Taazia: Dkt. Tamim Kutoka Kalamu ya Dkt. Dau

Taazia: Dkt. Tamim Kutoka Kalamu ya Dkt. Dau

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
TAAZIA: DR. TAMIM KUTOKA KALAMU YA DR. DAU GAZETI LA RAIA MWEMA

Tarehe 17 Mei 2024 Saa 1 asubuhi nimepokea simu kutoka kwa mwanangu Ahmed Dau. Wakati huo nilikuwa nipo safarini nchini Uturuki kuhudhuria Kongamano la 3 la Kimataifa kuhusu Halal Tourism ambapo niliombwa kuwasilisha mada kuhusu Halal Tourism in Tanzania.

Ujumbe wa mwanangu Ahmed ulikuwa mfupi. “Huku kumetokea msiba”. Kabla yajamaliza kunipa taarifa nikajua huo utakuwa msiba wa Dr Bushiri Salum Tamim. Nilijua kuwa ni Dr Tamim kwa sababu kabla sijasafiri, nilikwenda nyumbani kwake kumjulia hali kutokana na maradhi yake ya Saratani.

Katika mazungumzo yetu, kwa sauti ya chini kabisa akaniambia Jumatatu tarehe 6 Mei atakwenda hospitali ya Ocean Road kwa matibabu. Taarifa ya ugonjwa wake alinipa mwaka jana wakati alipokwenda India kwa matibabu ambapo madaktari wake walimwambia kuwa saratani imeshasambaa sana kiasi ambacho hawana tiba ya kumpa.

Dr Tamim kanipa taarifa hizo kwa sharti kuwa nisimwambie mtu yoyote hata miongoni mwa familia yake. Sababu yake kubwa ni kuwa nitawashituwa na kuwatia simanzi. Nami nikafanya hivyo hadi leo.

Mara tu baada ya kupata taarifa ya msiba, mambo mawili yakanijia haraka. Kwanza, nilijuwa kuwa watu wengi watatarajia niandike taazia ya Dr Tamim. Pili, niliingia unyonge mkubwa kukosa kumzika rafiki na ndugu yangu wa miaka mingi.

Nimeshawahi kuandika huko nyuma kuwa kazi ya kuandika Taazia si nyepesi. Ugumu wake unakuja kutokana na ukweli kuwa, kwa kawaida, mtu huandika taazia kwa mtu anayemfahamu na ni mtu wa karibu nae sana kama nilivyo mimi kwa Dr Tamim.

Mara chache ambazo nimeshawahi kuandika taazia hutarajia kuwa hiyo ndio itakuwa ya mwisho. Lakini Mwenyezi Mungu Ndie Mpangaji wa mambo yote. Ni yeye tu Ndie Anaejua nani katika waja wake atangulie na nani abaki.

Pili ilinijia hofu ya kushindwa kuhudhuria maziko yake kwani kwa kawaida yetu Waislamu, mtu aliyefariki alfajiri ya saa 10, ni dhahiri kuwa atazikwa siku hiyo hiyo saa 10 jioni. Nikakumbuka yaliyonifika wakati wa kifo cha Mzee Kitwana Kondo ambaye pamoja na wosia wake kuwa akitangulia yeye, mimi niwe mmoja kati ya watu 5 watakaoingia kaburini kumzika, sikuweza kufanya hivyo kwa sababu nilikuwa Malaysia na nisingeza kuwahi kuzika.

Nilimwomba sana Mwenyezi Mungu kuwa yasinikute yale yaliyonikuta wakati wa msiba wa Mzee Kitwana Kondo.

Nimemjua Dr Bushiri Salum Tamim tokea miaka ya 1980s mara tu baada ya kurudi kwenye masomo yake ya Udaktari nchini Urusi. Wakati huo, mama yake mzazi alikuwa anakaa Magomeni mtaa mmoja na nyumba ya marehemu mzee Dau.

Pamoja ya kuwa mara baada ya kurudi nyumbani alipangiwa kazi kwenye hospitali ya Wilaya ya Mahenge, kila alipokuja Dar es Salaam kumtembelea mama yake tulikuwa tunaonana na kuzungumza mengi.

