Hivi hayo ambayo tunang'ang'ania yana faida gani kwa mtanzania?
i) Hiyo ardhi ambayo tunadai ni ya kwetu, mara ngapi wananchi wamenyang'anywa na kupewa wawekezaji uchwara (kwa long-term lease) kwa dhana kuwa ardhi ni mali ya umma? Mara ngapi wananchi maeneo yao yamegawiwa kwa wenye nazo, na hao wakalipwa bei ya mafenesi yaliyomo wakati wajanja wa ardhi wanavuta mamilioni?
ii) Matumizi haya ya pasi si yanawafaidia jamaa wa immigration zaidi ya wananchi wa kawaida? Tangu lini mtu mwenye nazo amaeshindwa kupata pasi ya Tanzania? Nchi zote zenye ushirikiano wa karibu zinalegeza masharti ya matumizi ya pasi. Hii ni kweli kuanzia Nafta hadi E.U. Leo tunataka tubakie na ukiritimba wa pasi halafu tunasema tunataka ushirikiano zaidi?
iii) Nchi nyingi tu zina mpango wa ukazi wa kudumu. Watanzania wengi tu wamefaidika na hiyo. Ni wangapi walio marekani wamebeba Green Card? Wangapi wako ulaya kama permanent resident? tunaona shida gani kumruhusu mganda, mrundi au mkenya kuja kuishi kwetu ili mradi havunji sheria? Mbona na sisi wengi tu wako Nairobi, Mombasa, Jinja na kwengineko?
iv) Tulikuwa kwenye Comesa ambamo hivyo vipengele vyote vya biashara viliondolewa au kulegezwa. Usafirishaji wa mizigo ulirahisishwa na mengineyo. Pamoja na faida zote hizi, tukajitoa kwa mbinde tukithamini zaidi ushirikiano wetu na nchi za kusini kwetu. Ushirikiano uliokuwa zaidi wa kisiasa na si wa kiuchumi! Tulibembelezwa tubaki, hatukuta kusikia. Sasa leo tunalalamikia nini?
Hapana, kwenye hili sisi ni kikwazo. Hatuwezi kusema sisi kwenye hizi ishu hatugeuki halafu tukajidai ati tunataka maelewano! Bora tuwaambie wenzetu kuwa huo Muungano wanaoutaka sisi hatuna mpango nao. Tutafute njia mbadala ya kushirikiana nao bila kuwa sehemu ya huo ushirika. Lakini tutakaoumia ni sisi na si wao kama tunavyojidanganya!
Mtoto akililia wembe, mpe. Kama ilivyokuwa Comesa, hivyo hivyo itakuwa kwenye EAC. Ingawa safari hii ni wenzetu watachoka kutuvumilia na kutuacha sisi tukumbatie visivyo na faida.
Amandla.....
Ngawethu!
Kaka Fundi Mchundo, ahsante kutusaidia kuangalia upande wa pili, na kuepuka kwenda na muono wa kuhisia, kusikia, kukisia, na mtima. Lakini binafsi nimeshindwa kushawishika kwamba hapa tutajutia msimamo wetu.
Swala la ardhi, kama wananchi wananyang'anywa maeneo na kupewa wawekezaji uchwara, matajiri, hilo kosa halirekebishiki kwa kuruhusu wengine, Wakenya. Hitilafu ya pili haihalalishi ya kwanza. Hililafu ya kwanza inatokana na ufisadi na pia watu kutokuwa na elimu juu ya haki zao ambazo zinaweza kutafutwa iwapo tutaimarisha misingi ya nguvu za dola. Hitilafu ya pili inaepukika, hatutaki kuwapa Wakenya ardhi kwa sababu wao hawana ya kutupa. Kosa la kuungana katika mazingira ambayo sisi ndio tunabeba mzigo wa kuauni wenzetu tumelifanya mwaka 1964 na tusingependa kulirudia. (Wanzanzibari msitaabishwe hapo, maana hata nyinyi mnazo kero za muungano zinazowasumbua kama sisi, baadhi yetu, tunavyoona kwamba nyinyi kwetu ndio mzigo mzito kama gunia la karafuu. Kama karafuu ina uzito!) Hatutaki kurudia kosa lile lile na Wakenya.
