SoC03 Tanzania tajiri iliyokumbatia wakwasi wachache mafukara wengi

SoC03 Tanzania tajiri iliyokumbatia wakwasi wachache mafukara wengi

Stories of Change - 2023 Competition

GoJeVa

Member
Joined
Sep 15, 2021
Posts
41
Reaction score
60
TANZANIA TAJIRI, ILIYOKUMBATIA WAKWASI WACHACHE MAFUKARA WENGI.

Utangulizi: Makala hii itazungumzia mchango wa viongozi wetu juu ya kulinda rasilimali na utajiri uliomo ndani ya nchi yetu ya Tanzania. Makala hii imeandikwa kwa lengo kubwa la kukumbusha viongozi wetu juu ya wajibu wao kwa wananchi, kwa sababu kiongozi yupo kwenye nafasi inayompasa atumikie wananchi kwa weledi mkubwa.


800px-Flag-map_of_Tanzania.svg.png

Hii ni picha ya bendera ya Jamuhuri ya muungano ya Tanzania, yenye umbo la ramani ya nchi hiyo(chanzo cha picha mtandaoni).

Ukwasi ni utajiri mkubwa wakati Ufukara ni umasikini uliokithiri. Nchi yetu ni ardhi iliyobarikiwa utajiri mwingi, kama vile utajiri wa madini mbalimbali na vivutio vya utalii vya kila aina. Lakini, ni miongoni mwa nchi ambazo raia wake wengi wanaishi kwenye lindi la umasikini, hivyo inaonekana rasilimali zilizopo nchini hazisaidii watanzania wengi.

Je; nini chanzo cha rasilimali zetu kutosaidia watanzania tulio wengi?.

1. Ulafi wa viongozi wetu.
Viongozi wetu wengi wanaotuongoza wamejawa na ulafi. Wapo tayari kuhujumu uchaguzi, kupokea rushwa, kuingia mikataba mibovu na kuuza rasilimali za taifa ili wawe matajiri wao na vizazi vyao, bila kujali faini au adhabu ambazo nchi itazipata kutoka na mikataba hiyo mibovu. Mbaya zaidi wapo tayari kupeana vyeo, kama vile ubalozi, ukuu wa wilaya au ukuu wa mikoa kama fadhila ili kuendelea kulindana juu ya uovu wao.

Shairi.
“Wa dubai karibuni, bandarini tawaleni,
Hata kama ukoloni, maendeleo leteni,
Mkitaka magogoni, juu ya meza njooni,

Twajuana kwa viremba,ponda mali kufa kwaja.”

2. Taifa kutopata viongozi wenye dira na maono juu nchi yetu.
Viongozi wengi wanaochaguliwa hawana maono wala dira juu ya taifa letu. Hivyo wanajikuta wanafanya Mambo mengi ambayo yanapelekea nchi kuingia kwenye matatizo kwa mfano taifa kulipishwa fedha kutokana na kuingia mikataba mibovu. Uongozi unahitaji watu wenye maono, kiongozi inabidi afikirie baada ya miaka mia moja na zaidi taifa litakuwaje na watu wataishije na sio kufiri ndani ya uongozi wake tuu.

3. Viongozi kutokuwa na sifa za uongozi, kutokana na upendeleo kukithiri katika kupata viongozi. Nchi yetu inachangamoto kubwa katika kupata viongozi wa kuongoza nchi. Viongozi wengi kama vile; wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa, wakurugenzi, mabalozi, makatibu na viongozi wa idara mbalimbali wanapewa nafasi hizo kutokana na ukada wao Au ukaribu wao na viongozi wakuu. Hivyo inapelekea kukosa washauri na watetezi sahihi wa rasilimali za nchi. Pia vizazi vya watawala au waliokuwa watawala vinaendelea kupendelewa na kupewa nafasi kubwa bila kujali uwezo wao wa kuhudumu nafasi hivyo wanaishia kutoa vitisho kwa wananchi pale wanapotoa maoni na kuwatishia kwa kutumia vyombo vya dola. Ikumbukwe, “…mtu akikosa utajiri wa fikra, itapelekea kutumia nguvu kubwa na vitisho ili kunyamazisha wenye fikra chanya.”

NJIA ZA KUKOMBOA TANZANIA YETU.

1. Kupata katiba mpya (Rasimu ya Warioba) na tume huru ya uchaguzi.
Hii itasaidia kupelekea uchaguzi mkuu kufanyika vizuri na kupata viongozi ambao wamechaguliwa na watanzania. Pia, viongozi hawa watajua wanafanya kazi kwa kuzingatia maoni ya wananchi na sio kwa utashi wao na pia itapunguza watu kujipendekeza kwa viongozi ili wapate nafasi za kuteuliwa. Vilevile itasaidia watu kukosoa na kushauri pale ushauri unapohitajika bila unafiki.

2. Viongozi waache kutumia rasilimali za nchi kama mali zao binafsi.
Viongozi waheshimu rasilimali zetu. Ni ajabu viongozi kila mara husaini mikataba mibovu lakini bado hawajifunzi kutokana na makosa bali wao wanaendelea kusaini mikataba inayowapa faida wawekezaji pekee na kufanya umasikini kwa watanzania kuzidi kushamiri bila hofu yoyote. Hadi tunahisi sio watanzania wenzetu.

Shairi.
“Serengeti ngorongoro, hakika urithi wetu,
Mikumi Kilimanjaro, huu utajiri wetu,
Msipende migogoro, hivi nyie ni wenzetu?,

Tanzania yetu sote, sio mali ya wachache.”

3. Inapofika suala nyeti kama kusaini mikataba ya uwekezaji, Uchama wa vyama vya siasa uwekwe pembeni na kusiwe na usiri, wananchi pia wajue kile kilichomo kwenye mkataba. Wachaguliwe watu wenye utimamu wa taaluma husika na wenye uwezo mkubwa kichwani wa kupembua mambo.Tanzania ni nchi yenye watu wenye vipaji vikubwa sana kama vile wanasheria, wachumi, Madaktari hawa wote vipaji vyao vikizingatiwa na kuhusishwa katika masuala ya kitaifa ni rahisi kulinda rasilimali zetu na kusaini mikataba ambayo itakuwa na tija kwa watanzania wote.

4. Kujenga taasisi imara.
Moja ya changamoto katika nchi yetu ni kutojenga taasisi imara bali tunajenga watu(Viongozi wenye madaraka makubwa) hii inapelekea viongozi hata wakikosea inakuwa ngumu kuathibiwa. Taasisi kama vile; Vyombo vya habari, Vyama vya siasa, Taasisi za kuzuia na kupambana na rushwa zikiwa imara inakuwa rahisi kuthibiti ubadhirifu wa viongozi na kuwafanya wawe viongozi bora na sio bora viongozi. Kukosekana kwa taasisi imara tunaona mapungufu mengi kwa mfano; ripoti za wakaguzi wakuu wa hesabu za serikali(CAG) kila zikitoka zinaonesha ubadhirifu mkubwa na hasara kubwa kwa taifa lakini hatua za kuwajibisha viongozi waliofanya ubadhirifu ni hafifu.
AHSANTE
 
Upvote 1
Back
Top Bottom