Wakuu nadhani habari iliyomchefua spika ni hii hapa, hebu tuiangalia kama kweli inachafua au mzee 6 ameghafilika tu
Wasomi wachambua ubinafsi wa wabunge
:: Wakosoa namna wanavyochangia bajeti
:: Wasema wanatazama uchaguzi ujao pekee
:: Profesa Baregu aliita bunge la
marehemu
Na Sarah Mossi
BAADHI ya wasomi wamekosoa aina ya uchangiaji mjadala wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2009/2010 unaofanywa na wabunge wakidai uchangiaji huo haulengi kuisaidia serikali katika kuinua uchumi wa kitaifa, badala yake unatazama kuwanufaisha wabunge kisiasa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili juzi, wasomi hao walisema, mjadala wa bajeti unaofungwa leo mjini Dodoma haukulenga kutazama maslahi ya kunyanyua uchumi wan chi badala yake wabunge walitumia kila nafasi waliyopata kujinufaisha wao kisiasa kwa kuzungumza lugha tamu zinapendwa kusikika na wapiga kura.
Mmoja wa wasomi hao ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) Dk Richard Mushi aliliambia Rai kuwa; wabunge wengi hawakutazama jukumu lao la kutoa hoja za kitaifa badala yake wanawaza kuhusu uchaguzi mkuu unaofanyika mwakani.
Mhadhiri huyo alisema; tungetegemea wabunge wasimame na kuzungumzia masuala kama fedha za Halmashauri ziongezwe, suala la barabara na sio kuzungumzia masuala yao ya majimbo pekee, anazungumza na kuongeza:
"Kule bungeni kuna watu wachache wazuri sana, lakini sasa hivi wana presha kubwa ya kuchaguliwa mwakani na wanazikumbuka zile ahadi walizotoa katika uchaguzi mkuu uliopita."
Msomi mwingine aliyezungumza na Rai ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mwesiga Baregu ambaye alisema; sasa hivi wabunge hawawezi kuzungumzia masuala ya kitaifa kwa kuwa wanawaza zaidi majimbo yao.
Kufuatia hali hii, Profesa Baregu alifafanua kuwa, mahudhurio ya wabunge kwa sasa ni hafifu pia ukilinganisha na mabunge mengine yaliyopita na hii inatokana na hali ya wabunge kuwa na mguu mmoja ndani ya bunge na mwingine nje ya bunge.
Hili si bunge la kujenga taifa. Ni la mkao wa uchaguzi wa mwakani, hata mahudhurio unayaona.
Watatoka kwenda kwenye majimbo yao, hili ni bunge marehemu kwani nyoyo na fikra za wabunge zinatazama uchaguzi tu, anasema Profesa Baregu na kuongeza:
"Sijui kama uwezo wao wa kuzungumzia masuala ya kitaifa kama ni mdogo ama vipi...Lakini ninachoweza kusema kwamba safari hii wanazungumza wengi na hata wale wanaolala hawatalala kwenye bunge hili. Akili zao zimeanza kuota kurudi ama kutorudi.
"Na hili angalau vyombo vya habari mmeliona mapema na mnapaswa kulipigia kelele, labda wanaweza kurudi," anasema Profesa Baregu.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni Mchumi Kitaaluma, aliliambia Rai kuwa wabunge katika bunge hili wameonyesha upeo mdogo wa mambo ya kitaifa.
"Lakini wengine wanaelewa wanachofanya, lakini wao ni wanasiasa wameweka mbele maendeleo ya maeneo yao. Wanataka wasikike kile wanachofanya sasa na tutarajie hilo na hapatakuwa na chochote cha kufanya na wao kama wanasiasa watataka wananchi wawasikie, hili ni jambo la kisiasa," anasema Profesa Lipumba.
habari zaidi
hapa