SoC02 Spana: Shemeji yako kafia kwako, utasikilizwa?

SoC02 Spana: Shemeji yako kafia kwako, utasikilizwa?

Stories of Change - 2022 Competition

ABDalali

Member
Joined
Sep 9, 2021
Posts
6
Reaction score
0
“Nayeyuka huku nikiweweseka kiwendawazimu” ni kauli maarufu sana katika hizi juma chache zilizopita miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania. Kauli hii inatumiwa sana na Mtanzania, Bwana Joramu Nkumbi aliyejizolea umaarufu katika mitandao ya kijamii kwa matumizi ya lugha sanifu ya Kiswahili. Nimeanza andiko hili na kauli hiyo ili kukutia moyo msomaji kwamba andiko hili halitatumia lugha nzito kama ya mlumbi Nkumbi, bali itatumia lugha nyepesi sana kueleza hadithi ya jamii hii. Huenda sio hadithi tamu kama za “mtasha” Bwana Fortunatus Buyobe, au hadithi za visa kama Shigongo, ila ni hadithi muhimu mithili yake.

Hadithi ya kweli na isiyozungumzwa ni kwamba- wanadamu sisi hukosea. Hata wale mashujaa wanaoonekana kutokuwa na ubaya kama; Mwanamapinduzi Ernesto Che Guevarra daktari aliyezunguka na pikipiki bara la Amerika ya Kusini na kwa mapenzi kwa wananchi alisaliti taaluma yake ya utabibu na kugeukia bunduki. Che alianza na nia njema ila baadae hamu ya mapinduzi ilizidi utu akageuka muuaji kama anavyokiri kwenye shajara (diary) zake – alikosea kwa namna yake. Au mpambanaji Kanali Muammar Gaddaffi aliyeshika mtutu kuundoa utawala fedhuli na kutamani kuiunganisha Afrika (United States of Africa) huku akigawa mpaka mahari kwa wanaume nchini mwake, alikosa kwa kukaa madarakani muda mrefu na kuikanyaga demokrasia nchini Libya (najua zipo hoja za mabeberu) – ila alikosa kwa namna yake. Wafalme kama Daudi katika maandiko matakatifu ambao walichaguliwa si kwa boksi la kura bali na MUNGU mwenyewe – walikosea pia. Mzazi, Mlezi, Mtoto, Mume, Mwalimu, Viongozi, Maalim, Wachungaji – sisi sote hukosa.

Habari njema ni kwamba lipo rekebisho. Tofauti kati ya ‘kukosa’ na rekebisho lake ni herufi (irabu) ‘o’ peke yake – KUKOSOA. Mfano, katika ngazi za familia walezi huita watoto na kuwarekebisha inapohitajika. Ikishindikana huita mpaka vikao ya ukoo kukosoa utovu wa nidhamu.Katika ngazi ya nchi, wabunge hulipwa fedha (posho) katika kila siku ya kikao cha Bunge ili kutimiza majukumu yao ikiwemo kushauri (kukosoa) Serikali. Pia vitabu vya kiimani huhimiza sana kuonya na kukosoa kama njia ya kufata. Hivyo nadhani kialisia ipo haki na wajibu wa kukosoa pale inapohitajika.

Mpaka sasa nafahamu ndugu msomaji utakua ‘unanikosoa’ kwamba “Alaa! mbona kichwa cha hili andiko hakisadifu yaliyomo ?”, sikukatazi kuwaza hivyo maana ni haki yako. Ila acha nikufikirishe kidogo katika kisa hiki:

