TANESCO: Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) kuhusishwa na athari za mafuriko ya Kibiti na Rufiji ni kupotosha Umma

TANESCO: Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) kuhusishwa na athari za mafuriko ya Kibiti na Rufiji ni kupotosha Umma

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
Maji rufiji.jpg

UFAFANUZI KUHUSU ATHARI ZA MAFURIKO YA KIBITI NA RUFIJI KUHUSISHWA NA UJENZI WA BWAWA LA JULIUS NYERERE (JNHPP)

Alhamisi, 11 Aprili 2024
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linapenda kutoa ufafanuzi kwa Umma kuhusu athari za mafuriko yanayoendelea katika maeneo ya Wilaya za Rufiji na Kibiti ambayo yanahusishwa na ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP).

Tunapenda kuujulisha umma kwamba uwepo wa Mradi wa Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere umesaidia kwa sehemu kubwa kupunguza athari ya mafuriko katika Wilaya za Rufiji na Kibiti ukilinganisha na miaka ya nyuma kabla mradi haujajengwa.

Historia ya kitakwimu inaonesha kuwa maeneo ya Rufiji na Kibiti yamekuwa yakikumbwa na mafuriko kwa miaka mingi ya nyuma kwa kiwango kikubwa kuliko hali ilivyo hivi sasa. Mwezi Mei, 1974 kiwango cha juu cha mafuriko katika mto Rufiji kilifikia mita za ujazo 13,200 kwa sekunde.

Mwaka 1988 kiwango cha mafuriko kilifikia mita za ujazo 8,383.9, mwaka 2016 kiwango cha mafuriko kilifikia mita za ujazo 8,974,7, mwaka 2020 kiwango cha mafuriko kilifikia mita za ujazo 7158.5 na tarehe 15 Februari 2024 kabla ya Bwawa la Julius Nyerere kujaa maji, kiwango cha mafuriko ya maji kilichokuwa kinaingia kwenye Bwawa kilifikia mita za ujazo 8,444 kwa sekunde.

Hata hivyo mafuriko hayo hayakufikia maeneo ya Kibiti na Rufiji kwa sababu Bwawa halikuwa limejaa, kiufupi ni kwamba Bwawa liliendelea kuhimili maji ya mafuriko tokea mwezi Disemba 2022 lilipoanza kujazwa maji mpaka mwishoni mwa mwezi Februari 2024 lilipojaa.

Baada ya Bwawa kujaa, maji ya mafuriko ya Mto Rufiji yaliendelea kupita mtoni kama ilivyo asili yake na hivyo kusababisha mafuriko katika maeneo ya Kibiti na Rufiji jambo ambalo ni la kawaida kwa kila msimu wa mvua kwa mto huu.

Hivyo, kama Mradi wa JNHPP usingejengwa basi maji haya yangefika moja kwa moja kwenye maeneo ya Rufiji na Kibiti na hivyo kusababisha athari kubwa zaidi ya mafuriko na kwa vipindi virefu kuliko tulivyoshuhudia sasa.

Lakini kwa kuwa maji hayo ya mafuriko yalikuwa yakimezwa kwanza na Bwawa la Mradi na kutunzwa kwa muda mrefu, jambo hilo lilisaidia mafuriko kutotokea au kuonekana kwa mapema katika maeneo hayo ya Kibiti na Rufiji.

Ikumbukwe kwamba moja wapo ya sababu ya kuanzishwa Mradi wa Bwawa la kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) katika maeneo ya Rufiji ni kwa sababu ya uwepo wa maji ya mafuriko katika Bonde la Mto Rufiji hali iliyopelekea Serikali kuamua kuyatumia mafuriko hayo ya maji kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Kama eneo hilo la Bonde la Mto Rufiji lisingeonekana kuwa na maji mengi ya mafuriko kila mwaka basi hata Serikali isingeamua kuwekeza mradi wa Bwawa katika eneo hilo.

Tunapenda Umma ufahamu kwamba mwaka huu (2024) kumekuwepo na mvua kubwa za El-nino ambazo zimepelekea kuwepo kwa mafuriko makubwa katika maeneo mengi ya nchi yetu ikiwemo maeneo yanayopeleka mtiririko wa maji ya mvua kwenye Bonde la Mto Rufiji.
Umeme Bwawa.png
Hivyo, kiwango kikubwa cha mafuriko katika maeneo hayo ya Kibiti na Rufiji kimesababishwa na mvua kubwa za El-nino zinazoendelea kunyesha.

