Sitta: Bunge liombewe
2008-06-24 12:20:46
Na Boniface Luhanga, Dodoma
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Samuel Sitta, amewaasa waumini wa dini mbalimbali nchini, kuwaombea wabunge wanaoshambuliwa kutokana na kupigania haki.
Spika Sitta amesema waumini hao wanapaswa kufanya maombi hayo kwa kuwa Bunge kwa wakati huu linapita katika kipindi kigumu.
Alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa kuhitimisha semina ya wiki moja ya Neno la Mungu kama ilivyofundishwa na Mwalimu Christopher Mwakasege.
Mwalimu Mwakasege, alimkaribisha Spika Sitta kutoa salamu kwa washiriki wa semina hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Jamhuri, mjini hapa.
Bila kuwataja majina, Bw. Sitta alisema baadhi ya wabunge wanaopigania haki wanashambuliwa, hivyo maombi ni muhimu.
``Baadhi ya wale wanaosema haki wanashambuliwa, lakini tutashinda,``alisema Spika mbele ya maelfu ya waumini waliokuwa wakisikiliza Neno la Mungu.
Akimnukuu Ayubu wa kwenye Biblia, Spika Sitta alisema: ``Lakini mteteaji wangu yu hai, na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.``
Mbali ya Spika Sitta, pia wabunge kadhaa walihudhuria siku hiyo ya mwisho ya semina hiyo ya Neno la Mungu.
Tangu kuibuliwa kwa sakata la mafisadi wanaotuhumiwa kuchota fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na mkataba wa uzalishaji umeme wa kampuni Richmond, baadhi ya wabunge wamejitokeza kulipigia kelele suala hilo huku wengine wakitaka wahusika wabanwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Katika semina hiyo, Mwalimu Mwakasege aliwafundisha Wakristo mikakati ya kumiliki na kutawala kwa kutumia maombi.
Aidha, katika mafundisho yake juzi, Mwalimu Mwakasege aliwaasa Wakristo kuchunga mno aina ya chakula wanachokula na marafiki wanaokuwa nao.
Alifafanua kuwa, chakula na marafiki wanaweza wakasababisha mahusiano yao na Mungu yaharibike.
Alisema kwa mwombaji, akibadilisha aina ya chakula anachokula, anaweza kushindwa kuomba.
Kwa upande wa viongozi wakiwemo wabunge, Bw. Mwakasege alisema mara nyingi hubadilika kutokana na aina ya chakula wanachokula na aina ya marafiki wanaokuwa nao.
``Mwangalie mbunge katika kipindi cha miaka miwili baada ya kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo, anakuwaje� Kuna vitu amekula kwenye ile nafasi,`` alisema.
Bw. Mwakasege aliongeza vivyo hivyo kwa kiongozi aliyekula rushwa ambapo hubadilika baada ya muda.
``Anapoteza hukumu ya haki� Bila shaka kuna kitu amekula au anashirikiana na baadhi ya watu,`` alisisitiza.
Bw. Mwakasege jana alitinga Bungeni na kutambulishwa na Spika kuwa ni mgeni wake. Alimsifia kwamba alimsikia akitoa mafundisho mazuri alipohudhuria mahubiri yake.