SoC01 Tanzania karne ya 21 bado tunahitaji kuhamasishwa juu ya usafi wa vyoo?

SoC01 Tanzania karne ya 21 bado tunahitaji kuhamasishwa juu ya usafi wa vyoo?

Stories of Change - 2021 Competition

Chaki na Ubao

New Member
Joined
Sep 13, 2021
Posts
4
Reaction score
8
Eti Choo Jamani, Dah!

Moja ya kampeni kubwa kabisa kufanyika katika nchi hii ni “Nyumba Choo”, kampeni inayohamasisha ujenzi na utumiaji wa vyoo bora katika kaya zetu. Haina ubishi, ni suala nyeti hili kwa kulinda afya katika jamii zetu, lakini ninapata ukakasi kidogo na kujiuliza, katika karne hii ya 21 tunayoambiwa ni karne ya sayansi na teknolojia huku tukitakiwa kuwekeza katika viwanda, ni kweli bado tunahitaji kuhamasishwa juu ya usafi, tena usafi wa choo?

Choo cha shule.jpg

Naibu waziri TAMISEMI, Mhe. Silinde akikagua choo cha shule mojawapo kusini mwa Tanzania mapema mwaka huu (Picha: jamiiforum.com)

Ninapata jibu la swali hili pale ninapopata fulsa ya kusoma taarifa iliyoandikwa na shilika lisilo la kiserikali la TLDS, taarifa inayotokana na utafiti mdogo walioufanya ili kubaini hali ya mazingira katika shule za umma. Pamoja na changamoto nyingine zilizoainishwa kwenye taarifa hiyo, suala la ukosefu vyoo bora linaainishwa kuwa ni tatizo kubwa. Naridhia taarifa hii kwa kupitia vyombo vya habari vya mtandaoni. Hii inanifanya nirudi nyuma kidogo na kujiuliza, shule haina choo bora, sasa suala la afya ya watoto linazingatiwaje? au si la umuhimu?

Nachukuwa makabrasha kadhaa kujiridhisha; Sera ya Taifa ya Mtoto, ninasoma sura ya 3 na kubaini imeelekeza kiunagaubaga juu ya umuhimu wa afya ya mtoto, naliweka kando andiko hilo nikiwaza, labda ni kwa sababu halihusiani na elimu moja kwa moja, nachukua Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo, sura ya 6, hususani kipengere cha 6.2, nakutana na kilekile, msisitizo wa elimu ya afya kuanzia ngazi ya awali kabisa. Ndipo naamua kuchukuwa mtaala wa elimu, tena elimu ya awali, ninakuta moja ya umahili ulioelekezwa kujengwa kwa mtoto ni kumudu afya, dah!

Pamoja na kuwepo na maelekezo ya mtaala ambao unamtaka mwalimu kwa kushirikiana na wazazi na jamii kwa ujumla, kuhakikisha mtaala unatekelezwa ipasavyo na kumwezesha mtoto kujenga umahili unaokusudiwa , bado kumekuwa na tatizo la kiutekelezaji ambalo limepelekea matokeo ya elimu yetu kuwa si yale yanayokusudiwa.

Ikiwa tutawaenzi wahenga kwa ule usemi usamao “samaki mkunje angali mbichi” basi tutakuwa tukiamini kwamba msingi imara wa maisha ya ujifunzaji hujengwa katika umri mdogo wa utoto, hivyo, tunakubali kuwa elimu ya awali ni chachu ya mafanikio ya mtoto kwa maisha ya baadaye. Hii ina maana kwamba endapo mtoto atajengewa umahiri fulani katika umri huu (miaka 0 – 8), atadumu nao na kutokuwa na shida ya kutumia umahiri huu kujifunza zaidi kwa siku zijazo, hili linagusa pia suala ya kumudu afya.

Haina pingamizi kuwa choo ni muhimu katika suala zima la afya na endapo mtoto katika umri mdogo atashiriki ipasavyo katika elimu inayosaidia kujenga ustadi wa kutumia na kutunza choo, basi mtoto huyu ataona umuhimu wa kuwa na choo bora katika maisha yake yote.

Kwa mtoto, vitendo ndiyo muhimu zaidi katika ujifunzaji wake. Vitendo hivi vifanyikapo katika mazingira asili na salama humwezesha mtoto kujenga ujuzi na kuhusisha ujuzi huu na maisha halisi ya jamii yake. Na hapa ndipo ninapoingiwa na shaka, ni kwa vipi basi mtoto ataweza kujenga ustadi huu ikiwa mazingira harisi hayamwezeshi?

Hebu angalia mazingira ya vyoo vya shule zetu, hususani shule za umma, vyoo vingi ni duni sana na hata vile vilivyoboreshwa ama kujengwa kisasa havitunzwi vema na hivyo kupoteza ubora. Itawezekanaje basi kwa vyoo hivi kutumika kama zana za ujifunzaji na ufundishaji?. Kwa mazingira haya itawezekanaje kumfundisha mtoto umuhimu wa choo bora wakati yeye anamuingiliano na choo duni? Hatuoni hii ndiyo sababu inayotupelekea kuwa na kampeni kama hii, “Nyumba Choo” na kutakuwa na umuhimu gani wa kampeni kama hizi wakati tunazidi kujenga jamii isiyotambua umuhimu wa choo?

Ni Dhahiri kwamba tunahitaji kuwekeza zaidi katika mazingira rafiki kwa mtoto ili aweze kuyatumia mazingira haya kujifunza na kujenga umahiri kwa kuhusisha kile anachojifunza na maisha halisi. Tufanye juhudi katika kuboresha vyoo vya shule zetu ili watoto wapete mahala salama pa kujifunza kwa vitendo, wajifunze utumiaji na utunzaji wa vyoo kwa ajili ya ustawi wa afya zao wenyewe na wengine.

Uchafuzi wa choo.jpg

Uchafuzi na uharibifu wa makusudi wa vyoo vya shule hutokana elimu duni ya umuhimu wa vyoo.

Suala la afya si suala la serikali, ni suala la jamii, yaani mimi na wewe, serikali haiugui wala kupata maladhi, ni mimi na wewe, hivyo ni lazima tujifunze kulinda afya zetu wenyewe kwa njia yoyote ile ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya vyoo vya shule zetu na kuwawezesha watoto kutambua umuhimu wa vyoo na kuvitunza.

Imani yangu kubwa iko kwa mwalimu na mzazi kaatika utekelezaji wa jambo hili, endapo kutakuwa na ushirikiano wa kina kati ya pande hizi mbili, basi uhakika wa kutokomeza maladhi yatokanayo na uchafu wa chooni ni mkubwa. Endapo mwalimua atafanya juhudi za dhati katika utekelezaji wa mtaala na mzazi atathamini kazi hii na kushiriki kikamilifu katika kuboresha mazingira, mtoto atakuwa na shauku ya kujifunza na matokeo ya elimu yetu yatakuwa yale yanayotarajiwa katika jamii.

Swali ni kwa vipi mzazi ataweza kuthamini kazi ya mwalimu? Ni kwa kuangalia alama anazopata mtoto wake katika mtihani au majaribio? .Jibu la swali hili analo mwalimu mwenyewe kwami kitaaluma amesheni mbinu kedekede za kuweza kumshirikisha mzazi na jamii kwa ujumla katika suala zima la maendeleo ya mtoto. Basi ni vema mwalimu akatumia mbinu hizi ili kujenga jamii inayoendana na uhitaji wa karne ya 21.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom