TAKUKURU yautambua mchango mkubwa wa JamiiForums katika kuendeleza mapambano dhidi ya Rushwa nchini

TAKUKURU yautambua mchango mkubwa wa JamiiForums katika kuendeleza mapambano dhidi ya Rushwa nchini

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
Salaam Wakuu,

TAKUKURU yautambua mchango mkubwa wa JamiiForums pamoja vyombo vya habari Nchini katika kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa nchini. Tukio hilo limefanyika leo 28 Januari Jijini Dar Es Salaam wakati wa Uzinduzi wa Chaneli mpya ya TAKUKURU TV ya YouTube.

Tukio lhili imeambatana na ugawaji wa vyeti kwa JamiiForums na vyombo vya habari kama shukuruni na kutambua mchango wao katika kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa nchini.

IMG_20210128_171406_405.jpg

Mkurugenzi wa Elimu wa Umma, Bw, Joseph K Mwaiswelo amesema kwamba anatambua kwamba Vyombo vya Habari ni mdau muhimu na kiungo kikuu kati ya Taasisi ya TAKUKURU na jamii ya Watanzania. Bila vyombo vya habari, Jamii haiwezi kufahamu rushwa ni nini na madhara yake kwa jamii ni yapi, hata ione umuhimu wa kuchukua hatua kuikabili.

Kasema sasa TAKUKURU imeingia YOUTUBE kwa kuanzisha TAKUKURU TV. Juhudi zote hizi zinafanyika ili kuhakikisha mwananchi anafikiwa kadiri ya njia iliyo rahisi kwake kuitumia au kufikiwa na kumshirikisha katika mapambano dhidi ya rushwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig. Jen. John Mbungo amesema wanazuoni hudai kuwa ‘kalamu, wakimaanisha maandiko au maandishi, yana nguvu kuliko upanga’(the pen is mightier than the sword). Sisi wote ni mashahidi wa nguvu ya ‘kalamu’ ya mwanahabari inavyoweza kutumika kushawishi au kuchochea watu kufanya kazi za maendeleo. Hili limefanyika sana nchini Tanzania.

Ni kwa sababu ya kutambua mchango wa vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya rushwa nchini, leo TAKUKURU tumeona tuwatunuku vyeti (certificate of appreciation), kama ishara ya kutambua na kuthamini mchango wenu katika mapambano dhidi ya rushwa.

Tunaamini vyeti hivi vitawahamasisha zaidi kuendelea kuzingatia weledi na uzalendo kwa kuwakumbusha kuwa Mkakati wa Kitaifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji (NACSAP) unamtaka kila mdau, vikiwemo vyombo vya habari, kushiriki kikamilifu katika kuzuia na kupambana na rushwa.

Hapa chini ni Hotuba Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig. Jen. John Mbungo

========
HOTUBA YA MKURUGENZI MKUU WA TAASISI YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA (TAKUKURU) BRIGEDIA JENERALI JOHN J. MBUNGO WAKATI WA HAFLA YA UZINDUZI WA TAKUKURU TV NA KUKABIDHI VYETI KWA VYOMBO VYA HABARI ILIYOFANYIKA DAR ES SALAAM,

JANUARI 28, 2021


Wakurugenzi wa TAKUKURU, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Habari, Viongozi na watumishi wenzangu wa TAKUKURU, Ndugu WanaHabari, Mabibi na Mabwana, Habari za asubuhi.

Mosi, naomba nitumie fursa hii adhimu kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uhai na afya na kutuwezesha kukutana mahali hapa siku ya leo.

Pili, nitumie pia fursa hii kuwashukuru kwa kukubali wito wetu wa kujumuika nasi siku ya leo. Karibuni hapa katika jengo ofisi ya TAKUKURU mkoa wa Dar es Salaam (PCCB HOUSE). Tunatambua mna majukumu mengi ya kila siku lakini mmetenga muda wa kuwa nasi hapa. Mmetupa heshima kubwa nasi tunawashukuru.