Swala la pasi ilichofanya Tanzania – na ndicho walichokubaliana wote watatu, 1999 – ndio hicho kinafanywa sehemu nyingi duniani, zikiwemo hata hizo jumuiya ulizozitaja Fundi. Kwamba vizingiti bado vipo, na walioviondoa wameenda taratibu mno, na kuna waliojitoa katika makubalioano ndani ya jumuiya. Tanzania inasema tubaki na huu mpango wa kutoa pasi ya EA (ambayo kwa kweli ni kama visa tu, manake yabidi ugongewe tena mihuri kila baada ya miezi sita, haikupi uraia, na inatumika jumuiani tu. Ni visa tu ile.)
Na ndicho wanachofanya wengine. Katika NAFTA, mfano wako, Wakanada na Wamexico wanalazimika kuomba TN (Trade NAFTA) visa status kuingia na kutoka US mpaka kesho. Tena kuipata, inabidi uthibitishe kwamba unaenda kujihushisha na – na una ujuzi na taaluma ya kufanya – moja ya kazi ya kitaalam iliyoorodheshwa katika "TN Visa List of Qualifying Occupations." Huwezi kujiingilia ingilia na kutoka kama unasafirisha magunia ya mazao ya biashara kutoka Singida kwenda Shinyanga.
Ukiondoa vikwazo vya visa, ukaruhusu kuingia na kutoka ovyo ovyo maana yake umehalalisha makazi ya kudumu kwa sababu hakutakuwa na kuulizana. Wamarekani na wengine wenye sheria za makazi ya kudumu wao walihitaji watu. Li-nchi lao kihistoria lilikuwa tupu, lilikuwa kubwa, lilikuwa na maliasili za kumwaga, lilikuwa linatoka udenda wa kutamani nguvukazi na akilikazi za watu wa dunia. Sisi hatuna baraka zote hizo. Hata maji yanatukaukia siku hizi. Ziwa Victoria linakauka, samaki wanapukutika, misitu inapukutika, vijijini wananunua kuni! Kaka Fundi Mchundo nimekwenda kijijini kwetu miaka michache iliyopita nimekuta wanasema kuna wakati wanauziana kuni! Maliasili zinakwisha. Ukihalalisha makazi ya kudumu maana yake itabidi uruhusu wageni wanunue makazi, na nyumba, na ardhi. Hilo tumesema hivi, wao hawana cha kutupa, hatutaki. Mpango wa chetu chao, chao chao hatutaki. Kwanza hawana chao!
Kwa hiyo mpango wa kuondoa vizingiti mipakani ni wa kuuendea taratibu. Hata EU, mfano mwingine ulioutoa, nao ni mwaka jana mwishoni tu ndio wamepitisha azimio la kuondoa vikwazo vya kusafiri iwapo una pasi ya mojawapo ya nchi, Schengen passport. Na bado kuna wengine wameshtuka, wamekataa mpango wa Schengen Passport, wakina Great Britain, Ireland, Romania, Cyprus na wengine. Na sisi huu mpango tuukatae!
Kingine, Comesa hatukujitoa ili tujiunge na wa kusini, sidhani. Hata mwenyewe umesema shirikisho moja ni la kisiasa zaidi ya kiuchumi. Tungeweza kuwatumikia mabwana hawa wote wawili kwa mpigo. Kikubwa kilichotufanya tujitoe Comesa ni tukio la fedheha la sabasaba ya mwaka 2000: Hakukuwa na wafanyabiashara wa kibongo! Tukaona isiwe tabu, hatuko tayari. Heri lawama, tukajitoa. (
Source ) Na mpaka sasa hivi hatuna uhakika kama tuko tayari. Juzi waziri Nagu katangaza haturudi Comesa. Maana yake bado hatujaumia kutosha kujitoa. Tukiumia tutatia akili. Lakini inaonekana bado tuko poa. Comesa nayo isubiri.
Lakini pointi yako ya mwisho Fundi Mchundo, nakubaliana na wewe, na nadhani Dar-es-Salaam na Waziri Kamala wanawazugazuga Wakenya na wengine kujifanya tunataka wakati tunaogopa. Anasema EAC ilivunjika kwa unafiki halafu yeye mwenyewe analeta ajizi, dilatory schemes za kwenda kuongelea akiwa Zanzibar. Hapana, tuwe wazi. Tusileteane ajizi, tusiwayeyushe. Tuwaambie usoni:
Hatutaki mpango wa kuondoa vizingiti vya kuingia na kutoka kama kwenye shamba la bibi maana hiyo ni sawa na kuruhusu makazi ya kudumu. Hatutaki mpango wa kuruhusu makazi ya kudumu maana itabidi uwape haki ya kujipatia makazi, na ardhi, ya kudumu. Hatutaki mpango wa kugawa ardhi kama hisani kwa wale ambao hawana cha kutupa kwa sababu sisi sio baba huruma!