Mnamo Februari 2013, katika eneo la Mwananyamala jamaa mmoja aliingia na mpenzi wake katika nyumba mojawapo, ila wakati wa kutoka mwanamke hakutoka na hamna aliyegundua hilo. Hamna aliyegundua kuwa bwana huyo alikuwa rafiki wa Tumaini aliyekuwa na umri wa miaka ishirini na tatu (23) wakati huo. Japo majirani walitambua mpangaji wa eneo hilo ni Bwana Tumaini. Akihojiwa na chombo cha habari hapa nchini, Tumaini Mabula anaeleza rafiki yake huyo alimuomba nyumba yake ya kupanga maarufu kama ‘gheto’ ili akutane na mpenzi wake. Tumaini aliwaacha na baadae aliporejea akamkuta mwanamke huyo akiwa amefariki dunia ndani kwake. Kama si mara yako ya kwanza kusikia kisa hiki au kinachofanana na hiki, haitakushtua sana. Ila kama ndiyo kwanza unasikia, basi lazima tumbo licheze na ganzi zihusike. Tumaini alijikuta akikaa lupango kwa miaka tisa (09) huku kesi yake ikirindima.

Ndugu zangu miaka tisa ni mingi sana. Hata Tembo- mnyama mwenye kubeba mimba kwa muda mrefu zaidi duniani (longest gestation period) anaweza kujifungua watoto watano katika muda huu. Katika miaka hii tisa, Tumaini hakumshuhudia hayati Magufuli kuanzia anaapishwa mpaka umauti unamfika. Tumaini hakumshuhudia Dr.Shika, hakushuhudia Mo Dewji akitekwa, hakushuhudia Makamu wa Rais mwanamke, hakushuhudia anguko la klabu ya Manchester United, hakushuhudia Diamond Platnumz akipanda kimuziki, ni mengi sana Tumaini hakushuhudia na inanisikitisha sana.

Mnamo Agosti 30,2022, Rais Samia ameagiza kufutwa kwa kesi za watuhumiwa 1,840 na kuachiwa huru kwa kukosekana Ushahidi. Mimi si nabii wa Kiyahudi ila si muda mrefu huenda tutasikia simulizi za kusikitisha kama za Tumaini, katika hao ndugu 1,840. Huu ni mfano tu wa namna gani mfumo wa utoaji haki hapa nchini una makandokando. Changamoto hizo zimekuwa zikikosolewa miaka nenda rudi ikiwemo hiyo ya kuweka watu ndani kabla ya kukamilisha upelelezi. Endapo wanaokosolewa wangesikiliza mapema basi Tumaini Mabula na ndugu 1,840 wasingepatwa na masaibu hayo. Mfumo wa haki ungekuwa bora kiasi kwamba hata kama shemeji yako angefia kwako, ungesikilizwa!

Mfumo wa utoaji haki nchini ni tatizo moja kati ya mengi yanayotukumba. Na matatizo hayatokani na viongozi wetu pekee bali kwetu sisi pia. Upo ukatili unaofanyika katika ngazi za familia kama vile unyanyasaji wa kijinsia na ulawiti ila sisi tumeyakalia hayo na hatuyasemi, hatuyakosoi. Maovu yanatendeka katika nyumba za ibada na baadhi ya viongozi wa dini hawayakosoi katika mimbari zao. Baadhi ya Vyombo vyetu vya Habari navyo haviibui changamoto, vinatumia muda mwingi zaidi kutangaza kamari (nafahamu ni biashara) kuliko kuzikemea changamoto kutoka ngazi ya familia mpaka kwenye mamlaka. Baadhi ya redio nazo husuta zaidi kuliko kukosoa, husahau kwamba kupiga vijembe pasipo mtiririko mzuri wa hoja, si ukosoaji bali ni ‘kuchamba’.

Ndugu zangu maudhui ya vyombo vya Habari si mahusiano pekee, si masuala ya “mume afanye hiki, mke afanye kile, wakwe hili, wifi lile!”. Zipo changamoto: kukithiri kwa mapenzi ya jinsia moja, kupwaya kwa elimu za vyuo vikuu, mazingira hatarishi kazini na mishahara kijungujiko, wauguzi wa kujitolea kutolipwa, kukosekana utamaduni wa kujisomea, kudharau na kuingilia utafiti, huduma mbovu kwa wateja nchini, kukosekana kwa usiri wa taarifa nchini (mfano wauguzi huropoka taarifa za wagonjwa kwa sauti awapo katika foleni) n.k. Haya yote na mengineyo tuyaseme.