Ndugu Wageni Waalika, Mabibi na Mabwana, Leo tumekusanyika hapa kwa ajili ya matukio mawili muhimu.

La kwanza: Ni la kutambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kuendeleza - mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Sisi kama TAKUKURU, tunatambua, tunathamini na tunawashukuru wanahabari kwa kuwa nasi wakati wote wa mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Tukio la pili: Ni la kuzindua chaneli ya televisheni mtandaoni ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Chaneli hii inaitwa TAKUKURU TV, ambayo lengo lake kuu ni kuuhabarisha umma na watanzania kwa ujumla, juu ya dhamira ya Awamu ya Tano ya uongozi wa Mhe. Rais, na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Jemedari katika Mapambano dhidi ya Rushwa, lakini pia utekelezaji wa ILANI ya Chama cha Mapinduzi katika kutokomeza Rushwa, Ufisadi, Uonevu na dhuruma kwa wananchi wanyonge nchini. Kama inavyofafanuliwa na SURA ya sita (6), aya ya 113,114 na 115 naomba ni nukuu aya ya 113.

“Mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ni suala muhimu kwa kuwa athari zake ni kubwa katika harakati za kufikia maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Endapo suala la rushwa litaendelea kutokuchukuliwa hatua stahiki, juhudi za kujenga uchumi imara ambao utachangia kupunguza kiwango cha umasikini wa wananchi hazitoweza kuzaa matunda. Chama Cha Mapinduzi kwa kutambua umuhimu wa kutokemeza adui rushwa na ufisadi, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015-2020), kiliisimamia Serikali kuendeleza vita dhidi ya rushwa na ufisadi kwa kuchukua hatua mbalimbali na kupata mafanikio makubwa.

Hatua hizo Ni pamoja Na kuendelea kuimarisha vyombo vinavyohusika Na vita dhidi ya rushwa Na ufisadi, hususan Taasisi ya Kuzuia Na Kupambana Na Rushwa Na ufisadi nchini Kwa kufungua Ofisi mpya 21 katika Wilaya zote ambazo hazikuwa Na Ofisi za TAKUKURU….”
Mwisho wa kunukuu.

Ndugu Wageni Waalika, Mabibi na Mabwana, Najua si jambo rahisi kwangu ambaye sio mwanahabari kwa taaluma kuongea nanyi ‘lugha moja’. Si jambo rahisi. Ila naamini angalau naweza kubadilishana nanyi uzoefu kidogo kuhusu nguvu ya tasnia ya habari katika maisha ya kila siku ya mwanadamu na jamii kwa ujumla.

Ndugu Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Waandishi Melvin L. DeFleur na Everette E. Dennis katika kitabu kiitwacho Understanding Mass Communication toleo la nne cha mwaka 1991, waliandika kuhusu tukio moja lililohusisha kituo cha redio cha CBS nchini Marekani. Waliandika hivi:

“Oktoba 30, 1938, viumbe hatari kutoka sayari ya Mars viliivamia Marekani na kuua mamilioni ya watu kwa kutumia mionzi. Hivi ndivyo walivyoamini watu karibu milioni sita waliosikiliza kipindi kiitwacho ‘Mercury Theater of the Air’ kupitia kituo cha redio cha CBS jioni ya siku hiyo.

* Kipindi hicho kilihusu igizo lakini kiliwasilishwa katika hali ya uhalisia kama vile ni taarifa ya habari.

* Wasikilizaji wengi waliochelewa kuanza kusikiliza kipindi hicho na hivyo kukosa maelezo ya mwanzo kuwa lilikuwa ni igizo, walidhani ni taarifa ya habari.

* Watu walipatwa na hofu; baadhi walisali, wengine walijificha, wengine walilia au kukimbia.

* Ingawa hakuna mtu aliyekufa, maelfu ya watu katika Marekani walijiona wajinga pale walipokuja kugundua kwamba lile lilikuwa igizo.

