangua kicheko kwa sauti ya juu. Sikuelewa kwa nini amecheka kiasi hicho, nikabaki na viulizo vingi ndani ya kichwa changu.
Baada ya kukubaliana na Junaitha, niligeuka na kuanza kurudi kule sebuleni, akina Raya, Shamila na Firyaal wakatukimbilia kwa pamoja na kunikumbatia mimi na Junaitha.
“Mpo salama jamani?”
“Tupo salama wala msijali, niliwaambia hii kazi ni nzito sana, vipi yaani nyie ndiyo mnaamka saa hizi?” alisema Junaitha, nikawaona kila mmoja akikosa cha kujibu.
“Sasa muacheni Jamal akapumzike, nyie njooni huku kuna dawa niwape maana inatakiwa mrudiwe na nguvu zenu, bado kuna kazi kubwa, si mnaona purukushani iliyopo?”
“Yule kule aliyekuwa ananguruma kama mnyama ni nani?” Firyaal aliuliza swali, nikawaona wenzake wote wakitingisha vichwa, kuunga mkono swali hilo.
“Ni stori ndefu kidogo, ngoja nitawaeleza lakini njooni kwanza huku niwape dawa,” alisema.
Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 58



ILIPOISHIA:
“Yule kule aliyekuwa ananguruma kama mnyama ni nani?” Firyaal aliuliza swali, nikawaona wenzake wote wakitingisha vichwa, kuunga mkono swali hilo.
“Ni stori ndefu kidogo, ngoja nitawaeleza lakini njooni kwanza huku niwape dawa,” alisema.
SASA ENDELEA...
Wote wakamfuata mpaka kule kwenye kile chumba walichokuwa wamelala, akawaamuru wote wakae kwenye mkao wa kutengeneza duara, akatoka na kuelekea chumbani kwake, aliporudi muda mfupi baadaye, alikuwa na kichupa kidogo kilichokuwa na mafuta yaliyokuwa yananukia vizuri sana, akaanza kumpaka mafuta yale kichwani na usoni mmoja baada ya mwingine.
“Itabidi mkae dakika ishirini kisha mkaoge, baada ya hapo tutakamilisha kazi ya kumzindua Shenaiza, tumeelewana?”
“Mi nasikia njaa inaniuma sana.”
“Hatutakiwi kula chchote mpaka tukamilishe kwanza kazi hii, ukishakula tu utasababisha nguvu kubwa ambazo zinatakiwa kutumika kichwani mwako, zielekezwe tumboni kwa ajili ya mmeng’enyo wa chakula, jambo linaloweza kusababisha tukakwama, tumeshakula mbuzi mzima, hatuwezi kushindwa kumalizia mkia,” alisema Junaitha akimjibu Firyaal.
Wote walionesha kuelewa walichoambiwa na kwa sababu shauku ya kila mmoja ilikuwa ni kumuona Shenaiza akisimama tena, walikubaliana naye. Ilibidi mimi niwaache wakiendelea kusubiri hizo dakika ishirini ziishe, nikaenda kwenye chumba changu ambacho tangu niingie ndani ya nyumba hiyo nilikitumia kwa muda mfupi sana.
Kwa jinsi nilivyokuwa nikijisikia uchovu, nilipoingia tu, nilienda kujibwaga kitandani, nikawa najisikia jinsi mwili ulivyokuwa ukivuta kwa uchovu. Nilitulia nikitafakari mambo mengi ndani ya kichwa changu. Sikujua mwisho wa yote yale ungekuwa nini, nilishachoka kutangatanga, nilitamani haya mambo yafike mwisho ili nirudie maisha yangu ya kawaida kama zamani.
“Vipi umelala?”
“Hapana, nimejipumzisha tu,” alisema Junaitha huku akifungua mlango na kuingia ndani ya kile chumba. Nilijihisi kukosa amani kwa sababu nilijua kwa vyovyote, lazima akina Raya watamuona Junaitha akitoka chumbani kwangu na kuwafanya waanze kutuhisi vibaya.
Ni kweli alikuwa amenilambisha asali ambayo sikuwa tayari kuiacha lakini suala la tofauti ya umri kati yetu, lilinifanya niwe na aibu sana kuwa naye. Nilitaka kila kitu kati yetu kiendelee kuwa siri kwa sababu niliamini umebaki muda mfupi kabla ya kukamilisha mambo yote yaliyokuwa yametuelemea kisha kila mtu akaendelee na maisha yake.
Niliamini nitakuwa huru zaidi nikiwa kwangu ambapo kichwani nilishapanga kwamba mambo yakitulia tu, naenda kutafuta chumba sehemu nyingine na kuhama kabisa eneo lile.
“Najua umebaki na maswali mengi kuhusu kile ulichokiona kule ndani lakini halikuwa lengo langu kukuficha ndiyo maana nimekuja ili tuzungumze.”
“Ok sawa Junaitha lakini sidhani kama huu ni muda muafaka wa sisi kuzungumza, watatushtukia.”
“Usijali, nimewapa dawa maalum ya usingizi, hakuna atakayeamka sasa hivi, inabidi walale ili tupate nafasi nzuri ya kukamilisha hiki tulichokianza,” alisema Junaitha huku akinisogelea pale kitandani nilipokuwa nimelala, akanibusu kwenye paji la uso wangu na kunifanya nisisimke kiasi. Sikusisimka sana kama kawaida yangu kwa sababu ya uchovu na maswali mengi yaliyokuwa yakitembea ndani ya kichwa changu.
