Sokoine na Kolimba, vifo vyao vilimkera Mwalimu kiasi gani?

Sokoine na Kolimba, vifo vyao vilimkera Mwalimu kiasi gani?

Nimefuatilia taarifa ya habari ya saa 2 jioni kwenye TBC 1 wakiwa wanatuonyesha wananchi makatibu wakuu waliowahi kushika wadhifa huo kuanzia mwaka 1977 tokea chama hicho kianzishwe katibu wa kwanza kabisa enzi hizo akiitwa katibu mkuu mtendaje ndugu Pius Msekwa hadi huyu aliejiuzulu bwana Yusufu Makamba!

Kupitia luninga hiyo kutonyesha picha moja hadi nyingine cha ajabu kilichonishangaza kufikia kwenye picha ya marehemu Horace Kolimba waliweka giza lakini picha za makatibu wote walizionyesha!

Je ndio kuwa marehemu Kolimba tokea kifo chake hata historia ya chama hicho hata picha yake hawaitaki tena? kulikoni chama cha mapinduzi kuhusu marehemu Kolimba?
 
Mungu akisamehe hicho chama kwani hakijui kitendalo.Kolimba astarehe kwa amani amini

Kifo chake Kolimba kilikuwa na utata fulani,hatujui kilichotokea,sababu ya kutokuonyesha ni makusudi au bahati mbaya?
 
Hayati Kolimba, alipata kukikosoa chama chake kwa kubainisha kuwa kimekosa dira na mwelekeo, kauli ambayo ilikiweka chama katika wakati mgumu. Kwa wasiokumbuka historia, kwa ufupi Kolimba alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) na Waziri wa Mipango katika serikali ya awamu ya pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi.

Kauli ya Kolimba kuwa chama kimekosa dira na mwelekeo ilisababisha mtafaruku mkali kiasi cha kufanya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) imuite kujieleza na baada ya kujieleza Kolimba alifikwa na mauti.

Swali la kujiuliza msomaji, nini hasa kilitokea pale Dodoma na kusababisha kifo cha Horace Kolimba?
 
Kifo chake Kolimba kilikuwa na utata fulani,hatujui kilichotokea,sababu ya kutokuonyesha ni makusudi au bahati mbaya?

Mkuu kifo cha Kolimba haina utata. Inajulikana kabisa kuwa aliuawa, lakini swali lililopo ni kuwa ni kwanini aliuawa, nani alitoa amri ya kumuua, na ni nani aliyeweka ile simu kwenye microphone. Mabare Marando anaweza kuwa na jibu la swali hili.

Sio siri tena kuwa kuna watu wengi wameuawa na kuna siku maswali yote kuhusiana na mysterious deaths za watanzania wenye nia nzuri na Tanzania, yatakuja kujibiwa na kuna uwezekano kuwa watu ambao wamekuwa mstari wa mbele kuua watanzania in the name of uslama wa taifa watakuja kuwajibika.

Lakini alichosema Kolimba kuwa chama kimepoteza mwelekeo ni kweli kabisa, chama kilipoteza mwelekeo toka wakati ule Kolimba alipotoa kauli ile, kwa hiyo kama ndio tunaona sasa, waliokuwa ndani waliona mapema zaidi. Kuna siku tuliambiwa Mrema ni mjinga, lakini leo inaonekana kuwa yote aliyekuwa anasema Mrema ni kweli, kuna siku Kingunge alisema Slaa ni mwongo, lakini ikaja kuwa proved otherwise.
 
Tunajadili mawazo ya marehemu kwani sisi tulio wazima leo hii hatuna tena mawazo? Akili zetu zimebadilishwa na mifumo ya Computer (Software)? Wewe mtoa mada ungesema CCM wamekwama wapi na nini wanatakiwa wafanye ili kujikwamua

Hapo sasa!
 

