Simulizi ya Mahusiano: Meseji Moja

Simulizi ya Mahusiano: Meseji Moja

kallase

Member
Joined
Mar 18, 2020
Posts
27
Reaction score
43
MESEJI MOJA...........(01)

Imeandikwa Na SALUM KALASE.

MAWASILIANO: 0625000557

SEHEMU YA KWANZA.

Kwa majina naitwa James Daudi ni kijana wa miaka ishirini na tano. Katika umri wangu huu sijawahi kuwa na mpenzi hata mara moja. Kwa lugha nyepesi naweza sema sijawahi kuijua radha ya mwanamke inavyofanana hadi kufikia umri huu.

Sababu hiyo imefanya washikaji zangu wawe wananicheka sana kwa kudai kuwa mimi ni domo zege, yaani sijui kutongoza kitu ambacho si cha kweli hata kidogo kwani kati ya vijana wenye Juhudi ya utongozaji nauhakika hauwezi kunitoa mie.

Kwa haraka haraka mimi huwa naweza kutongoza hata wadada ishirini kwa wiki moja lakini cha ajabu huwa naishia kukataliwa na wadada wote. Ni kama huwa nina gundu hivi ambayo sielewi imetokea wapi kwani nikijitazama najiona kabisa kuwa ni mwanaume niliyekamilika.

Namshukuru Mungu hakuniumba kuwa mfupi, nina urefu ule wa kunifanya niwe mwanaume ninayejiamini, mwili wangu ni wa mazoezi kiasi kwani kila ninapopata muda ni lazima niende gym kufanya mazoezi ili kujiweka sawa.

Rangi yangu si haba naweza kusema ni maji ya kunde na hata sura yangu nayo namshukuru Mungu inatazamika. Najua japo si vizuri kwa mtoto wa kiume kujisifia uzuri wa sura ila mimi ni mzuri bhana!!

Ukiachana na hayo, pia mimi napenda kupendeza, kila ninapotoka huwa najitahidi sana kuvaa vizuri na kupulizia pafyumu nzuri ili ninukie vizuri.

Lakini pamoja na juhudi zote hizo huwa naishia kuangukia pua kila ninapojaribu kuongea na wasichana. Kuna muda huwa nahisi labda nimerogwa maana kama ni kutongoza mimi ni fundi haswa. Natongoza kweli kweli yaani nikimuweka chini mtoto wa watu anisikilize huwa nahakikisha namweleza maneno matamu ambayo nina uhakika hajawahi kuyasikia kwingine kokote kule.

Sio kwamba najisifia lahasha! Ila huo ndio ukweli wenyewe kwani hata washikaji zangu kadhaa wale wanaonichekaga nimeshawahi kuwasaidia kupata mademu kwa kuwafundisha swaga zangu.

Swaga ambazo kwao huwa zinakubali ila kwangu huwa zinabuma sijui hata kwanini.

Nimeshajaribu njia kadhaa za kujaribu kuisafisha nyota yangu kwani kama ni kwa waganga nimeshakwenda kutazama nyota yangu, Na nikapewa dawa za kujisafisha nyota yangu lakini hakuna kilichobadilika.

Nikajaribu kwenda kanisani kufanya maombi, na kama haitoshi nikawa nafunga kabisa kula hata kwa siku tatu mfululizo kumuomba Mungu anisafishe nyota yangu lakini wapi kwani licha ya juhudi zangu zote hizo hakuna kilichobadilika.

Kwangu kila kukicha nilikuwa na kutana na mkatao mpya kila nilipojaribu kutongoza lakini pamoja na yote hayo sikukata tamaa.

Ndani mwangu, yaani moyoni mwangu kuna imani ilikua inaniambia zamu yangu itakuja tu hivyo hapakuwa na haja ya kukata tamaa. Niliamini kama nitakata tamaa ni kama nitakua naukubali uhalisia wa kuwa mie nimechafuliwa nyota yangu hivyo niliendelea kupambania kombe la kutaka kuingia kwenye mahusiano.

"Mambo!!"

Ujumbe wa meseji ulisomeka hivyo kwenye kioo cha simu yangu. Ujumbe ambao niliusoma mida ya saa kumi na mbili za asubuhi baada ya kuwa nimeamka kutoka usingizini.

Kwa haraka haraka niliwaza ujumbe kama huo hawezi kutuma mwanaume mwenzangu.

"Ni demu huyu!!" Niliwaza ila swali kichwani likawa ni nani huyo aliyenitumia ujumbe huo bila kujitambulisha na kwa nilivyoitazama ila meseji ilionekana kuingia usiku sana wa saa nane usiku.

Nikawaza haraka wacha nijifanye kama naitumia pesa namba ile ili kiona jina la usajili wa ile namba nitasoma nani,

"PRISCA PAULO PALESTINA"

Majina matatu ya usajili yalisomeka, na jina moja tu la PRISCA ndilo lililoiteka akili yangu,

"Ni manzi huyu!!" Nilijikuta natamka maneno hayo yaliyoufanya moyo wangu ujawe na furaha kiasi cha kunifanya nijikute naanza kuruka ruka kitandani kwangu kwa shangwe.

"Poa!! vipi mwenzangu mzima wewe?"

Niliijibu meseji ile kisha nikakaa kusubiri jibu langu. Japo ilikuwa ni asubuhi sana bado lakini nilikuwa naomba Prisca awe ameshaamka.

"Mie nipo salama kabisa James za tangu juzi"

Prisca alinijibu, jibu lake ndilo lililonichanganya zaidi, nikawaza "Inamaana Prisca ananifahamu kumbe!" Ila cha ajabu mie sikuwa namkumbuka, nadhani ni kwa sababu ya idadi za wanawake ninaokutana nao kwa siku. Isingekuwa rahisi kumkumbuka kila mdada niliyezungumza nae kwa upande wangu.

