Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
Naibu Waziri Londo amezitaja changamoto hizo zilizotatuliwa kuwa ni;- ulinganifu wa viwango vya upimaji mafuta kupitia Makubaliano ya Mkataba wa Kutambua Matokeo ya Vipimo kati ya Mamlaka zinazohusika na Vipimo, ili kuhakikisha ufanisi na uaminifu wa mchakato wa upimaji mafuta; Kuondolewa kwa marufuku ya usafiri wa usiku nchini Zambia, hatua inayowezesha magari ya mizigo kusafiri saa 24 na hivyo kuongeza ufanisi wa usafirishaji na mtiririko wa biashara; na Maboresho ya usimamizi na uchakataji wa nyaraka za mizigo kupitia utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mfumo wa kubadilishana taarifa za forodha na kuanza kwa awamu ya pili ya uwianishaji wa mifumo.
Aidha, Naibu Waziri Londo alibanisha kuwa kutatuliwa kwa changamoto hizo ni hatua muhimu katika kuimarisha biashara ya mipakani, kuboresha usimamizi wa mipaka na kuongeza ufanisi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Tunduma–Nakonde (One Stop Border Post – OSBP), kukuza biashara, uwekezaji na uongezaji thamani wa bidhaa, pamoja na kurahisisha huduma za usafirishaji wa watu, mizigo na huduma mipakani.
Biashara kati ya Tanzania na Zambia imeendelea kuongezeka, ambapo thamani ya biashara imepanda kutoka dola za Marekani milioni 312 mwaka 2024 hadi dola milioni 349 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 11.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ulijumuisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Millya (Mb), Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Munde (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali wakiongozwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Denis Londo.