SoC04 Tanzania Tuitakayo: Siri ya mafanikio ni kuwekeza kwenye teknolojia

SoC04 Tanzania Tuitakayo: Siri ya mafanikio ni kuwekeza kwenye teknolojia

Tanzania Tuitakayo competition threads
Joined
Apr 30, 2024
Posts
6
Reaction score
2
Tanzania Tuitakayo: Siri ya mafanikio ni kuwekeza kwenye teknolojia

Na Alpha Isaya Nuhu

Kwa TANZANIA TUITAKAYO miaka 5 au 25 ijayo, hakuna mjadala kwamba nyanja ya sayansi na teknolojia ndiyo itakuwa mhimili utakaotawala maendeleo na maisha ya Watanzania tunaposhuhudia kasi kubwa ya mabadiliko yaliyoletwa na fani hiyo miongo mitatu iliyopita.

Nyanja hii siyo tu kwamba imebadili namna ya kuendesha uchumi na biashara, bali pia imegusa na kutikisa eneo nyeti la soko la ajira na changamoto mpya zilizoambatana na utandawazi.

Kwa miongo mitatu, hasa kuanzia miaka ya 1990, tumeshuhudia kwamba hakuna kurudi nyuma kwa kasi ya mabadiliko jinsi teknolojia inavyogusa na kubadili maisha yetu ya kila siku.

MSHANGAO WA UJIO WA TEKNOLOJIA

Mabadiliko haya yenye spidi kali ya dunia ya dijitali yamewaacha Watanzania wengi kwenye butwaa, wakishangaa wasijue nini kinachotokea katika maisha yao.

Wanashangaa kasi ya mapinduzi kwenye sekta ya mawasiliano kwa ujio wa simu za mkononi na kutoweka kwa simu za zamani za kukoroga za kumsubiri opereta akuunganishe na mtu unayetaka kuzungumza naye.

Si hivyo tu, bali pia wanashangaa ujio wa kompyuta zilizorahisisha tasnia za uchapishaji na upashanaji habari kupitia intaneti.

Mshangao huo pia umegusa sekta ya uchukuzi pale Watanzania wanapoona ujio wa treni ya umeme badala ya ile waliyoizoea kwa miaka mingi yenye mngurumo wa “kata-mti-panda-mti” inayoendeshwa kwa makaa ya mawe au mafuta ya dizeli ambayo tuliachiwa na wakoloni wa Kijerumani na Waingereza.

Leo hii wataalam walioko kwenye sekta ya usafiri wanatwambia kwamba safari ya kwenda mji mkuu wa Dodoma ambayo zamani ilikuwa ikichukua karibu saa 15 kwa treni inayotumia dizeli sasa itachukua wastani wa saa tatu kwa treni ya umeme. Mafanikio hayo yote ni matokeo ya mapokeo ya teknolojia ya kisasa katika sekta ya usafiri na kwa ujumla sekta zote za maendeleo kiuchumi.

Kwa hakika, teknolojia, ambayo kwa lugha ya utani imebatizwa jina la “Teke Linalotujia”, imeendelea kuwashangaza Watanzania jinsi ilivyorahisisha maisha yao wakikumbuka changamoto za miaka mingi walizokuwa wakikumbana nazo siku za nyuma.

Wapo Watanzania wengi vijana ambao leo hawajui kwamba kulikuwepo enzi za kuandikiana barua ili kujuliana hali; hawajui kwamba kulikuwepo na simu za kukoroga au analojia, ili opereta akuunganishe na mtu unayetaka kuwasiliana naye. Na ili upate mawasiliano ya simu hizo, ilibidi ukubali kupoteza muda wako adimu ukisubiri opereta akuunganishe na mtu unayetaka kuongea naye.

Vijana wa leo pia hawajui kwamba huko nyuma, maofisini kulikuwepo vurugu za kelele zenye kukera zilizosababishwa na matumizi ya taipureta kwa shughuli za uchapishaji; hawajui kwamba shughuli nyingi za kiofisi ziliendeshwa kwa mfumo wa makaratasi badala ya kijiditali.

Mambo yote haya sasa yamekuwa ni historia kutokana na ubunifu na uvumbuzi wa mwanadamu wa kurahisisha aina ya utendaji kazi kwa kipindi kifupi na kwa kasi isiyomithilika. Maajabu mengi, ambayo hatujayaona, yataendelea kutokea kwenye nyanja hii ya sayansi na teknolojia katika karne hii ya 21 ambayo yataisukuma TANZANIA TUITAKAYO kuwa taifa maarufu lenye uchumi imara na maisha bora kwa wananchi wake.

Andiko hili linaweza kuonekana kama ni ndoto ya kufikirika ya Abunuwasi lakini kwa Watanzania watakaobahatika kuishi na kuiona Tanzania ya miaka 5 au 25 ijayo watasimulia ukweli wa maono haya.