"Salama kabisa nimeisubiri sana simu yako ujue best" Nilimjibu Prisca kwa kujiamini japo sikuwa nakumbuka ni kitu gani nilichokuwa nimezungumza nae, sio hilo tu mbaya zaidi hata sura yake sikuwa naikumbuka kwani hata jina nililolitazama kwenye ule muamala lilikuwa jipya kabisa kwangu.

Lakini pamoja na yote hayo sikutaka kuipoteza bahati ya kumpoteza Prisca kwani tangu nimeanza kutongoza huyo ndiye aliyekuwa binti wa kwanza kunitafuta mwenyewe kwa ridhaa yake.

Hivyo kivyovyote vile nilihitaji kupata Prisca, kumpoteza ni kitu ambacho sikutaka kabisa kukisikia kwenye fikra za ubongo wangu.

ITAENDELEA TENA KESHO.

Ili kupata simulizi zangu nyingine nyingi kama hii karibu ujiunge kwenye group langu la WhatsApp kwa kubonyeza link hii hapa chini [emoji116][emoji116][emoji116][emoji116]KAKA MKUBWA STORIES.
20241014_081947.jpg
 
MESEJI MOJA...........(02)

Imeandikwa Na SALUM KALASE

MAWASILIANO: 0625000557

SEHEMU YA PILI.

"Acha kunitania basi James" Prisca alinijibu kwani hakuyaamini maneno yangu ya kuwa nilikuwa naisubiri simu yake.

"Haki tena nakuambia Prisca nimeisubiria sana simu yako nakuambia" Nilimjibu Prisca kwa kujiamini.

"Ila nina swali kwako James"

"Uliza tu hata usijali"

"Umelifahamu vipi jina langu wakati hata sijajitambulisha kwako bado" Prisca aliniuliza swali ambalo kwangu halikunipa shida kulijibu.

"Prisca bhana!!! Acha basi kunichekesha"

"Kwanini tena? Wee nieleze basi"

"Nina uhakika ni wewe tu Prisca kwani tangu juzi tulivyobadilishana mawasiliano hakuna mwanamke mwingine yeyote yule niliyewasiliana nae"

Ilibidi nimdanganye Prisca, japo sikuwa na uhakika wa kile nilichokuwa nakizungumza lakini ilinibidi nikiamini. Nilijua fika kama Prisca angeufahamu uhalisia wa tabia yangu ya kupenda kutongoza tongoza wanawake hovyo basi ningempoteza.

"Ila wanaume nyie ni waongo yani" Prisca alinieleza

"Kwa kusema hivyo unamaanisha kuwa hauniamini au?!" Nilimuuliza

"Hapana hata sio hivyo J"

"Ila kumbe ni nini sasa?"

"Hamna hata hebu tuachane na hayo kwanza" Prisca alinieleza nami nikamjibu meseji yake kwa kuchombeza kidogo

"Okay sawa vipi umeshaamka mrembo wangu"

Ila baada ya kumjibu vile Prisca alitulia kidogo kwa muda kama wa dakika kumi hivi bila kunijibu meseji yangu.

Kidogo nikaanza kupata woga ya kuwa huenda Prisca hakupenda nilivyomuita mpenzi lakini sikuwa na kitu cha kufanya zaidi ya kusubiria meseji yake nione atanijibu vipi,

"Heh!! Ila wee mwanaume mara hii nimeshakuwa na mpenzi wako jamani!!!"

"Hahahahahaha!! Vipi kwani haiwezekani au[emoji24][emoji24]"

"Mmmmmh! Unalia nini sasa"

"Si wewe hapo Piih unataka kuukataa moyo wangu"

"Hapana sio hivyo James"

"Kumbe ni nini sasa Prisca?! Niambie"

"Naona kama unataka kuyapeleka mambo haraka sana" Prisca alinieleza.

Maneno yale ya Prisca yakawa kama yameniamsha hivi, ni kama yalikuwa na ukweli ndani yake kwani kiuhalisia Prisca sikuwa namfahamu kwa chochote kile zaidi ya jina lake tu. Sasa ningewezaje kumtongoza mwanamke ambae sikuwa hata namfahamu kwa sura, niliwaza na kujiona mjinga kiasi.

"Oooh! Samahani kama nimekukosea naomba nikaoge basi nataka kwenda kazini"

"Okay sawa bye!!" Prisca alinijibu

" Ila kabla sijaenda kuoga naomba basi unitumie hata picha zako nimekumic sana ujue" Nilimuomba Prisca.

"Mbona nimeshakutumia tayari WhatsApp tangu jana usiku"

Maneno yale ya Prisca yalinifanya nishtuke kidogo, kutazama mtandao wa kwenye simu yangu nikagundua kuwa nilikuwa nimeuzima na tangu niamke nilikuwa bado sijauwasha hivyo nikafanya hivyo upesi sana.

Jumbe kadhaa zikaingia WhatsApp, nikafungua na kutazama zawadi niliyokuwa nimetumiwa na Prisca.

Lahaula!!! Macho yangu yalitua mbele ya malaika, ndio haujakosea kusoma ni hivyo hivyo kama nilivyoandika macho yangu yalitua mbele ya malaika kwani urembo aliokuwa nao binti yule sikuwahi kuuona kwa binti yeyote yule.

Urembo ule aliokuwa nao Prisca si tu kwamba ulinivutia bali ulizifungua pia akili zangu kwani hapo ndipo nilipogundua ya kuwa sikuwa nimekutana na Prisca hata mara moja kwani ile sura niliyoiona kwenye zile picha nilikuwa sijawahi kukutana nayo hata mara moja.

