Sio kwamba sitaki kukuoa Pamela, embu niambie nitakuoaje?

Sio kwamba sitaki kukuoa Pamela, embu niambie nitakuoaje?

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
28,297
Reaction score
68,017
SIO KWAMBA SITAKI KUKUOA PAMELA, EMBU NIAMBIE NITAKUOAJE?

Anaandika, Robert Heriel.

Miaka imepita, unasema uhusiano wetu umegeuka Uchumba sugu, umechoshwa na danadana zangu, za mwaka huu hauishi, mwezi Fulani nitaenda kutoa mahari, umechoka ahadi zangu zisizotimia. Hata Mimi Kwa kweli nimechoka kukuahidi Pamela.
Nnapokuahidi mwaka huu jua ninayodhamira ya kweli,

Lakini wewe hunielewi, unasema ninakupotezea muda wako, mara wasema; ninautumia mwili wako kujistarehesha. Pamela hujui ni kiasi gani ninaumia, moyo wangu unavuja uchungu wa makali ya maneno yako. Unajua ninakupenda lakini tatizo unajifanya hulijui,

Kila mwaka unanitajia orodha ya rafiki zako walioolewa, kisha unahitimisha Kwa wadogo na ndugu zako walioolewa, unasema umebaki pekeako, wewe ndio unachekwa mtaani, tena wazazi wako wamekupigia kelele uachane na Mimi Taikon ambaye wananiona sina mbele Kama matembele, wala sina nyuma Kama sukuma wiki. Zote hizo ni mboga zinazoongeza damu ya kutufanya tuishi Mpenzi wangu, Pamela.

Nakumbuka tulikutana tukiwa Vijana wadogo kabisa. Wewe ulikuwa binti mrembo mwenye ngozi mwororo na Sura nzuri Kama Malkia wa shamu, ulikuwa waona aibu nikizishika Chuchu konzi zako zilizokuwa zimesimama Dede, ulikuwa mrembo Sana Pamela. Umenisahau siku zile sikuwa hata na ndevu lakini ona sasa mpaka kidevu changu kinachoma Kwa visiki Mkuki wa ndevu.
Muda kwenda haupunguzi mapenzi yangu kwako Pamela, kadiri siku zinavyosonga ndivyo ninavyozidi kukupenda, ingawaje nashindwa na Mali sina wee! Ningekuoa Pamela uliyemalaika wangu.

Elimu tulimaliza, matarajio yakiwa kuishi pamoja baada ya kupata kazi. Lakini maisha hugeuka Kama bendera juu ya mlingoti, upepo utakapoelekea bendera hufuata.
Tulitarajia Sisi ndio tuwe upepo twende tutakavyo lakini sivyo Pamela, maisha mara zingine hutuamulia tuwe hata vile tusivyotaka.

Unajijua wewe ni mwanamke mzuri, msomi na Mwanamke wa kisasa. Hayo najivunia kutoka kwako lakini nitavumiliaje kukuona ukiteseka na maisha magumu tena mtesaji nikawa Mimi Kwa kushindwa kukuhudumia.

Embu tazama ngozi yako ilivyo nzuri, nitajilaani nikishindwa kuitunza.

Sio kwamba nakataa au sipendi kukuoa Pamela wangu, embu niambie nitakuoaje? Niambie basi kipenzi changu.

Hiki chumba kidogo kisicho na nafasi ya kutosha hata ya hewa ndipo unataka uishi na Mimi? Nambie Pamela.

Usikione kilivyo kidogo hata Kodi yake ni ndogo tuu, Shilingi za kitanzania 30,000/= Kwa mwezi lakini kinanitoa jasho na mate kulipia. Usishangae kuna wakati ninagongewa mlango na mwenye Nyumba kunidai na wakati mwingine kunitukana matusi ya nguoni, je unataka utukanwe na wewe? Haya niambie nitakuoaje?

Niliulizia huko kwenu mahari sio lelemama, Haipungui milioni moja bila ya pesa hivyo bado sijakuchukua. Huwezi amini Pamela tangu nizaliwe mpaka hivi leo ninamiaka 32 bado sijawahi kushika hiyo milioni moja, kila nikijtahidi kuzikusanya zinaishia laki Saba, na punde matatizo huzuka Kama mzuka na pesa yangu inaisha yote. Embu niambie sasa nitakuoaje ikiwa mahari bila milioni moja sikutoi kwenu nami ndio hivyo tena!

Humu ndani naishi kama kaburini, tena Bora baadhi ya makaburi hutembelewa lakini Mimi ni lile kaburi la Baba Fukara aliyekufa Kwa umasikini, kaburi lake likatelekezwa, tena wala halikuwa na jina, Pamela nimegeuka Kaburi lisilo na Jina.
Hakuna wakunitembelea zaidi yako, ndugu jamaa na marafiki walinikimbia tangu walipogundua Mimi sina msaada kwao zaidi ya kuwa mzigo walioshindwa kuubeba,.
Nilifuga Paka lakini alinikimbia tangu alipogundua kuwa mara nyingi Ninalala na njaa. Fikiria Paka kanikimbia itakuwaje kwako Pamela? Upo tayari kulala njaa hapa kwangu.
Unataka aliyekuumba anilaumu Kwa kumtesa kiumbe wake mzuri Kama wewe. Embu niambie nitakuoaje ikiwa hata kujilisha mwenyewe ni kipengele.

