TAAZIA: Sheikh Hassan Mnjeja maisha yake ndani ya historia ya warsha na BAKWATA

TAAZIA: Sheikh Hassan Mnjeja maisha yake ndani ya historia ya warsha na BAKWATA

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
TAAZIA: SHEIKH HASSAN MNJEJA NIMJUAYE

upload_2018-7-18_0-19-38.png

Sheikh Hassan Mnjeja

Leo katika Makaburi ya Kisutu tumemzika Sheikh Hassan Mnjeja.

Nimefahamiana na Sheikh Hassan Mnjeja miaka takriban 30 iliyopita pale nilipojiunga na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na kumkuta yeye akiwa Katibu Mtendaji wa Umoja wa Wanafunzi Waislam wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, maarufu kwa jina la MSAUD, yaani Muslim Student Association of the University of Dar es Salaam. Nilikuwa ikiwa siko ‘’Lecture Theatre,’’ maktaba basi nitakuwa MSAUD ofisini kwa Hassan Mnjeja. Ofisi hii ilikuwa pembeni mwa msikiti wa Chuo Kikuu na ndani ya ofisi ile kulikuwa na maktaba nzuri sana ya vitabu vya Kiislam. Nathubutu kusema kuwa hakuna maktaba nchi nzima inayoweza kushindana na maktaba hii kwa vitabu vya Kiislam.

Ikiwa Sheikh Sheikh Hassan hana kazi basi ataniingiza katika mazungumzo kuanzia siasa za dunia na Uislam hadi fikra nini tufanye kama vijana kuusukuma mbele Uislam juu ya vikwazo ambavyo Uislam ulikuwa unakutananavyo ndani na nje ya nchi. Miaka ile tatizo kubwa lilikuwa uongozi ndani ya BAKWATA. Ikawa sasa mimi nimepata mwalimu na si mwalimu tu bali ni mwalimu bingwa wa siasa za Uislam katika Tanzania na ulimwenguni na kwa hakika nilichuma mengi kwa Sheikh Mnjeja. Katika vitu vilivyoleta athari kubwa na kuifanya MSAUD iwike na ifahamike ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa wakati ule ni jinsi Sheikh Hassan Mnjeja alivyoweza kuwashirikisha wanafunzi wa zamani kujihisi wao bado ni wana – MSAUD ingawa wengi walikuwa tayari wametoka chuoni hapo miaka mingi. Hili la kwanza.

Jambo la pili ni jinsi Sheikh Mnjeja alivyoweza kuwavuta hata wale ambao hawakuwa wanafunzi popote wala hawategemei kuwa iko siku watakujakuwa wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hivyo kuwa wanachama wa MSAUD kuiona MSAUD kama taasisi yao. Katika kundi hili Sheikh Mnjeja aliwaleta karibu walimu wa madras za mjini na masheikh kutoka sehemu tofauti za Dar es Salaam na nje ya mipaka yake hadi bara kwenye miji mikubwa na midogo hadi vijijini. Ikawa MSAUD inatiwa nguvu kila upande kwanza na wanafunzi wenyewe waliopo chuoni, Ex-MSAUD yaani wanachama wa zamani wa MSAUD na masheikh na walimu wa madras na Waislam wa kawaida. Ikafikia hali watu wengi wakawa wanatoka mjini kuja kusali Ijumaa msikiti wa MSAUD. Ikitokea mtu katoka nje ya Dar es Salaam kaja Dar es Salaam basi ataweka katika mizunguko yake lazima afike MSAUD angalau kusalimia ikiwa hana shughuli rasmi. MSAUD ilikuwa na gazeti Al Islam ambalo lilipendwa sana.

