Nilipokuwa chuoni mwaka wa kwanza, zoezi la timu yetu darasani ilikuwa ni 'IWAPO MRADI WA VITAMBULISHO UNAFAA HAPA UINGEREZA AU LA'' na haya ni maelezo yangu kwa kumbu kumbu na maoni yangu:
Suala la ID CARDS duniani kote lina utata. Utata baina ya serikali na wanaodai haki za binadamu kuwa ni kuingiliwa uhuru binafsi.
Pili utata unaojitokeza ni katika suala zima la fedha kuwa kiasi kikubwa sana kinahitajika na vipi utaweza kukidhi matakwa yote ya utambulisho wa mtu ili kutetea (justify) gharama kubwa sana za Vitambulisho vya Taifa.
Hapa Uingereza hivi sasa mdahalo ni mkubwa sana wengi wakidai mradi huo hauna maana yeyote na vitambulisho walivyonavyo wahusika vinatosha kabisa, ie. Kwa Uingereza mkaazi yoyote mwenye umri wa miaka 16 na kuendelea ana kadi ya bima {insurance number} ambayo inamuelezea mchango wake katika mfuko wake wa pensheni kwa jinsi anavyofanya kazi, pia hiyo hutumiwa na BODI YA MIKOPO YA SHULE kujua mchango wake uweje na alipwe kiasi gani.
Aidha ni kadi hiyo hiyo ndio hutumiwa na mamlaka ya kodi kumtoza mhusika kodi.
Lakini kadi hiyo ina walakini kiasi kwa vile haina sura ya mtu, taarifa zake nyingi ni za siri na polisi huhitaji kadi hiyo pale tu wanapohitaji kujua baadhi ya mambo kuhusu mtu husika.
Wanaodai Vitambulisho vipya wanatoa hoja kwamba ongezeko la ugaidi duniani limezua hitajio jipya kabisa la vitambulisho vyenye nembo ya macho na pengine alama za vidole ili kumtambua mtu, na mjadala ni je hivi vitu viwe ni sehemu ya leseni ya gari ya mwenye nayo au iwe ni kadi 'stand alone'? Bado mijadala ni mingi....
Kwetu Tanzania, kwa wananchi walio wengi hawana aina yoyote ya utambulisho kuwa ni mtanzania..Passport ni kwa wenye nazo na wanaozihitajia {bado nchini mwetu Pasi ya kusafiria ni mpaka ukiihitaji sio 'haki' ya mtu husika}
Ni aghalabu kumkuta mtu anatembea na pasi bila matumizi yeyote.
Ni kweli kwamba Tanzania tunahitajia wananchi wetu wawe ni kitambulisho cha aina fulani ili waweze kuwa na uwezo wa kupata huduma za jamii vizuri na pia kujua mtanzania 'halisi' ni nani.
Kwa Tanzania nadhani Kitambulisho kitasaidia na kuwa na manufaa pale tu iwapo kitatumika kama ni moja ya nyenzo ya kurahisisha huduma za serikali kwa wananchi.
Kwa mfano, Ikiwekwa kwamba lazima mtoto anaemaliza elimu ya msingi awe na kitambulisho, na kila unapoomba kazi lazima utoe kitambulisho hicho kisajiliwe, kiwe na 'link' ya moja kwa moja na TRA na NSSF na kuweza kurekodi malipo yako ya uzeeni tangu ukianza kazi au ukijiajiri...
Kadi hiyo hiyo itumike katika fomu mbali mbali za serikali na huduma za jamii na iwe ndio kadi na utambulisho rasmi wa kutoa mikopo ya wanafunzi {ULIPAJI WAKE UTAKUWA RAHISI} kwani mwanafunzi akimaliza tu chuo akiajiriwa 'data' zake zitakuwa zinatumika kulipia madeni aliyokopeshwa....
Na vile vile kwa upande wa usalama iwe ni hivyo, ukitaka pasi basi ni lazima utoe kitambulisho, ukitaka leseni lazima utoe kitambulisho, ukikamatwa ama kwa kushukiwa au 'at random' uwe na aina fulani ya kuthibitisha kweli wewe ni saidi au kitila.
Lakini mradi huu wa vitambulisho pia kuna mambo yawe wazi:
- Uwe ni mradi mama ''super project'' utakaoweza kufanya maisha ya mtanzania yawe nafuu kwa kuunganisha huduma za serikali, kama ilivyoelezwa hapo juu.
- Ijulikane nani ataweza kulipia gharama, hapa UK imesemwa itagharimu paundi 39 kwa kila mwananchi na kelele ni nyingi.
- Ili mradi huu ufanikiwe lazima kuwe na sheria kuwa LAZIMA UWE NA KITAMBULISHO la sivyo haitokuwa muafaka.
Kwa muktadha huu nadhani binafsi naunga mkono wazo la msingi la kuwa na vitambulisho Tanzania.