SoC04 Tanzania tuitakayo 2050: Miundombinu ya kukabiliana na mafuriko isanifiwe kiuhandisi kuakisi ongezeko la watu na ukuaji wa makazi nchini

SoC04 Tanzania tuitakayo 2050: Miundombinu ya kukabiliana na mafuriko isanifiwe kiuhandisi kuakisi ongezeko la watu na ukuaji wa makazi nchini

Tanzania Tuitakayo competition threads

Librarian 105

JF-Expert Member
Joined
May 6, 2023
Posts
261
Reaction score
356
Utangulizi:
Kwa muda mrefu mafuriko yamekuwa yakiharibu miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji nchini, pia kuleta maafa ya vifo kwa raia na mali zao, na kwa ujumla hurejesha nyuma kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Na mara nyingi viongozi wa serikali hutazama majanga ya mafuriko na kuchukua uelekeo mwepesi wa kuwaasa raia wake kutokujenga kwenye mikondo ya maji na mabondeni kisha huja na mapendekezo ya bajeti za kukarabati miundombinu iliyoharibika.

Walakini, ukweli ni kwamba, nchi yetu inayo uhaba wa mifumo ya ukusanyaji wa maji ya mvua na njia za uchepushaji wa maji hayo kulingana na ukuaji wa makazi na ongezeko la watu.

Tathmini ya andiko hili ya chanzo cha mafuriko nchini:
Ukuaji wa makazi na ongezeko la watu ni suala linalochangia kwa asilimia kubwa athari ya mafuriko nchini. Hapa kwa upande mmoja kuna tatizo la ujenzi wa makazi holela yasiyofuata kanuni za mipango miji, na upande wa pili kuna uhaba wa mifumo ya mitaro mikubwa na njia za uchepushaji maji ya mvua yanayokusanywa kupitia mapaa ya nyumba na majengo mengine mbalimbali. Hatua zifuatazo zinapaswa kuchukuliwa na wizara ya ujenzi na wizara ya miundombinu kukabiliana na mafuriko:
  1. Ujenzi wa mitaro mikubw a ya chini ya ardhi kwenye barabara teule kimkakati za Tanroads/Tarura: Miji yetu mbali ya kuwa na makazi yaliyosongamana pia inazo barabara ambazo mitaro yake mingi ya maji ni miyembamba na mifupi kwa kina au haina kabisa hususan za mitaani. Hivyo usanifu na uratibu wa ujenzi wa mitaro mikubwa mithili ya njia za mahandaki ya chini ya ardhi ni mpango mwafaka mmojawapo wa kukabiliana na maji ya mvua yasababishayo mafuriko. Kwani hata uchimbaji na utandazaji wa mifumo hiyo nchini utakuwa wenye kufanyika chini kwa chini pasina kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii moja kwa moja kwa mitandao yake kuanzia katikati ya miji kuelekea nje ya miji husika kufuatana na njia kuu za maji hayo. Kuhusu mitaro ya sasa itasalia kutumika na baadaye kuja kuboreshwa kama njia za kuchepushia maji ya mvua baada ya utafiti wa jiografia za mikondo ya maji hayo kufahamika vyema ili yawe yenye kuelekezwa kwenye mito mikubwa na hata baharini.
  2. Uchimbaji wa mabwawa ya kuvunia maji ya mvua : wizara ya ujenzi na wizara ya miundombinu endapo wakishirikiana bega kwa bega na wizara ya kilimo na uvuvi sambamba na wizara ya maji kuja na mpango mahsusi wa uchimbaji wa mabwawa ya kuvunia maji ya mvua. Janga la mafuriko nchini tutakuwa tumelipunguza kwa kiasi kikubwa. Isitoshe pia tutachochea uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji na ufugaji wa samaki na kuongeza fursa zingine za kiuchumi na kibiashara sanjari na vyanzo vipya vya kodi na mapato ya ndani. Vivyo hivyo pia kukabiliana na baa la njaa, ukame, na kutanua wigo wa vyanzo vya maji nchini. Kwa namna moja au nyingine, uhandisi na utandazaji wa mifumo na mitandao hii ya uvunaji wa maji ya mvua inahusisha wizara zaidi ya moja, hii inajenga hoja kwamba hata bajeti yake inaweza isiwe yenye kuumiza uchumi wa nchi.
  3. Ulinzi wa miundombinu na mazingira yake : kuna juhudi zisizoridhisha za utunzaji wa mazingira nchini. Kwa maana kwamba mitaro mingi kwa sasa utakuta imejaa taka ngumu hasa za plastiki kiasi cha kuziba makalavati kwenye barabara za Tanroads/Tarura nyakati za mvua hasa masika. Hii inatoa picha wizara zetu hazishirikiani kikamilifu kuleta ustawi wa wananchi na taifa lao kwa kusimamia utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Pia halmashauri zinapaswa kuwajibishwa kwa kuwa ndio zenye kutoa zabuni za uzoaji taka nchini, hakuna mlango wa nyumba au fremu za maduka na vizimba vya masokoni visivyotozwa fedha za usafi na uzoaji taka kila mwezi, lakini cha ajabu unakuta taka zimesambaa mitaani na kwenye miundombinu ya barabara. Uzembe huu unachangia mafuriko kwani unasababisha maji ya mvua kukosa uelekeo maalumu hata kugeuka mafuriko.
Hitimisho:
Utekelezaji wa mpango huu:
Ukirejea majibu ya waziri wa fedha bungeni kuchangia bajeti ya wizara ya ujenzi juu ya mpango wa serikali kuja na bajeti mahsusi kwa ajili ya kukarabati barabara zilizoharibiwa na mvua nchi nzima. Kwa ujumla fedha zitakazotumika ni nyingi sana na halikadhalika wananchi wanaweza kuumia kiuchumi kwa kuzingatia kuwa bungeni kumeshatolewa rai na mbunge mmoja serikali ifikirie kupitisha tozo kupitia simu za mikononi kuchangia mfuko wa barabara.

