SoC01 Tamthilia za kutoka Ng'ambo: Tujihadhari, tupo kwenye vita vya kiutamaduni

Stories of Change - 2021 Competition

Bishop Hiluka

JF-Expert Member
Joined
Aug 12, 2011
Posts
7,147
Reaction score
14,699

Tangazo la tamthilia ya Sultan toka Uturuki

MWAKA 2010 nilifanya mawasiliano na kampuni ya Sony Pictures yenye makao yake Los Angeles (Culver City) nchini Marekani. Sony Pictures ni kampuni kubwa ya burudani huko Hollywood iliyoanzishwa Agosti 7, 1991 baada ya kujitenga kutoka kampuni ya Columbia Pictures Entertainment.

Kampuni hii inafahamika kwa filamu zake kama The Karate Kid, Ghostbusters, Spider-Man, Men in Black, Underworld, Robert Langdon, The Smurfs, Sniper na nyingine nyingi.

Niliwasiliana na Sony Pictures kuwataarifu kuhusu utitiri wa DVDs za filamu za Hollywood zinazorudufiwa kiharamia toka nchini China na kisha kusambazwa katika kila kona ya Afrika Mashariki na kuwataka wachuke hatua. Walichonijibu Sony Pictures ni kwamba, hawajali kuona filamu zao zikisambaa kama nilivyoeleza maana walikwisha pata faida maradufu kupitia box office na kusambaa kwa DVDs kunawasaidia kuwatangaza zaidi!

Hapo ndipo shaka yangu ilipoanzia, maana sababu kubwa ya kuwasiliana na Sony Pictures ilikuwa ya msingi kutaka kunusuru soko la filamu zetu kwa kuwa filamu za nje zilikuwa zinaingizwa kinyemela na hazilipi kodi huku wasanii wetu wasio na mitaji wala dhamana katika taasisi za kifedha wakibanwa kulipa kodi bila uhakika wa soko lao.

Miaka michache tu baada ya mawasiliano yangu na kampuni ya Sony Pictures nikaanza kushuhudia hali ikianza kubadilika kutoka uharamia wa filamu kwenye DVDs hadi mashindano ya kurusha filamu na tamthilia zilizotafsiriwa kwa Kiswahili kwenye vituo vyetu vya runinga.

Sekta ya televisheni duniani ni sehemu muhimu sana ambayo haiwezi kukosekana katika maisha ya kila siku ya mtu, iwe mtu huyo anamiliki seti ya runinga au la. Kwa kutazama vipindi mbalimbali vya runinga mtu huweza kufahamu mambo mengi makubwa yanayoendelea nchini na hata nchi za nje, na kwa kutazama runinga unapata burudani za kila aina.

Tanzania na Ukuaji wa Sekta ya Digitali: Changamoto na fursa

Japo sekta ya televisheni nchini inakabiliwa na fursa nzuri ya maendeleo kutokana na dunia kuingia zama za dijitali lakini pia ina changamoto kubwa.

Kwa upande mmoja, maendeleo ya haraka ya dijitali yameiletea sekta hiyo fursa nzuri ya kujiendeleza, na kwa upande mwingine, aina za uenezi wa habari zimekuwa nyingi, kwa mfano, televisheni mtandao, simu za mkononi zinaendelea haraka na makundi mengi ya runinga ya nchi za nje yameingia kwenye soko la televisheni nchini. Hali hii imesababisha shinikizo kubwa kwa sekta ya televisheni na filamu nchini.

Ili kuongeza nguvu za ushindani sekta ya televisheni nchini lazima iendeleze ubunifu bila kusita, ndipo inapoweza kukidhi mahitaji ya watazamaji yanayoongezeka siku hadi siku, na kuwavutia wawekezaji wa matangazo ya biashara. Pamoja na aina mbalimbali za uenezi wa habari zinavyoendelea haraka na kuwa nyingi, sekta ya televisheni nchini inakabiliwa na shinikizo kubwa la ushindani.

Hadi kufikia Mei 2021, kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) tunavyo vituo 48 vya televisheni vilivyopewa leseni, kati ya hivyo, vituo vinavyorusha matangazo bure (Free-To-Air) ni 27, na ndiyo miongoni mwa vinavyoangaliwa zaidi. Pia tuna vituo vingine kama Cable TV (15), satellite TV (3), Pay DIT (3) na televisheni mtandao 451.

Vipindi vya televisheni hutiliwa maanani sana kwa kuwa taarifa zake huambatana na picha hai za matukio, hivyo katika hali ya ushindani kama huu vipindi vyote vinavyotangazwa katika vituo vya televisheni lazima viwe na mvuto mkubwa na wakati wote na vinapimwa kwa ‘idadi ya watazamaji’ ili kuhakikisha vipindi vinavyorushwa ni bora.

