Mbaya zaidi kamanda Suleiman Kova anaiita jinai ni swala binafsi, hili linakera. Katika jeshi hakuna cheo bali majukumu na majukumu haya huendana na weledi wa mhusika, kwa hadhi ya CP nilitegemea afande Kova ni mtu wa weledi wa hali ya juu na pasipo shaka anaitambua The Sexual Offences Special Provisions Act(1998) ambayo inatamka kuwa hakuna ridhaa ya binti wa chini ya miaka 18 sembuse mwanafunzi kufanya mapenzi na mwanamume yeyote yule and specifically mazingira yanayosimuliwa katika mkasa mzima wa ndugu Kapuya. Sheria hii inaondoa hali zote za ridhaa ya wawili na kutamka kuwa ni ubakaji. Kamwe ubakaji haujapata na hautapata kuwa ni swala binafsi. Si kuwa nasema pasipo shaka kwamba ndugu Juma Kapuya mbunge wa Urambo ya Magharibi na profesa wa botania amembaka binti wa miaka kumi na minne(14), hapana, ninachokisema ni kuwa jeshi la polisi litimize wajibu wake wa kuchunguza jinai kwa mamlaka lilopewa ili haki si tu itendeke bali pia ionekane kutendeka.