Habari za kawaida Posted Date::2/4/2008Bunge: Fukuto la Richmond,Spika aahirisha ziara ya Marekani* Waziri Mkuu, Makamba wateta kwa saa tatu
* Wabunge CCM kukutana leokuweka mkakati
* Yadaiwa kuna mpango wa kuzuia mjadala
Na Tausi Mbowe, Dodoma
SPIKA wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta ameahirisha safari yake ya kwenda Marekani.
Taarifa ya kusitishwa kwa ziara hiyo ilitolewa jana na Naibu Spika, Anna Makinda na kufahamisha kwamba leo Spika atakuwepo Bungeni kuendelea na shughuli za Bunge.
Hata hivyo katika tangazo hilo la Naibu Spika Makinda hakutaja sababu ya
Spika kuahrisha safari hiyo.
"Wabunge kama mnakumbuka, Spika alitangaza kuwa atasafiri leo na kurudi siku ya Alhamisi, ameniagiza kutangaza kuwa amesitisha safari hiyo ya Marekani na kwamba kesho (leo) atakuwepo bungeni kuendelea na shughuli za Bunge kama kawaida," alisema Makinda.
Hata hivyo wachunguzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa Spika amefikia uamuzi huo ili kuokoa jahazi kutokana na hali ya kisiasa kuchafuka kufuatia msimamo ulionyeshwa na wabunge kutaka ripoti ya Richmond iletwe bungeni kwanza kwaajili ya kujadiliwa.
Wakati anawaaga wabunge, Spika Sitta alimuagiza Naibu Spika, Anna
Makinda asije akakurupuka na kuyavamia mambo yote ?nyeti? na kuyazungumza au kuyatolea maamuzi katika bunge hilo wakati yeye hayupo.
Sitta alisema kuwa mambo yote 'nyeti' yatasubiri mpaka atakapokuwepo na kwamba Naibu Spika asije akarudhusa kujadili mambo makubwa wakati hayupo.
Spika alitolea mfano wa sakata la ufisadi la Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na la Richmond na kusisitiza kuwa ili kujadili masuala hayo lazima yeye awepo.
Kauli hiyo ya Spika ina maana kuwa ripoti hiyo isingejadiliwa mpaka yeye yaani wiki ya mwisho ya kikao cha 10 cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma.
Juzi wabunge walisusia semina iliyoandaliwa na na Wizara ya Nishati na Madin ikwa lengo la kuwaelimisha kuhusu muswaada wa Sheria za Umeme na Biashara ya mafuta ya Petrol wakidai wapewe kwanza ripoti ya Kamati ya Richmond ili waijadili kabla ya kuupitisha muswada huo.
Wabunge hao pia walisema kuwa hawana imani na wizara hiyo pamoja na Shirika lake la Umeme Tanesco kwa kuwa taasisi hizo zimejaa uchafu na kwamba hawawezi kujadili masuala ya mikataba mengine mpaka wajisafishe.
Taarifa zilizopatikana kutoka miongoni mwa wabunge mjini hapa, zilieleza kuwa ili kuua mjadala bungeni, serikali inataka kutumia Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (Takukuru), kukamata baadhi ya maafisa na kuwafikisha mahakamani.
Chanzo chetu cha habari kilisema, juhudi zilikuwa zikifanyika tangu mwishoni mwa wiki kwa viongozi wakuu wa serikali kuwasiliana na Takukuru kwa ajili ya kuchukua hatua hizo.
Inadaiwa kuwa, kupelekwa kwa maafisa hao kuwatanyima haki wabunge kujadili suala hilo kwasababu ya utaratibu wa kuheshimu utawala wa sheria, lengo likiwa ni kuwaziba midomo wabunge hasa kutokana na cheche walizoonyesha mwishoni mwa wiki.
"Viongozi wanahaha kuhusu Richmond. Zimeenea habari kuwa viongozi wanaotaka kuua hoja hiyo bungeni wataitumia Takukuru kuwafungulia kesi maafisa kadhaa wa serikali kuwa walikula njama za kuihujumu Tanesco, iliwa na lengo la kuzuia mjadala bungeni," alisema Mbunge mmoja wa CCM na kuongeza:
"Upo uwezekano mkubwa watu hao watakamatwa kabla ya kikao cha wabunge wa CCM kinachofanyika leo."
Hata hivyo, Takukuru iliwahi kutoa taarifa za kuwasafisha maafisa waliohusika na kwamba hakuna rushwa iliyotumika kwenye mchakato mzima wa kufikia utoaji wa zabuni yenye mashaka ya Richmond.
Taarifa hiyo ya Takukuru ilipingwa na wananchi, huku Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Edward Hosea akisimama kidete kuwa hisia za rushwa ni juu ya mkataba huo ni majungu.
Kwa mujibu wa maelezo ya awali ya Spika, safari ya nchini Marekani ilikuwa na lengo la kuliongezea Bunge uwezo katika masuala mbalimbali yanayohusu shughuli zake na kwamba ingekuwa ya muda mfupi na kuahidi kurudi siku ya Alhamisi na kuendelea na shughuli kama kawaida na kujadili mambo hayo nyeti.
Siku hiyo pia Spika aliliambia Bunge kuwa bado mashauriano baina ya ofisi yake na serikali yanaendelea kuhusu ripoti nzima ya Mahesabu ya Akaunti ya Nje ya Nchi (EPA), kupelekwa bungeni kwaajili ya kujadiliwa.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Yussuf Makamba jana walikutana kwa dharura kuweka mikakati itakayowezesha Wabunge wa CCM kuwa na kauli moja kutokana kuwepo kwa mgawanyiko mkubwa kwa wabunge hao dhidi ya ripoti ya Richmond.
Viongozi hao wajuu wa chama hicho walikutana jana kwa zaidi ya saa tatu katika
Ofisi za Bunge ili kuokoa jahazi kutokana na mgawanyiko huo unaonekana kutokea wazi wazi.
Habari zaidi zinasema kuwa wabunge wote wa CCM watakutana leo kwa ajili ya kuweka mkakati kabambe ikiwa ni pamoja na kuwa na kauli moja katika sakata hilo lilosababisha Spika Sitta kukatisha safari yake ya Marekani. Kwa upande wa wabunge wengi walionekana kuwa na shauku kubwa kutaka ripoti hiyo ifikishwe bungeni kwanza ili wapate fursa ya kuijadili kwa undani ripoti hiyo