Ndiyo maana mara kwa mara hutokea ushindani mkubwa sana kwa vituo vya televisheni kugombea kurusha matangazo ya mashindano ya soka kama Kombe la Dunia au Ligi za Soka za Ulaya, kwa kuwa matangazo haya hupata watazamaji wengi kuliko matangazo mengine.

Vipindi vya burudani huvutia watazamaji wengi na matangazo mengi ya biashara. Kwa sasa vituo vyote vya televisheni vinajitahidi kuwa na vipindi mbalimbali vya burudani: tamthilia, drama na vichekesho ili kuwavutia watazamaji.

Lakini kutokana na athari ya vipindi vya televisheni vya nchi za nje, sekta ya televisheni nchini iliyoanza kujitafutia uhai na maendeleo, imejikuta ikiingia kwenye shinikizo la mazingira ya utandawazi wa duniani, na taratibu imeanza kumezwa na utamaduni wa kigeni.

Katika miaka ya karibuni, sekta ya televisheni nchini imekabiliwa na ushindani mkubwa zaidi, vituo vya televisheni nchini vinakabiliwa na changamoto kubwa kutoka vipindi vya televisheni vya nje. Watu sasa wametekwa kuangalia vipindi mbalimbali kutoka nje, kwa mfano, matangazo ya moja kwa moja ya Ligi Kuu ya Uingereza, tamthilia, filamu, na picha za katuni na maonesho ya mambo mbalimbali.

Tunaweza kujifunza kutoka kwa wenzetu

Hivi sasa ukiangalia kwenye vituo vyetu vya runinga kumejaa tamthilia kutoka Uturuki, China, Ufilipino, Mexico, India, Korea n.k. ambazo zinaruka karibu kila kituo na tunashuhudia hata matangazo yakinakshiwa na miziki kutoka nje. Vipindi kutoka nje, filamu, picha za katuni na maonesho ya mambo mbalimbali vimetawala nchini na watu wametekwa kuangalia vipindi hivyo.

Na katika mkumbo huo, wasambazaji wakubwa wa filamu nchini wameachana na kusambaza filamu zetu na badala yake wanasambaza filamu na tamthilia kutoka nje hususan zinazotoka China, India na Uturuki zilizorudufiwa kwa tafsiri za Kiswahili.

Kuna wakati nilikwenda Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa (Alliance Française) kutafuta udhamini kwa ajili ya kutengeneza filamu, walinitaka nipeleke script iliyo katika lugha ya Kifaransa ili nipewe udhamini na kwamba wamekuwa wanatoa fedha nyingi kufadhili filamu na vipindi mbalimbali vya runinga duniani, kwa sababu wanaamini filamu ndiyo chombo kikuu kilichoisaidia Ufaransa kutangaza utamaduni wake duniani.

Kwa miaka mingi Ufaransa imefanikiwa sana kuitumia sekta ya televisheni na filamu kutangaza utamaduni wao duniani. Ufaransa imekuwa ikitoa msaada mkubwa wa bajeti za kutengenezea filamu na vipindi vya televisheni kwa nchi zinazoongea Kifaransa (Francophone). Kama hiyo haitoshi, wamepanua wigo na sasa wanatoa fedha hata kwa nchi zingine kama Tanzania.

Ndiyo maana, yeyote atakayeandika script yake ya filamu au kipindi cha televisheni na kuitafsiri kwa Kifaransa, atapewa udhamini wa maelfu ya Euro na ubalozi wa Ufaransa ili atengeneze. Unaweza ukashangaa, kwa nini wanatoa udhamini kwa watengeneza filamu katika nchi zetu? Nadhani unaanza kupata picha kuwa sasa dunia imeingia kwenye vita vya kiutamaduni, yaani kutawalana kiakili!

Utamaduni wetu ulindwe

Utamaduni ni jinsi binadamu anavyokabili maisha katika mazingira yake. Hiyo inajumlisha ujuzi, imani, sanaa, maadili, sheria, desturi n.k. ambavyo mtu anajipatia kama mwanajamii. Kama sifa maalumu ya binadamu, inayomtofautisha na wanyama, utamaduni ni suala la msingi, ukihusisha yale yote yanayopokezwa katika jamii fulani, kama vile lugha.

Wajanja wanajua kuwa sekta ya televisheni na sinema ni chombo muhimu sana katika kueneza utambulisho, utamaduni na fikra za nchi husika. Ndiyo maana nchi za China, Korea Kusini au India zinaingia gharama kubwa za kutafsiri filamu na tamthilia zao kwa Kiswahili kisha kuzitoa zioneshwe bure katika vituo vyetu vya televisheni.

Kwa mfano, China kupitia Idhaa ya Kiswahili ya CRI ilikuwa ya kwanza kwa kufanya kazi kubwa ya kutafsiri tamthilia ya ‘Doudou na Mama Wakwe zake’ na kutia sauti pamoja na kukamilisha maandalizi ya tamthilia hii kwa zaidi ya miezi 10, kwa ajili ya watazamaji wa Tanzania na Afrika ya Mashariki.

