Taarifa Rasmi ya Chama cha ACT Wazalendo Juu ya Chaguzi za Marudio

Taarifa Rasmi ya Chama cha ACT Wazalendo Juu ya Chaguzi za Marudio

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
Joined
May 5, 2014
Posts
631
Reaction score
1,577
Taarifa Kwa Vyombo vya Habari

UZOEFU WA ACT WAZALENDO KATIKA KUSHIRIKI CHAGUZI ZA MARUDIO ZA 16 MEI 2021

Chama cha ACT Wazalendo kilishiriki katika chaguzi ndogo za marudio katika Majimbo ya Muhambwe na Buhigwe na Kata 5 kati ya Kata 17 zilizokuwa zinachagua Madiwani. Tuliamua kushiriki katika chaguzi hizi kama kipimo cha kuona kama kutakuwa na Mabadiliko yeyote katika uendeshaji wa chaguzi katika Awamu ya Sita ya Uongozi wa Nchi yetu kutoka hali iliyokuwapo Wakati wa Awamu ya Tano.

Kutokana na ushiriki wetu katika chaguzi hizi tumeweza kuona sura mbili tofauti za uendeshaji na usimamizi wa uchaguzi chini ya Tume Moja ya Uchaguzi;

1. Sura ya kwanza ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi kwa uhuru na haki kwa vyama vyote. Hali hii imejitokeza kwenye jimbo la Muhambwe na Kata kadhaa. Katika maeneo haya Chama chetu kiliweza kushiriki kwenye kampeni bila bughudha kipindi chote cha kampeni, siku ya uchaguzi mawakala wetu waliruhusiwa kutekeleza majukumu yao wakati wote hadi zoezi lilipo kamilika na utangazaji wa matokeo uliakisi matokeo halisi yaliyotoka katika vituo vya kupigia kura. Licha ya kuwa na hitilafu ndogo ndogo kama vile vitisho kwa baadhi ya viongozi wetu, kutekwa kwa Kiongozi wetu mmoja siku ya uchaguzi, bado tunaweza kusema Msimamizi na wasimamizi wasaidizi kwenye maeneo haya waliendesha uchaguzi kwa uhuru na haki. Katika hatua hii tulikubali matokeo na kuwapongeza walioshinda, utamaduni mzuri kabisa katika kukomaza demokrasia yetu. Mgombea wa ACT Wazalendo alimpongeza Mgombea wa CCM kwa ushindi. Kiongozi wa Chama chetu pia alikipongeza Chama cha Mapinduzi kwa ushindi huo. Vile vile tulimpongeza Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Muhambwe kwa kuendesha uchaguzi kwa mujibu wa sheria, kanuni na utamaduni wa Demokrasia ya Vyama Vingi. Utamaduni huu ni muhimu kuendelezwa Nchini kwetu.
2. Sura ya pili ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi - NEC kusimamia uchaguzi kwa kukandamiza uhuru wa vyama vingine na kupendelea wagombea wa chama tawala, CCM. Hali hii imejitokeza kwenye jimbo la Buhigwe na kata za Miuta Wilaya ya Tandahimba, Ligoma Wilaya ya Tunduru na Buziku Wilaya ya Chato. Licha ya kuwa zoezi la Kampeni liliendeshwa vizuri lakini siku ya uchaguzi iligubikwa na hila na uvunjifu wa sheria dhidi ya wagombea wa Chama chetu. Hitilafu na hila zilizojitokeza ni kama zifuatazo;