Nako itakuwa jambo lenye kugharimu wananchi na fedha za umma mwaka hadi mwaka kutokana na kuegemezwa kwenye kutatua matokeo ya majanga ya mafuriko. Walakini serikali kupitia wizara zake zikijikita kutatua chanzo cha mafuriko yatokanayo na maji ya mvua itakua aula zaidi na suluhisho la muda mrefu la kulinda miundombinu yetu ya usafirishaji na uchukuzi.

Kwa mantiki hii, mpango huu wa mitaro mikubwa ya chini ya ardhi na njia za uchepushaji wa maji na mabwawa ya kuvunia maji ya mvua, kwa vile utakuwa kwenye dira na mipango ya nchi ina maana kila mwaka kutakuwa na fungu rasmi la bajeti la kuitekeleza hatua kwa hatua. Uoni wangu unatazamia ndani ya miaka 25 ijayo tunaweza kuwa taifa lisiloathiriwa vikubwa na mafuriko ya mvua za masika.

Hivyo napendekeza kwenye ule mpango mkuu wa miundombinu ulioarifiwa na wizara ya ujenzi hivi karibuni; serikali izingatie pia usambazaji wa miundombinu ya kukabiliana na mafuriko kuakisi ongezeko la watu na ukuaji wa makazi ya watu mijini na vijijini kulingana na kila sensa ya watu na makazi.

Na itapata wepesi endapo itapangilia ramani za makazi ya miji na vijiji mapema kwa kuzingatia vigezo vya mipango miji kabla ya wimbi la raia kustawisha nyumba zao kiholela.
 
Upvote 1
Ujenzi wa mitaro mikubw a ya chini ya ardhi kwenye barabara teule kimkakati za Tanroads/Tarura: Miji yetu mbali ya kuwa na makazi yaliyosongamana pia inazo barabara ambazo mitaro yake mingi ya maji ni miyembamba na mifupi kwa kina au haina kabisa hususan za mitaani. Hivyo usanifu na uratibu wa ujenzi wa mitaro mikubwa mithili ya njia za mahandaki ya chini ya ardhi ni mpango mwafaka mmojawapo wa kukabiliana na maji ya mvua yasababishayo mafuriko.
Kila barabara iendane na mitaro. Maana hata barabara zenyewe bila mitaro zinaharibika mapema sana.

Na itapata wepesi endapo itapangilia ramani za makazi ya miji na vijiji mapema kwa kuzingatia vigezo vya mipango miji kabla ya wimbi la raia kustawisha nyumba zao kiholela.
Japa ndipo pataashiria tunayo akili sasa, maana mipango inatakiwa ianze kabla ya matumizi na sio kinyume chake
 
Back
Top Bottom