Wakuu, naomba nitangulie kwa kujitambulisha kuwa mimi ni muafrika, mzaliwa na raia wa Tanzania. Pili mimi si mwanauchumi wala mwanasheria kwa hiyo uchambuzi wangu ni kwa uelewa wa mwananchi asiye na taaluma hizo mbili. Nimejaribu kusoma chambuzi kwenye vyombo vya habari, mkataba wenyewe na muhtasari mbalimbali wa mikataba hiyo ya EPA.
Nikijikita kwenye mada yenyewe:
- Moja, kwa uelewa wangu mikataba yoyote ile lazima kuna majadiliano ya pande husika. Kwa maana hii mikataba hii ilijadiliwa nchini kwetu, kisha Tanzania na wanachama wenza wa EAC, hadi hatua ya EAC na EU.
- Pili, majadiliano ya mikataba hii yalichukua zaidi ya miaka kumi, tangu enzi za Mh. Rais Mstaafu William Mkapa mpaka mwaka 2014.
- Tatu, kulikuwa na hatua mbalimbali ambazo kabla hujavuka kila hatua, lazima maridhiano ya pande zote mbili yafikiwe. Mpaka hatua iliyofikiwa sasa wanachama wote wa EAC na EU waliridhia mikataba hii kwa kuweka sahihi Oktoba 2014, ikimaanisha kuwa wanachama wa pande zote mbili (EAC na EU) wameridhia mikataba hiyo na hakuna nafasi tena ya kubadilisha yaliyomo zaidi ya kuhakiki lugha kabla ya sahihi za nchi wanachama (ratification).
- Nne, katika hatua zote Tanzania ilikuwa na jopo la wataalam wake na viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali waliohusishwa na waliochangia katika kuandaa mikataba hii; kwanzia ngazi ya taifa, ukanda wa EAC na kati ya jumuiya hizi mbili. Wengine walisafirishwa na kwenda Brussels kwenye mafunzo ya mikataba, majadiliano, nk.
Kwa mantiki hiyo, kwa nini hoja ya kupinga mikataba hii tunaisikia katika hatua hizi za mwisho? Kwa nini katika hoja hizo hatuwasikii wale wataalam na viongozi waliohusishwa wakizungumza? Je, wao waliona makosa hayo tangu mwanzo au yamekuja kufahamika hatua ya kumalizia ng'ombe mkia?
Ninashangaa sana kuwalaumu wazungu kwenye jambo tuliloshirikishwa tangu mwanzo. Kama tunao uwezo wa kukataa katika hatua hii, je tulishindwaje kukataa katika hatua zilizopita? Tena tunawasema kuwa wanaturudisha kwenye ukoloni. Tukumbuke hawa wenzetu hawako kwenye kutoa misaada tu, bali kutengenezea nchi zao vyanzo vya mapato. Tunahitaji tuache mawazo ya kujinyongesha na kuona tunastahili tu misaada kwa sababu ya historia; tunajigeuza watumwa na tutaendelea kubaki watumwa wa mawazo yetu.
Halafu hatuwasikii wazungu wakilizungumzia hili wala kutupa upande wa pili. Hivyo nikajitahidi kupitia vyanzo nilivyokuta kwenye mtandao kufuatilia zaidi. Mkataba nimeukuta hapa:
http://trade.ec.europa.eu/doclib/docs/2015/october/tradoc_153845.compressed.pdf
Tafadhali kama kuna wataalam wa Uchumi na Sheria, nikotayari kukosolewa na kueleweshwa (bila matusi tafadhali). Ila nimepata yafuatayo:
Kulikuwa na hoja ya Mh Zitto Kabwe, kuwa nchi itakosa vyanzo vya mapato kwa kutotoza ushuru. Kwanza nchi za EAC zitafungua milango yake baada ya miaka saba kwa baadhi ya bidhaa za Ulaya hadi baada ya miaka 25 kwa bidhaa takribani asilimia 82, bila kutoza ushuru wa forodha. Bidhaa hizo pia zinatakiwa ziwe kitu tunachozalisha nchini. Kipengele cha tatu Ibara ya 100 ya mkataba huo kinasema kuwa EU itatoa rasilimali fedha kujazia hasara serikali itakayoingia kutokana na kukosa mapato yatokanayo na kuondoa au kupunguza ushuru wa forodha
Vile vile ibara hiyo hiyo ya 100 inazipa nafasi nchi wanachama wa EAC, kupitia mikataba hii, nafasi ya kuboresha au kuendeleza sekta za uzalishaji, kukuza taaluma na kuongezea uwezo nguvu kazi katika sekta za uzalishaji; na hata kutoa mwanya wa kushughulikia mapungufu au matatizo yatakayoathiri usalama wa chakula na lishe, maendeleo ya vijiji, usalama wa riziki na mapato ya nje
Nimekutana pia na ibara ya 142 inayowapa nafasi pande zote mbili kupitia upya mkataba huu kila baada ya miaka mitano na kutoa mapendekezo ili kurekebisha mahusiano ya kibiashara chini ya mkataba huu kulingana na uzoefu wa miaka mitano iliyoisha. Hivyo kuna nafasi ya mabadiliko kwa baadhi ya masuala
Kwa upande mwingine mkataba huu ni kweli unamapungufu hasa changamoto ya utayari wa nchi yetu kufikia viwango vya kuuza kwa wingi soko la Ulaya. Kwa sasa EBA (Everything But Arms) inatutosha kufurahia fursa za kuuza Ulaya bila kutozwa ushuru wowote. Tukumbuke tu kuwa hatutakuwa na uchumi wa chini siku zote, hivyo tusitukane mkunga na uzazi ungalipo.
Japo kuna changamoto za kuingia mikataba mingine na nchi nyingine ikiwa tutaingia kwenye mkataba huu, siyo kweli kuwa mkataba huu unatuzuia kuingia mikataba na nchi nyingine. Nilichoelewa ni kuwa, Nchi za Ulaya zimeweka sharti la kuwapa wao dili nzuri kwenye baadhi ya bidhaa. Na ikiwa nchi nyingine zitataka dili nzuri zaidi katika bidhaa hizo basi EU wanahaki ya kuomba dili kama hilo. Hii itakuja kutuchanganya kwenye biashara na nchi nyingine kama China na India tunazofanya nazo biashara zaidi.
Kikubwa ni kuwa, tujitahidi kujadili mambo kwa kuangalia uhalisia wa jambo lenyewe na siyo kutumia hisia na siasa kwenye kuamua kila kitu.
Ni hayo tu kwa leo.