  • Mawakala wetu walitolewa kwenye vyumba vya kupigia kura
  • Kukamatwa kura bandia kwa mfano Kijiji cha Kasumo kata ya Kajana jimbo la Buhigwe na Kata ya Ligoma Wilayani Tunduru.
  • Wasimamizi wa vituo kutumika kuingiza kura kwenye masanduku ya kupigia kura, sambamba na wasimamizi ambao sio wapiga kura ndani ya jimbo la Buhigwe kuruhusiwa kupiga kura
  • Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Buhigwe kubainika kupiga kura mara tatu (kwenye vituo vitatu tofauti)
  • Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kuongeza kura Kwa mgombea wa CCM Wakati wa kutangaza matokeo katika Kata ya Ikizu Wilaya ya Chato
  • Kutekwa kwa baadhi ya wanachama wetu
  • Kukamatwa kwa Kiongozi wetu, Katibu wa Mkoa wa Selou (unaojumuisha majimbo ya Tunduru Kusini, Tunduru Kaskazini na Namtumbo) Ndg. Mtutura Abdallah Mtutura na viongozi wengine watatu kukaa Polisi kwa zaidi ya Siku sita kinyume cha Sheria kwa makosa ya kubambikiwa.
  • Vyombo vya dola kutumia nguvu kubwa ikiwemo kupiga mabomu vijiji vyenye uchaguzi usiku wa manane bila kuwepo vurugu yoyote ili kutisha wapiga kura. Hili lilitokea Kata ya Ligoma Wilaya ya Tunduru.

Kwa hiyo, kutokana na hali tuliyoiona katika chaguzi hizi, kwa sasa bado uendeshaji wa uchaguzi unategemea utashi na hisani ya mtu anayesimamia uchaguzi (Msimamizi wa Uchaguzi). Hizi ni dalili za hatari kwa uhai wa demokrasia ya vyama vingi.

Chaguzi zinapaswa kuendeshwa kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni na utamaduni wa misingi ya demokrasia ikisimamiwa na chombo kinachoaminika na pande zote zinazoshiriki katika Uchaguzi.

Hivyo Basi,

A. Tumeamua kuchukua hatua za kukata rufaa mahakamani kupinga matokeo katika Jimbo la Buhigwe na Kata za Miuta, Ikizu na Ligoma.

B. Kiongozi wa Chama Ndg. Zitto Zuberi Ruyagwa Kabwe amemuandikia Barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumweleza changamoto zilizotokea ili Hatua ziweze kuchukuliwa.
Kiongozi wa Chama amemweleza Rais kuwa mifano ya yaliyojiri katika chaguzi hizi haitoweza kutimiza nia Yake Njema aliyonayo juu ya kuendeleza demokrasia, na kuweka mwelekeo wa shughuli za kisiasa zenye tija na maslahi kwa Nchi yetu kama alivyoahidi katika hotuba Yake Bungeni alipolihutubia Taifa.

Katika barua hiyo, Chama cha ACT Wazalendo imewasilisha Kwa Rais Samia Suluh Hassan mapendekezo yafuatayo ili kuzifanya chaguzi kuwa za ushindani, huru na zenye uwanja sawa wa vyama vyote vina vyoshiriki;

1. Kuanzishwa Kwa mchakato wa kuifanya Tume ya Taifa ya uchaguzi kufanya shughuli zake kwa uhuru. Kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi iwe na Watumishi wake wanao wajibika kwa Tume tu na wasiwe ni makada wa chama kingine cha siasa.
2. Kuanzishwa Kwa mchakato shirikishi wa kupitia upya Sheria ya Vyama vya Siasa ili kuondoa vifungu vyote vinavyobana uhuru wa vyama vya siasa kutekeleza majukumu yake. Tumetaka Vyama vya Siasa viwe na Uhuru wa kufanya mikutano yake bila bugudha.
3. Kwa kupitia Taasisi zinazomilikiwa na Vyama vya Siasa Nchini hususan Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Rais aanzishe majadiliano miongoni mwa Vyama ili kujenga kuaminiana na kutatua migogoro kwa njia za amani pale inapotokea.
4. Kutekelezwa Kwa makubaliano ya Mabadiliko ya Msingi katika Katiba na Sheria ya Uchaguzi (minimum reforms) ya Septemba 2014 kati ya Serikali na Vyama vya Siasa kupitia TCD ili kuwezesha Siasa zenye Tija na chaguzi kuwa Huru.
5. Kuvinasihi vyombo vya Ulinzi na Usalama kutenda haki kwa wote na kuachia mara moja Wanachama wetu na wa vyama vingine vya Siasa waliokamatwa na kuwekwa magerezani nyakati za chaguzi.