Godfrey Dilunga


Raia mwema

HORACE Kolimba ni miongoni mwa viongozi waandamizi nchini ambaye Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alitofautiana naye na baadhi ya wenzake kuhusu masuala ya msingi katika uongozi na mwelekeo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lakini mbali na Mwalimu, Kolimba alitofautiana na chama chake (CCM), angali Katibu Mkuu, akiweka bayana chama hicho kimepoteza dira.
Kwa ujumla, hakuna ubishi kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa akifahamu mifumo yote ya uongozi wa nchi kwa sababu ameshiriki kuibuni n kuiridhia, akiwa kiongozi mkuu.
Bila shaka, alielewa wapi apate taarifa ipi na kuhusu nani au nini. Kubwa zaidi, watoa taarifa katika vyombo nyeti nchini walijitolea kumdokeza kwa kadiri ilivyowezekana wakiamini ndiye mtu wa uhakika asiye na hila kwa nchi yake. Asiye na mikono michafu dhidi ya nchi.

Lakini pia hakuna ubishi Mwalimu huyo huyo, alifahamu tabia na mienendo ya viongozi karibu wote waandamizi nchini. Ikumbukwe, asilimia kubwa ya viongozi ‘aliwalea' baada ya kuwaingiza katika mfumo wa uongozi.


Kwa hiyo, ni sahihi kusema Mwalimu alitambua uhodari na udhaifu wao na alijenga mazingira ya kuingilia majukumu yao kwa kadiri mambo yanavyoanza kwenda kombo katika ofisi alizowakabidhi chini ya kauli mbiu; "cheo ni dhamana."


Na pengine tatizo lililokuwapo ni kwamba wakati mwingine; ‘ndoto' nzuri alizokuwanazo Mwalimu kuhusu Tanzania bora isiyotegemea wahisani kujiendesha na isiyoongozwa na mchanganyiko wa viongozi wezi na waadilifu wanaovumiliana na hata kuwa genge moja dhidi ya umma, hazikusambaa vizuri kwa baadhi ya viongozi wenzake.


Na kwa hiyo basi, pengine alikuwa akihisi wenzake wanavuruga ‘ndoto' yake bila kujua kwamba ndoto hiyo haieleweki kwao au inaeleweka lakini kwao haina ‘mashiko'. Kwamba wakati yeye akiwa ameridhia hata mshahara wake upunguzwe ili kukabili hoja za mgomo wa wanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) bila kulalamika maisha yake yatakuwa magumu (Msasani sio Dodoma kama sasa), wenzake wengi walitamani mshahara mkubwa zaidi.


Na kwa mantiki hiyo kutokana na baadhi ya hatua alizokuwa akichukua kama kiongozi wa nchi na hata baada ya kustaafu, wengi wanaamini ilikuwa vigumu kwa viongozi wengi waandamizi kubishana hadharani na Mwalimu Nyerere.

Ni kama vile uadilifu wa Mwalimu ulikuwa kikwazo au silaha kwa baadhi kumshambulia hadharani, ingawa kwa nadra ilijitokeza wachache kufanya hivyo huku wengine wakiishia kulalamika pembeni (mitaani).
Kati ya ambao miongoni mwao hawakuridhiki na walitumia mbinu nyingine za kumjibu Mwalimu ni pamoja na Horace Kolimba, kama tutakavyoona katika mfululizo wa makala hizi.

Kimsingi, inawezekana viongozi wengi waandamizi waliamini kwamba mbele ya umma, nguvu za Nyerere ni kubwa zaidi hasa kwa kigezo cha uadilifu na kwa hiyo, si rahisi kumpinga katika hali ya kumdhalilisha na ukabaki salama.

Imani hii ya uadilifu wa Nyerere ndiyo bila shaka, iligeuzwa na Watanzania kuwa dhamana kwa Benjamin Mkapa asiyekuwa ‘mwenyeji' kwao, na wakampigia kura za urais 1995.

Urais ambao baadhi ya machapisho yanabainisha kuwa Kolimba naye alikwishaonesha nia mapema zaidi, takriban miezi 10 kabla (mwishoni mwa mwaka 1994).


