Replica
JF-Expert Member
- Aug 28, 2017
- 1,681
- 8,887
Serikali ya Jamhuri ya Korea imeipatia Tanzania mkopo wa gharama nafuu wa Tsh. Bilioni 310 kwa ajili ya upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na uendelezaji na utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi.
Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo baina ya Serikali ya Tanza na Korea Kusini itakayotolewa kupitia benki ya Exim ya Korea, imefanyika leo Alhamisi, Oktoba 27, 2022 katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Korea Kusini iliyopo Seoul.
Mkataba wa awamu ya pili ya mradi wa upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa NIDA una thamani ya Tsh. Bilioni 161 na mkataba wa uendelezaji na utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi ambao una thamani ya Tsh. Bilioni 149.
Akizungumza wakati wa halfa hiyo ambayo ambayo pia ilishuhudiwa na Waziri Mkuu wa Korea Han Duck-Soo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania na Korea zinajivunia mahusiano yaliyodumu kwa miaka 30 ambayo yamekuwa chachu katika kukuza uchumi wa nchi hizo mbili katika sekta mbalimbali.
Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Balozi wa Tanzania Nchini Korea Kusini, Balozi Togolani Mavura, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Aboud Hassan Mwinyi na watendaji wengine wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.