Katika mazingira haya ndipo nilipoanza masomo yangu kwa mwalimu wangu Sheikh Mnjeja. MIaka hii ndipo pia nilipokuja kuwa karibu sana kufahamiana na vijana wengi wa Kiislam waliokuwa wakiutumikia umma kama Burhani Mtengwa, Mussa Mdidi, Uledi Kayemvya, Hamza Soko, Sheikh Mubarak, Ali Kilima, Saad Fungafunga, Prof. Hamza Njozi, Dk. Ramadhani Dau wakati huo anasoma American University, Cairo, kwa kuwataja wachache. Wahadhiri Waislam pale Chuo Kikuu kama Prof. Juma Kapuya, Dr. Ibrahim Lipumba, Dr. Ibrahim Msabaha walikuwa hawapungui katika ofisi za MSAUD. Nilijuana pia kupitia MSAUD na ofisi ya Sheikh Mnjeja na Mwalimu Said Ilyas ambae alikuwa akifundisha Shule ya Jabal Hiraa, Morogoro. Mwalimu Said Ilyas kila akija Dar es Salaam alikuwa hakosi kupita MSAUD kuonana na Sheikh Mnjeja. Mwalimu Said Ilyas alikuwa na uzoefu mkubwa sana katika elimu na kusomesha kwani kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar alikuwa mwalimu visiwani.

Katika ofisi hii ya Sheikh Mnjeja ndipo nilipokutana na kujuana na Sheikh Abdillah Nasir wa Mombasa wakati ule akiwa Katibu wa World Association of Muslim Youth (WAMY) iliyokuwa na makao yake makuu Nairobi. Chini ya uongozi wa Sheikh Mnjeja, MSAUD ilivuma ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Hassan Mnjeja aliiweka MSAUD karibu sana na mashirika ya Kiislam ambayo yalikuwa na ofisi zao Tanzania mathalan, World Muslim League (WML) maarufu kwa jina la Rabita, Africa Muslim Agency (AMA) na nyinginezo na aliimarisha uhusiano na taasisi kama International Islamic Thought Institute (IITI) na nyinginezo ambazo hizi zilikuwa zimejikita zaidi katika kueneza fikra na mafunzo ya Kiislam.

Siku moja katika mazungumzo Sheikh Mnjeja akaniambia maneno ya mwalimu wake Sheikh Hussein Malik, ‘’Mohamed ikiwa Waislam hawajui kuwa kuna dhulma basi hiyo dhulma haipo. Waelimishe wadhulumiwa waijue dhulma kisha ndiyo uwadaie haki zao, lakini ukianza kuwadaia haki zao ilhali wao wenyewe hawajua kama wanadhulumiwa wao watakuwa wa mwanzo kukupiga vita.’’ Sheikh Mnjeja akanieleza kuwa hayo ndiyo yalikuwa mafunzo ya Sheikh Malik kwa wanafunzi wake. Hili lilikuwa somo kubwa sana kwangu. Kauli hii Sheikh Mnjeja aliitoa katiwa wakati ambao ulikuwa Uislam ulikuwa unapitia kipindi kigumu sana. Miaka ile ya 1980 ilikuwa miaka ya changamoto zaidi kwa Waislam wa Tanzania kwa kuwa hapakuwezekana kwa Waislam kufanya lolote bila ya kupitia BAKWATA kupata idhini na wao walikuwa na kazi moja tu nayo ni kuzuia kila lilionekana litaunufaisha Uislam.

Lakini si kama Waislam walikaa hawafanyi mambo ya kupambana na dhulma hii, la hasha kulikuwa na harakati kubwa na za chini kwa chini zikiongozwa na Warsha kuwaamsha Waislam watambue hali iliyokuwa inawakabili ikafikia kipindi vijana wa Kiislam wengi wao kutoka MSAUD waliweza kujipenyeza na kuchukua uongozi ndani ya BAKWATA kwa nia ya kuigeuza sura na haiba yake. Vijana hawa walikuwa, Hassan Mnjeja, Burhani Mtengwa, Mussa Mdidi na Abbas Kilima kwa kuwataja wachache. Vijana wakiwa ndani ya BAKWATA walianzisha gazeti, lililoitwa, ‘’Muislam,’’ lililokuwa linatoka kila siku ya Ijumaa na walikuwa na kipindi cha Kiisam Radio Tanzania Dar es Salaam kila siku ya Ijumaa.