Dr Tamim alikuwa mtu mwema sana. Mengi kuhusu wema wake ameshaandika ndugu yangu Mohamed Said. Mohamed ameelezea namna ambavyo Dr Tamim alikataa kujiunga kwenye mgomo wa madaktari wakati wa utawala wa Awamu ya Nne.

Sababu yake kubwa ilikuwa hawezi kuacha wagonjwa wanateseka kwa sababu tu ya maslahi madogo ya kazi. Binafsi nilipomuuliza na kutaka kujua Madaktari wenziwe watamuonaje ikiwa anaendelea kuhudumia wagonjwa wakati wao wamegoma.

Siku zote jibu lake lilikuwa “Hajji (kama alivyokuwa anapenda kuniita) sisi tumetoka kwenye familia za masikini. Hawa wagonjwa ambao watu wanawagomea ndio katika sisi masikini “.

Kauli hii ilithibitishwa na Sheikh Mahmud bin Sheikh Nurdin Hussein bin Sheikh Mahmud wakati wa kueleza wasifu wa Dr Tamim kabla ya swala ya maiti kwenye Msikiti wa Shaadhuly.

Sheikh Mahmud nae alitaka kujua kutoka kwa Dr Tamim sababu za yeye kutogoma kama walivyofanya madaktari wenziwe. Jibu lake lilikuwa Muhimbili ni Hospitali ya Rufaa na kuna wagonjwa waliokuja siku za nyuma na kupewa miadi (appointment) ambayo kwa bahati mbaya imeangukia siku hizo za mgomo. Iwapo atakataa kuwahudumia wagonjwa hao kwa sababu tu ya mgomo, na ikitokea bahati mbaya mmoja kati yao akapoteza maisha, yeye Dr. Tamim atakwenda kujibu nini siku ya hesabu mbele ya Allah?

Mwaka 1988 Dr Tamim alikwenda kufanyakazi kwa miaka miwili kwenye kisiwa cha Penrhyn, Cook Islands (visiwa vya Pasifiki). Wakati huo mimi nilikuwa masomoni Wellington, New Zealand.

Baada ya kumaliza mkataba wake alikuja Wellington kututembela mimi na familia yangu. Alikuja yeye, mkewe Bi Maryam na watoto wao wawili; Haytham aliyezaliwa Tanzania na Hawla aliyezaliwa Cook Island mwezi Septemba 1989.

Tulikaa nao Wellington kwa kıasi cha miezi 3. Kutokana na ucheshi, upole, msaada na wepesi wake wa kuamiliana na watu, ghafla Dr Tamim alikuwa maarufu kuliko mimi ambaye niliyekaa Wellington miaka 2.

Mara tu baada ya kupata taarifa za msiba na kuwafahamisha marafiki zetu wa New Zealand ambao baadhi yao wamehamia Sydney na Melbourne Australia, simu yangu imekuwa ikiita na kupokea salaam za rambi rambi kila dakika. Salaam zipo nyingi sana na siwezi kuzinukuu zote.

Baadhi ya salaam hizo zimesema:

“Bro I am very saddened by this news. He was such a nice and humble person. He came to visit me and brought me a mango from his tree if you recall. Also, he came to see me off when I was coming back to Sydney. May Allah SWT Grant him forgiveness and grant him Jannatul Firdous. Ameen. Please pass on my condolences to the family -Aniz“.

Kwa tafsiri isiyo rasmi:

“Ndugu, nimesikitishwa sana na taarifa hizi. Alikuwa mtu mzuri sana na asiyependa kujikweza. Alikuja kunitembelea na kuniletea embe kutoka kwenye mwembe wake kama utakumbuka. Pia, alikuja kuniaga wakati narudi Sydney. Namuomba Allah Amsamehe na Ampe Pepo ya daraja ya juu (Jannatul Firdous). Ameen. Naomba unifikishie rambirambi zangu kwa familia - Aniz.”

Mwengine aliandika:

“Innallillah wainnaillahi raajiuun. May Allah grant him a place in Jannah. Very nice humble man.”

“Kwake Ndiko tunakotoka na Kwake Ndio marejeo yetu. Namuomba Allah Ampe nafasi katika Pepo (Jannah). Mtu mzuri sana asiyependa kujikweza.”