"Manzi mkali kama huyu ametokea wapi tena?!!" Niliwaza.

Pumzi zangu kwa muda ule zilikuwa zinatoka kwa shida sana, akili na mawazo yangu yote yalikuwa yametekwa na urembo wa Prisca kiasi cha kufanya nijikute nashindwa kupumua vizuri.

"Huyu ni wewe?!!" Nilijikuta namtumia Prisca ujumbe huo kutaka kupata uthibitisho wa kile nilichokuwa nimekishuhudia kama ni cha kweli ama lah!!

"Ndio ni mimi huyo vipi kwani?" Prisca alinijibu.

"Anha Hapana hata, vipi jioni leo naomba tutoke basi" Nilimweleza Prisca.

"Tutoke? Kwenda wapi?" Prisca alinihoji.

"Nahitaji nikutoe out (tamka: Auti) ili tufahamiane zaidi"

"Oooh!! Sawa James muda wa kutoka utaniambia sasa" Prisca alinijibu.

Jibu lake lilinipatia furaha sana, nikajikuta napiga kelele za shangwe mule ndani ya chumba changu. Na kama kuna majirani zangu walinisikia basi najua waliwaza sana ni nini kilichokuwa kimenisibu lakini kwa muda ule sikuwa na muda wa kuwawaza hata kidogo kwani furaha ya moyo wangu ndicho kitu nilichokijari kwa muda ule.

Nilikwenda bafuni na kuoga kisha nikajiandaa na kwenda kazini.

Siku yangu nzima ya siku ile ilikuwa nzuri sana. Furaha niliyokuwa nayo moyoni mwangu haikuelezeka. Nilijikuta nafanya kazi kwa moyo sana siku ile,

Ngoja kwanza sikuwaeleza kuhusu kazi yangu si ndio, basi mimi hapa ni akauntanti kwenye moja ya benki maarufu sana kwenye Halmashauri yetu ya mji wa Kahama.

Kama mnavyojua benki huwa zinafungwa saa kumi na moja tu za jioni basi muda ulivyofika tulitoka kazini mimi na wafanyakazi wenzangu ili kuelekea makwetu.

Nikiwa njiani narudi nyumbani, mkono wangu wa kulia tayari ulikuwa umeshaikamata simu yangu na kumpigia rafiki yangu wa faida Zege kwa ajili ya kumuomba aniazimishe gari lake kwani nililihitaji kulitumia kwa usiku ule.

Zege hakuwa na hiyana akanielekeza ni wapi nielekee kulichukua kwa ajili ya matumizi yangu.

" Mamaa vipi umeshindaje?"

Niliamua kumtumia meseji Prisca kwani sikuwa nimewasiliana nae kabisa tangu niingie kazini.

"Salama kabisa za wewe vipi?"

"Safi tu.... Vipi sasa nikufuate wapi hiyo baadae" Nilimuuliza Prisca.

"Kwani tunatoka saa ngapi J"

"Saa moja hivi au unasemaje?"

"Sawa ni muda mzuri ili niwahi kurudi nyumbani"

"Okay sawa nitakukuta wapi sasa?"

Nilimuuliza tena swali langu Prisca kwa mara ya pili akanielekeza hivyo tukaagana nikaita mtu wa boda na kumwelekeza anipeleke alikokuwa Zege ili nikachukue gari.

Sikutumia muda sana nikawa nimeshalichukua gari na kuondoka nalo kwenda nalo nyumbani nilikokuwa naishi.

Kufika huko nilikwenda na kujiandaa kisha nikabadili nguo na kuvaa nguo nilizoziaminia, waswahili hupenda kusema nilivunja kabati kisha nikapulizia unyunyu kwa mbali ili kunifanya niwe nanukia harufu nzuri.

Baada ya kuwa nimemaliza kujiandaa nilimtafuta Prisca na kumuuliza kama yupo tayari nimfuate, akanikubalia, hivyo nikatoka hadi nje na kupanda ndani ya gari langu na safari moja kwa moja hadi alipokuwa amenielekeza Prisca.

"Nadhani nimefika hapa njoo sasa tuondoke"Nilimtumia meseji Prisca ambae hakukawia kuijibu.

"Sawa nakuja nisubirie kama dakika moja hapo"

Hivyo nikabaki ndani ya gari nikawa namsubiria Prisca atoke.

Kichwani mwangu kwa muda ule nilikuwa nawaza mambo mengi sana. Uoga kwa mbali na wasiwasi kidogo vilinitawala kwani kila kilichokuwa kinaendelea kwa muda ule nilikuwa naona ni kama maigizo ya kwenye sinema.

Mabibi na mabwana ule muda tuliokuwa tunausubiria kwa hamu sana ukawadia. Geti la nyumba ya geti kali likafunguliwa na kisha binti mmoja mrembo akatoka ndani ya nyumba ile.

Kwa dakika chache nilihisi kama muda umesimama kwani kila hatua aliyokuwa anaipiga Prisca kuja pale nilipokuwa nimelipaki gari langu ndivyo nilivyozidi kuuona urembo wa Prisca.

Prisca hakuwa mfupi sana wala mrefu sana ni alikuwa na urefu wa hapo kati tu. Mwili wake haukuwa mnene sana na wala haukuwa mwembamba kihivyo ni alikuwa hapo kati pia kwani Mungu alijitahidi kumbalansia nyama kiasi kwenye mapaja yake zilizoendana vyema na umbo lake lenye mfano wa namba nane na muda wote aliokuwa akitembea nyama zake za nyuma hazikusita kumtii kwa kutetema na kuwafanya wavimba macho waumie mioyo yao kwa kumtamani.

