a) Umiliki wa Katiba
Katika kutizama dhana ya umiliki wa Katiba kama tulivyoona hapo juu, ili kupata uhalali wa Katiba [Legitimacy of Constitution] ni lazima Wananchi wawe wamiliki Katiba hiyo. Swali la msingi linaloibuka ni kuhusu jinsi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 ilivyotungwa na ikiwa wananchi wa Tanzania walishirikishwa katika kuitunga. Kisha ni vema kutizama ikiwa wananchi wanaifahamu Katiba yao. Jambo lingine la msingi ambalo husahaulika mara kwa mara ni kuhusu nafasi ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 katika Muungano.
b) Umiliki wa Taifa
Tarehe 9 desemba 2010 ambayo ilikuwa ni sikukuu ya kukumbuka Uhuru wa Tanganyika, kaulimbiu ilikuwa ni kudumisha uzalendo. Uzalendo wa kweli na wa dhati huzaliwa, kujengwa na kudumishwa pale ambapo kuna heshma misingi ya usawa na wananchi kuwa na nafasi katika kumiliki raslimali za nchi. Swali linalozuka mara nyingi hutokana na wananchi kuhoji mara kwa mara ‘serikali ni nini?' ila inayoitwa mali ya ‘umma' kwa kawaida huwa ni ya nani? Ikiwa wawakilishi wa wananchi [Bunge] hawana ruhusa ya kuona [mathalan] mikataba ya nchi na wawekezaji, mfano mikataba ya madini, n.k swali linabaki je, "Umma ni nani?'
Matabaka yanayojengeka katika jamii kutokana na mfumo mpya wa elimu unaoifanya elimu kuwa bidhaa badala ya haki ya msingi; afya na huduma za kijamii nazo kukosa udhibiti wa kutosha huku walio wengi wakikosa huduma muhimu na wachache kuwafaidi yote haya ni mazingira ya kuua na kudidimiza uzalendo katika taifa.
c) Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Katika kipengele hiki kumekuwa na utata mkubwa zaidi. Kumekuwa na hoja nyingi na maswali mengi ambayo hayajajibiwa. Kuhusu Bunge la Muungano kutunga sheria zisizokuwa na nguvu Zanzibar, kuhusu wabunge toka Zanziba kushiriki katika kutunga sheria zinazohausu mambo yasiyo ya muungano, n.k. Pili maswali mengine yamehoji Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo haina mamlaka ya kisheria kufanya shughuli zake Zanzibar hata kama ni kuhusu swala la Muungano, na nafasi ya Mahakama ya Rufani hasa baada ya Mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 yaliyofanywa na Baraza la wawakililishi Mwaka 2010. Sura nzima ya Nne ya Katiba ya Sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepitwa na wakati na inapaswa kwafanyikwa marekebisho makubwa ikiwa ni pamoja na kutambua nafasi ya Makamo wa Kwanza na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
d) Ushiriki wa Wananchi Katika Uongozi wa Nchi
Miongoni mwa changamoto nyingine za msingi ni suala zima la ushiriki wa wananchi katika uongozi wa nchi. Hii ni pamoja na kuhoji usahihi wa mfumo mzima wa uchaguzi, uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, na mamlaka ya Mahakama katika kuhoji na kuamua kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais. Hoja ya ushiriki ikienda mbali zaidi inahoji ikiwa kweli kuna demokrasia kwa kuwanyima wananchi nafasi ya kuchaguliwa ikiwa hawapendelei kujiunga na chama fulani cha siasa. Suala la Mgombea huru nalo limetia dosari hata Uhuru wa Mahakama pale ambapo Mahakama ya Rufani ilipoacha kutumia mamlaka yake kisheria ya kutafsiri sheria na badala yake kuliachia Bunge. Katiba haitoi nafasi ya jinsi ya kuiwajibisha Mahakama pale inapoacha kutumia mamlaka iliyopewa.
e) Uhusiano Kati ya Dola na Mwananchi
Mwananchi wa kawaida hujiuliza mara kwa mara je ni nini wajibu wa polisi na Askari mgambo? Je haki ni nini na mahakama ni chombo cha namna gani? Maswali yote haya yanamwelekeo wa kuashiria kwamba wananchi wanahoji imani yao kwa vyombo vya utendaji haki. Kwa sababu hiyo tatizo la wananchi kujichukulia sheria mikononi linaendelea kuwepo kutokana na [pamoja na sababu nyingine] wananchi kutokuwa na imani na vyombo vya utoaji haki. Katiba haijaweza kutoa majibu kuhusu hali ya uadui/uhasama unaoendelea kujengeka kati ya vyombo vya dola na raia.
f) Haki za Binadamu
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kwa mara ya kwanza ilitoa ulinzi kwa baadhi ya haki za binadamu mwaka 1984 na zikaanza rasmi kutekelezwa mwaka 1988. Hata hivyo, haki za binadamu katika Katiba bado hazina ulinzi wa utosha. Kwa upande wa Zanzibar Kwa Mfano, Baraza la Wawakilishi kwa sasa haliwezi kubadili kifungu chochote cha haki za binadamu mpaka tu pale amabapo ridhaa ya wananchi kupitia kura ya maoni itakuwa imepatikana. Pamoja na kuwepo kwa ibara zinazotoa ulinzi kwa haki za binadamu, Katiba ya Tanzania bado ni dhaifu katika kuzilinda, na wakati mwingine katiba hiyo hiyo ina ibara zinazopingana. Ibara ya 30 ya Katiba inaruhusu uvunjaji wa Haki uendelee hata baada ya hukumu ya mahakama hadi pale bunge litakapokuwa limetunga sheria husika au muda utakaokuwa umetolewa na Mahakama.
g) Dira/Lengo Mahsusi la Taifa
Ibara ya 3 ya Katiba inasema kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia nay a kijamaa isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi. Lengo la Ibara hii ilikuwa ni kutoa taswira na mwelekeo wa Taifa la Tanzania. Hata hivyo mwelekeo huu ni potofu kutokana na sera kinyume za ubinafsishaji na mfumo wa soko huria. Kwa sasa swali linalojengeka ni kuhusu mustakabali wa taifa la Tanzania, je ni wapi tunataka kwenda kama taifa? Kukosekana kwa lengo Mahsusi au Dira ya Taifa kunasababibishwa na Katiba iliyopo. Ibara ya 9 inasisitiza utekelezaji wa misingi ya kijamaa ambayo ni kuweka njia kuu zote za uchumi mikononi mwa umma, pia ibara ndogo ya (c) inasema kuwa shughuli za serikali zinatekelezwa kwa njia ya ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa taifa unaendelezwa , unahifadhiwa, na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa ujumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine, haya yote yamepuuzwa na kuifanya Katiba iliyopo kuonekana kuwa imepitwa na wakati, bado haitoi jibu la swali linaloulizwa sasa, Je, ni nini dira ya Taifa la Tanzania?