Vijana hawa wasomi walifanya utafiti ulioonyesha kuwa idadi ya vijana wa Kiislam Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam haijafikia hata asiliamia 10%. Taarifa ya utafiti huu ilisambazwa kwa Waislam wa Tanzania nzima na kwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati ule Bunge linakaa Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam. Taarifa hii ilipoenea na kuanza kusomwa, nchi nzima ilizizima kwani hapajatokeapo kitu kama hiki kufanyika na tatizo hili la elimu kwa vijana wa Kiislam kuwekwa bayana hadharani. Waislam walijiuliza baada ya kusoma utafiti ule iweje hali iwe hivi zaidi ya miaka 20 ya uhuru? Serikali ilipata mshtuko mkubwa. Haikuwa na majibu ya kuridhisha kwa Waislam. Kufuatia haya vijana wa Warsha wakazibadili shule za Kibohehe, Moshi na Shule ya Kinondoni, Dar es Salaam kuwa seminari isomeshe vijana wa Kiislam peke yao. Kipindi hiki shule hizi za Waislam zilianza kufanya vizuri katika mitihani na katika nidhamu pia.

Palitokea mntafaruku mkubwa ndani ya BAKWATA bila shaka uliosababishwa na utaiti ule wa elimu na Sheikh Mnjeja na wenzake walifukuzwa BAKWATA na mipango yote ya elimu iliyokuwa imewekwa na kuanza kutekelezwa ikawa ndiyo mwisho wake. Lakini kubwa ikatoka amri serikalini kuwa hawa vijana wasiachiwe kuongoza taasisi yoyote ya Kiislam. Mshauri mkuu wa Warsha na mwalimu wa akina Sheikh Hassan Mnjeja na wenzake akina akafukuzwa nchini kama, ‘’Prohibited Immigrant,’’ yaani muhamiaji asiyetakiwa.

Baada ya hayo serikali ikatoa amri kuwa shule hizo zirejeshwe kama hali yake ya zamani. Katika mkutano wa kujadili amri hii ya serikali uliofanyika Shule ya Kinondoni, kikao cha Waislam kikajiwa na askari wakiwa na amri kuwa mkutano uvunjwe na Waislam watawanyike. Aliyekuwa akiongooza kikosi hiki cha askari kutoka Kituo cha Polisi cha Oyster Bay alikuwa kijana wa Kiislam, Msafiri Himba. Himba alizungumza na Waislam kwa lugha ya kiungwana sana na bila vitisho. Marehemu Sheikh Abbas Kilima ndiye alikuwa akiongoza kikao hiki. Hawa walikuwa hakika waja wema wa Allah. Hawakukaidi walitii amri na kutafuta njia nyingine ya kukabiliana na changamoto hizi. Changamoto hizi ndizo zilizokuja kufanya Waislam wajenge Masjid Quba na Islamic Centre ambako ipo shule ya Kiislam iliyopewa jina Masjid Quba.

Miaka mingi baadae nilikutana na Himba na nikamuuliza kuhusu sakata lile la kuongoza askari kuvunja mkutano wa Waislam waliuokuwa wanajadili elimu ya watoto wao na hali yao ya baadae katika elimu. Jibu lake lilinitoa machozi. Himba alinambia, ‘’Mimi kama Muislam nilikuwa najua wanachokipigania watu wale ni haki ya kukataa dhulma na dua yangu ilikuwa Allah ajaalie wale viongozi wanisikilize wasikaidi amri ikabidi mimi niamrishe askari wangu kutumia nguvu kuwaondoa pale.’’ Ikumbukwe kuwa kipindi hiki Warsha ilikuwa kila Ijumaa ikisambaza misitini makala zilizoandikwa kwa umahiri mkubwa kuhus hali ya Waislam Tanzania na changamoto zao. Ujumbe ulikuwa unapenya na ukweli ukawa sasa uko wazi. Maneno ya Himba yalithibitisha ukweli huu.

