...Spika: Sijashinikizwa kutokwenda Marekani
Na Hassan Abbas
SPIKA wa Bunge, Bw. Samwel Sitta, amesisitiza kuwa kuahirisha safari yake ya Marekani hakukutokana na shinikizo la uongozi wa juu serikalini, bali alisikiliza kilio cha wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi.
Akizungumza na Majira kwa njia ya simu jana akiwa njiani kurejea Dodoma mara baada ya kuahirisha safari hiyo na kuwa tayari kuanza kuendesha vikao vya Bunge leo, Bw. Sitta pia alikiri kuwa mjadala huo una maslahi ya kitaifa.
"Sijashinikizwa na kiongozi yeyote. Nashangaa wanaohusisha taarifa hizo, watu wanakwenda mbali hadi kumtaja Rais. Haya ni mashambulizi dhidi ya heshima yangu binafsi. Niliposema nakwenda Marekani na kuahirisha kuijadili ripoti hiyo watu walinielewa vibaya, naelewa ni kutokuelewa kanuni tu na watu hawataki kujishughulisha kujua.
"Kwa mujibu wa Kamati ya Uongozi, awali tulipanga mjadala huo uwe mwishoni mwa Bunge, kwa hiyo nikaona naweza kusafiri kwa siku mbili tatu hizi na kurejea kuwahi kuuendesha. Nimeshafafanua kuwa kanuni zinamtaka Spika mwenyewe awepo pindi kunapokuwa na mijadala muhimu bungeni," alisema na kuongeza:
"Safari yangu ya Marekani ilikuwa ya manufaa kwa Bunge. Unajua Bunge hivi sasa lina mfuko maalumu wa kujiendesha. Kule kulikuwa na kikao cha viongozi katika jitihada zetu za kupata nguvu ya kujiendesha. Sasa unapoitwa tena kwa wadhifa wako unapaswa kuheshimu, hii si kumdharau mtu mwingine."
Akizungumzia zaidi sababu za kufikia hatua ya kuamua kubaki nchini, Bw. Sitta aliiambia Majira kuwa alizingatia matakwa ya wabunge.
"Jumapili baada ya wabunge kutoa tamko kwenye semina na kukataa kujadili muswada (wa sheria mpya ya umeme), nilipigiwa simu na kuelezwa hoja hiyo kuwa wengi walikuwa wakitaka kwanza ijadiliwe ripoti ya Richmond.
"Kwa kuona suala hili sasa limeletwa na wawakilishi wa wananchi wakitaka mjadala huu uje mapema kuliko tulivyopanga awali, ndipo nikaona kuna haja ya kubaki kusimamia suala hilo," alisema.
Alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge, yeye si anayeamua na kuidhinisha kila jambo. "Hapa ndipo wengi wanapokosea, watu wanadhani mimi ndiye naweza kukaa tu na kuamua hiki kifanyike ninavyoona, nasimamia kanuni na sheria.
"Ili mjadala wa Richmond ufanyike mapema zaidi, ni lazima Kamati ya Uongozi ambayo mimi ni Mwenyekiti wake, ikae tena na kupitia tena ratiba.
"Hilo ndilo ambalo limenibakiza nchini ili tukutane na kuusogeza mjadala huo ujadiliwe mapema zaidi. Hivi ninavyozungumza na wewe leo (jana) jioni, Kamati ya Uongozi inakutaka kupanga siku ya kuijadili ripoti hiyo. Kila kitu kiko wazi," alisema.
Akizungumzia tuhuma kuwa amekuwa akishiriki katika kile kinachoelezwa kuwa mkakati wa chini kwa chini wa 'kupoteza muda,' juu ya kujadiliwa ripoti hiyo, Spika Sitta alisema:
"Mimi ndiye nilisimamia mjadala wa kuundwa Kamati ya kuichunguza Richmond. Mimi ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, ambayo iliipanga ripoti hiyo kujadiliwa kwa mujibu wa kanuni ambazo kwanza zinataka miswada ya Serikali ndiyo ijadiliwe. Ningekuwa na upande, mjadala huo usingefika hata bungeni. Kwa hiyo madai hayo hayaeleweki."