Sam Gidori
Senior Member
- Sep 7, 2020
- 165
- 417
Baada ya kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona duniani mwanzoni mwa mwaka jana, dunia ilianza kutafuta chanjo, na hadi kufikia mwishoni mwa mwaka, kampuni kubwa tano za Pfizer-BioNTech, Moderna, AstraZeneca na Johnson & Johnson zilikuwa zimetengeneza chanjo za kukabiliana na ugonjwa huo.
Ufanisi wa Chanjo
Licha ya baadhi ya chanjo kuonesha mafanikio katika kupambana na virusi hivyo, kama chanjo ya Pfizer-BioNTech iliyotengenezwa na kampuni za Ujerumani na Marekani, baadhi ya chanjo zilitajwa kusababisha madhara kwa watumiaji wake ikiwa ni pamoja na kuganda kwa damu.
Ulimbikizaji wa Chanjo
Changamoto nyingine ni kukosekana kwa usawa katika ugawaji wa chanjo, mataifa yenye uchumi mkubwa yakijizolea kiwango kikubwa cha chanjo kuliko mataifa maskini. Wakati tayari zaidi ya dozi bilioni 3 za chanjo ya corona zikiwa zimeshatolewa duniani mpaka sasa, ni asilimia 0.9 pekee ya dozi hizo zimewafikia watu wanaoishi katika nchi zenye uchumi mdogo.
Takwimu za chanjo kutoka Our World in Data zinaonesha kuwa baadhi ya nchi zimejilimbikizia chanjo zaidi ya mahitaji yake. Mfano, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ndio unaoongoza duniani kwa kuwa na malimbikizo makubwa ya chanjo, ukiwa na wastani wa dozi 155 za chanjo kwa kila watu 100, Visiwa vya Malta vikiwa na dozi 130 kwa kila watu 100, Bahrain ikiwa na dozi 129 kwa kila watu 100 huku Israel na Chile zikiwa na dozi 119 kwa kila watu 100 kila mmoja.
Wakati huohuo, katika nchi za Afrika, taifa la Mauritia ndilo linalojitutumua kwa kuwa na kiasi kikubwa zaidi cha dozi kwa ajili ya wananchi wake, ikiwa na dozi 56 kwa kila watu 100, ikishika nafasi ya 49 duniani, Morocco ikiwa na dozi 52 kwa kila watu 100, ikishika nafasi ya 52 duniani, Guinea ya Ikweta ikiwa na dozi 19 kwa kila watu 100 duniani, ikishika nafasi ya 98, huku Tunisia na Visiwa vya Cape Verde vikiwa na dozi 15 kwa kila watu 100, vikishika nafasi za 103 na 105 kila mmoja duniani.
Nchi za Canada, Uingereza, Israel, Italia, Ujerumani na Marekani zimefanikiwa kutoa angalau dozi moja ya chanjo kwa zaidi ya asilimia 50 kwa wakazi wake, huku barani Afrika kwa ujumla, utolewaji wa chanjo ni chini ya asilimia 1 kwa wakazi wote.
Mpango wa COVAX
Kwa kuona uhitaji wa kuzisaidia nchi zenye kipato kidogo kupata chanjo, mpango wa chanjo wa COVAX ulianzishwa, ikisimamiwa na Taasisi tatu (CEPI, GAVI na WHO) kwa lengo la kufanikisha usambazaji wa Vifaa Tiba vya kukabiliana na Corona, ikiwamo chanjo.
Nchi 172 tayari zimejiunga na mpango huu duniani, huku nchi tajiri zikichangia gharama kuzisaidia nchi 92 zenye uwezo mdogo kifedha. Barani Afrika, mataifa mawili tu ya Burundi na Eritrea ndiyo ambayo bado hayajajiunga na mpango huo. Lengo la mpango wa COVAX kwa Afrika ni kutoa dozi bilioni 2.6 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2022 ili wakazi wote bilioni 1.3 wa bara hili waweze kupata dozi mbili kila mmoja.
Mpaka sasa, ni dozi milioni 53 pekee ndizo zilizoweza kutolewa barani Afrika, idadi hiyo ikiwa sawa na dozi zote zilizotolewa nchini Uturuki pekee.
Mgawanyo wa Chanjo
Mpaka sasa, dunia imeshuhudia utengenezwaji wa aina 17 tofauti za chanjo, zote zikiwa na lengo la kuisaidia kinga ya mwili kupambana na virusi vinavyosababisha homa kali ya mapafu.
Chanjo hizo ni pamoja na Oxford-Astrazeneca ambayo inatumika katika nchi 178 duniani, Pfizer-BioNTech, inayotumika katika nchi 106 duniani, Moderna ya Marekani inayotumika katika nchi 55 duniani, Gamaleya (Sputnik V) ya Urusi inayotumika katika nchi 46 duniani na Sinopharm ya China inayotumika katika nchi 35 duniani.
Kati ya chanjo zote 17, chanjo 9 zinatumika barani Afrika, chanjo ya Oxford-Astrazeneca ikiwa inatumika kwa zaidi ya asilimia 74 katika nchi zote za Afrika, ikifuatiwa na chanjo ya BBIBP-Corv ya China, ikitumika katika nchi 14.
Chanjo zingine zinazotumika ni Pfizer-BioNTech (9%), Moderna (5%), Gamaleya au Sputnik V ya Urusi (14%), Sinopharm ya China (9%), Sinovac (12%), Bjarat Biotech ya India (1%) na Johnson & Johnson kwa asilimia 3.