Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
- Thread starter
- #21
JokaKuu,Mohamed Said,
..POLE kwa kuondokewa na Mwalimu wako.
..Marehemu ni mzaliwa wa wapi?
..kabla ya kufika UDSM alipitia wapi?
..hapo UDSM alisomea fani gani?
..baada ya kuhitimu alifanya kazi wapi?
..binafsi ningependa kupata historia ya Sheikh Mnjeja kwa kirefu zaidi.
Nishapoa.
Nakuwekea nyingine:
TAHARIRI, AL HUDA JULAI 19, 2018
Buriani Sheikh Hassan Mnjeja, mchango wa maandiko unabaki
Ni wachache katika chipukizi ya wanaharakati wa kiislamu wa leo wanaotambua kwamba, Bakwata miaka ya 1976 hadi 1980 ilikuwa na idara ya uandishi na uchapaji ikichapisha vitini vya elimu ya dini ya kiislamu, zama hizo ikiongozwa na marehemu Mtengwa Burhan mshiriki mwingine akiwa Saad Fundi.
Aidha ni wachache wanaofahamu kuwa, katika jitihada za kuwatumikia Waislamu na Uislamu, Mwanaharakati hatakiwi kuwa “mlalamikaji” au “mng’ang’anizi” bali awe mwenye unyumbufu wa kimkakati kuweza kufanya kazi na yeyote kwa lengo la kuupatia tija Uislamu akijiamini kuwa hakuna itikadi, taasisi au mtu yeyote anayeweza kupiku hazina ya mafunzo sahihi ya Uislamu na maadili yake.
Kwa ufahamu huu, Marehemu Mtengwa Burhan, Musa Mdidi na Hemed Slimu waliingia Bakwata wakishirikiana na marehemu Ahmad Mubaarak akiwa WARSHA pamoja na Mohmmed Kassim aliyekuwa Mkuu wa Shule ya Masjid Quba na mmoja wa waandishi wa vitabu vya mafunzo ya Uislamu vilivyokuwa vikichapishwa na WARSHA.
Kwa minajili hiyo, kuanzia mwaka 1982 hadi 1984 vijana hao walikuwa nguvu iliyomsaidia aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza hilo Sheikh Mohammed Ali al Bukhri hadi pale alipoondolewa nafasi hiyo kwa hila aliyekuwa katibu mkuu aliyemfuatia.
Vijana watatu, wakiongozwa na Mtengwa, wakiwa ndani ya Bakwata, walianzisha chombo cha habari, Gazeti la Muislamu sanjari jitihada nyingine ya kukumbukwa ambayo ni kuingiza somo la dini(Islamic Studies) kuwa moja ya masomo yaliyofunzwa na kufanyiwa mitihani kidato cha sita shule za serikali.
Marehemu Hemed Slimu Mwanaharakati mnyoofu asiyefahamika na wengi ambaye alikuwa mpiga chapa wa maandiko yote ya WARSHA ya waandishi wa kiislamu, MSAUD na Bakwata, alipata kutaja jina la Hassan Mnjeja kuwa ni mmoja wa wafasiri wazuri zama hizo.
Marehemu Slimu, ambae alifariki dunia mwaka 1988 na kuzikwa eneo la Magole nje kidogo ya mji wa Morogoro, alimsifu Hassan Mnjeja kuwa alifanya kazi nzuri kufasiri kitabu chenye maudhui yanayobeba moyo wa dini ya kiislamu.
Jumatatu ya Julai 16, 2018 ilikuwa siku ya kutimu kwa Qadari ya mfasiri huyo mkongwe, Sheikh Hassan Mnjeja innalillahi wainnailaihi raajiuun.
Mnjeja ameacha mambo ya kukumbukwa. Miaka mingi nyuma, “Jihad”, kwa wengi, ilifahamika kimakosa kama “Vita Vitakatifu”. Lakini Sayyid Abul ‘Ala Maududi, mwanazuoni mkubwa wa karne ya 20 nchini Pakistan na ulimwenguni kwa ujumla, alifanya kazi tukufu ya kusahihisha maana ya dhana ya Jihad.
Kitabu chake Jihad in Islam, kina maudhui ya kufutilia mbali fikra potofu zilizoizingira dhana hiyo kwamba Jihad ni mapambano ya silaha, au ni lipualipua ya mabomu ya kujitoa muhanga, au ni kunoa majambia na mapanga kuwakata shingo wapinzani wa Uislamu!
Maududi akarekebisha mtazamo huo kwa kuainisha kuwa Jihad ni jitihada yoyote aifanyayo mtu kwa sura ya utumishi wa kumtumikia Mungu ndani ya muktadha wa Uislamu. Hivyo basi, kushika kalamu, kufundisha, na kadhalika ni miongoni mwa mambo yanayotimiza ainisho la Jihad.
Al-marhum Maududi aliandika Kitabu chake kwa Lugha yake ya Kiurdu, wanafunzi wake nao wakakitafsiri kwa Kiingereza. Ni almarhum Hassan Mnjeja aliyefanya kazi muhimu ya kuleta maudhui ya Kitabu hicho katika tafsiri ya Kiswahili.