Usinione mzembe kupata ni majaliwa, NG'OMBE amenyimwa Ndevu lakini Mbuzi kapewa, waliimba wanamuziki Pamela.
Najua utasema ninafikra fupi hilo sitakukatalia Kwa sababu masikini siku zote ni lawama.

Unakumbuka nilikuambia usimuonee huruma Masikini? Ndivyo hivyo Pamela, sisemi hayo ili ujionee huruma na ukabwela wangu. Hasha! Bali nasema ili ujipime na kufanya maamuzi kuwa uendelee kusubiri mpaka kabwela atakapo pata pesa za miujiza au uamue kuolewa na mtu mwingine.

Hivi vitu vya ndani waviona, havikutoshi wewe Kama Mwanamke, wapi Jiko la Gesi, wapi Frampeni, wapi kibao na kirungu cha kusukumia Chapati, wapi Feni na joto hili, wapi Luninga na Sabufa achilia mbali Kisimbuzi, wapi Jokofu, ati Pamela wewe mapenzi yamekugeuza kipofu na siku nikikuoa utageuka kipofu aliyeona mwezi.
Utagundua sikuwa nimejiandaa vyakutosha, baada ya kuona tuna kitanda, godoro na kasofa kawatu wawili, labda hizi bakuli mbili, sahani na sufuria.
Vipi hautanuna baada ya ndoa kuondoa upofu wako WA mapenzi?

Pamela jua Taikon anakupenda, lakini hajui atakuoaje wakati wewe hustahili maisha ya dhiki Kama ninayoishi.

Lakini kama utavumilia basi Taikon nitaendelea kuhangaika huku na huko mpaka siku Mola atakapotukumbuka.

Nakupenda Pamela!

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
Kwa sasa Bagamoyo
 
Oooh! Wanawake wanapenda pesa! Sijui blah! Blah! Sasa si utafute pesa kama unawapenda HAO wanawake, Kama huwezi kutafuta pesa temana nao, fanya mambo mengine, sio kulalamika hapa Kama mpuuzi!
Ulifikiri ukiwalalamikia wanawake watakuona huruma, hakuna Duniani na mbinguni ama mahali popote wanapoonea huruma malofa.
MALALAMIKO KWENYE UBORA WAKE

 
MALALAMIKO KWENYE UBORA WAKE


Mimi silalamiki Mkuu.
Najaribu kumuelezea Pamela wangu hali halisi ili aamue kusuka au kunyoa.
 
Mimi silalamiki Mkuu.
Najaribu kumuelezea Pamela wangu hali halisi ili aamue kusuka au kunyoa.
Oooh! Mungu nakuomba unipe Baraka! Mpuuzi wewe! Mungu akupe mara ngapi, kuzaliwa tuu ni baraka inayokutosha, unataka baraka gani Kama sio kumchosha Mungu na kukuona lofa.
Watu wangu wanaangamia Kwa kukosa maarifa!
 
Mimi silalamiki Mkuu.
Najaribu kumuelezea Pamela wangu hali halisi ili aamue kusuka au kunyoa.
Tafuta fedha mkuu, ndio maana sisi ni wanaume tumepewa vichwa viwili, Anza kufikiri kwa kutumia kichwa chenye ubongo ndani, tafuta na uwe tayari to take risks katika utafutaji wako,acha kulia Lia kama spoiled child, pull up your socks na nenda out there and fight ili lengo lake la to marry Pamela lifikiwe, good luck
 
Tafuta fedha mkuu, ndio maana sisi ni wanaume tumepewa vichwa viwili, Anza kufikiri kwa kutumia kichwa chenye ubongo ndani, tafuta na uwe tayari to take risks katika utafutaji wako,acha kulia Lia kama spoiled child, pull up your socks na nenda out there and fight ili lengo lake la to marry Pamela lifikiwe, good luck
Kwani hapo kalalamika si anajibu malalamiko ya Pamela wake, kama Pamela atavumilia maisha aliyoyashindwa paka SAWA!
 
Tafuta fedha mkuu, ndio maana sisi ni wanaume tumepewa vichwa viwili, Anza kufikiri kwa kutumia kichwa chenye ubongo ndani, tafuta na uwe tayari to take risks katika utafutaji wako,acha kulia Lia kama spoiled child, pull up your socks na nenda out there and fight ili lengo lake la to marry Pamela lifikiwe, good luck

😊😊

Kwani sitafuti hizo Pesa.
Natafuta Ila mambo bilabila, ndio namuambia Pamela aamue kusuka au kunyoa
 
Back
Top Bottom