Sura sasa hata sina haja ya kuielezea tena, labda niseme jambo moja nadhani picha zile alizokuwa amenitumia hazikumtendea haki kwani Prisca alikuwa ni mrembo haswa zaidi hata ya yule wa kwenye zile picha alizokuwa amenitumia.

"Mambo James" Prisca alinisalimia,

"Oooh Mungu wangu nimekwisha!!"

Niliwaza baada ya kuisikia sauti ya Prisca kwani Prisca alikuwa na sauti nzuri sana ndio ile watu husema sauti nyororo.

Sauti ile ilipenya moja kwa moja hadi moyoni mwangu na kunifanya nijikute nakuwa mzito hata kuijibu salamu ile kwa wenge nililokuwa nalo tayari.

Kitendo kile cha kuchelewa kumjibu Prisca kilimfanya anisalimie tena.

"James nakusalimia.... vipi uko poa kweli?" Prisca aliniuliza.

ITAENDELEA TENA KESHO.

Karibu kujiunga kwenye group langu la WhatsApp la stori kwa kubonyeza link hii hapa chini [emoji116][emoji116][emoji116]

 
MESEJI MOJA........(03)

Imeandikwa Na SALUM KALASE

MAWASILIANO: 0625000557

SEHEMU YA TATU.

"Enhe! Niko poa mie" Nilimjibu Prisca kisha nikashuka kutoka ndani ya gari na kuzunguka kuelekea kwenye mlango wa upande wa pili na kuufungua kisha nikamuomba Prisca aingie ndani ya gari, akafanya hivyo.

Nami nikarudi upande wa pili wa gari kisha nikaingia na kuketi kwenye siti yangu ya dereva. Nilivyoketi nikamtazama tena Prisca kwa muda kwa matamanio ya wazi wazi ambayo yalimfanya Prisca aanze kujishtukia,

"Mbona unanitazama hivyo?" Prisca aliniuliza

"Hivi unajua kuwa wewe ni mrembo sana" Nilimweleza Prisca ambae alianza kuona aibu

"Kawaida tuu mbona"

"Hapana hii sio kawaida Prisca acha nikupe maua yako Mungu amejua kukuumba aisee" Niliendelea kumsifia Prisca ambae alikuwa anatabasamu muda wote.

Baada ya muda niliamua kuwasha gari na kuondoka zangu kuelekea sehemu moja ya kuitwa Paris Beach iliyokuwa inapatikana mitaa ya Nyahanga, sehemu tulivu sana kwa ajili ya wapendanao.

Niliamua kumpeleka huko kwani nilihitaji kutafuta sehemu ambayo ingetufanya mimi na Prisca kuzungumza kwa kuelewana zaidi.

"Hivi na wewe ni mzaliwa wa hapa hapa Kahama?" Nilimuuliza Prisca baada ya kuwa tumeshaketi na kuagiza vyakula pamoja na vinywaji.

"Ndio, mii ni mzaliwa wa hapa" Prisca alinijibu

"Weeeh!!! Acha kunitania basi"

"Kweli kabisa nimezaliwa hapa hapa na nimesomea hapa hapa Kahama hadi kidato cha nne"

"Mmmh kama ni kweli hayo uyasemayo basi Kahama imebarikiwa sana"

"Kwanini unasema hivyo?"

" Prisca bhana!!! Ujue sikuwahi kuwaza kama Kahama yetu hii inaweza kuwa na mtoto mzuri kama wewe"

Kusikia vile Prisca akaanza kucheka.

"Ila James una masihala sana" Alinieleza

"Sio hata masihala ujue ni ukweli mtupu naouongea hapa"

Tulizungumza sana pale. Mazungumzo hayakukatika midomoni mwetu, ni kama tulikuwa tunajuana tangu zamani kwani hatukupata shida kuzungumza kabisa na tulijikuta tukizungumza kwa kupokezana, ni mada tu ndizo zilizokuwa zinabadilika kwa muda ule.

"Natamani kwenda sehemu yenye makelele" Prisca alinieleza

"Sehemu yenye makelele kama club (tamka: klabu) hivi ama?" Nilimuuliza.

"Ndio yaani ni kama umeisoma akili yangu vile" Prisca alinieleza.

Kutazama muda tayari ilikuwa imeshafika saa nne za usiku.

"Lakini muda umekwenda sana hautagombezwa nyumbani?" Nilimuuliza

"Hata usijali hakuna wa kunigombeza, baba na mama wote wapo safarini".

Kusikia vile sikuwa na haja ya kuhoji tena zaidi ya kunyanyuka na kumuomba Prisca tuelekee kwenye gari kwa ajili ya safari ya kuelekea club.

Toroka Uje Club ndio safari yetu ilipoishia, club maarufu sana iliyokuwa inapatikana mitaa ya Nyakato. Japo ilikuwa ni mapema bado kwa club nyingi kuwa zimeshachangamka lakini hilo lilikuwa Tofauti kabisa pale Toroka Uje kwani watu wengi walikuwa wameshakusanyika tayari kwa ajili ya kupata burudani.

Tulilipia kiingilio na kuingia ndani ambako tulikuta Mziki mkubwa unapigwa.

"Vipi huwa unatumia pombe?" Prisca aliniuliza kwa sauti ya juu ili nimsikie kwani kelele zilizokuwamo mule ndani nisingeweza kumsikia kama angeongea taratibu.

"Hapana" Nilimjibu kisha nikamuuliza

"Vipi wewe kwani unatumia?"

Prisca hakunijibu zaidi ya kunitazama kwa tabasamu pana usoni mwake na kabla sijasahau muda wote huo tulikuwa tumeshikana mikono hivyo alianza kunivuta hadi kaunta ambako alikwenda na kuagiza bia mbili ambazo alizinywa mfululizo mfano wa mtu aliyekuwa anakunywa maji.