Lakini hata hivyo, ni dhahiri kuwa nyuma ya nguvu hizi za Mwalimu Nyerere katika jamii aliyoshiriki kusaka uhuru wake dhidi ya watawala wa kigeni, kulikuwa pia na nguvu za dola zilizokuwa na jukumu la kusukuma na kusimamia hoja zake za kitaifa.

Wengi mtakumbuka jinsi Mwalimu alivyotofautiana dhahiri na aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela, achilia mbali Katibu Mkuu wa
CCM (chama tawala), Horace Kolimba.


Na kwa namna ya kipekee, Mwalimu pia alitofautiana kuhusu namna Mzee Ali Hassan Mwinyi alivyokuwa akiongoza nchi katika baadhi ya masuala ya msingi, ingawa wakati mwingine alimtetea kuwa anashauriwa vibaya.


Nini hasa kilitokea?


Kutokana na tofauti hizo na hasa kwa kuangalia viongozi hao watatu, Kolimba, Malecela na Mwinyi, itakumbukwa Mwalimu aliandika kitabu; Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania.


Sijui kwa sababu zipi hasa ambazo pengine Mzee Ali Hassan Mwinyi na Mzee John Malecela wanaweza kuzieleza kwamba hawakutaka kujibishana na Mwalimu Nyerere, tofauti na alivyofanya Horace Kolimba.


Hata hivyo, Kolimba naye hakufanya majibizano na Mwalimu moja kwa moja hadharani, anadaiwa kutumia vyombo vya habari vya Chama cha Mapinduzi (magazeti ya Uhuru na Mzalendo) akiwa Katibu Mkuu, kumjibu Nyerere.


Inaaminika katika hali inayothibitisha nia ya Kolimba kuwania urais mwaka unaofuatia (1995), mwaka 1994 mwanasiasa huyo alijipanga kwanza kujinasua na mashambulizi ya Mwalimu Nyerere kwake na hata kwa wenzake (Mwinyi na Malecela ambao walikaa kimya). Mashambulizi hayo yamo kwenye kitabu cha Nyerere; Uongozi wetu na hatima ya Tanzania.


Maswali zaidi yanajitokeza katika mkakati huo wa Kolimba kama ambavyo pia tutazidi kubaini katika mufululizo wa makala hizi.

Kwa mfano, wakati Kolimba akidaiwa kutumia vyombo vya chama kumjibu Nyerere katika ‘staili' ya kipekee ambayo ilifichuliwa na magazeti mengine nchini, Mzee Mwinyi akiwa Mwenyekiti wa chama, alikaa kimya.

Kupitia magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Kolimba anadaiwa kuwatumia waandishi ambao inadaiwa pia walikuwa wakitumia majina tofauti, kama ilivyopata kufichuliwa na gazeti jingine la binafsi baadaye.


Baadhi ya makala hizo ni zile zilizotolewa katika gazeti la Uhuru la Novemba 8, mwaka 1994 ukurasa wa saba na Novemba 18, mwaka huo huo, pia ukurasa wa saba. Makala hizi inaelezwa ziliandikwa na Kolimba lakini kwa jina la mwandishi aliyejiita Alex Kowe.

Makala hizi (ambazo nitazichambua siku zijazo) ziliandikwa katika wakati ambao kwanza ni mwaka mmoja kuelekea Uchaguzi Mkuu huku Kolimba akidaiwa kutaka kuwania urais.

Lakini pia ni yeye ambaye kuelekea uchaguzi huo huo wa 1995, aliweka bayana chama anachokiongoza kimepoteza dira, ikielezwa angegombea kwa chama kingine.


Na kwa namna ya kipekee katika kile kinachoelezwa ni kujibu mapigo ya Mwalimu Nyerere kwa kitabu chake cha "Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania" Novemba 4, mwaka 1994, Kolimba alijigamba mbele ya waandishi kuwa; hajioni kuwa na kasoro kama Mtendaji Mkuu wa CCM na kwamba uamuzi ni wa wananchi.


