Nadhani tuwe fair, tuseme JK hajatimiza ahadi zake kwa x% ambayo hiyo x ni kubwa kulizo 0%. the moment unavyosema hajafanya chochote (yaani 0%)... yet kuna
habari kama hii..yeyote anayefanya hivyo anaonekana ana matatizo.
Habari yenyewe kwa wenye uvivu wa ku-click link.
UDOM ni matunda ya ahadi ya JK
RAIS Jakaya Kikwete leo anatimiza miaka minne tangu alipoingia Ikulu, ana kila sababu ya kujivunia utekelezaji wa ahadi zake ikiwemo ya kuratibu mchakato wa kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM).
Ni chuo cha aina yake nchini chenye eneo kubwa ambalo si rahisi kutembea kwa miguu na kulimaliza kwa vile lina ukubwa wa ekari 15,000.
Shughuli za awali za chuo zilianza katika jengo mashuhuri la CCM la Chimwaga, ambalo pia wakati fulani lilikusudiwa kuwa jengo la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwandishi wa makala haya alipotaka kufahamu wapi lilipotoka wazo la kuanzishwa kwa chuo kikubwa namna ile, Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Idris Kikula anasema:
Sisi ni wanataaluma, tumeandika kitabu kuhusu uanzishwaji wa Udom ambamo tumeeleza kwamba suala zima la Udom limetoka kwa Rais Jakaya Kikwete katika kampeni zake.
Ingawa haikuainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, lakini katika kampeni zake, aliahidi kuanzisha chuo kikubwa kama atashinda uchaguzi na kweli ametekeleza ahadi yake ambayo haikuwa kwenye Ilani ya Uchaguzi.
Rais Kikwete amenipa ushirikiano mkubwa na anaendelea kufanya hivyo katika kuhakikisha kuwa Udom inafikia malengo yake na kinakuwa chuo cha mfano nchini, ndiyo maana unaona maendeleo haya ya majumba, mandhari na maelfu ya wanachuo, hadi ametuunganisha na kampuni ya IBM ya Marekani. Nitakueleza mengi, yote ni kazi ya Rais Kikwete.
Profesa Kikula anasema Rais Kikwete ametoa ruhusa kwa Udom kutafuta wahadhiri ndani na nje ya nchi, ambapo hadi sasa chuo kimepata 19 kutoka India; Urusi na Cuba, na zimekubali kutoa walimu na hivi karibuni wataajiriwa.
Kutokana na ruhusa hiyo, Udom inaajiri wahadhiri wa muda kutoka nje ya nchi wenye sifa ya kufundisha, akiwamo Mwenyekiti wa Baraza la Udom, Dk. Mohamed Gharib Bilal ambaye ni gwiji wa Fizikia.
Yeye anafundisha kwa muda chuoni hapo. Watanzania wengine wenye sifa pia wanakaribishwa kufundisha kwa muda.
Katika kuonesha busara zake, Rais Kikwete ametekeleza ahadi ya kujenga chuo kikuu kwa faida ya Taifa na anasimamia ahadi yake hiyo kwa nguvu zake zote, tena katika mazingira magumu ya kutokuwa na fedha za kuendeshea mradi huu mkubwa nchini.
Mkuu wa Udom ni Rais mstaafu Benjamin Mkapa, wakati Mwenyekiti wa Baraza la Udom ni mwanasiasa msomi na Dk Bilal ambaye pia ni Waziri Kiongozi mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Udom haina mfano wa kulinganishwa nao nchini na hata Afrika Mashariki kwa sababu nyingi tu, lakini Profesa Kikula anasema ndicho chuo kikuu pekee nchini ambacho kimeanzisha mafunzo ya Shahada za Lugha za Kijapani, Kikorea na Kichina.
Kama vile haitoshi, Udom ndicho chuo kikuu pekee nchini chenye mfumo wa utawala wa makao makuu na kuwa navyuo huru vinavyojitegemea ambavyo vinaratibiwa na ofisi ya makao makuu. Tayari vipo vyuo viwili na taasisi mbili, vyote vikitoa shahada, lakini lengo ni ifikapo mwaka 2012 chuo kiwe na vyuo sita vitakavyoratibiwa na ofisi ya makao makuu, anasema Profesa Kikula.
Lengo la chuo kikuu cha Udom ni kwamba ifikapo mwaka 2012 kiwe na uwezo wa kudahili wanafunzi 40,000 wa shahada mbalimbali.
Hadi sasa kuna jumla ya wanachuo 7,305 na kati yao, wanachuo 2,158 ni wanawake sawa na asilimia 30 ya wanachuo wote wa Udom hadi Julai mwaka huu. Kufikia Oktoba, idadi ilitarajiwa kuongezeka hadi 10,000 na kuifanya Udom kufikisha wanachuo 17,305.
Hiyo ni habari maalumu, anasema Baltazaar, ambaye ni Ofisa Uhusiano wa Udom. Profesa Kikula anasisitiza kuwa hii ni historia kubwa na ya kwanza kutokea, na kuongeza:
Rais Kikwete atabaki katika vitabu vya kumbukumbu nzuri milele ya watu mashuhuri waliotoa mchango usiosahaulika kukuza elimu kwa kuzingatia mlolongo wake tangu msingi, sekondari na chuo kikuu.
Maneno haya yanatoa changamoto kwa watu makini, kupima ukweli na uongo kwa vile utekelezaji unaonekana kwa macho na wala si kwa ramli ya mganga wa kienyeji.
Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza anayetoka Kigoma, Vumi Omari anayechukua Shahada ya Biashara, anasema mjadala wa madai kuwa JK kashindwa kazi, waachiwe watoto wa wakulima wanaosoma Udom ambao watachambua pumba na mchele kwa wazazi, walezi, marafiki na jamii kwa jumla warudipo likizo na wakati mwafaka ukifika.