* Baada ya wiki kadhaa, kituo cha redio cha CBS kilikabiliwa na kesi za madai zilizofikia karibu USD dola 750,000.

* Ilidaiwa kipindi hicho kiliwasababishia baadhi ya wasikilizaji majeraha, kuharibika kwa mimba na madhara mengine…”
Mwisho wa kunukuu maelezo hayo.

Ndugu Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Je, kwa nini nimerejea tukio hilo? Nimefanya hivi ili, kama nilivyosema awali, nibadilishane nanyi uzoefu kidogo kuhusu nguvu ya tasnia ya habari. Mtakubaliana nami kuwa vyombo vya habari ni nyenzo thabiti ya mawasiliano. Mawasiliano hayo yanaathiri kwa urahisi na haraka mawazo, mitazamo, matendo na tabia za watu. Athari hiyo inaweza kushuhudiwa na kipindi hicho cha kituo cha redio cha CBS.

Hii ndio maana baadhi ya wanazuoni hudai kuwa ‘kalamu, wakimaanisha maandiko au maandishi, yana nguvu kuliko upanga’. Najua msemo huu mnaufahamu zaidi kwa lugha ya kiingereza, yaani ‘the pen is mightier than the sword’ kwani unahusu zaidi taaluma ya habari.

Sisi wote ni mashahidi wa nguvu ya ‘kalamu’ ya mwanahabari inavyoweza kutumika kushawishi au kuchochea watu kufanya kazi za maendeleo. Hili limefanyika sana nchini Tanzania. Pia sisi ni mashahidi wa jinsi gani ‘kalamu’ hiyo ilivyotumika katika baadhi ya nchi kushawishi au kuchochea chuki, mifarakano, fujo na hata mauaji

*TAKUKURU tunatoa Rai kwenu wanahabari, mtumie vyema na kwa usahihi kalamu zenu katika kutuunganisha kuwa wamoja, kutushawishi tudumishe amani, kuchochea maendeleo na kuhamasisha kuendelea kupambana na maovu ikiwemo rushwa.

Ndugu Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Ni kwa sababu ya kutambua mchango wa vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya rushwa nchini, leo TAKUKURU tumeona tuwatunuku vyeti (certificate of appreciation), kama ishara ya kutambua na kuthamini mchango wenu katika mapambano dhidi ya rushwa. Tunaamini vyeti hivi vitawahamasisha zaidi kuendelea kuzingatia weledi na uzalendo kwa kuwakumbusha kuwa Mkakati wa Kitaifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji (NACSAP) unamtaka kila mdau, vikiwemo vyombo vya habari, kushiriki kikamilifu katika kuzuia na kupambana na rushwa.

Awamu ya Tatu ya Mkakati huu (NACSAP) katika ukurasa wa 55 inataja ‘Majukumu ya Vyombo vya Habari’. Moja kati ya majukumu matano yaliyotajwa ni ‘kukuza na kufuatilia maadili ya jamii kitaifa kama njia ya kupambana na rushwa na makosa mengine nchini’. Niseme kwa uwazi kabisa, jukumu hili mmelitekeleza vizuri.

Vyombo mbalimbali vya habari vya redio na televisheni, ikiwemo televisheni mtandaoni, vimeandaa na kurusha vipindi vya kuhamasisha jamii kukabili tatizo la rushwa. Jambo hili limefanywa pia na magazeti na blogu mbalimbali ambazo zimechapisha habari na makala zinazohimiza mapambano dhidi ya rushwa.

Sisi katika TAKUKURU ni mashuhuda wakubwa wa jinsi vyombo mbalimbali vya habari vilivyotupa nafasi ya kuelimisha umma kuhusu mapambano dhidi ya rushwa au kusambaza taarifa kuhusu juhudi za Serikali na wadau kuzuia na kupambana na rushwa. Hakika hamjatuacha kila tulipohitaji uwepo wenu katika mikutano na vyombo vya habari kama mlivyofika leo. NDIYO MAANA TUNAWASHUKURU SANA NA KUTAMBUA JUHUDI ZENU.