Kauli yake kwamba; "uamuzi ni wa wananchi" ilizua maswali mengi kwa baadhi ya watu na hasa waliopata kuhisi au kuelezwa kuwa Kolimba anataka kuwania urais mwaka 1995. Kwamba alitaka awe Amiri Jeshi Mkuu wa tatu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Maswali ni mengi na miongoni mwa hoja zilizoibuka ni kwanza; Kolimba ambaye si kiongozi wa kuchaguliwa (mteule) ni kwa vipi aseme wananchi wawe waamuzi wakati hawakuwahi kumchagua?

Je, alitaka kwenda kujipima kwa wananchi kwa njia ya kupigiwa kura baada ya kuachana na wadhifa wa kuteuliwa? Na je, kupigiwa kura katika nafasi ipi ya uongozi? Je, ni urais?


Swali kubwa zaidi ni; je, kwa kauli hiyo kama Kolimba angekwenda kugombea urais, asingeungwa mkono na Mwalimu Nyerere? Kama jibu ni hapana, je, angeungwa mkono na Mwinyi pamoja na viongozi wengine waliotofautiana na Mwalimu kuhusu uongozi wa nchi na hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995?


Lakini katikati ya kile kinachoelezwa kuwa ni majibu ya Kolimba kwa Nyerere kupitia vyombo vya habari vya chama, wapo waandishi wa habari waliodokezwa kuhusu mipango ya Kolimba na ‘wakachochewa' ili kwenda kumuuliza Mwalimu.

Wamuulize kwanza; kama amesoma mfululizo wa makala kwenye magazeti ya chama ambazo ingawa zimeandikwa na ‘waandishi' (kwa majina mengine si Kolimba) lakini zinamjibu na hata kumshambulia.

Pili, nini majibu yake. Tatu, anadhani Kolimba anapata wapi ‘ujasiri' huo wa kutumia hata vyombo vya chama kwa maslahi yake kisiasa? Yalikuwa maswali ya kumchokoza Mwalimu na hata kupima upeo wake wa busara.


Majibu ya Mwalimu Nyerere ambayo pia yamenukuliwa katika baadhi ya machapisho nchini yanaeleza kwa kifupi lakini katika hali ya upeo mkubwa wa busara, pengine kinyume cha hata matarajio ya wanahabari hao kwamba Mwalimu angehamaki.

Mwalimu Nyerere ananukuliwa kuwajibu waandishi waliomfuata katika hali ya utulivu akitamka maneno sita tu. Akawajibu akisema; mwacheni aendelee, tutajibizana hoja kwa hoja."

Majibu haya ya Mwalimu bila shaka hayakukidhi matarajio ya waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia sakata hilo kwa kina, na hapa bila shaka, Katibu Mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa sasa, Kajubi Mukajanga, anafahamu hili kwa namna fulani, wakati huo akiwa Mhariri wa gazeti la kila wiki la WAKATI ni HUU.


Lakini pia maneno hayo sita tu ya Mwalimu katika suala pana la mgogoro wa kiuongozi, yalithibitisha Mwalimu alikuwa na taarifa za Kolimba kutumia vyombo vya chama kumjibu, kisichojulikana dhahiri ni je, ‘wakubwa' gani walikuwa kambi ya Kolimba dhidi ya Nyerere?


Kwa kuzingatia mazingira hayo, wanahabari walizidi kuhoji kwa mfano; pamoja na kwamba Rais Ali Hassan Mwinyi, ni Mwenyekiti wa CCM na ameelezwa kuhusu ‘matatizo' hayo ya Kolimba kutumia vyombo vya chama kwa kadiri anavyotaka, kwa nini hafanyi lolote?


Maswali hayo na mengine yaliongeza joto na kwa kipekee, ukali wa joto uliongezwa na majibu ya Nyerere; mwacheni tutapambana kwa hoja. Hatimaye, kutokana na joto hilo Mzee Mwinyi akapewa tafsiri kuwa alikuwa akimuunga mkono Kolimba na hasa ikieleweka kuwa naye ni majeruhi katika kitabu cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania.

