MAHUDHURIO hafifu ya mashabiki katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa baina ya Taifa Stars na Brazil uliofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam Juni mwaka huu yameleta mageuzi mapya kwenye masuala ya viingilio hapa nchini.
Mchezo huo wa Juni uliohudhuriwa na mashabiki kiduchu tofauti na wengi walivyodhania Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilipanga kiingilio cha juu Sh 200,000 na cha chini ni Sh 30,000.
Kwa kawaida michezo mingi inayofanyika kwenye uwanja huo, kiingilio cha juu huwa ni Sh 50,000 wakati kile cha chini huwa ni Sh 3,000 ama Sh 5,000, lakini wakati huo TFF ilisema kulingana na gharama kubwa za kuileta Brazil nchini ndio sababu waliweka viingilio vikubwa.
Jana TFF ilitangaza kuwa mchezo wa Jumamosi ijayo kati ya Taifa Stars na Morocco utakaofanyika kwenye uwanja huo kuwania kufuzu fainali za Afrika mwaka 2012 kiiingilio cha juu ni Sh 30,000 wakati cha chini ni Sh 5,000 na hiyo ni kutokana na fundisho walilopata kwenye mechi ya Stars na Brazil.
Mechi ya Stars na Brazil viingilio ilikuwa Jukwaa la Viti Maalum A (VIP A) Sh 200,000, VIP B Sh 150,000, VIP C Sh 100,000.
Jukwaa la Rangi ya Chungwa Mkabala na VIP Sh 80,000 na Jukwaa la Rangi ya Chungwa nyuma ya magoli shilingi 50,000 na Jukwaa la Rangi ya Bluu Mzunguko pamoja na Jukwaa la rangi ya kijani sehemu hizo ilikuwa Sh 30,000.
Kwa mazingira hayo mashabiki wa soka wenye vipato vya chini maarufu kama wenye uchungu na mpira walitakiwa kujikamua zaidi ili wafike uwanjani, lakini walikwama matokeo yake waliangalia kupitia televisheni zaidi, hivyo uwanja ukajaa wenye nacho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Rais wa TFF Leodegar Tenga alisema kitendo cha kupandisha kiingilio cha chini katika mechi ya Stars na Morocco kutoka Sh 5,000 hadi Sh 30,000 kiliwatenga wapenzi wengi wa soka na kuwa matokeo yake viti vingi vilibakia wazi.
Tenga alisema hali hiyo haitotokea tena katika michezo ijayo ya kimataifa na kuwa ana matumaini viingilio vilivyotangazwa jana vitakuwa nafuu kwa mashabiki.
Kwa upande wake Ofisa Habari wa TFF, Florian Kaijage alitaja viingilio hivyo kuwa ni Sh 30,000, Sh 20,000, Sh 15,000, Sh 7,000 na Sh 5,000.
Alieleza kuwa Morocco inatarajiwa kuwasili kesho saa nne usiku na kuwa mchezo huo utachezeshwa na waamuzi kutoka Mauritius ambao ni Sochurn Raji, Botun Barkishna na Vally Vivian, wakati Kamishina atakuwa Mohammed Aziz kutoka Kenya.
Rekodi ya juu ya mapato yanayotokana na viingilio iliwekwa Septemba mwaka 2007 kwenye uwanja huo huo, wakati wa mchezo wa mwisho wa kuwania kufuzu fainali za Afrika kati ya timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' na Msumbiji, ambapo kiasi cha Sh 605,020,000 kilipatikana kati ya Sh 644,530,000 zilizotarajiwa kupatikana.
Kulikuwa na upungufu wa Sh 39,510,000 uliotokana na viti 1,612 ambavyo tiketi zake zilidaiwa hazikuuzwa. Kiingilio kilikuwa Sh 50,000, Sh 40,000, Sh 30,000 Sh 20,000, Sh 10,000 na Sh 3,000.
Lakini rekodi hiyo ilivunjwa Juni katika mchezo wa Stars na Brazil ambapo kiasi cha Sh bilioni 1.6 kilipatikana.
Uwanja huo una uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 walioketi kulingana na takwimu zilizotolewa mwaka 2007 na aliyekuwa Mkurugenzi wa Michezo, Henry Ramadhan, siku chache kabla ya mchezo wa Taifa Stars na Msumbiji.
Kama mambo yangeenda kama TFF ilivyopanga kwenye mchezo wa Stars na Brazil ingevuna zaidi ya Sh bilioni 2.7, kwani kwa kiingilio cha Sh 200,000 kwa jukwaa kuu A (VIP), ambalo lina viti 748, zingepatikana Sh 149, 600,000.
Jukwaa B kiingilio cha Sh 150,000 na kuna viti 2,260 zingepatikana Sh 339,000,000, huku Jukwaa Kuu C kwa kiingilio cha Sh 100,000 na kuna viti 2,404 zingehifadhiwa Sh 240,400,000.
Jukwaa la rangi ya chungwa linaloangalia jukwaa kuu kwa kiingilio cha Sh 80,000 na kuna viti 6,460, kiasi cha Sh 516, 800,000 kingepatikana, huku majukwaa ya nyuma ya magoli, ambapo kiingilio ni Sh 50,000 na kuna viti 7, 300 zingepatikana Sh 365,000,000.
Jukwaa la bluu mzunguko lenye viti 18,364 kiingilio cha Sh 30,000 zingepatikana Sh 550,920,000, wakati jukwaa G ambalo lina viti 19,590 linalojulikana pia kama jukwaa la kijani, ambalo ndilo Watanzania walio wengi hujihifadhi hapo kwa kiingilio hicho cha Sh
30,000 basi zingevunwa Sh 587,700,000.
Kama zingeuzwa tiketi zote kiasi cha 2,749,420, 000 kingepatikana, ambapo kihesabu ni sawa na kusema Sh bilioni tatu.
Lakini kwa vile wangekuwepo watu wachache wangeingia bure kutokana na sababu mbalimbali, inawezekana labda kungekuwa na upungufu wa Sh milioni 200.