Ndugu Wageni Waalika, Mabibi na Mabwana, Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma ameeleza ni kwa namna gani TAKUKURU inaelimisha umma kwa madhumuni ya kuushirikisha katika mapambano dhidi ya rushwa. Tumetumia njia nyingi kama semina, mikutano na wananchi, mijadala na hata vyombo vya habari.

Njia hizi kwa muda mrefu sasa zimesaidia sana kuuelimisha umma na kuuhamasisha ushiriki mapambano dhidi ya rushwa. Pia zimekuwa njia nzuri za kupata mrejesho wa kile tunachowaelimisha wananchi na wakati mwingine chanzo kizuri cha taarifa za vitendo vya rushwa.

Kwa kuzingatia Mkakati wa Mawasiliano wa TAKUKURU (PCCB Communication Strategy) unaohimiza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), tumeanzisha TAKUKURU TV. Tunaamini, kupitia chaneli hii inayopatikana katika mtandao wa YOUTUBE tutawafikia wanajamii wengine wanaotumia zaidi mitandao. Leo kupitia hadhara hii nitazindua rasmi TAKUKURU TV. Kauli mbiu ya chaneli hii ni ‘TAKUKURU TV, RUSHWA NI ADUI WA HAKI.’

Ndugu Wageni Waalika, Mabibi na Mabwana, Kupitia TAKUKURU TV tutatoa elimu na habari kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali, TAKUKURU na wadau wengine kuendeleza na kuimarisha harakati za kuzuia na kupambana na rushwa nchini.

Elimu hiyo itagusia pia historia ya mapambano hayo ili umma ufahamu tumetokea wapi, tupo wapi na tunaelekea wapi katika kuhakikisha rushwa inadhibitiwa.

Pia tutaelimisha kuhusu maana ya rushwa, makosa ya rushwa kisheria na madhara ya rushwa kwa mtu, jamii na Taifa.

Tutaelimisha juu ya manufaa ya kuzuia na kupambana na rushwa, wajibu wa wadau na jinsi ambavyo kila mmoja wetu, taasisi au jamii anavyoweza kushiriki kukabili tatizo hili.

Ni matarajio yetu kuwa elimu hiyo itamhamasisha kila mmoja wetu kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa kwa maendeleo ya Tanzania.

Naomba nitumie fursa hii kuwaomba wamiliki, viongozi wakuu na wahariri wa vyombo vya habari kutupa ushirikiano katika kufanikisha uendeshaji wa chaneli hii pale tutakapohitaji msaada kutoka kwenu kama vile kupata video clips au kufanya mahojiano nanyi.

Pia nitumie fursa hii kuwaomba wanajamii wote nchini wenye nafasi ya kutumia mtandao kufuatilia kazi zetu za uelimishaji kupitia TAKUKURU TV na kushiriki katika vipindi mbalimbali pale tutakapowafikia kwa lengo hilo.

Aidha, namkumbusha kila mtumiaji kubofya neno ‘SUBSCRIBE’ anapotembelea TAKUKURU TV kwa mara ya kwanza. Hatua hii itamwezesha awe anapata taarifa kuhusu vipindi vyetu kila tunapoviweka mtandaoni.

Ndugu Wageni Waalika, Mabibi na Mabwana, Baada ya kusema hayo, nipo tayari sasa kukabidhi vyeti vya kutambua mchango wa vyombo vya habari katika kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa nchini na baada ya hapo kuizindua TAKUKURU TV.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.​
 
Wangefuta zile kesi zote za jamii forums na member wake ndio ntaona wanamaanisha kitu wakiendelea kuwa mahakamani kwa kesi za jamiiforums na huku wanatoa vyeti hakuna maana hapo...
Mkuu, nadhani haufuatilii. Hakuna kesi ambayo Takukuru wameishitaki Taasisi ya Jamii Forums, Mfanyakazi wake wala Mwanachama wa JamiiForums.
 
Back
Top Bottom