"Hapa nimechangamka sasa" Alisema Prisca kwa furaha, hakujua kama kitendo kile kiliniacha mdomo wazi japo sikutaka kumwonesha mshangao wangu wa waziwazi.

Ila cha ajabu sasa nilijikuta nazidi kumpenda zaidi Prisca. Nadhani nilipenda zaidi ujasiri wake wa yeye kutokuniigizia maisha.

"Twende tukacheze mziki" Prisca alinieleza bila hata kunisikiliza jibu langu kwani tayari alikuwa ameshaanza kunivuta hadi katikati ya umati wa watu waliokuwa wanacheza mziki kisha tukaanza kucheza.

Prisca alicheza sana mbele yangu na aliniruhusu nimshike popote pale nitakapo. Kiukweli Prisca alijua kunidatisha sana, na tulijikuta tukicheza mfululizo kwa muda wa kama nusu saa hivi, naweza kusema nusu saa yangu bora sana kuwahi kutokea kwenye ulimwengu wangu wa mahaba tangu nizaliwe.

"Hapa nipo sawa sasa tuondoke" Prisca alinieleza baada ya kuwa ameshatosheka kucheza.

Sikuwa na ubishi, nikamkubalia ombi lake tukatoka nje ya ile club na kuanza kuondoka kuelekea kwenye gari letu kwa ajili ya kuianza safari ya kurudi nyumbani.

"Asante sana James I never expected to have fun like this ( Asante sana James sikutegemea kufarahia sana hivi kwa siku ya leo)" Prisca alinieleza.

Muda huo tayari tulikuwa tupo ndani ya gari tukielekea nyumbani kwao na Prisca.

"Anything for you my baby (Chochote kwa ajili yako mpenzi)" Nilimjibu Prisca ambae muda wote alionekana kuwa na furaha sana.

"Inaonekana huwa unapenda sana kutoka out?" Nilimuuliza Prisca

"Mimi?!! Nah!! Hata sipendi huwezi kuamini hii ndio mara yangu ya kwanza naenda club" Prisca alinieleza.

"Wee usinitanie basi" Nilishangaa

"Kweli kabisa James ila ni kitu nilichokuwa natamanigi sana kukifanya" Prisca alinieleza.

"Sasa kama ulikuwa unatamani kukifanya kwanini ulikuwa haujawahi kufanya" Nilimuuliza

"Mazingira tu yalikuwa hayaniruhusu, nyumbani huwa tunabanwa sana ni hivi tu wazazi wangu hawapo ndio maana nimeweza kutoka leo tena usiku hivi" Prisca alinieleza.

"Inamaana kwa kusema hivyo, tuseme hii ilikuwa ni bahati yangu sio?"

"Ndio hivyo James" Prisca alinijibu, kisha wote tukajikuta kunacheka kwa furaha.

Tayari tulikuwa tumeshafika kwao na Prisca hivyo nilipaki gari langu pembeni kidogo ya nyumba yao.

"Nadhani tumefika sasa Piih" Nilimweleza Prisca

"Hata mimi naona" Alinijibu kisha wote tukajikuta tupo kimya tunatazamana bila kuzungumza chochote. Ni kama miili yetu ilikuwa bado inahitaji kuwa pamoja japo muda wa kuachana ulikuwa umeshawadia.

"Prisca hivi nikikuomba nikubusu nitakuwa nakosea" Ilibidi nimuulize Prisca kile kilichokuwa akilini mwangu kwa muda ule.

Prisca alinitazama na kutikisa kichwa chake kuashiria kuwa sitakua namkosea hivyo sikutaka kusubiria ishara nyingine zaidi ya kumsogelea alipokuwa Prisca kisha tukaanza kubadilishana mate.

ITAENDELEA TENA KESHO.

Ili kujiunga na Group langu la simulizi la WhatsApp karibu kwa kubonyeza link hii hapo chini [emoji116][emoji116][emoji116]

 
MESEJI MOJA......(04)

Imeandikwa Na SALUM KALASE

MAWASILIANO: 0625000557

SEHEMU YA NNE.

Prisca alishuka kutoka ndani ya gari na kuelekea nyumbani kwao. Mie sikutaka kuondoka kwanza kwani nilitaka kuhakikisha namuona Prisca akiingia ndani kwanza ndio niondoke.

Prisca aligonga geti la nyumbani kwao na baada ya muda kidogo kupita geti lilifunguliwa, Prisca akanipungia mkono kuniaga nami nikamrudishia muago wake kwa kumpungia mkono wangu kisha nikawasha gari na kuondoka zangu.

Hadi hapo moyo wangu ulikuwa umejawa na furaha sana, na safari yangu yote ya kurudi nyumbani kwangu ilikuwa ya shangwe sana kwani nilijiona kama mshindi aliyeshinda vita iliyopiganwa kwa muda mrefu sana.

"Usiku mwema mpenzi wangu" Nilimtumia meseji Prisca kumtakia usiku mwema.

Hiyo ni baada ya mimi kuwa nimeshamaliza kuoga na nilikua tayari kwa ajili ya kulala lakini Prisca hakunijibu meseji yangu nikawaza atakuwa ameshalala hivyo nami nikaamua kulala kwani sikutaka kumsumbua zaidi na usiku ulikuwa umeshakwenda sana.

Asubuhi kama kawaida niliamka mapema na jambo la kwanza ilikuwa ni kuitazama simu yangu kuona kama Prisca alinitafuta, lakini hapakuwa na ujumbe wake wowote hivyo nikaamua kumtumia meseji nyingine

"Za asubuhi mpenzi wangu"

Kisha nikaiweka simu pembeni na kwenda kuoga zangu.

