TAJ MAHAL(taji la ikulu) ni mfano thabiti wa uhandisi wa kale wa himaya ya Mughal,mchanganyiko wa mitindo ya kiujenzi ya Kiindi,Kiajemi na Kislamu na moja ya kazi safi ya Mhandisi Ustad Ahmad Lahauri, Mhindi mwenye asili ya Kiajemi. Ili kukamilisha kazi hii waashi,wachongaji,wapaka rangi,wachoraji na wataalam wengine wengi wa masuala ya ujenzi na uwekaji nakshi walikusanywa kutoka sehemu mbalimbali za himaya ya Mughal,Asia na Uajemi.
Upekee wa TAJ MAHAL upo katika uhandisi uliotumika na dhamira kuu ya ujenzi wake. Eneo kubwa la ekari 12 limebeba geti kuu la kuingilia,bustani nzuri yenye bwawa la kutengeneza na mifereji ya maji,huku jengo kuu lililohifadhi makaburi mawili ya mtawala Shah Jahan na malkia Mumtaz Mahal likiwa katikati ya majengo mengine mawili yanayofanana,moja kila upande,moja likiwa msikiti na jingine nyumba ya wageni ambayo pia huitwa jawab.Jengo hili huitwa jawab ikiwa na maana ya jibu,sababu limejengwa ili kuleta mlingano wa kiuhandisi likiwa linafanana Kila kitu kwa nje na msikiti ambao upo upande mwingine.Inaaminika kwamba jengo hili lilijengwa ili kuhifadhi wageni waliokuwa wanafika kutoa heshima katika kaburi la malkia Mumtaz.
Taj Mahal inachukuliwa kama kilele cha mafanikio ya kiuhandisi ya tamaduni za Kiindi na KIislam.Utaalam wa hali ya juu umetumika kusanifu majengo,kuyaweka katika mpangilio mzuri,kuyajenga na kuyapamba kwa nakshi mbalimbali zilizoleta mvuto wa kipekee kwa vizazi vilivyodumu mpaka leo .Bustani na majengo yote katika eneo hili,kuanzia geti kuu,jengo lililohifadhi makaburi na majengo pacha ya msikiti na nyumba ya wageni yamepangiliwa katika namna ya kipekee kiasi kwamba unaweza kukata katikati na kupata sehemu mbili zinazofanana kwa kila kitu. Kuta za nje za TAJ MAHAL ni tofali zilizonashkiwa kwa marumaru zilizosuguliwa haswa,kuta hizi hubadilika rangi na uvuli kulingana na mng’ao tofauti wa mwanga wa jua na mwezi.Nyumba ya wageni au jawab na msikiti vimejengwa kwa marumaru na mawe mekundu ambayo huyapa majengo haya muonekano wa rangi nyekundu. Ujenzi wa TAJ MAHAL ulichukua miaka 22 kukamilika. Ujenzi ulifanyika kwa awamu,awamu ya kwanza inakadiliwa kuchukua miaka 12 ilihusisha jengo kuu lililobeba makaburi. Ujenzi wa majengo pacha ya msikiti na nyumba ya wageni uliendelea kwa miaka 10 mpaka kukamilika kwake mwaka 1653. Mwishoni mwa karne ya 19 chini ya serikali ya kikoloni ya uingereza TAJ MAHAL ilifanyiwa marekebisho makubwa baada ya kuanza kuchakaa. Katika kipindi hiki Bustani ya TAJ MAHAL ilibadilishwa kuwa katika muonekano wa kizungu unaoonekana leo.
Japokuwa TAJ MAHAL ilijengwa ili kuhifadhi mwili wa malkia Mumtaz,mwili wa Mtawala Shah Jahan ulikuja kuhifadhiwa humo mwaka 1666 baada ya kifo chake.
Licha ya kusimama kwake kwa miaka mingi,TAJ MAHAL imepata maadui wengi katika vipindi tofauti tofauti. Mwaka 1942 wakati wa vita ya pili ya dunia serikali ililazimika kuiwekea TAJ MAHAL nguzo za miazi ili kuwapoteza marubani wa ndege za kivita za Kijapan kupata muonekano tofauti kutokea angani. Mbinu hiyo ilikuja kutumika tena mwaka 1965 na 1971 wakati wa vita kati ya India na Pakistan. Uchafuzi wa mazingira ndio adui wa sasa,mto Yamuna unaopakana na TAJ MAHAL unasaidia kusogeza uchafu karibu na kusababisha mvua za tindikali. Uchafuzi wa mazingira umeanza kubadili rangi ya asili ya TAJ MAHAL. Kupambana na uchafuzi huu serikali ya India imetenga eneo lenye kilometa za mraba 10,400 kuzunguka TAJ MAHAL lenye masharti makali yenye kuilinda.
TAJ MAHAL inahesabiwa kama moja ya majengo mazuri kuwahi kutokea katika uso wa Dunia. Mwaka 2020 gharama za ujenzi wa TAJ MAHAL ilikadiliwa kuwa ni dola za kimarekani bilioni 1,zaidi ya trilioni 2 kwa shilingi za Kitanzania. Ni moja kati ya maajabu saba ya Dunia. Mwaka 1983 shirika la umoja wa mataifa la sayansi na utamaduni UNESCO liliitambua TAJ MAHAL kuwa sehemu ya urithi wa dunia. Takwimu za mwaka 2014 ilikadiliwa watalii milioni 7 mpaka 8 walitembelea TAJ MAHAL,ni moja kati vyanzo vikubwa vya mapato kupitia utalii nchini India.
TAJ MAHAL ni lile taji la malkia,kuta za marumaru zilizosimama kuelekea anga la nchi ya India. Ni alama inayoishi ya upendo wa dhati wa kale. Ushahidi usio na shaka wa kilele cha mafanikio ya zamani ya sanaa na uhandisi.
Makala hii imeandaliwa kutoka katika vyanzo mbalimbali mitandaoni.