Chuo pia kimewezeshwa kuwa kituo cha Uenezi wa Taaluma ya Mawasiliano (IT) Tanzania, ambayo ni muhimu katika maendeleo ya kisiasa. Kutokana na jitihada za Rais Kikwete, chuo kimepata wataalamu kutoka kampuni ya IBM, Marekani.
Hapa ndipo lile suala la kulaumu safari za Rais nje ya nchi linapopatiwa jibu, kwamba Udom ina kituo chenye hadhi ya kutoa shahada za taaluma ya mawasiliano ambayo kinapata msaada wa kitaaluma ya mawasiliano kutoka IBM, mabingwa wa IT wa Marekani.
Tungepataje misaada hiyo haraka hivyo kama si kwa Rais mwenyewe kujishughulisha? Huu ni upande wa pili wa sarafu, hasa kwa wale wachache wanaodai Serikali ya Awamu ya Nne haijafanya kitu.
Kinachotakiwa kwa watu hao ni kuwaeleza kwa takwimu ili kubainisha kwamba wanayosema si sahihi na kwa yeyote anayepinga na aende Udom akaone maendeleo ya elimu ya juu.
Katika hali ambayo haikutarajiwa kabisa katika chuo chochote nchini, Udom imejipambanua vilivyo kwani hadi Julai mwaka huu, kimefundisha shahada mbalimbali 56 na lengo lake ni kutoa shahada 63 ifikapo mwaka 2012.
Haya ni maendeleo makubwa. Udom sasa ina vyuo vinne: Chuo cha Sayansi za Jamii na Lugha, Chuo cha Elimu, Chuo cha Sayansi za Kompyuta, na Chuo cha Sayansi Asilia na Hisabati.
Katika jitihada za kukabiliana na tatizo la walimu wa shule za sekondari hususani za kata, hadi Julai mwaka huu Udom ilikuwa na wanachuo 4,000 wanaosomea Shahada ya Ualimu. Udom pia imewezesha kuajiriwa wahadhiri wapatao 300 wakiwamo wa muda na watumishi wengine 200 wameajiriwa.
Shughuli za ujenzi wa chuo katika kipindi cha kati ya mwaka juzi na mwaka jana, zimewezesha kuajiriwa vibarua zaidi ya 10,000, anasema Baltazar.
Ili kujitosheleza kwa mahitaji ya wahadhiri, Udom inafundisha walimu wake ndani na nje ya nchi katika ngazi za Shahada za Uzamili na Uzamivu (PhD). Katika hali isiyokuwa ya kawaida, muundo wa Udom ni tofauti.
Katika eneo la chuo lipo kwa ajili ya shughuli za kitaaluma tu na wafanyakazi wote wanakaa nje ya chuo, na huu ndio mpango mkakati wake unavyoelekeza na kutenganisha maeneo ya vyuo vyake mbalimbali.
Kwa mujibu wa Profesa Kikula, mpango mkakati umeelekezwa pia katika kukifanya chuo kuwa kituo cha utalii mjini Dodoma na kwamba mkandarasi ameshapatikana wa kuweka mandhari itakayokifanya kufikia lengo hilo.
Kila mwanafunzi ana kitanda chake na amewekewa nafasi ya kusomea bila msongamano. Chumba kimoja kikubwa kinalaza wanafunzi wanne, kila mmoja akiwa na sehemu yake ya kusomea na kuweka kompyuta kwa ajili ya huduma za mtandao chumbani.
Kwa chuo kinachojengwa kwa thamani ya Sh bilioni 772.8, kati ya bajeti hiyo, tayari ujenzi umegharimu karibu nusu ya fedha hizo yaani Sh bilioni 300. Kwa mujibu wa utafiti, Udom imebadili shughuli za kiuchumi Dodoma ambazo sasa zimeshamiri.
Soko la Dodoma limekua na kuongeza shughuli mbalimbali za kibiashara tofauti na zamani ambapo tegemeo kubwa lilikuwa shughuli za Bunge ili kuboresha biashara, anasema Musa Jama, mwandishi mkongwe na mwakilishi wa Radio Uhuru mjini Dodoma.
Hivyo ujio wa Udom umekwenda sambamba na Ilani ya Uchaguzi katika kukuza uchumi, kupambana na umasikini na kutoa ajira, kwani magari mengi yamepata kazi ya kupeleka wafanyakazi na wanafunzi chuoni na kuwarejesha mjini.
Vifaa vya kuandikia na huduma mbali mbali hali kadhalika zimeongezeka, kama vile vyakula katika migahawa ya kawaida vinauzika.
Udom imechangamsha Dodoma, anasema mkazi wa barabara ya Saba, Joseph Mazengo. Pamoja na mafanikio yote hayo, Profesa Kikula anasema changamoto kubwa ya Udom hivi sasa ni uchanga wa chuo unaokifanya kuwa na uhaba wa walimu, ikifuatiwa na uhaba wa nyumba za walimu ukiwamo ukosefu wa nyumba ya hadhi kwa Makamu Mkuu wa Chuo na watumishi.
Changamoto nyingine ni upatikanaji wa maji safi, wingi wa wanachuo, miundombinu ya kutupa majitaka ya chuo na wizi.
Profesa Kikula anavishukuru vyombo vya habari nchini kwa kukitangaza vyema Chuo Kikuu cha Dodoma na kuwezesha mwaka juzi kupokea maombi ya udahili 15,000 na mwaka jana maombi 19,000 na mwaka huu maombi 29,000.
Udom itaanzisha shahada ya Taaluma ya Habari na Mawasiliano na Umma muda si mrefu, ujao ambao Profesa Kikula hakupenda kutoa tarehe rasmi.