Kolimba ambaye kama tulivyoona hapo juu, tayari alikuwa na nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995. Inawezekana ukosoaji wa Mwalimu dhidi yake aliutafsiri kama kikwazo na kwamba Mwalimu ameingilia nia yake hiyo (lugha ya siku hizi kumchafua-sio kumkosoa).


Inadaiwa kuwa Kolimba kupitia kwa mwandishi aliyetambulishwa kwa jina la Alex Kowe, aliandika makala katika gazeti la Uhuru, Novemba 8, 1994, takriban miezi 10 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 1995.


Miongoni mwa hoja zake katika makala husika ni malalamiko dhidi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Anamlalamikia Nyerere kwa kile anachokieleza kuwa ni hatua yake ya kumlazimisha Rais Ali Hassan Mwinyi, asipokee ushauri wake (Kolimba).


Ni Nyerere pekee angeweza kufafanua hili ingawa pia inawezekana alimuonya Mwinyi kutopokea ushauri wa Kolimba pengine baada ya kubaini ni aina ya kiongozi asiyeaminika kwa kiwango cha kuridhisha katika baadhi ya masuala ya kiuongozi.


Ni kutokana na maelezo ya Nyerere kwa Mwinyi kwamba ushauri wa Kolimba ni wa shaka, Kolimba mwenyewe anapinga hilo akisema haikuwa sahihi kwa sababu anaamini si wakati wote angekuwa na ushauri mbaya au ushauri wenye nia mbaya kwa Rais Mwinyi.


Ni katika mazingira hayo ya kumuonya Mzee Ali Hassan Mwnyi kutoamini moja kwa moja ushauri wa Kolimba, kuna maelezo pia yanayodai kwamba Nyerere alikuwa akimwona Rais Mwinyi kuwa ni kiongozi aliyezongwa na udhaifu wa kiuongozi.


Udhaifu aliouona Nyerere kwa Mzee Mwinyi unadaiwa ni kuhusu namna ya kuchuja (kupima) ushauri kutoka kwa viongozi wengine wanaomsaidia na hapa, izingatiwe kuwa, ushauri mbovu ni msingi wa uamuzi mbovu.


Kwa hiyo, Kolimba kupitia makala hiyo ambayo inadaiwa kuandikwa naye ingawa ilipewa jina (by-line) la Alex Kowe, anapingana na Nyerere kuhusu hoja ya udhaifu wa Mwinyi kiuongozi. Katika kupinga, Kolimba anadai kwamba udhaifu wa Mwinyi si kushindwa kuchuja (kupima) ushauri bali ni uungwana wake kupita kiasi.


Anasema Mwinyi ni muungwana kupita kiasi. Kwa mujibu wa Kolimba, msingi wa uungwana huo wa Mwinyi uliovuka mipaka ni mwelekeo wake wa kuchelea kumuudhi (kutompinga) Baba wa Taifa na hivyo kumpa mwanya wa kumyumbisha.


Kwa lugha nyingine, wakati Nyerere anaamini Mzee Mwinyi ni dhaifu katika baadhi ya masuala ya kiuongozi na hasa kupima ushauri anaopewa na wasaidizi wake, Kolimba aliamini huo si udhaifu kwa tafsiri halisi ya udhaifu, bali ni uungwana uliopita kiasi ambao Nyerere ‘aliutumia' kumyumbisha Mwinyi kiuongozi.


Kolimba anamgeukia Nyerere akijibu mapigo kutoka kitabu cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania dhidi yao (Kolimba na wenzake Mwinyi, Malecela) akimwelezea (Nyerere) kuwa ni mtu ambaye haambiliki na ni king'ang'anizi.


Katika mashambulizi yake kwa Nyerere ambaye tayari katika makala iliyopita tuliona alifuatwa na waandishi wa habari na wakamuuliza kuhusu mashambulizi dhidi yake kutoka kwa Kolimba naye akawajibu; mwacheni aendelee nitajibishana naye hoja kwa hoja, Kolimba anasema Nyerere akishikilia jambo lake huwa hashauriki kwa urahisi na wala hashawishiki.


