Wakuu,
Kuna taarifa inayosambaa kwenye Makundi sogozi na Mitandao ya kijamii ikieleza kuwa TAMISEMI imetoa waraka unaopendelea wasichana kwenye upangaji wa nafasi Shule za kidato cha 5 tofauti na Wanaume.
Kama mdau wa Elimu, naomba kufahamu usahihi wa Taarifa hii.
Kuna taarifa inayosambaa kwenye Makundi sogozi na Mitandao ya kijamii ikieleza kuwa TAMISEMI imetoa waraka unaopendelea wasichana kwenye upangaji wa nafasi Shule za kidato cha 5 tofauti na Wanaume.
Kama mdau wa Elimu, naomba kufahamu usahihi wa Taarifa hii.
- Tunachokijua
- Ofisi ya Rais TAMISEMI (OR-TAMISEMI) ni miongoni mwa Wizara Kongwe Nchini zilizoanzishwa mara baada ya kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika, mnamo mwaka 1961 ikiwa na dhima ya Kuwa Taasisi inayoongoza katika kuwezesha Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.
Majukumu ya OR-TAMISEMI
Majukumu ya OR-TAMISEMI yanatekelezwa katika ngazi ya Makao Makuu, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Kwa kuzingatia Hati ya Rais ya Mgawanyo wa Majukumu (Presidential Instrument) iliyotolewa na Rais Aprili 2016, majukumu ya OR-TAMISEMI ni pamoja na:-
- Kuratibu utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Mijini na Vijijini na Upelekaji wa Madaraka kwa Umma (D by D);
- Kuratibu huduma mijini kama vile usafirishaji, maji na usafi wa mazingira;
- Kusimamia Tume ya Utumishi wa Walimu;
- Kuratibu na Kusimamia Tawala za Mikoa ili ziweze kuziwezesha Halmashauri kutekeleza wajibu wake;
- Kuratibu Usimamizi na Uendeshaji wa Shule za Msingi na Sekondari nchini kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM);
- Kujenga uwezo wa watumishi wa OR-TAMISEMI ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi; na
- Kusimamia utendaji wa Mashirika, Taasisi, Programu na miradi iliyo chini ya OR-TAMISEMI.
Kwa kurejea hati ya mgawanyiko wa Majukumu iliyotolewa na Rais kama ilivyoelezwa hapo juu kwenye jukumu la 5, Wizara hii inayo Mamlaka kisheria ya kutekeleza hoja inayotajwa na mdau.
Usahihi wa Waraka husika
Baada ya kufuatilia suala hilo, JamiiForums imebaini kuwa taarifa hiyo haina ukweli.
Aidha, madai haya yanakanushwa pia na Barua Rasmi ya OR TAMISEMI iliyotolewa Mei 25, 2023 ambayo sehemu ya maneno yake inasema;
“Taarifa hiyo siyo ya kweli na haijatolewa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI. Taarifa ya upangaji wa wanafunzi wa kidato cha Tano kwa mwaka 2023 bado haijatolewa na hadi sasa hakuna mwanafunzi yeyote aliyekwishapangiwa shule.”
Sehemu nyingine ya barua hiyo inawasihi wazazi na walezi kuipuuza taarifa hiyo na waendelee kuwa na subira. Taarifa itakapokamilika itatolewa na Waziri mwenye dhamana kupitia vyombo vya habari na itapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI pamoja na mitandao ya kijamii.
JamiiForums inatoa wito kwa wadau wote wa Elimu kupata taarifa sahihi wanazohitahi kuhusu Upangaji wa Shule za Sekondari kwa wanafunzi kupitia tovuti Rasmi ya Wizara ambayo ni www.tamisemi.go.tz au kwa kuwasiliana na Kituo cha huduma kwa wateia cha Ofisi ya Rais- TAMISEMI kwa namba za simu 026 2160210 au 0735 160210.