Historia ya Masjid Quba ni historia tosha ya kueleza jitihada za Waislam katika kutafuta elimu na kujua juhudi walizofanya watu kama Sheikh Mnjeja. Baada ya shule kufunguliwa na watoto kuanza kusoma serikali ikakataa kuisajili. Hili lilikuwa pigo kubwa kwa Waislam. Vipi shule itakuwapo bila usajili? Wanafunzi watafanya vipi mitihani yao ikiwa shule haina usajili? Huu haukuwa mtihani kwa shule peke yake bali kwa wazazi pia. Wakati wa mgogoro wa kubadili shule za Kiislam kuwa seminari viongozi wa BAKWATA walisikika wakisema kuwa kama hao vijana wanataka kuwa na shule zao kwa nini hawajengi? Maneno haya waliyasema wakijua umasikini waliokuwanao hawa vijana kuwa hawawezi kujenga shule. Lakini shule kwa rehema za Allah ikajengwa sasa imewekewa vizingiti vya usajili. Hili halikuwakatisha tamaa shule iliendelea kusomesha bila ya usajili. Ilikuwa Prof. Malima alipokuwa Waziri wa Elimu mwaka wa 1987 ndiye aliyeipa Masjid Quba usajili.

Nilikuwa sichoki kumsikiliza Sheikh Mnjeja. Haya nilikuwa mimi nayapata katika vibaraza vya kahawa na katika misikiti yetu mjini. Nikiwa na Hassan Mnjeja nilikuwa sasa nasomeshwa na kuelezwa kila kitu kama kilivyokuwa na kilivyotendeka kwa majina ya wahusika wenyewe na kwa tarehe zake. Nilimuusudu Sheikh Mnjeja na kumpenda sana. Hakika niikuwa nimepata mwalimu. Ikawa Sheikh Mnjeja kunipa hiki kusoma kunipa kile nipitie kisha tukikaa ataniuliza na kutaka kusikia fikra zangu.

MSAUD ya Mnjeja ilifanya kazi kubwa kwa vijana wa Kiislam. Ilikuwa ukitoka pale baada ya kumaliza masomo unatoka si kama ulivyoingia. Unatoka mtu mpya na ukiwa kazini kila mtu atahisi utu na uungwana wako katika kazi kwani utaifanya ile kazi kwanza kwa kmridhisha Allah na pili kwa njia hiyo hata muajiri wako atafurahi kwa kazi yako. Aliwafunza vijana wengi kuwa vioo vya Uislam katika jamii.

Nilipokuwa mwanafuzni wa mwaka wa pili Mnjeja alipendekeza jina langu niwe katibu wa MSAUD. Siku moja Sheikh Mnjeja alinipa jalada akaniambia, ‘’Mohamed hebu msome Dk. Mayanja Kiwanuka msikilize anavyoileza historia ya BAKWATA.’’ Hii ilikuwa tasnifu yake: ''The Politics of Islam in Bukoba Districtí (1973),’’ katika kutunukiwa shahada ya pili. Ilikuwa wakati huu wa ndipo Sheikh Hassan Mnjeja aliponionyesha jalada la Mzee Bilal Rehani Waileka lililokuwa na nyaraka zote zinazohusu mgogoro wa EAMWS lililokuwa limehifadhiwa pembeni likionyeshwa watu makhsusi tu kisha likarudishwa na kuhifadhiwa.

Tasnifu hii ilivuruga akili yangu kwani ilikuwa historia iliyojaa uongo. Nilipokuja kuijadili na Sheikh Mnjeja alihisi ile hamaki yangu kwa kuona historia inapotoshwa. ‘’Sikiliza Mohamed, kukasirika hakusaidii kitu. Unapokutana na vitu kama hivi unafanya kama alivyofanya yeye, unaandika unajibu hoja kwa hoja. Huyu anatakia ajibiwe na watu wasome jibu lake kama wewe ulivyomsoma, lakini ghadhabu, zaidi sana zitaumiza nafsi yako.’’ Mjenja alikuwa na namna ya kuzungumza jambo zito na kubwa lakini kwa njia ya upole kama vile si kitu cha kukasirisha na hii nimeona kwa wanafunzi takriban wote wa Sheikh Malik.