Nilivyorudi niliitazama simu yangu, Prisca hakuwa amenijibu hivyo nikajiandaa na kwenda zangu kazini huku nikiwasiliana na rafiki yangu Zege aliyenielekeza niiache nyumbani gari yake kwani atahitaji kuitumia hapo baadae.

Nilifika kazini naakuanza kazi. Kazi hazikuwa zinaenda kama kawaida kwani akili na mawazo yangu yalikua yametekwa na ukimya wa ghafla wa Prisca ambao sikuuelewa.

Tayari ilikuwa imeshafika saa saba za mchana lakini Prisca hakuwa amenitafuta licha ya juhudi zangu kadhaa za kumtumia meseji kadhaa ambazo zote zilionesha kumfikia muhusika lakini majibu ndicho kitu ambacho hakikunirudia.

"Wacha nimpigie simu" Niliwaza wazo ambalo niliona ni sahihi kwa muda ule.

Hivyo nikaikamata simu yangu na kumpigia Prisca. Simu ikaanza kuita, ikaita na kuita tena hadi ikakatika bila kupokelewa. Sikukata tamaa nikapiga tena lakini hakuna kilichobadilika kwani simu iliita tena hadi ikakatika. Nikasema hapana wacha nijaribu kwa mara ya tatu nikafanya hivyo lakini pia simu haikupokelewa.

"Prisca vipi umekumbwa na nini mbona haushiki simu zangu" Niliamua kumtumia meseji ambayo nayo ilifika lakini haikujibiwa.

Mawazo akilini mwangu yakanitawala ghafla, mawazo juu ya Prisca hasa niliwaza ni nini hasa kilichokuwa kimemsibu hadi akawa anashindwa kunipokelea simu zangu wala kunijibu meseji zangu.

Sikupata jibu hivyo nikawaza nikishatoka tu kazini safari ya kwanza ni kwenda kwao ili nikajue ana tatizo gani hadi ashindwe kukamata simu zangu.

Jioni ilifika kweli japo kwa tabu sana. Nuru yote niliyokuwa nayo usoni mwangu ilipotezwa kabisa na mawazo niliyokuwa nayo juu ya Prisca.

Nilitoka hadi nje na kuita bodaboda ambayo niliielekeza sehemu nayotaka kwenda nikapelekwa.

Nilifika hadi nje ya geti la nyumba yao na Prisca nikasimama. Sikuwa najua pa kuanzia kwani sikuwa naelewa nitakwenda kujieleza vipi pindi wahusika watakapotoka nje kunifungulia geti kama nikiwagongea.

Lakini sikuwa na muda wa kuyawaza yote hayo kwani akili yangu ilimuwaza Prisca tu na nilijihisi kuchanganyikiwa kama nisingeweza kumuona kwa siku ile hivyo nilianza kuzipiga hatua zangu taratibu kulielekea lile geti la nyumba ya kina Prisca.

Nililifikia geti na kuanza kuligonga kwa muda bila kupata majibu na baada ya kama dakika kumi kupita ndipo geti likafunguliwa na mlinzi wa nyumba ile.

"Kaka kwema?" Nilimsalimia

"Kwema kabisa vipi nikusaidie nini?" Yule mlinzi aliniuliza.


"Namuulizia Prisca kama nimemkuta" Nilimweleza yule mlinzi, sikuona haja ya kujizungusha sana kwani nilikuwa kwenye hali ya kusaidiwa ama kutosaidiwa na yule mlinzi na nilimpa machaguo achague mwenyewe cha kunijibu.

"Wahusika wa hapa wote wametoka" Alinijibu yule mlinzi kwa ustaarabu kabisa.

"Wametoka? Watakuwa wameelekea wapi kwani?' Nilimuuliza

"Hata sielewi ila nachojua mimi ni kuwa familia nzima haipo hapa tangu jana usiku" Yule mlinzi alinijibu.

Nikabaki nimesimama nisijue cha kuongea zaidi.

"Kwani namba yake hauna? Ingekuwa vizuri ukamtafuta kwenye simu kama una shida nae sana maana hata mie nipo hapa ila sijui kinachoendelea ndani ya hii familia'' Yule mlinzi aliongeza.

Maneno yake sikuyaelewa sana japo ilibidi nikubaliane nayo nikaaga. Kichwani mwangu nikawa nawaza ni nini kilichokuwa kinaendelea kwenye familia hiyo kiasi cha kufanya hata mlinzi asielewe chochote kile kilichokuwa kinaendelea. Sikupata majibu.

Hivyo nikaamua kujaribu kumpigia tena simu Prisca ambazo ziliita tu bila kupokelewa.

"Sijui nimekosea wapi au umekumbwa na nini mpenzi wangu kiasi cha wewe kuwa kimya hivi ila nitaisubiri simu yako, Mpenzi wako hapa James" Niliamua kumtumia meseji Prisca ambayo ilionesha kumfikia mlengwa.

Tayari nilikua nimeshamkatia tamaa Prisca hivyo Nilimtumia meseji ile kwa lengo la kumueleza kuwa kama atakuwa ananihitaji bado basi alikua huru kunitafuta muda wowote ule.

Moyo wangu ulikuwa unaniuma sana kwa muda ule. Nilijikuta nawaza mambo mengi sana, Zaidi niliwaza huenda Prisca alijutia kitendo cha mimi na yeye kubadilishana mate usiku wa jana yake hivyo alikuwa anataka kukata mawasiliano na mimi. Niliumia sana na kujikuta nakosa hata hamu ya kula hivyo nilielekea hadi nyumbani na moja kwa moja hadi kwenye chumba changu kisha nikajitupia juu ya kitanda changu kwa lengo moja kuu nalo ni kulala ili japo kukiruhusu kichwa changu kipumue kwani kilikua kinaniuma sana.