Sehemu nyingine kumesababishwa na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi ambapo kutokana na kupanda kwa vina vya bahari, kumekuwepo na upungufu wa spidi ya maji ya mito kuingia baharini hasa wakati maji ya bahari yanapokuwa yamejaa yaani "High Tide".

Hivyo, kwa maelezo yaliyopo kwenye taarifa hii, Shirika la Umeme Tanzania linakanusha taarifa zozote za upotoshaji zinazohusisha Bwawa la Julius Nyerere na mafuriko ya Kibiti na Rufiji na linakemea upotoshaji unaofanywa na baadhi ya Watu wasio na nia njema kubeza juhudi za Serikali katika kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme nchini kwa ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere.

Shirika linaendelea kuwasihi Wananchi kuwa watulivu na kuendelea kufuatilia taarifa sahihi zinazotolewa na mamlaka husika ili kuendelea kujiweka katika hali ya usalama na kuondoa taharuki isiyo na ulazima.

Imetolewa Na;
KURUGENZI YA MAWASILIANO NA UHUSIANO KWA UMMA
TANESCO-MAKAO MAKUU
DODOMA


PIA SOMA


TUHUMA ZA UFISADI NA HUJUMA

HISTORIA
 
Cha kujiuliza kwa nini sasa si siku yoyote kabla?

Waitishe uchunguzi huru tujiridhishe.
 
Tanesco acha blah blah hizi,elewa kuna watanzania wengi sio wapumbavu,toa pia report ya mazingira (zote mbili )hapa ili ukweli ujulikane,binafsi ninaamini mafuriko ya Rufiji ni man made
 
Taarifa haijafafanua kuhusu maji zidio kwenye bwawa yanaelekezwa wapi?!
 
Kwa hiyo Ile hadhari mlitoa ya nini wakati mnafungulia maji? Kwa nini Mafuriko yake baada ya kufungulia hayo maji?

Bwawa limesaidiaje kudhibiti hayo mguriko Sasa kama Bado yanatokea?
 
Taarifa za chadema,maria sarungi na choicevariable tulikwisha zipuuza!
Mjumbe hauwawi 🤣🤣🤣🤣

Zitto: Mafuriko Rufiji ni uzembe wa Serikali
Shirika la @tanescoyetutz lilijua kuwa Bwawa la Mwalimu Nyerere linajaa na lazima maji yafunguliwe.Maji yalifunguliwa bila kutoa tahadhari kwa wananchi wa ‘downstream’.Serikali itueleze ilichukua hatua gani baada ya kufahamu kuwa lazima wafungulie bwawa?

Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa ilijua kuwa mvua ni nyingi mwaka huu na Bwawa litajaa kabla ya muda uliotarajiwa. Serikali haikuchukua hatua za kuwalinda wananchi wa Rufiji.

Taarifa ya CAG ya mwaka 2021 ilionyesha mapungufu makubwa ya usanifu wa Mradi na kupendekeza hatua za kuchukua.Serikali mpaka sasa haijatueleza utekelezaji wa Hoja za CAG.

Watu wa Rufiji pamoja na Kibiti na wilaya zingine zinazozunguka mradi wa Bwawa la Nyerere wana Fedha zao za CSR karibu shilingi bilioni 290. Fedha hizi zingeweza kutumika kufanya ‘flood mitigation’ downstream kwa miradi ya Kilimo cha Umwagiliaji kwa wananchi.Serikali ieleze wananchi fedha hizi zipo wapi?

Suala la mafuriko Rufiji na Kibiti ni zaidi ya misaada ya kibinaadam. Ni suala la uwajibikaji. Serikali ichukue dhima"
 
Kwa hiyo Ile hadhari mlitoa ya nini wakati mnafungulia maji? Kwa nini Mafuriko yake baada ya kufungulia hayo maji?

Bwawa limesaidiaje kudhibiti hayo mguriko Sasa kama Bado yanatokea?
Wewe unasoma na kuelewa?
Mbona wameeleza bwawa limesaidiaje hujasoma?
Ulikuwa unafaulu kwenye section ya comprehension wakati ulipokua shuleni?
 
Back
Top Bottom