Huyo ndio Dr Tamim. Miezi 3 tu aliyokaa Wellington mwaka 1990, ameacha athari ya kukumbukwa hadi leo, miaka zaidi ya 30 tokea aondoke New Zealand. Abraham Lincoln aliyekuwa Rais wa 16 Marekani alisema “In the end it’s not the years in your life that counts, it’s the life in your years“.

Kwa tafsiri ısiyo rasmi “mwisho wa yote, sio miaka uliyoishi ndio yenye tija, bali ni namna ambavyo umeishi kwenye hiyo miaka (umri wako). Dr Tamim ameiishi kauli ya Abraham Lincoln kwani ameondoka na kuacha alama kubwa itakayofanya endelee kukumbukwa na wengi sio tu Tanzania bali hata nje ya nchi kutokana wema wake.

Mchana wa siku hiyo hiyo ya msiba, mwanangu Ahmed kanipigia kuniarifu kuwa maziko ya Dr Tamim ni siku ya Jumamosi tarehe 18 Mei saa 7 mchana. Pale pale nikasema Alhamdullillah, dua yangu imejibiwa. Hivi niandikavyo nipo kwenye ndege ya Turkish Airlines tunapita anga ya Ethiopia kurudi nyumbani. In Shaa Allah tutatuwa saa 8 usiku na kuwahi Sinza kwenye msiba na hatimaye kumzika kaka na rafiki yangu wa muda mrefu.

Waswahili wasema kweli “kila mtu na mzishi wake”. Baada ya kufika mazikoni, nikaarifiwa kuwa mimi nimeteuliwa kuwa miongoni mwa watu 4 watakaoingia kaburini kumhifadhi Dr. Tamim!

Palepale nikakumbuka ule usemi wa Waswahili: “Ziada huwekwa kwenye fungu.”

Kwa Dr Tamim mimi nimepata kumzika na ziada ya kuingia kaburini.

Alhamdullillah.

Taazia hii nimeifanya kuwa fupi sana tofauti na zile nilizopata kuandika kwa sababu mbili.

Kwanza Wahariri wa magazeti wamekuwa wakilalamika kuwa Taazia zangu ni ndefu mno.

Pili mazingira ambayo niliyonayo wakati naandika taazia hii. Zaidi ya 99% ya Taazia hii (ukiacha ile sehemu ya msikitini na kaburini) nimeiandika kwenye ndege nikiwa narejea nyumbani kuwahi kuzika.

Buriani Dr Bushiri Salum Tamim. Dunia itakukumbuka kwa wema wako. Kwa hakika Tanzania tumempoteza Daktari mahiri na mzalendo wa kweli.

Itakuwa vyema iwapo Serikali itamtunuku nishani (posthumously) kwa uzalendo na ujasiri aliouonesha kwenda kuhudumia wagonjwa wakati Madaktari wengine wamegoma.

Allah Akupe kauli Thabit na In Shaa Allah Mwenyezi Atukutanishe Jannat Firdous tukiwa na familia zetu.

Amin.

Innallillahi wainnaillahi raajiuun.
 
Sh Mohamed
Mwenyeezi Mungu amsameh marehem makosa yake, Dr Tamim
Kama marehem Mzee wetu Maalim Ali Hassan Mwinyi aliwahi kusema “hakika maisha ni khadithi”, ikiwa unataka kusemwa kwa vizuri basi uwe na tabia nzuri
Pia kama alivyosema Dr Dau kuwa “sio miaka uliyoishi ndio yenye tija, bali ni namna ambavyo umeishi kwenye hiyo miaka (umri wako)”
Hakika kweli watu wa zamani walisema mauti ni somo kubwa kwa walio hai na kuhudhuria maziko ni elimu kubwa
Ahsante
 
Sh Mohamed
Hakika huwa ninakuwa na majonzi makubwa na kama ninaweza kulitumia neno “uchoyo” basi ningelitumia kwa kusema
Naona uchoyo kuona watu wanavyosemwa kwa mema yao, kila nikijitizama mimi sijui lipi nitakalosemwa nikiondoka duniani, hakika huwa na majonzi makubwa kila nikifikiri nitakapoondoka katika dunia hii
Mwenyeezi Mungu anajua zaidi
Mwenyeezi Mungu atupe mwisho mwema
 
Back
Top Bottom