Usingizi mzito ulinipitia, kuja kushituka ilikuwa tayari imeshafika mida ya saa kumi za alfajiri hivyo niliikamata simu yangu kuona kama kuna chochote kilichokuwa kimebadilika.

Ile kuitazama simu yangu nilikutana na kitu ambacho sikukitegemea. Simu yangu ilionesha ilikuwa imepigiwa zaidi ya mara kumi na mpigaji alikuwa ni Prisca.

Usingizi wote ulinikata kwani sikuamini kilichokuwa kimetokea,

"Ni vipi sikuweza kusikia simu zote hizo na wakati simu ilikuwa na muito wake kabisa" Niliwaza bila kupata majibu.

Nikawaza nijaribu kumpigia muda ule ule lakini kabla sijafanya hivyo nikagundua kuwa kulikuwa na ujumbe nimetumiwa hivyo nikaufungua kuusoma kuona unasemaje,

"Oooh!! James nisamehe sana kwa kutokushika simu zako kabisa ila mwenzako sipo sawa kabisa leo, mama yangu mzazi amefariki"

Nilishituka kuusoma ujumbe ule, kwa haraka haraka nikawaza na kujiona mjinga sana kwani wakati mimi nawaza mambo mengine juu ya Prisca, huenda yeye alikuwa anapambana kuokoa uhai wa mama yake mzazi. Niliumia sana na kujikuta nguvu zangu zote zikiniisha kabisa nisijue cha kufanya kwa muda ule.


ITAENDELEA TENA KESHO.

Ili kujiunga na Group langu la WhatsApp la simulizi karibu kwa kubonyeza link hii hapa chini [emoji116][emoji116][emoji116]

 
MESEJI MOJA..........(05)

Imeandikwa Na SALUM KALASE

MAWASILIANO: 0625000557

SEHEMU YA TANO.

Dakika kama kumi zilipita nikiwa sijui cha kufanya, na cha ajabu zaidi nilijikuta naanza kutokwa na machozi bila kutarajia. Kitu hicho kilinifanya nijishangae kwa kutokuamini kilichokuwa kinanitokea Kwani sikuamini kama ningeweza kulia kisa mtu nisiyemfahamu.

Baada ya muda kupita nilijipa ujasiri kisha nikaamua kumpigia simu Prisca. Simu iliita na haikuchukua muda Prisca akapokea.

"Hey! Lover boy mamboo"

Prisca alinisalimia kwa sauti ya kukwaruza, ni dhahiri kuwa ilionesha kuwa ni sauti ya mtu aliyekuwa ametoka kulia sana na alikua akijikaza mbele yangu asilie kwa kulazimisha uchangamfu.

"Msiba unafanyikia wapi?"

Nilimuuliza Prisca swali bila hata kumuitikia salamu yake.

"Tupo Igunga huku kwa babu yetu na baba ndio msiba unafanyikia huku" Prisca alinijibu

"Okay sawa nakuja huko leo" Nilimweleza Prisca.

"Okay sawa James asante sana" Prisca alinijibu, tayari sauti yake ilikua Inaonesha kama mtu aliyetaka kuanza kulia tena.

"Nikifika Igunga nitakutafuta kwa ajili ya maelekezo zaidi" Nilimwambia Prisca kisha nikakata simu bila kusikia jibu lake kwani sikutaka kukisikia kilio chake ambacho nilijua kingeniumiza zaidi moyo wangu.

Bila kupoteza muda nikachukua begi langu la kusafiria na kuweka nguo kadhaa pamoja na vitu kadhaa nilivyovihitaji kwa ajili ya safari, kisha nikatoka nje na kuanza kutembea kwa lengo la kuelekea stendi kuu ya mabasi yaendayo Dar es Salaam ili nikapande basi moja wapo kwa lengo la kuianza safari ya kuelekea Igunga.

Mida ya saa tatu asubuhi nilishuka kwenye stendi kuu ya Igunga. Baada ya kushuka nilichukua simu na kumpigia Prisca aliyenielekeza sehemu ya kwenda nikafanya hivyo.

Msibani nilikuta watu wengi sana wakiwa wamekusanyika na ibada ilikuwa ikiendelea. Sikutaka kumtafuta Prisca kwa muda ule zaidi niliamua kutafuta sehemu nikaketi na kuanza kumsikiliza mchungaji aliyekuwa anahubiri.

"Kaka samahani unaitwa pale" Jamaa mmoja alinisemesha huku akinielekeza kule ninakoitwa, nikatazama na kumuona jamaa mmoja akinipingia mkono.

Kwa kumtazama sikuweza kumfahamu ila sikuwa na haja ya kuuliza maswali mengi zaidi ya kusimama na kumfuata pale alipokuwa amesimama.

"Habari yako ndugu" Alinisalimia

"Salama kabisa vipi za wewe"

"Safi tu kwa majina naitwa Amosi ni kaka yake na Prisca ameniambia kuhusu ujio wako"

"Oooh sawa nashukuru kukufahamu poleni sana na msiba" Nilimweleza.

"Tumeshapoa kaka, sasa kama unavyoona ratiba inayofuatia hapa ni ya kwenda kumsitiri mama yetu hivyo ntakuomba uje upande kwenye lile gari pale la ndugu wa karibu wakati wa kuelekea mazikoni" Amosi alinieleza, nikamuelewa na tukawa tumekubaliana kisha sote tukakaa kimya na kuendelea kumsikiliza mchungaji.

