Sitta azuia hoja ya EPA, Richmond
na Peter Nyanje, Dodoma
Tanzania Daima
HATIMA ya hoja kuu mbili zinazoonekana kugusa hisia za watu mbalimbali, ile ya Kashfa ya ubadhirifu wa fedha zilizotengwa katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (Bot) na inayohusu utata katika mkataba wa kuzalisha umeme kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni binafsi ya Richmond Development zinaendelea kubakia kitendawili ndani ya Bunge.
Kitendawili hicho kimetokana na kauli iliyotolewa bungeni jana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta, ambaye alitangaza kusitisha mjadala wa hoja hizo kwa muda kutokana na yeye kuwa nje ya nchi kikazi kwa siku kadhaa wiki ijayo.
Katika tangazo lake hilo la jana, Sitta, alisema alikuwa akitarajia kusafiri Jumatatu ijayo kwenda Marekani kwa mwaliko rasmi wa Baraza la Wawakilishi la nchi hiyo na atarejea nchini Alhamisi ya wiki hiyo hiyo ijayo.
Sikutaka Naibu Spika (Anne Makinda) akurupuke na kuvamia masuala haya nyeti, itabidi yasubiri mpaka pale nitakaporejea
tunayo wiki nzima ya kuyaangalia haya, alisema.
Dalili za kupigwa danadana kwa suala la EPA kwa mfano zimeanza kuonekana mapema bungeni jana, wakati wa kipindi cha maswali na majibu.
Mwelekeo huo ulianza baada ya Spika kuzuia kujibiwa kwa swali la nyongeza la Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohammed (Wawi-CUF) aliyetaka maelezo kutoka kwa Naibu Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo kuhusu kujadiliwa kwa suala la EPA bungeni.
Aliposimama kuuliza swali la nyongeza, Hamad Rashid alisema kuwa Kanuni za Bunge, zinaipa mamlaka taasisi hiyo ambayo ni mhimili wa dola, kujadili jambo lolote linalochunguzwa na taasisi nyingine yoyote nchini ukiacha mahakama.
Hata hivyo, kabla Naibu Waziri hajasimama kujibu, Spika alisimama na akatoa maelezo kuwa, alishatoa maelezo awali kuwa majadiliano na serikali kuhusu suala hilo la EPA yanaendelea na atalitaarifu Bunge hatima ya majadiliano hayo.
Majibu hayo ya Spika yalisababisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) kusimama kwa lengo la kuuliza swali la nyongeza, juhudi ambazo hata hivyo zilizimwa kwa mara nyingine tena na Sitta, aliyemzuia kwa kusema maelezo aliyoyatoa yameizima hoja hiyo kuendelea kuhojiwa.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, mapema wiki hii, Spika aliliambia Bunge kuwa, ndani ya wiki hii angetoa taarifa kuhusu matokeo ya mashauriano kati ya ofisi yake na serikali kuhusiana na suala la kuwasilishwa bungeni kwa ripoti kamili iliyoandaliwa na kampuni ya kimataifa ya ukaguzi wa hesabu ya Ernst & Young kuhusu EPA.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili nje ya Bunge baada ya kipindi cha maswali na majibu, Zitto alisema kuwa lengo lake la kusimama halikuwa kuulizia masuala ya EPA.
Inaonekana mzimu wa EPA umetuvaa, kila kitu wao wanaona kama EPA
mimi sikutaka kuulizia kuhusu EPA, hoja yangu ilikuwa ni kuwa Naibu Waziri hakujibu swali lililoulizwa.
Swali liliuliza kuhusu Debt Conversion Scheme, hizi ni fedha zilizoliwa na wafanyabiashara waliouziwa madeni, hilo ndilo lililoulizwa, lakini waziri alikwepa kulijibu hilo, alisema Zitto.
Katika swali hilo lililoulizwa na Hamad Rashid kwa niaba ya Dk. Willibrod Slaa (Karatu-Chadema), mbunge huyo alitaka kujua ni watu gani walichukua fedha kupitia mpango huo wa kubadilisha madeni.
Aidha, pamoja na kutaka kujua majina ya watu hao, Dk. Slaa alitaka kufahamishwa kiasi cha fedha kilicholipwa na watu hao hadi Desemba mwaka jana, na iwapo hawajalipa, serikali imewachukulia hatua gani?
Katika majibu yake, Mkullo alisema kuwa hakuna mpango kama huo uliotajwa na Dk. Slaa na kuwa, kama serikali ilivyotoa maelezo bungeni Januari 29, mwaka huu, suala hilo (akimaanisha EPA) linashughulikiwa kulingana na maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete, hivyo ni vema wabunge wakasubiri matokeo yake.
Kikao hiki cha Bunge ndicho ambacho kimepangwa kujadili Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza zabuni iliyozaa mkataba kati ya Tanesco na Richmond ambao ulizua utata mkubwa tangu mwanzoni mwa mwaka jana.
Kutokana na hilo, Bunge lililazimika kuunda kamati teule iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Harisson Mwakyembe, ambayo ilipewa kazi ya kubainisha Kampuni ya Richmond ni ya nani na ina uwezo kiasi gani wa kufanya kazi, kutathimini mchakato wa upatikanaji wa zabuni wa kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na kuhakiki uhalali wa mkataba kati ya kampuni hiyo na Tanesco.
Kazi nyingine ya kamati hiyo ambayo ilielezwa wazi kwamba ripoti yake ingewekwa wazi katika kikao cha sasa cha Bunge, ilikuwa ni kubainisha uwezo wa Kampuni ya Richmond wa kutoa huduma ya umeme, kupitia taarifa ya Mamlaka ya Zabuni (PPRA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) na kutolea maoni na kutathimini vitu vingine vyovyote vinavyohusu suala hilo.
Uamuzi wa Bunge kuunda kamati hiyo ulitotokana na pendekezo la Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara, inayoongozwa na Mbunge wa Bumbuli, William Shellukindo (CCM), la kutaka kuundwa kwake kutokana na kuwapo kwa shaka kwenye mkataba huo jambo ambalo alisema lisingepaswa kufumbiwa macho wala kupuuzwa.
Kwa upande wa Kashfa ya EPA, Bunge lilikuwa likitarajia kupatiwa ripoti kamili ya kampuni ya ukaguzi wa mahesabu ya Ernst & Young ambayo iligundua upotevu wa shilingi bilioni 133 katika kipindi cha kati ya mwaka 2005/2006.
Ugunduzi huo ulitokana na uamuzi wa serikali uliotangazwa wakati wa Bunge la Bajeti katikati ya mwaka jana baada ya kutokea kwa hoja nzito za wabunge waliofikia hatua ya kutaka kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza madai ya ubadhirifu ndani ya Benki Kuu.
Wiki iliyopita, wabunge kadhaa walimtaka Spika kuitaka serikali kuwasilisha bungeni ripoti nzima ya Ernst & Young ili kutoa fursa kwa Bunge kuipitia na kuijadili kama walivyoahidiwa na serikali Agosti mwaka jana.
Kugundulika kwa Kashfa ya EPA, kulisababisha Rais Kikwete alazimike kutengua uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa BoT, Daudi Ballali na akatangaza kuanza rasmi kwa uchunguzi kuhusu suala hilo, ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa kwa hatua za kinidhamu kwa wale wote watakaobainika kuhusika katika ubadhirifu huo.