Katika sentensi fupi akimwelezea Nyerere, Kolimba kupitia makala anayodaiwa kuiandika na kubandika jina la Alex Kowe, anamtafsiri akisema kwake (Nyerere); "msimamo kwanza na maslahi baadaye."


Kolimba anatetea tafsiri yake hiyo dhidi ya Nyerere (msimamo kwanza na maslahi baadaye) akiorodhesha mambo ambayo anaamini Nyerere aliyasimamia kwa kutanguliza msimamo badala ya maslahi ya nchi na hivyo, hayakuwa na mafanikio mazuri kwa nchi.


Mambo hayo ambayo Kolimba anaamini yalitekelezwa kwa msimamo usioridhia ushauri ni kwanza; Azimio la Arusha. Pili, operesheni vijiji. Tatu, kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyokuwa ikiundwa na nchi tatu- Tanzania, Kenya na Uganda (mwaka 1977).


Nne, mapambano yake (Nyerere) ya muda mrefu dhidi ya sera za Shirika la Fedha duniani (IMF), kwa wakati huo Mwalimu akikerwa mno na masharti ya shirika hilo kwa nchi masikini akifikia hatua kutamka IMF si Wizara ya Fedha ya Dunia.


Kolimba katika makala hiyo anayodaiwa kuiandika yeye, anamkabili Mwalimu akisema mambo hayo manne ni mifano na vielelezo vya misimamo mikali ya kisiasa ya Mwalimu Nyerere, ambayo haikutanguliza mbele maslahi ya taifa na watu wake.


Wiki ijayo tutachambua namna wakati fulani Kolimba alipofurahia ‘kusita' kwa Mzee Mwinyi kukidhi haja za shinikizo la Mwalimu Nyerere, kutaka yeye (Kolimba) na Malecela waondolewe madarakani. Tutaangalia je, Kolimba alichukuliaje uamuzi huo wa Mwinyi ambao hata hivyo, baadaye waliondolewa madarakani.


Kwake yeye Kolimba, kitendo cha Rais Mwinyi kukataa shinikizo la Mwalimu Nyerere kutaka Malecela na yeye waondolewe madarakani (jambo kuchelewa kutekeleza shinikizo hilo) ni kitendo cha ujasiri na wala si kielelezo cha udhaifu kama ambavyo Nyerere angetaka Watanzania waamini.


Kama tulivyoona hapo juu, ni Kolimba ambaye hakuwa tayari kukaa kimya kutojibu mapigo ya Mwalimu Nyerere tofauti na wenzake Mwinyi na Malecela ambao walikaa kimya, ingawa haijulikani walikuwa wakiunga mkono uamuzi huo wa Kolimba au la. Hata hivyo, tuliona Kolimba alijibu mapigo ya Mwalimu japo si kwa kujitokeza moja kwa moja hadharani. Alimjibu akitumia magazeti ya chama (CCM) ya Uhuru na Mzalendo, kwa kuandika makala zilizopewa jina la mwandishi Alex Kowe.


Leo tutaendelea na uchambuzi wa hoja za Kolimba ikiwa ni majibu dhidi ya mapigo ya Mwalimu Nyerere kupitia kitabu cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania. Kama nilivyodokeza wiki iliyopita, yapo maelezo kutoka duru za kiserikali kuwa wakati fulani Rais Mwinyi alisita kuufanyia kazi moja kwa moja ushauri au shinikizo la Mwalimu Nyerere kutaka Kolimba na Melecela waondolewe madarakani.


Uzito huo wa Rais Mwinyi kuwaondoa madarakani Malecela na Kolimba unathibitishwa na maelezo ya Kolimba katika makala zake, akitafsiri kuwa kitendo hicho cha Mzee Mwinyi cha kukataa shinikizo la Mwalimu Nyerere kuwaondoa wao madarakani ni cha ujasiri. Kwa mujibu wa Kolimba, kitendo hicho si kielelezo cha udhaifu kama ambavyo Mwalimu Nyerere angetaka Watanzania waamini.