Watasimulia sayansi na teknolojia ilivyogusa na kubadili maisha yao kwa kila shughuli wanazofanya; wataimba nyimbo za kutukuza maendeleo ya teknolojia yalivyoleta neema kwao na kwa watoto na wajukuu zao.

UWEKEZAJI KWENYE ELIMU YA TEKNOLOJIA

Lakini ili kufaidi matunda ya sayansi na teknolojia kwa TANZANIA TUITAKAYO miaka 5 au 25 ijayo, ni lazima kuwekeza kwenye elimu katika fani hiyo muhimu. Elimu hiyo lazima itumike kuzalisha vijana wengi wabunifu na wavumbuzi kwa ajili ya kukabili changamoto za ushindani dunia ijayo.

Kwa kutabiri, kama kutabiri ni neno sahihi kwa muktadha huu, TANZANIA TUITAKAYO haitakuwa nchi ya watu mbumbumbu na maamuma; itakuwa ni taifa jingine jipya linaloongozwa na wabunifu na wavumbuzi wenye vipaji, karama na ujuzi wa hali ya juu wa kuyatafutia ufumbuzi au majawabu matatizo au changamoto za wakati huo.

Nchi yetu itakuwa taifa la watu magwiji tunaowasoma kwenye vitabu vya historia kama akina Thomas Alva Edison, Albert Einstein, Alexander Graham Bell, Alexander Fleming na wengine wengi waliokuwa maarufu karne ya 19 na 20 waliojitwalia sifa za ubunifu na uvumbuzi. Utundu wao utaendelea kukumbukwa daima kwa kuiweka dunia mahali pema pa kuishi.

Ni jambo la faraja kwamba kwa Tanzania ya leo jitihada za kujiandaa kwa changamoto zililetwazo na mabadiliko ya teknolojia zinafanyiwa kazi kwa uwekezaji wa raslimaliwatu katika kila nyanja ya uchumi.
Hata hivyo, bado jitihada hizo haziendi kwa kasi inayofanana na mabadiliko ya teknolojia yenyewe. Kasi ya mabadiliko haya ya teknolojia ni kama mwanariadha anayewania medali kwa mbio za mita 100 ambaye anatakiwa atimue mbio kama upepo wa tsunami.

Kwa maono ya andiko hili, uso wa TANZANIA TUITAKAYO ya miongo miwili na nusu ijayo hautakuwa huu tunaouona sasa – uso uliosinyaa na kujaa huzuni. Uso wa Tanzania ya kesho utakuwa ni uso angavu uliojaa kicheko cha matumaini ya ushindi kwa watu wote.

Kasi ya matumizi ya teknolojia kadri inavyobadilika wakati hadi wakati pia italibadili taifa hili kubwa la Afrika Mashariki kuwa kivutio kwa watu mbalimbali duniani watakaokuja kujionea yale yanayotendeka kwa nchi ambayo kwa miongo kadhaa ilikuwa ikionekana kana kwamba imelala usingizi fofofo katika historia ya maendeleo.

HITIMISHO
Kwa muhtasari, andiko hili lililenga kuelezea nyanja ya sayansi na teknolojia na umuhimu wake kwa maendeleo ya taifa la Tanzania na pia kugusa maono kwa TANZANIA TUITAKAYO robo karne ijayo. Kwa changamoto za maisha ya binadamu zilizoletwa na utandawazi, kuwekeza kwenye sekta ya teknolojia si suala tena la mjadala.

MWISHO
 
Upvote 2
Leo hii wataalam walioko kwenye sekta ya usafiri wanatwambia kwamba safari ya kwenda mji mkuu wa Dodoma ambayo zamani ilikuwa ikichukua karibu saa 15 kwa treni inayotumia dizeli sasa itachukua wastani wa saa tatu kwa treni ya umeme. Mafanikio hayo yote ni matokeo ya mapokeo ya teknolojia ya kisasa katika sekta ya usafiri.
Ishara ya wazi kwamba tunasonga mbele, mdogo mdogo.

Andiko hili linaweza kuonekana kama ni ndoto ya kufikirika ya Abunuwasi lakini kwa Watanzania watakaobahatika kuishi na kuiona Tanzania ya miaka 5 au 25 ijayo watasimulia ukweli wa maono haya.
Tupe vitu, ndoto kubwa ndizo zinaleta maendeleo makubwa tukiziamini. Muda mfupi tu uliopita ndoto ya viwanda si unaona ilivyotubadilisha.

Kwa muhtaari, andiko hili lililenga kuelezea nyanja ya sayansi na teknolojia na umuhimu wake kwa maendeleo ya taifa na pia kugusa maono kwa TANZANIA TUITAKAYO miaka 5 au 25 ijayo. Kwa changamoto za maisha ya binadamu zilizoletwa na utandawazi, kuwekeza kwenye sekta ya teknolojia si suala tena la mjadala.
Ahsante

Nyongeza: Edit uiondoe hiyo attached pdf/word msimu huu walisema haihitajiki bro. Labda weka tu vipichapicha.
 
Back
Top Bottom