Watazamaji wanavutiwa na vipindi vya nje kwa sababu vipindi vyetu havivutii na havina ubora unaokubalika kimataifa, vituo vya televisheni nchini vimechukulia hili kama fursa ya kuonesha vipindi vilivyotafsiriwa kutoka China, Uturuki, Korea Kusini na India kwa kuwa wanavipata bure (au kulipia fedha kiduchu).

Hivi hatujiulizi: Kwanini nchi za China na Korea Kusini wanaingia gharama kubwa za kutafsiri tamthilia zao kwa Kiswahili na kuzitoa zioneshwe bure kwenye vituo vyetu vya runinga? Kwa nini Sony Pictures au nchi ya Marekani hawataki kudhibiti filamu za Hollywood zinazorudufiwa kiharamia na kusambaa kila kona ya Afrika?

Au hatujiulizi kwa nini India nao wameruhusu filamu zao zitafsiriwe Kiswahili na kuuzwa kwenye nchi zetu? Ni kwa sababu hii ni vita ya utamaduni, vita ya kutawalana kiakili.

Hivi tunaandaa taifa (kizazi) la aina gani? Kwa mfumo huu kizazi chetu tunakiachia urithi wa aina gani wa utamaduni? Tuamke, huu ni mkakati maalumu wa kujenga jamii itakayobadilisha tamaduni zake na kujifunza tamaduni za nje, na hivyo kutawaliwa kiakili.

Nadhani tunajenga jamii ya watu waliochanganyikiwa. Hatulioni sasa ila ni uhakika lina madhara makubwa sana kwa jamii zetu na mustakabali wa nchi yetu. Tunafungia vichupi vya vijana wetu kwenye video za miziki zinazooneshwa kwenye vituo vyetu vya televisheni, tutazuiaje hizo wakati vituo hivyo vinarusha video za nje zenye vichupi?

Ukiangalia kwa makini, hata mfumo wa utangazaji katika baadhi ya vituo vya redio na runinga zetu umeigwa kutoka Magharibi, kitu kinachotoa taswira ya kuua suala la ubunifu na kubaki watupu tusio na kitu chochote.

Bahati mbaya sana katika dunia hii ya vita ya kiutamaduni, ukitaka kupata fedha nyingi kwa urahisi basi fanya jambo linalodhalilisha utamaduni wako au taifa lako au fanya jambo linalotukuza utamaduni wa mataifa ya Magharibi.

Kwa sasa, katika tasnia ya muziki na filamu, Watanzania tumebakiwa na kitu kimoja tu tunachoweza kujivunia kwamba ni cha kwetu: lugha ya Kiswahili. Lakini bahati mbaya ni kwamba lugha hii, hata hivyo, wasanii wetu hawaijui vyema, ndiyo maana si ajabu kukuta wakichanganya R na L, DHA na ZA n.k.
 
Upvote 6
Siku hizi umeanza ugomvi wa majina ya watoto wanapozaliwa unakuta mme anataka mtoto aitwe Shelukindo au waitara au Kishole au Masanja au mshana, mke anataka mtoto aitwe lolenzo, camila, .....hapo hujagusa majina ya kichina na kihindi.
 
Filam za bongo kwanza waende wakajifunze acting, halafu wajifunze kiswahili chenyewe siyo kile cha mitaani.

Na waache kuiga vya nje wajaribu kufanya vyao.
 
Bandiko zuri sana hili.!
Mimi pia huwa nashangaa Basata wanafungia wimbo wa Diamond wanaruhusu wimbo wa Rihanah au nick minaj ambao wako uchi nyimbo zinachezwa kwenye television zetu.!
Kuna waigizaji wazuri sana hapa kwetu wengi wanakosa mitaji na kuwezeshwa tu.!
 
Siku hizi umeanza ugomvi wa majina ya watoto wanapozaliwa unakuta mme anataka mtoto aitwe Shelukindo au waitara au Kishole au Masanja au mshana, mke anataka mtoto aitwe lolenzo, camila, .....hapo hujagusa majina ya kichina na kihindi.
Haha! Eti mama anataka mtoto aitwe Lolenzo!🤣🤣...
 
Filam za bongo kwanza waende wakajifunze acting, halafu wajifunze kiswahili chenyewe siyo kile cha mitaani.

Na waache kuiga vya nje wajaribu kufanya vyao.
Tayari wameshatekwa na utamaduni wa nje kwa kuwa hii ni vita ya kiutamaduni...
 
Umesema kweli kabisa, mkuu...
 
Tatizo wasanii wa kitanzania hawajui wajibu wao kama wasanii na ndio sababu utakuta msanii ameamua kujiunga na chama cha siasa au kuamua kufanya siasa na kusahau kabisa kama yeye ni msanii na ni kioo cha jamii
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…