Kwa hakika niliufuata ushauri wa Sheikh Mnjeja na nilikaa kitako kumjibu Dr. Mayanja Kiwanuka. Niiandika paper, ‘’ ‘’Islam and Politics in Tanzania.’’ Hii ‘’paper,’’ nilikuja mwaka wa 1989 kuiwasilisha kwenye mkutano Nairobi, ulioshirikisha wajumbe kutoka Kenya, Saudi Arabia, Sudan, Uganda, Malawi na Tanzania na Sheikh Mnjeja ndiye aliyeniteua nihudhurie mkutano ule. Siku moja Mnjeja kanipigia simu kuniomba tukutane tulipokutana akanifahamisha kuwa kuna mkutano Nairobi na angepanda mimi niende kuwakilisha nikatoe, ‘’paper,’’ kuhusu hali ya Uislam Tanzania.

Leo nikiangalia nyuma katika uhusiano wangu na Sheikh Mnjeja namshukuru Mungu kwa kunipa rafiki kama huyu na si hili tu bali naona Sheikh Mnjeja alitaka kunifundisha nije kuwa mwanafunzi mzuri na nitoe mchango wenye tija katika Uislam. Niliporudi kutoka Nairobi sikukaa sana Sheikh Mnjeja akanambia kuwa amependekeza jina langu kuhudhuria mafunzo ya uongozi, Khartoum Sudan. Nilihudhuria mafunzo haya na kwa hakika nilijifunza mengi.

Huwezi kummaliza Sheikh Mnjeja. Nimendika yake machache na nimeacha mengi. Mchango wake kwa Uislam Tanznaia ni mkubwa sana na naamini kama alivyonisomesha mimi aliwafunza wengi katika sisi vijana wa wakati ule mbinu za kufanyakazi katika kila namna ya hali.

Allah amsamehe makosa yake na amuweke mahali pema peponi.

Mohamed Said

17 Julai, 2018
 
Allah amuweke mahala pema panapolazwa wema..Ameen
 
Mzee Mohamed Said, naomba utupe historia ya Taasisi ya Balukta iliyokuwa chini ya uongozi wa Sheikh Yahya Hussein.
Madhumuni yake ya kuanzishwa na kwanini ilifutwa.
 
Mzee Mohamed Said, naomba utupe historia ya Taasisi ya Balukta iliyokuwa chini ya uongozi wa Sheikh Yahya Hussein.
Madhumuni yake ya kuanzishwa na kwanini ilifutwa.
Bujibuji,
BALUKTA iliundwa na Sheikh Yahya Hussein kwa ajili ya kuhifadhi Qur'an.
Sababu kwa nini ilifutwa sababu zake sijazijua kwa uhakika.
 
Innalillah wa Innaillahi Raajiuun,

Huyu sheikh Mnjeja ndiye wakati fulani alikua registrar wa Chuo Kikuu Cha Waislam Morogoro (MUM)?
 
Mohamed Said,

..POLE kwa kuondokewa na Mwalimu wako.

..Marehemu ni mzaliwa wa wapi?

..kabla ya kufika UDSM alipitia wapi?

..hapo UDSM alisomea fani gani?

..baada ya kuhitimu alifanya kazi wapi?

..binafsi ningependa kupata historia ya Sheikh Mnjeja kwa kirefu zaidi.
 
Kumbe Mzee Said ni alumni wa UDSM! Hongera sana na pole kwa msiba.

Vv
 
Kumbe Mzee Said ni alumni wa UDSM! Hongera sana na pole kwa msiba.

Vv
Vyama vingi,
Mimi ni wale wachache katika wengi.
Alhamdulilah.

Wenzangu wengi katika watoto wa Kariakoo hawakupata bahati hii.
 
Back
Top Bottom