“Niulize chochote unachotaka kujua,” alisema huku naye akijilaza pembeni yangu, akawa anatazama juu kama mimi nilivyokuwa nimelala.
“Ndani ya kile chumba kuna nini?”
“Kuna vitu vingi vinavyohusu mambo ya kichawi.”
“Kwani wewe ni mchawi?” nilimuuliza swali ambalo lilimfanya ashushe pumzi ndefu, akajigeuza na kuwa ananitazama.
“Sisi sote ni wachawi ingawa tunatofautiana kiwango cha uchawi.
“Sikuelewi, una maanisha nini?”
“Sikupenda kukwambia hili lakini ngoja tu nikwambie, mimi hapa ninapoishi, ndipo alipokuwa anaishi marehemu baba yangu na mama yangu. Ndani ya familia yetu, sisi tulizaliwa watoto wawili tu, mimi na dada yangu aitwaye Munaitha, ambaye ndiyo mama mzazi wa Shamila, rafiki yako,” alisema.
“Hata hivyo, kwa kipindi kirefu kumbe baba yetu alikuwa akijihusisha na mambo ya kichawi bila sisi kujua, mpaka alipokuja kufariki ndiyo tukaja kuambiwa ukweli na marehemu mama yetu ambaye naye alifariki muda mfupi baadaye na kutuacha mimi na dada yangu tu.
“Kwa kuwa mambo ya kichawi lazima apatikane mtu wa kurithi mikoba, mimi ndiyo nilichaguliwa kurithi lakini kwa kipindi hicho, nilikuwa pia tayari nimeshafika mbali kwenye masomo ya utambuzi.”
“Masomo ya utambuzi? Ndiyo yapi?”
“Ni kama uchawi tu lakini wenyewe unafundishwa darasani, unatumika sana kwenye nchi za Magharibi. Utambuzi unakuwa ni kwa lengo la kujifunza kuhusu mwili wako na nguvu tunazozalisha, ziwe ni nzuri au mbaya na huu una nguvu kuliko hata uchawi wenyewe unaoujua.
“Kwa hiyo nikawa na nguvu mara mbili, uchawi wa darasani na uchawi mweusi ambao ndiyo huu wa kutumia matunguli, mafuvu na madawa ya kienyeji. Kile chumba ndiyo ilikuwa ofisi ya baba yangu, tangu aanze kuitumia, hakuna mtu mwingine yeyote aliyewahi kuingia zaidi ya mimi na sasa hivi wewe, wengine huwa wanaingia wakiwa mateka kama tulivyomfanya yule mshenzi.
“Kuna siri nyingi sana ndani ya kile chumba, kimsingi ni kama ikulu inayojitegemea,” alisema Junaitha, akawa ni kama amezidi kunichanganya. Nilianza kutafakari kwa kina kuhusu hicho alichoniambia kuwa ni uchawi wa darasani na uchawi mweusi. Nilitaka kujua mambo mengi kwa wakati mmoja kwa sababu kuna siku nakumbuka alituambia kuwa hata ukitaka kuingia benki na kuchukua fedha kisha ukatoka bila kuonwa, inawezekana.
“Najua una shauku ya kutaka kujua vitu vingi lakini usiwe na wasiwasi, kila kitu utakijua vizuri kabisa ilimradi umeshatua kwenye himaya yangu, kinachotakiwa hapa ni kushirkiana kwanza kulimaliza suala la Shenaiza,” alisema, na mimi nikashusha pumzi ndefu na kumgeukia.
“Muda unazidi kusonga mbele Junaitha na hakuna kinachoeleweka, nahitaji kurudi kwenye maisha yangu ya kawaida kama zamani,” nilimwambia, akaniambia nisiwe na wasiwasi mbona kila kitu kimeshakaribia mwisho!
Aliniambia kwamba tukishamaliza kazi ya kumzindua Shenaiza ambayo ingefanyika muda mfupi baadaye, tutaandaa mpango maalum wa kumkamatisha baba yake Shenaiza kwenye mikono ya dola ili kukomesha biashara hatari aliyokuwa anaifanya.
“Usione kama unapoteza muda, nakuhakikishia baada ya kufanikisha hili suala la kumkamata baba yake Shenaiza, utakuwa maarufu sana wewe, dunia nzima itakujua na kukuheshimu na huo ndiyo utakuwa muda mzuri wa wewe kuishi maisha unayotaka kwa sababu kichwa chako kinazalisha nguvu kubwa sana ambayo ina uwezo hata wa kuhamisha milima,” aliniambia.
Maneno yake yalinipa nguvu sana, akaniambia kwamba aliwalaza usingizi mzito kwa makusudi wale wengine ili tukamalizie kazi ya kumzindua Shenaiza lakini akanipa taarifa ambazo zilinishtua mno. Aliniambia baba yake Shenaiza amejizatiti vilivyo kwa nguvu za nje na ndani na ili tufanikishe azma yetu, ilikuwa ni lazima mtu mmoja kati yetu afe.
“Afe?”
“Ndiyo, lazima afe mtu kwenye kafara.”
Je, nini kitafuatia?
 
Back
Top Bottom