Katika makala yake ya Novemba 18, mwaka 1994, Kolimba, kupitia kwa mwandishi Alex Kowe, anamshambulia Mwalimu kuhusu hoja ya Serikali tatu, ambayo Mwalimu alipata kuichambua vizuri kwa mwelekeo wa kuainisha kigezo cha udhaifu wa viongozi hao. Kolimba anamshambulia Mwalimu Nyerere akidai kuwa ameshindwa kuona ukweli juu ya hoja ya Tanganyika na Serikali tatu.


Kwa mujibu wa Kolimba ukweli alioshindwa kuuona Mwalimu ni kwamba; "hoja ya serikali tatu ndani ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar imetokana na ubovu wa misingi ambayo Muungano huo umesimikwa na si udhaifu wa viongozi. Mtazamo wa Kolimba ni kwamba kuzidi kuwakosoa viongozi kuwa ni dhaifu kwa sababu ya hoja hiyo ni sawa na "kumwaga damu" za viongozi husika na kwa hiyo, Kolimba anasema kwamba, bila kurekebisha misingi hiyo (ambayo Muungano umesimikwa juu yake) basi, "damu za viongozi zitazidi kumwagika".


Katika makala yake hiyo, Kolimba anarejea kile kilichopata kumkuta aliyekuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Aboud Jumbe. Anasema Aboud Jumbe alikumbwa na maafa mwaka 1984 pale hoja ya Serikali tatu ilipojitokeza. Lakini mbali na Jumbe, Kolimba anasema maafa hayo pia yalimfika aliyekuwa Waziri Kiongozi, Seif Sharrif Hamad, baada ya kuhisiwa kwamba alikuwa mchochezi wa chini chini wa kuitisha kura ya maoni Zanzibar, kuhusu uhalali wa Muungano.


Katika kufikisha ujumbe wake bila kubainika ni yeye aliyeandika makala hizo na kuzipa jina la Alex Kowe, Kolimba anaandika; "Safari hii, Mwalimu ameamua kuwakalia shingoni Malecela na Kolimba. Na inaelekea mzimu wa Tanganyika bado utaendelea kuhitaji damu zaidi."


Lakini anaendelea mbele kujibu mapigo ya Mwalimu Nyerere akihoji na kutafakari ni kwa nini Mwalimu Nyerere huyo huyo, hakumshambulia aliyekuwa Jaji Mkuu, Francis Nyalali, ambaye aliongoza Tume ya Mfumo wa Vyama na kujikuta akichambua masuala ambayo hayakuwa sehemu ya hadidu za rejea kwa tume hiyo, kwa sababu Nyalali naye alipendekeza kuwapo kwa Serikali tatu.


Hapo Kolimba anaandika; "...na sijui kwa nini Mwalimu hakudai kwamba damu ya Jaji Mkuu, Francis Nyalali nayo imwagike kwa kufufua hoja ya Tanganyika bila hata kutumwa na wananchi? Lakini baada ya kujiuliza na kutafakari, Kolimba mwenyewe anabuni majibu ambayo Mwalimu angeweza kuyatoa kuhusu "damu ya Nyalali" kutomwagwa kwa hoja ya Tanganyika. Anaingia katika fikra za Mwalimu na kubahatisha kuwa pengine Mwalimu angejibu kwa kusema "mjumbe hauawi," na kutokana na jibu hilo, Kolimba anaendelea kuhoji; "...lakini Jaji Nyalali katumwa na nani?"


Lakini kwa upande mwingine wakati Kolimba akiingia katika kile kilichopata kuelezwa na gazeti la WAKATI ni Huu kwamba ni malumbano dhidi ya Mwalimu Nyerere, katika wakati ambao Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, Malecela na Mwinyi wakitajwa kukaa kimya, duru za habari serikalini zilikuwa zikitafakari mazingira ya mgawanyiko mkubwa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kilikuwa katika ukingo wa safari kuteua mgombea urais ambaye atakuwa mrithi wa Ali Hassan Mwinyi ambaye mbele ya Mwalimu Nyerere, hakuwa kiongozi imara kiasi cha kutosha.