Baada ya mahubiri watu waliruhusiwa kwenda kuuaga mwili na baada ya kuaga mwili tulikwenda kwenye magari tuliyoelekezwa moja kwa moja tukaianza safari ya kwenda kuzika.

Hatukuchukua muda sana tukawa tumeshamaliza kumzika mama Prisca na safari ya kurudi nyumbani ikaanza. Lakini kwa muda wote huo kuna kitu nilikuwa sijakielewa bado, Prisca nilikuwa sijamuona kabisa kwenye shughuli zote hizo za kuanzia kuuaga mwili hadi kumzika mama yake Prisca hakuonekana kabisa jambo ambalo sikulielewa kabisa.

Muda wote nilitamani kumuuliza Amosi juu ya hilo lakini ni kama nilikuwa najishtukia kufanya hivyo ikabidi nibaki na dukuduku langu moyoni mwangu.

"James!"

Amosi aliniita baada ya kuwa tumeshuka kutoka kwenye gari zile zilizokuwa zimetupeleka mazikoni.

Niligeuka na kumtazama bila kusema chochote.

"Njoo huku, Prisca anakuita" Amosi alinieleza maneno ambayo nilitamani kuyasikia tangu muda mrefu sana. Hivyo niliamua kuongoza njia na kumfuata.

Tulifika kwenye moja ya chumba na kuingia, ndani ya kile chumba tuliwakuta wadada kadhaa kama wanne hivi na Prisca akiwa wa tano ila tofauti na wengine wote waliokuwa wameketi Prisca yeye alikuwa amelala kitandani.

Tuliwasalimia wale wadada ambao walituitikia salamu zetu kisha nikamtazama Prisca pale kitandani na kutabasamu

"Hey Lover boy umefika saa ngapi?" Prisca aliniuliza kwa sauti iliyojaa unyonge ndani yake

"Nina muda sana tangu nimefika, vipi wewe mbona upo hivyo kitandani hapo" Nilimuuliza.

"Najihisi kuumwa yani, mwili hauna nguvu kabisa" Prisca alinijibu

Kusikia vile niliamua kumsogelea pale alipokuwa amelala kisha nikamtazama usoni na kumpatia pole.

"Sio rahisi kumpoteza mama Prisca nakuelewa sana una haki ya kuhuzunika" Nilimweleza

"Asante sana James, una fikiri hata nguvu za kulia ninazo tena? Nimeshalia sana hapa nilipo"

"Umefanya vizuri kuliko ungejikaza na kuendelea kujiumiza bure..... Vipi umeshakunywa hata dawa kweli" Nilimuuliza

"Hapana sijanywa bado" Prisca alinijibu hivyo nikaamua kumuomba mdada mmoja aliyekuwamo mule ndani atusaidie kufata panado na maji kwa ajili ya Prisca ili asije akaanza kuumwa kichwa tena.

"Acha tu dada, wacha nimfatie mie" Amosi Alidakia kisha akatoka zake nje kwa ajili ya kufuata dawa.

"Kaka yako anaonekana ni mstaarabu sana" Nilimwambia Prisca

"Nani? Amosi? Hahaha mjinga huyo umemkuta kwenye siku zake nzuri tu" Prisca alinieleza.

"Acha basi kumpaka kijana wa watu ubaya huko" Nilimbishia Prisca

"Sasa wewe ndio kwanza umekutana nae leo alafu unataka kubishana na mimi ninayeishi nae siku zote".

Tulijikuta tumeanza kubishana pale na kidogo nilimuona Prisca akianza kuchangamka. Muda ulikwenda na Prisca aliamua kuwatambulisha watu kuwa mimi ni rafiki yake tuliyemaliza nae kidato cha nne pamoja, aliyeamini aliamini na ambae hakuamini tulimuacha abaki na jibu lake moyoni mwake.

Nilikaa pale kwa muda wa siku tatu tu kisha nikaomba niondoke kurudi Kahama ili nikaendelee na kazi zangu.

Prisca alihuzunika sana mimi kutaka kuondoka mapema vile lakini hakuwa na njia yoyote ile ya kunizuia kwani nilihitaji kuilinda kazi yangu pia iliyokuwa inaniweka mjini.

"Twende basi ukamuage baba yangu" Prisca alinieleza

"Okay sawa" Sikuwa na haja ya kukataa kwani tayari nilikua nimeshakutana nae mara kadhaa mzee yule.

"Baba.... James amekuja kukuaga anataka kuondoka" Prisca alimweleza baba yake

"Ya kweli haya kijana mbona unataka kutukimbia mapema sana"

"Nahitaji kurudi kazini mzee wangu, nilipewa ruhusa ya siku tatu tu"

"Aanh sawa kwani unafanya kazi kwenye kampuni gani?" Baba Prisca aliniuliza.

"Ni benki mzee wangu.... Benki ya serikali tawi la Kahama"

"Oooh kumbe!!! Basi mwanangu anajua kuchagua wanaume wa kuolewa nao kumbe" Baba Prisca alinieleza huku akiwa anajichekesha.

"Baba!! Unasema nini sasa hicho?" Prisca alimdakia mzee wake

"Nini sasa? Au naongopa kijana wangu?" Baba Prisca alinitazama na kuniuliza swali hilo ambalo nililikosea majibu ya haraka hivyo nikabaki nimeduwaa nisijue cha kuongea.


ITAENDELEA TENA JUMATATU ILA KWA WALE WALIO KWENYE GROUP LANGU KESHO TUNAENDELEA NAYO.

Ili kupata simulizi zangu karibu kujiunga kwenye group langu la WhatsApp kwa kubonyeza link hii hapa chini[emoji116][emoji116][emoji116]

 
Back
Top Bottom