diana chumbikino
JF-Expert Member
- May 29, 2018
- 428
- 368
SERIKALI imeridhishwa na uwezo wa viwanda vya ndani katika kuongeza thamani ya korosho ya Tanzania, huku mpaka sasa tani 40,050 zimeshapakiwa kwenye meli tayari kwenda nje ya nchi kupitia Bandari ya Mtwara. Aidha, hadi kufikia Septemba 23, mwaka huu, tani 607.75 za korosho zilibanguliwa na viwanda vidogo na kuwezesha wabanguaji wadogo 1,000 kupata ajira, huku tani 3,309.64 zilibanguliwa na viwanda vikubwa na kuwezesha kutoa ajira 2,511 ambapo waajiriwa wengi ni wanawake.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa vyombo vya habari jana, ubanguaji wa korosho hizo ulifanywa na viwanda vya aina mbili yaani viwanda vidogo vinavyosimamiwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) pamoja na viwanda vikubwa.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Joseph Buchweishaija alisema ubanguaji huo unafanyika katika viwanda vilivyopo mikoa ya Mtwara na Lindi na usafirishaji wa korosho hizo nje ya nchi unaendelea Bandari ya Mtwara. Profesa Buchweishaija alisema hadi kufikia Septemba 23, mwaka huu, tani 607.75 za korosho zilibanguliwa na viwanda vidogo na kuwezesha wabanguaji wadogo 1,000 kupata ajira huku tani 3,309.64 zilibangu liwa na viwanda vikubwa na kuwezesha kutoa ajira 2,511 ambapo waajiriwa wengi ni wanawake.
Alisema katika kutekeleza mpango wa ubanguaji, serikali kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) iliingia mikataba na viwanda vikubwa na SIDO kwa niaba ya viwanda au wabanguaji wadogo ili kubangua korosho hizo. Alivitaja viwanda hivyo vidogo katika Mkoa wa Mtwara kuwa ni Siwa Food Products, Mama Vitu Super Cashewnut, Mikindani Food Processing, Akross Ltd - SIDO, Mtwara na Kitama Farmers-Tandahimba na kwa Mkoa wa Lindi ni Waigero Ltd, Wabanguaji Wadogo BUCO na Uwakoru, Ruangwa.
Alisema mpaka sasa viwanda vitano vilivyo chini ya usimamizi wa SIDO Mtwara, vimekamilisha ubanguaji wa korosho na viwanda viwili ambavyo ni Waigero na Uwakoru chini ya usimamizi wa SIDO Lindi, vinaendelea na uzalishaji na ubanguaji. Mbali na viwanda hivyo vidogo, viwanda vingine ni Amama Farmers, Perfect Cashew, Hawte Investment Ltd na Al-Andalus Ltd ambavyo vinaendelea na ubanguaji wa kati, wakati Kiwanda cha Micronix na Korosho Afrika vimemaliza ubanguaji wa korosho ghafi kama makubaliano ya mikataba yao na kwa sasa viwanda hivyo, vinaendelea kubangua korosho walizouziwa na serikali tani 1,000.
Kuhusu usafirishaji wa korosho kutoka kwenye maghala kwenda melini, alisema kazi hiyo inaendelea vizuri na mpaka sasa tani 40,050 zimeshapakiwa kwenye meli tayari kwenda nje ya nchi kupitia Bandari ya Mtwara. “Hivi sasa ninavyozungumza tayari meli mbili zimepakia korosho na kuondoka, meli ya tatu imeanza kupakiwa ambapo itabeba kontena 1,015 ambazo sawa na tani 23,328 na kazi hii itakamilika kwa siku mbili ikizingatiwa kuwa kuna meli zingine mbili zipo majini na zitatia nanga na kuanza kazi ya kupakia korosho kwenda nje ya nchi,” alisema.
Majaliwa atembelea bandari Mtwara Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametembelea bandari ya Mtwara na ameshuhudia shehena ya korosho ziliyonunuliwa na Kampuni ya Tang Long zikipakiwa katika meli kubwa yenye jina la AS Christiana kwa ajili kusafirishwa kwenda nchini Vietnam. “Ni faraja kuona mzigo wa korosho ukiondoka na kutoa nafasi ya kuingiza mzigo mwingine mpya wa korosho utakaopatikana baada ya kuanza msimu mpya mwezi huu.
Na mnunuzi huyu ameahidi kununua tani 100,000 katika msimu wa mwaka huu,” alisema Majaliwa. Alitembelea Bandari ya Mtwara jana kwa ajili ya kujionea kazi ya usafirishaji wa korosho inavyofanyika na alisema ameridhishwa na kasi na utaratibu unaoendelea badarini hapo.
Alisema Kampuni ya Tang Long ya Vietnam licha ya kuahidi kununua korosho katika msimu wa mwaka huu, pia imeomba kupatiwa eneo kujenga kiwanda cha kubangua korosho na wapo tayari kuanza hata Desemba, 2019.
Waziri Mkuu alisema ujenzi wa viwanda vya kubangulia korosho nchini, utaongeza thamani na kuwezesha dunia nzima kutambua kuwa korosho hizo zimetoka Tanzania, kwa sababu kwenye vifungashio watakuwa wameandika, hivyo kuongeza soko.
Akizungumzia kuhusu msimu wa uuzaji wa korosho wa mwaka huu, Waziri Mkuu alisema kipaumbele cha kwanza watapewa wenye viwanda vya ndani na kisha tani zinazobaki zitauzwa kwa wanunuzi kutoka nje. “Wito wa Rais Dk. John Magufuli wa ujenzi wa viwanda unalenga katika kuongeza ajira kwa wananchi kwa kuwa viwanda vinaajiri watu wengi wenye kada tofauti. Wakuu wa mikoa endeleeni kurahisisha mazingira ya uwekezaji,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geoffrey Mwambe alisema licha ya kampuni ya Tang Long kununua korosho nchini, pia imeomba ikodishwe kiwanda kimojawapo cha serikali ili waanze ubanguaji wa korosho.