Na hapa ikumbukwe nafasi ya Mwalimu Nyerere katika mgawanyiko huo ambao ulikwishaanza kuonyesha dalili za wazi ndani ya CCM. Nafasi ya Mwalimu inayopaswa kukumbukwa hapa ni kwamba, ndiye kiongozi ambaye kwa wakati huo alikuwa na ushawishi mkubwa katika mifumo ya kidola na hususan idara nyeti ya usalama wa taifa, ikielezwa kuwa maofisa wengi wa idara hiyo waliamini katika uadilifu wa Mwalimu na uzalendo wake kwa nchi katika kiwango tofauti na Rais aliyekuwa madarakani kwa wakati huo.


Kwa hiyo, nguvu ya Mwalimu mbele ya umma na ndani ya mifumo wa kidola ilikuwa kubwa mno kiasi hata cha kutishia uhai wa CCM kuendelea kukamata dola katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, kama ingetokea Mwalimu Nyerere ambaye alipata kutamka CCM si mama yake na hivyo angeweza kukihama chama hicho na huku akionyesha mwelekeo wa kuvutiwa kwa kiasi fulani na chama ambacho hakikuwa na umaarufu wowote, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), lakini kikiongozwa na mtu ambaye alikwishawahi kufanya kazi na Mwalimu, Edwin Mtei.


Hata hivyo, kwa wakati huo CHADEMA kilichoonekana kumvutia Mwalimu kuliko vyama vingine maarufu kikiwamo NCCR-Mageuzi na CUF, hakikuwa kikiunga mkono wazi wazi na kwa ‘sauti' kubwa Muungano wenye sura ya Serikali tatu, ambazo Mwalimu Nyerere aliamini ni mwelekeo wa kuvunja Muungano na kubwa zaidi, ni udhaifu wa viongozi ambao wakati nchi kubwa zikihangaika kujenga mazingira ya kuungana, "vi-nchi" vidogo vinafikiria kutengana na hasa kwa sababu ya uroho wa madaraka na si maendeleo ya wananchi ambao umoja miongoni mwao ni nyenzo muhimu zaidi.


Wiki ijayo katika mwendelezo wa makala hizi, tutarejea mikasa au vituko alivyowahi kukumbana navyo Mwalimu Nyerere Ikulu ya Magogoni, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na siku ambayo alifika Ikulu kwa ajili ya kukutana na aliyekuwa Rais wa Ireland, Bi. Mary Robinson, Oktoba 1994.
 
Siwezi kucomment kitu ambacho bado kipo incomplete. Nasubiri taarifa ikamilike.
 
Sawa...lakini last time I looked Malecela naye alikuwa dini "yetu" na Kambona vivyo hivyo. Sasa hapo cha ajabu na Kolimba sijakiona.

lakini malecela si nasikia alienda tulidhania ameenda upande ule mwingine au ulikua uzushi tu kumbe yuko kwenye hii dini yetu bado?kambona alikua dini yetu lakini si upande wetu,ni ule upande mwingine ambao hatupendagi wakae kwenye kile kiti "chetu" na hatujawahi kuwarusu hata mara moja sijui safari ijayo!
 
lakini malecela si nasikia alienda tulidhania ameenda upande ule mwingine au ulikua uzushi tu kumbe yuko kwenye hii dini yetu bado?kambona alikua dini yetu lakini si upande wetu,ni ule upande mwingine ambao hatupendagi wakae kwenye kile kiti "chetu" na hatujawahi kuwarusu hata mara moja sijui safari ijayo!
alipewa jina J4
 
Eh nimekumbuka makala za Alex Kowe kumbe ndie alikuwa Kolimba,na kweli tokea kifo cha Kolimba sijawahi kuona tena makala za za huyo mwenye jina la Alex Kowe ,du zilikuwa makala kali kwelikweli na za mtu wa ndani ya serikali a.k.a jikoni kwa wakubwa
 
Back
Top Bottom