Sintofahamu yazidi kwa anayedaiwa kupigwa Risasi na mwajiri wake Morogoro

Sintofahamu yazidi kwa anayedaiwa kupigwa Risasi na mwajiri wake Morogoro

BARD AI

JF-Expert Member
Joined
Jul 24, 2018
Posts
3,591
Reaction score
8,826
Wakati kijana aliyepigwa risasi mkoani Morogoro, Benjamin Shinda (26) akiwa hospitali kwa matibabu, inadaiwa mtuhumiwa bado yupo uraiani.

Shinda (pichani) alidaiwa kupigwa risasi Januari 12, mwaka huu na mwajiri wake.

Akizungumza na Mwananchi jana, Shinda, mkazi wa Mtibwa mkoani Morogoro, alieleza, “mtuhumiwa hadi sasa hajakamatwa mimi naendelea kutaabika hospitali. Naomba Serikali iingilie kati.”

Hata hivyo, ilipopigwa simu ya mtuhumiwa iliita bila majibu.

Akisimulia tukio hilo, Shinda alieleza aliajiriwa na mtuhumiwa huyo kuwa dereva wa trekta kwa ajili ya shughuli za kilimo katika mashamba ‘vibarua’.

Mara ya kwanza alipokwenda nalo shambani, alieleza ilishindikana kufanya kazi kwa kuwa trekta lilikuwa bovu na alirudi nalo nyumbani kwa ajili ya matengenezo.

Alisema hata baada ya matengenezo halikuweza kufanya kazi na baada ya siku tatu alirudi nalo nyumbani, ili litengenezwe.

Alisema alipofika nyumbani alimkuta mwajiri wake na wageni watatu akiwemo mwanawe na shemeji yake walimfungulia geti na kuliingiza trekta ndani.

Kwa mujibu wa Shinda, mambo yalibadilika baada ya kumweleza mwajiri wake kuhusu tatizo la trekta, alimjibu kwa kudai anamwibia fedha zinazopatikana katika kazi za shambani.

Kijana huyo alisema alijitetea kwa kupiga magoti huku akimweleza mwajiri wake kwamba trekta ndilo linalosumbua.

“Alielekeza bunduki kwenye mguu wangu akasema anataka kuuvunja hadi nitakaposema, akakoki bunduki na kupiga kisha akaielekeza kwenye mguu mwingine, ndipo wale waliokuwepo wakamshika na kurudisha bunduki ndani,” alisema.

Kutokana na damu nyingi iliyokuwa inavuja, alidai mzee huyo alimpa Sh20,000 na kumtaka aende duka la dawa kupata huduma, badala ya hospitali kwa kile alichomweleza watahitaji fomu namba tatu (PF3).

“Nilikubali ili nitoke pale maana sikuona msaada, nilitoka kwa shida hadi getini nikapanda bodaboda nilipofika nyumbani nikawaeleza ndugu zangu uhalisia, wakanipeleka Kituo cha Polisi Mtibwa.

“Wakanipatia PF3 iliyoniwezesha kuja hospitali ya Bwagala, Mvomero kwa ajili ya matibabu na sasa naendelea vizuri,” alisema. Kuhusu kukamatwa kwa mtuhumiwa, alisema alipeleka malalamiko kwa diwani na baada ya kuingilia mtuhumiwa alikamatwa, lakini sasa ameambiwa ameachiwa.

Alipotafutwa kwa simu kuzungumzia hilo, Kaimu Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mvomero, Salim Abdallah alikiri kufahamu tukio hilo na kusema,“hapa kwangu hakuna mtuhumiwa anayehusika na masuala hayo ndiyo maana nikakwambia hakuna.”

Hata hivyo, alisema si mamlaka yake kuzungumza zaidi hilo, akieleza atafutwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mukama ambaye pia alijibu hafahamu kwa kuwa bado hajaingia ofisini tangu alipohamishiwa mkoani humo kutoka Songwe.

“Kesho (leo) tukutane ofisini naweza kuwa na chochote, lakini leo (jana) sijui chochoteniko safarini,” alisema.

Hata hivyo, diwani wa Mtibwa, Majaliwa Kayanda alisema anachofahamu mtuhumiwa amekamatwa na taratibu nyingine za kisheria zinaendelea.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom