Mafanikio hayataki kelele nyingi. Watu wengi huona matokeo ya mwisho, lakini hawaoni mchakato uliomfikisha mtu hapo. Ukikutana na mtu aliyefika mbali, mara nyingi atakuambia “usikate tamaa,” lakini ukimuuliza amepitia nini mpaka akafika hapo, si rahisi kukueleza kila kitu. Kuna mambo aliyapitia kiroho, kimwili, kiakili na kifedha ambayo huwezi kuyaona kwa macho.
Unaweza kuona mtu leo ana biashara kubwa, kampuni, nyumba au maisha mazuri, lakini hujui alianza na mtaji kiasi gani, alipoteza mara ngapi, alikataliwa mara ngapi au alilazimika kuanza upya mara ngapi. Mwingine alianza biashara ndogo, akapata hasara, akabadilisha mfumo na akaendelea. Mwingine alituma CV nyingi bila kupata kazi mpaka siku moja akapata nafasi iliyobadilisha maisha yake. Mwingine alifeli mara kadhaa lakini hakuruhusu kufeli kuwa mwisho wa safari yake.
Ndiyo maana usisubiri mtu akupe ABC ya mafanikio kana kwamba kuna njia moja inayofanya kazi kwa kila mtu. Kila mtu ana safari yake, changamoto zake na mazingira yake. Unaweza kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa, ukaiga principles zao na ukatumia uzoefu wao kama reference, lakini mwisho wa siku utahitaji kutengeneza njia yako mwenyewe.
Cha muhimu ni kuwa na direction, kufanya juhudi, kuwa na nidhamu, kujifunza kutokana na makosa na kutokata tamaa. Wakati mwingine unaweza kuwa unapiga hatua ndogo sana kiasi kwamba huoni kama kuna kinachoendelea, kumbe unajenga msingi wa kitu kikubwa. Usijilinganishe na mtu unayemuona leo amefika, kwa sababu hujui alianza lini wala alipitia nini.
Na pengine siku moja watu watakuangalia na kusema, “amefanikiwa sana,” bila kujua ni mara ngapi ulitaka kuacha. Hawataona machozi, jasho, makosa, hasara na maamuzi magumu uliyopitia. Wataona matokeo tu. Kwa hiyo kama bado hujafika unapotaka kufika, endelea. Jifunze, rekebisha, anza tena inapobidi, lakini usikate tamaa. Huenda umebakiza hatua chache tu kabla ya kuona kile ulichokuwa unakipigania kwa muda mrefu.