Tanzania imejitoa rasmi katika Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership-OGP) hatua ambayo inazua wasiwasi kuhusu utekelezaji wa sera ya uwazi na uwajibikaji iliyoasisiwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Hatua hiyo ya kujitoa kwa Tanzania imetangazwa na Kamati ya Uongozi ya mpango huo iliyokutana katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.
Hii ina maana kwamba kuanzia sasa mipango yote ya serikali itakuwa ikiendeshwa kwa usiri mkubwa (itafanyika gizani). Hakutakuwa na uwazi tena.
Moja ya athari za uamuzi huo ni nyaraka zinazohusu mambo nyeti ya nchi Mfano:- (matumizi ya pesa za Serikali, ugawaji wa ardhi) zitafichwa, na iwapo mwananchi atakutwa nazo atakuwa ametenda jinai na anaweza kushtakiwa (disclose of classified information), chini ya sheria ya usalama wa taifa ya mwaka 1971.
Bado haijaeleweka kwanini Tanzania imeamua kujitoa katika mpango huo na kuamua kuendesha mambo yake gizani, lakini, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kiksnda, Dr.Aziz Mlima amesema “Ni kweli tumejiondoa. Lengo ni kuutathmini mpango huo kama unaendana na masilahi ya Taifa. Kama tutaona una maslahi kwa taifa tutajiunga tena”
Tanzania ilijiunga na mpango huo mwaka 2011 na kuwa nchi ya pili barani Afrika ikitanguliwa na Afrika Kusini. Kwa sasa nchi zaidi ya 40 za Afrika zimesaini mpango huo wa kuendesha mambo kwa uwazi. Pia zaidi ya 75% ya nchi zote duniani zinatekeleza mpango huo.
Mpango huo unasaidia kuondokana na kasumba ya kuendesha mambo kwa usiri kati ya serikali na wananchi.
Kusaini mpango huu kulimpa sifa Rais Kikwete kimataifa kwa kuunga mkono kuendesha mambo kwa uwazi. Bado haieleweki kwanini Rais JPM ameamua kujitoa katika mpango huo, na kuamua kurudi gizani.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kuwa Tanzania kujitoa inaweza kuwa kwa sababu ya ushawishi wa Rwanda kwa kuwa Rwanda ni moja ya nchi ambazo hazijasaini mpango huo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki alipoulizwa kuhusiana na hatua hiyo amekataa kueleza lolote lakini akasema kuwa Serikali itatoa ufafanuzi itakapoona kuna umuhimu wa kufanya hivyo. “Nisikilize, sisi kama serikali tutalieleza hilo tutakapoona inafaa,” alisema Waziri Kairuki.
Nini maoni yako?