SoC04 Tanzania tuitakayo ndani ya miaka mitano-25 ijayo

SoC04 Tanzania tuitakayo ndani ya miaka mitano-25 ijayo

Tanzania Tuitakayo competition threads

KITANGITA MARO

New Member
Joined
May 29, 2024
Posts
1
Reaction score
0
Tanzania tuitakayo ndani ya miaka mitano-25 ijayo

MAENDELEO ya Taifa lolote lile duniani hutegemea sana mipango murua, nguvu kazi ya kutosha, uchumi usio wa mashaka na nyenzo madhubuti zinazowezesha ufanikishaji wa malengo ya kimkakati.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa katika Bara la Afrika yenye utajiri mkubwa katikati ya changamoto lukuki, lakini inayosifika kwa mipango mizuri isiyotekelezwa kwa ufanisi!

Mipango ni FIKRA na TARATIBU zinazowezeshwa kufikiwa kwa jambo lenye tija kwa jamii/nchi/taifa na lililokusudiwa kwa usahihi.

Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025-2050 ambayo inalenga kutengeneza UONI wa kimpango katika nchi kwa ajili ya maendeleo kila baada ya miaka mitano hapa nchini, ikitumiwa vyema kwa muktadha wake italeta tija katika nchi, ila kwa sasa imebaki ni REJEA tu katika vikao nyeti na makongamano.

Tanzania kwa kiwango kikubwa ina FURSA nyingi zinazoweza kuchochea ukuaji toshewlevu wa kiuchumi kwa ajili ya sehemu kubwa ya umma, lakini bado haujavunwa vya kutosha.

Kwa kuzingatia vipaumbele muhimu, vipo vitu muhimu ambavyo havina MBADALA wake ambavyo ni muhimu kutekelezwa kwa kuwa na usimamizi madhubuti ili kuwezesha raslimali lukuki za nchi hii ziweze kutumiwa inavyopaswa na Watanzania wote, tofauti na ilivyo sasa ili waweze kukutana na raslimali hizo kwenye uboreshaji wa mambo muhimu kwa ajiliya ustawi wa nchi na maisha ya watu, ujengaji wa mifumo imara yenye kuleta tija.

Utawala bora, hakuna shaka kwa nia njema ya serikali katika kusimamia utawala bora, uruhusiwe uhuru wa kisiasa ulioidhinishwa na KATIBA, kama uhuru wa kujieleza, kujumuika, maandamano ya amani, mikutano ya kisiasa, uhuru wa vikundi vya kijamii, uhuru wa kuabudu, usawa mbele ya sheria (kwa watu wote) na karibuni kabisa kuundwa kwa TUME YA HAKI JINAI, Tume huru ya Uchaguzi, udhibiti wa vitendo vya rushwa na uwepo wa uwazi wa mikataba ya nchi yote haya yakichakatwa VYEMA yataleta tija kubwa pasipo shaka kwa

Eneo la Utawala bora kwa ujumla wake likisimamiwa vyema ni eneo MTAMBUKA kwa mambo yote, litafungua milango mingine muhimu zaidi kwa uchumi na ustawi wa Mtanzania na Taifa kwa ujumla.

Eneo jingine ni la AFYA, Taifa lolote duniani ambalo watu wake wana afya mgogoro ni vigumu kupiga hatua ya kimaendeleo, Sheria ya BIMA YA AFYA kwa wote iwekewe mfumo wa utekelezaji kwa serikali kutangaza rasmi viwango vya uchangiaji vilivyo nafuu kwa wananchi wa kawaida.

Utekelezaji wa miundombinu bora ya reli, bandari, viwanja vya ndege na barabara, viwanda vya mbolea na viuatilifu, mafunzo kwa maofisa ugani, fedha za kutosha za kufanya utafiti, masoko ya uhakika ya mazao ya mkulima, ruzuku ya kutosha katika kilimo, kutiliwa nguvu kwa sheria zinazozingatia nidhamu katika utendaji na usimamizi wa shughuli za umma na binafsi pamoja na Benki Kuu kusimamia vyema mwenendo wa uchumi na thamani ya sarafu ya Tanzania.

Elimu bora hutajwa kuwa ufunguo wa maisha, uboreshaji wa mitaalana uanzishwaji wa elimu ya ufundi na amali endapo itatekelezwa kwa ufanisi tarajiwa utalifanya taifa kupiga hatua ya mchupo (a great leap ahead), lakini uwepo usawa wa utoaji wa mikoo kwa makundi yote ya vijana kwa wakati.

Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali(CAG): Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kutokana na majukumu yake ya kikatiba ndiyo MOYO wa nchi. Kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na upuuzaji wa waziwazi wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa ripoti hiyo kwa upande wa serikali na hata BUNGE na hivyo kuonekana kama taarifa hiyo ambayo inagharimu fedha nyingi katika uandaaji wake,

Taarifa hiyo huonekana kama ni KITU cha kawaida na kwamba miongoni mwa wale wanaoguswa serikalini( ama kwa kuhusika na ubadhirifu au kwa kusaidia kuwepo kwa ubadhirifu unaobainishwa na Ofisi hiyo ya UMMA, imefikia sehemu wanaiona ripoti hiyo ni kitu cha kawaida kabisa!

Upelekwe mswada wa sheria bungeni, sheria itungwe itakayosimamia ubainishaji wa mapungufu yanayobainishwa kwenye ripoti hiyo ikiwemo wale wanaoshindwa kuandaa bajeti na bakaa ya matumizi ya fedha za umma yanayotumiwa kwa shughuli na miradi ya serikali yobainishwa kwenye taarifa ya CAG kila mwaka kwa kisingizio cha kujibu hoja za ukaguzi baaa ya kutolewa kwa taarifa hiyo kwa umma.

Huu ni utaratibu DHAIFU unawafanya watumishi na watendaji serikalini kutowajibika vyema huku wakiiba fedha za umma kwa kisingizio cha kutojibiwa vyema kwa hoja za ukaguzi!

Mathalani katika taarifa hiyo ya CAG ya mwaka 2023/24 inaonyesha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa 25 zililipa Sh milioni 556.84 kwa watumishi wasiostahili , waliostaafu, waliofariki, waliotoroka na walioachishwa kazi.

Fedha hizo ni nyingi sana kwa mamlaka ya serikali za mitaa ambako ndipo walipo wananchi, zingeweza kujenga Kituo Kikubwa cha afya na kutoa huduma za tiba kwa wananchi.

Huu ni mchwa mwingine mkubwa unaotafuna raslimali za nchi hii, nikirejea hata taarifa ya hivi karibuni, wakati inakabidhiwa kwa mheshimiwa Rais, Rais mwenyewe alisema kuwa serikali itakwenda kujibu hoja za ukaguzi, ningetarajia kumuona RAIS akizungumza kwa UKALI zaidi kama MKUU WA NCHI.

Rais alisema na hapa namnukuu, “ Dosari hizi tutakwenda kukaa tuzifanyie kazi kisawa sawa, turekebishe na mwakani pengine hizi hazitajirudia, tutakuwa tumesogea”, mwisho wa kunukuu.

Serikali na taifa kwa ujumla ije na mfumo ambao utaiwezesha taarifa ya CAG kufanyiwa kazi kisayansi tofauti na mfumo ulipo sasa.

Jambo jingine, viongozi wanaoteuliwe baada ya uteuzi wapewe mkataba wa kisheria kwa ajiliya utekelezaji wa majukumu yao, mkataba huo wa kisheria utamke wazi kiwango cha ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu, wakishindwa kufikia kilengo cha ufanisi waondolewe kwa mujibu wa mkataba.

Mkataba huo pamoja na mambo mengine, uweke pia vigezo vya kuwatambua watendaji na viongozi wanaofanya vizuri katika kusikiliza na kutatua kero za wananchi, wananchi wanabiliwa na kero nyingi sana katika nchi hii kiasi cha kushindwa kabisa kuwa na furaha kwenye ustawi wa maisha yao.

Watendaji watakaofanya vyema katika eneo la kushughulika na matatizo ya wananchi watambuliwe na kuingizwa kwenye rekodi ya nchi ya utambuzi kwa ajili ya kutambuliwa, kuthaminiwa lakini pia kuenziwa kwa kazi kubwa waliyofanya ya kusaidia kuwepo kwa maendeleo endelevu kwa ajili ya ustawi wa maisha ya wananchi ambao kimsingi ndio wenye dhamana ya kisheria ya kuundwa serikali, bila wao viongozi na watendaji hawa wasingekuwepo.

Yote hayo yakitekelezwa kwa nia ya dhati na sio nia ovu, itakuwa MWAROBAINI wa mafanikio ya kuiona Tanzania tuitakayo ndani ya miaka mitano-25 ijayo.

MWISHO
 
Upvote 3
Back
Top Bottom