TANROADS Songwe walia mifugo kuharibu barabara

TANROADS Songwe walia mifugo kuharibu barabara

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
Screenshot 2025-02-20 093810.jpg

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe umeonyesha wasiwasi wake kuhusu uvamizi wa hifadhi za barabara unaofanywa na wafanyabiashara ndogo ndogo (machinga) pamoja na changamoto ya mifugo kupitishwa kwenye barabara, hali inayosababisha uharibifu wa miundombinu hiyo.

Taarifa hiyo ilitolewa leo, Februari 18, 2025, na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga, wakati akiwasilisha makisio na mapendekezo ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/26 katika kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa.

Mhandisi Bishanga alibainisha kuwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na uvamizi wa hifadhi za barabara ni miji ya Mlowo wilayani Mbozi, pamoja na Mpemba na Tunduma wilayani Momba, ambapo wafanyabiashara wanatumia sehemu za hifadhi ya barabara kwa shughuli zao za biashara.

Aidha, alisema kuwa suala la mifugo kupitishwa barabarani limekuwa changamoto kubwa, likisababisha uharibifu wa barabara na kuhatarisha usalama wa vyombo vya usafiri, abiria, na wananchi kwa ujumla.

Alisema ili kukabiliana na changamoto hizo, wakala huo unaendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali kupitia mikutano na semina, pamoja na kushirikiana na viongozi wa ngazi mbalimbali ili kuwajulisha jamii madhara ya kufanya biashara kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kama hifadhi za barabara, ikiwemo kupitisha mifugo.

Katika kikao hicho, wajumbe wa bodi ya barabara mkoa wa Songwe, chini ya mwenyekiti wa kikao hicho Mkuu wa Mkoa Daniel Chongolo, walipitisha mapendekezo ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/26 ya shilingi bilioni 9.344 kwa ajili ya matengenezo ya barabara.

Mhandisi Bishanga alifafanua kuwa TANROADS Mkoa wa Songwe inahudumia barabara zenye jumla ya urefu wa kilometa 1,035.41.

Akifunga kikao hicho, Mkuu wa Mkoa Chongolo aliwapongeza watendaji wa TANROADS, wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa, pamoja na watendaji wa ofisi yake wakiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Happness Seneda, kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwatumikia Wananchi.
 
Back
Top Bottom