Boniface Meena
BAADA ya kimya kingi, mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Subhash Patel, jana aliibuka na kujibu tuhuma za ufisadi papa zilizotolewa na mfanyabiashara mwenzake, Reginald Mengi huku akisema kuwa kama kuna tofauti, basi "zitatuliwe kibishara na si kuchafuana".
Patel anakuwa mtu wa tatu kuzungumzia tuhuma zilizotolewa na Mengi dhidi ya watu watano aliowaita kuwa ni mafisadi papa, akidai kuwa ni miongoni mwa watu 10 wanaoifilisi nchi.
Wengine ni mfanyabiashara Rostam Aziz, ambaye mbali na kukanusha tuhuma dhidi yake, alimwaga mlolongo wa tuhuma dhidi ya Mengi na kuwasilisha vielelezo ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili ianze kumchunguza.
Mwingine ni mfanyabiashara Yusuf Manji, ambaye siku ya tuhuma alijibu kwa kifupi tu kwamba Mengi ana wivu, chuki na ubaguzi na mwishoni mwa wiki aliwasilisha malalamiko kwenye Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) akidai mwenyekiti huyo wa IPP hakumtendea haki alipomwaga tuhuma kwenye televisheni yake na hivyo anataka kituo hicho kifungiwe kwa wiki moja.
Jana ilikuwa zamu ya Patel ambaye alikanusha tuhuma na kudai kwamba kama kulitokea matatizo katika uhusiano wake na Mengi kibiashara, basi hakuna budi kuyatatua kibiashara na si kwa kuchafuliana majina.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, ofisa uhusiano na mawasiliano wa kampuni inayoimilikiwa na mfanyabiashara huyo ya Motisun Holdings Limited, alisema Patel hana kampuni ambayo imewahi kupewa mradi wowote kati ya eneo la mradi wa chuma wa Liganga na makaa ya mawe ya Mchuchuma.
"Kuhusu tuhuma alizotoa Mengi katika mradi wa chuma wa Liganga na makaa ya mawe ya Mchuchuma, si Patel wala kampuni yake yoyote iliyopewa mradi wowote katika eneo la mradi wa makaa ya mawe," alisema ofisa huyo, Aboubakary Mlawa.
Alifafanua kuwa kilichopo ni kwamba moja ya kampuni za Patel iitwayo MM Steel Resources Public Limited ndiyo iliyoshiriki katika zabuni ya kutafuta mwekezaji wa ndani Aprili mwaka 2008 ili awe na ubia na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), katika kuzalisha na kuendeleza mradi wa kuzalisha chuma kiitwacho 'sponge' na siyo kampuni iliyotajwa na Mengi na vyombo vyake vya habari.
Kuhusu tuhuma za kutoa rushwa kwa wanakijiji wa vijiji mbalimbali ambavyo havikutajwa na Mengi, Mlawa alisema kuwa Patel hajawahi kutoa rushwa kwa wanakijiji wa kijiji chochote katika sehemu yoyote ya Tanzania.
Alibainisha kuwa anachofanya Patel ni kutumia haki aliyonayo kusaidia wananchi wenye matatizo mbalimbali na kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo na kijamii hapa nchini.
"Makampuni yametoa misaada mbalimbali ya maendeleo na ya kijamii inayozidi thamani ya Sh800 milioni," alisema.
Kuhusu umiliki wa gazeti la Sauti Huru, ofisa huyo alisema kuwa Patel hamiliki, hafadhili, wala hana hisa katika gazeti hilo wala chombo kingine chochote cha habari kama Mengi anavyomtuhumu.
Akizungumzia madai ya kutorosha fedha nje ya nchi, alisema Patel hajawahi kufanya kitu kama hicho kwa kuwa anatambua hilo ni kosa la jinai kwa sababu yeye ni Mtanzania.
Alisema kuwa kutokana na tuhuma hizo Patel angependa kujua ni nini hasa kiini cha kuchafuana majina na kuchonganishana kwa jamii kunakofanywa na Mengi dhidi yake.
Alisema kuwa bado hajafikia uamuzi wa kwenda mahakamani, lakini akiamua atakwenda kwenye chombo hicho cha sheria.