Hadithi yangu ni hadithi ya mabadiliko. Hadithi inayoisimulia jamii kuupokea ‘ukweli kama ushauri’ na si ‘ukweli kama uadui’. Kama nilivyotanabaisha katika aya ya pili - sisi sote hukosea. Kukosea hutokea pia katika kuwasilisha ukosoaji wetu. Matusi, lugha ovu, kumshambulia mtu na si hoja, hayo si ukosoaji! Ukosoaji ni hoja, na “hoja zijibiwe kwa hoja si nyundo”-Kikwete. Kuanzia nyumbani tuwajengee watoto uwezo wa kuwasilisha hoja. Kabla ya kumchapa tuseme kwanini. Tuwape hata maandiko wasome kisha waelezee. Katika jumuiya zetu za kidini majumbani ni sehemu nzuri ya mtoto kujua kuzungumza, mwambie atoe tafakari katika vitabu vitakatifu. Mashuleni turudishe midahalo, Vyuoni tuhudhurie midahalo na tuzungumze. Tujenge taifa la wajenga hoja. Kwa sisi watu wazima turekebishane ili kutumia lugha ya staha. Hoja zetu zinaweza kuwa nzuri ila zikikosa staha labda zitapwaya. Na ieleweke wazi, kuwa kutokua na suluhisho haitunyimi haki ya kukosoa. Najua tuna hasira na uchungu ila tupige ‘spana’ na si ‘spana vimeo’.

Nafahamu unasema “tukosoe wapi sasa? Na hata tukikosoa hawasikilizi”. Nafahamu kiudhaifu teknolojia imeunganisha dunia lakini imetenganisha wanadamu, ila bado ina nafasi ya kumfikia hata yule mkubwa akuumizaye. Vyombo vya Habari vyenye weledi bado vipo tuwape taarifa, madawati ya jinsia yapo tukasemee unyanyasaji, kesi zipo tukubali kutoa Ushahidi, ni heri tuzitoe taarifa kuliko kukumbatia unyonyaji. Kukalia kwako taarifa, kukumbatia kwako faili kunaweza kumweka Tumaini Mabula mwingine ndani miaka tisa(9)!

Ndugu tuinusuru Jamii kwa kuongeza/kuzungusha ‘o’ kwenye KOSA – KOSOA (kwa staha). Na usiache kupiga ‘spana’, walengwa wanasoma mpaka comments (maoni) !

Wabaadu watakabahu fakiri. Nayeyuka huku nikiweweseka kiwendawazimu.​

HISANI: MAHOJIANO (VIDEO) YA TUMAINI MABULA NI KWA HISANI YA MILLARD AYO NEWS.

#Zungusha_O #Zungusha_O_kwenye_Kosa
 
Upvote 5
Moja ya insha bora sana za Shindano la mwaka huu
 
Nimependa lugha ya sanaa uliyotumia hapa. Ila japo kwa ufupi nifafanulie 'hoja' bora kwako ikoje?
 
Hongera sana kwa makala nzuri, Ila ningependa kufahamu mtazamo wako juu ya mbinu au hatua za kufata pale wanaokosolewa wakishindwa kubadilika
 
Andiko zuri sana mkuu. Inabidi tuamke sasa tuwe tayari kupokea ukweli
 
Nimependa lugha ya sanaa uliyotumia hapa. Ila japo kwa ufupi nifafanulie 'hoja' bora kwako ikoje?
Kwangu mimi pamoja na yote Hoja bora inahitajika iwe hoja shawishi. Hoja inayoleta muunganiko kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Na sio lazima hoja hii itolewe na wanazuoni hapana. Waziri mkuu wa zamani wa UK Bwana Winston Spencer Churchill alisema 1947 na nakuu "Hoja bora kinzani dhidi ya demokrasia ni mazungumzo ya walau dakika tano na mpiga kura wa kawaida".