Imetolewa na

Salim Bimani
Katibu wa Uenezi na Mawasiliano Kwa Umma
ACT WAZALENDO
19/5/2021

IMG-20210417-WA0014.jpg
 
Mnawasifia ccm kuwa kuna sehemu moja wameshinda kihalali, ila sehemu nyingine zote wameshinda kwa figisu, si ajabu hata hiyo sehemu waliyoshinda kihalali ni kwakuwa walijua lazima watawashinda, ndio maana wakajifanya wema, ila sehemu nyingine zote ambazo hawakuwa na uhakika ikabidi wafanye fitina kama kawaida yao.

Ngoja tuone kama hiyo barua yenu mliyoandika kwa huyo mama kama itakuwa na mwitikio wowote wa maana.
 
Ziitto badala ya kudai tume huru ya uchaguzi yeye anapendekeza kwa rais minimum reforms za hapa na pale kwenye tume ya uchaguzi. Namna hii upinzani tayari hauna msimamo wa pamoja kwenye tume ya uchaguzi.

Halafu mambo ya uchaguzi unamuandikia rais na Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi ili afanyeje? Unadhani anaweza kukubali chochote kitakachoumiza chama chake?, Tume huru ya uchaguzi itapatikana kwa presha na sauti moja na siyo kubembeleza.
 
Salim Bimami,wewe ni mtu makini Sana siku nyingine usikubali kupewa kipepelushi Kama hiki na Zitto Kabwe,

ni kujishushia heshima, anzeni mapema mchakato wa kuunda chama chenu kipya, ili ikifika uchaguzi 2025, mwachieni Zitto chama chake, atawahalibia taswila na uaminifu kwa wazanzibari na watanzania kwa ujumla,

Zitto ni CCM na anasafilia yota ya CUF ya Sharif Hamad.
 
Ziitto badala ya kudai tume huru ya uchaguzi yeye anapendekeza kwa rais minimum reforms za hapa na pale kwenye tume ya uchaguzi. Namna hii upinzani tayari hauna msimamo wa pamoja kwenye tume ya uchaguzi.

Halafu mambo ya uchaguzi unamuandikia rais na Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi ili afanyeje? Unadhani anaweza kukubali chochote kitakachoumiza chama chake?, Tume huru ya uchaguzi itapatikana kwa presha na sauti moja na siyo kubembeleza.
Zitto siyo mpinzani ni mjasiriamali wa siasa
 
Mnawasifia ccm kuwa kuna sehemu moja wameshinda kihalali, ila sehemu nyingine zote wameshinda kwa figisu, si ajabu hata hiyo sehemu waliyoshinda kihalali ni kwakuwa walijua lazima watawashinda, ndio maana wakajifanya wema, ila sehemu nyingine zote ambazo hawakuwa na uhakika ikabidi wafanye fitina kama kawaida yao.

Ngoja tuone kama hiyo barua yenu mliyoandika kwa huyo mama kama itakuwa na mwitikio wowote wa maana.
Haya haijabadilika na haitabadilika kwa kuandika barua. Barua ina ''brain prints'' zote za Zitto. Mahesabu yake ni 2025 waachiwe washinde vile viti vya Pemba vya jadi walivyoporwa na Magufuli na bara wapate viti vichache ili wawe chama kIkuu cha upinzani cha kuisindikiza CCM huku wakiteuliwa kwenye baadhi ya nyadhifa na ku-enjoy maisha.

Hata kuondoka kwa Maalim kutafanya chaguzi zisiwe tena na ushindani mkubwa kule Zenji. Ushindani mkali wa Zenji ulitokana zaidi na nia binafsi ya Maalim kukitaka kiti cha urais kuliko sera au mitazamo ya wananchi
 
Back
Top Bottom