Hivyo, katika ukosoaji wetu pasipo kujali elimu wala wadhifa sote huweza kutoa hoja bora maadamu tu ina mtiririko mzuri na ni shawishi.
 
Hongera sana kwa makala nzuri, Ila ningependa kufahamu mtazamo wako juu ya mbinu au hatua za kufata pale wanaokosolewa wakishindwa kubadilika
Nashukuru sana mwanajukwaa kwa kuipenda makala.

Mwanafalsafa Aristotle alishawahi kusema "Kukosoa ni jambo tunaloweza kuliepuka kwa urahisi kwa kutosema lolote, kutofanya lolote, na kutokuwa chochote.” Nadhani upokezi wa wakosolewa sio jambo sisi tunapaswa kupata sonona nalo ndugu mchangiaji.

Kwetu sisi tutimize wajibu wetu, tuutimize kwa nguvu nyingi na kwa sauti moja. Tukifanya hivyo sauti yetu husikika. Kama watu fedhuli zaidi duniani walitii amri kwa sauti ya umma basi hakuna lishindikanalo.

Watu mithili ya: Louis XVI aliyepinduliwa Ufaransa baada ya mkewe Maria Antoinette kuuambia umma "kama hawawezi kununua mikate wale keki". Huyu naye nguvu ya umma ilimuadabisha.

Naamini hata sasa nguvu hiyo inaweza tenda kazi kwa mazingira yetu haya ya kitanzania. Tusiache kukosoa ; utawala ukiwa mbovu, mmonyoko wa maadili, ubadhirifu, mifumo hatarishi, vyombo vya habari dhaifu n.k Tupaze sauti tu, walengwa watabadilika maana "sauti ya wengi ni sauti ya Mungu"
 
Andiko zuri sana mkuu. Inabidi tuamke sasa tuwe tayari kupokea ukweli
Nashukuru sana Ndugu.

Kama nilivyotanabaisha hapo awali na narudia - "Hadithi yangu ni hadithi ya mabadiliko. Hadithi inayoisimulia jamii kuupokea ‘ukweli kama ushauri’ na si ‘ukweli kama uadui’ "- ABDalali (SoC 2022)
 
Nashukuru sana mwanajukwaa kwa kuipenda makala.

Mwanafalsafa Aristotle alishawahi kusema "Kukosoa ni jambo tunaloweza kuliepuka kwa urahisi kwa kutosema lolote, kutofanya lolote, na kutokuwa chochote.” Nadhani upokezi wa wakosolewa sio jambo sisi tunapaswa kupata sonona nalo ndugu mchangiaji.

Kwetu sisi tutimize wajibu wetu, tuutimize kwa nguvu nyingi na kwa sauti moja. Tukifanya hivyo sauti yetu husikika. Kama watu fedhuli zaidi duniani walitii amri kwa sauti ya umma basi hakuna lishindikanalo.

Watu mithili ya: Louis XVI aliyepinduliwa Ufaransa baada ya mkewe Maria Antoinette kuuambia umma "kama hawawezi kununua mikate wale keki". Huyu naye nguvu ya umma ilimuadabisha.

Naamini hata sasa nguvu hiyo inaweza tenda kazi kwa mazingira yetu haya ya kitanzania. Tusiache kukosoa ; utawala ukiwa mbovu, mmonyoko wa maadili, ubadhirifu, mifumo hatarishi, vyombo vya habari dhaifu n.k Tupaze sauti tu, walengwa watabadilika maana "sauti ya wengi ni sauti ya Mungu"
Shukrani sana mkuu kwa jibu zuri
 
Back
Top Bottom