Tanzania yapaa kuelekea Bima ya Afya kwa wote chini ya Magufuli

Tanzania yapaa kuelekea Bima ya Afya kwa wote chini ya Magufuli

Gilga

New Member
Joined
Jan 1, 2016
Posts
3
Reaction score
1
Serikali ya CCM imepiga hatua kubwa sana katika kuelekea lengo la Bima ya Afya kwa wote. Japo suala hili limeibuka kwa kasi katika kipindi cha kampeni mwaka huu natumaini Watanzania wenzangu mtakubaliana nami kwamba Serikali imekwisha piga hatua kubwa sana kuelekea katika bima ya Afya kwa wote.

Hadi sasa zaidi ya watanzania milioni 16 ni wanufaika wa Mifuko ya Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF) ambao unatekelezwa katika halmashauri 117 nchini.

Idadi ya wananchi wanaonufaika na Bima za Afya ni kukubwa ikilinganishwa na nchi nyingi za Afrika mashariki na kusini mwa Afrika-Ukiondoa nchi ya Rwanda ambayo imepiga hatua katika mfuko wa bima ya afya wa Jamii (CHF).

Kufikia Bima ya Afya kwa wote ni mchakato wa muda mrefu ambao hadi sasa Tanzania imeshapiga hatua kubwa sana.Nchi pekee duniani iliyofikia hatua ya Bima ya Afya kwa wote kwa muda mfupi ni Jamhuri ya Korea ya Kusini ambayo ilitumia miaka 12 pale ilipotunga sheria iliyofanya bima ya afya kuwa ya lazima mwaka 1977 na kuachana na mifumo ya hiari iliyodumu kwa miaka mingi bila mafanikio.(Voluntary Schemes).Tanzania ipo hatua ya mwisho kufikia kileleni kwa kutunga sheria ya bima ya Afya kwa wote.

KUTUNGWA KWA SHERIA YA BIMA YA AFYA KWA WOTE
Alipokuwa akisoma makadirio ya bajeti ya wizara ya Afya mwezi tarehe 7/05/2019, waziri mwenye dhamana ya Afya, mheshimiwa Ummy Mwalimu alieleza azma ya serikali kuwasilisha muswada kuhusu uanzishwaji wa Bima ya Afya kwa wote.Muswada huo pia unalenga kuunda taasisi moja ya Bima ya Afya nchini na kuweka utaratibu wa kuwasaidia watu masikini kuhakikisha wanawezeshwa kupata bima ya Afya.Hatua hii ni kubwa, Muhimu na ya kupongezwa.

Mheshimiwa Waziri wa Afya alieleza pia baadhi ya Wabunge walifanya ziara katika nchi ya Rwanda na Ghana ili kupata uzoefu wan chi hizo katika kuelekea hatua ya Bima kwa wote.Nadhani katika kipindi hiki Mheshimiwa Tundu Lissu alikuwa nje ya nchi hivyo ni dhahiri kwamba hakujua kuwa nchi imepiga hatua kubwa katika jambo hili.

UWEZEKANO WA KUTEKELEZEKA
Ingawa wagombea kadhaa wanaahidi kutekeleza sera ya bima ya Afya kwa wote hata hivyo kwa maoni yangu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ina nafasi kubwa ya kutufikisha katika utimilifu wa Bima ya Afya kwa wote kwa haraka zaidi kwa sababu zifuatazo;

i). Uzoefu wa kitaasisi, sera na ukuaji wa hatua kwa hatua (Step wise growth)
  • Serikali ya TANU na baadae CCM ilianza kutoa huduma za Afya bila malipo tangu 1961 hadi 1990.
  • Azimio la Arusha lilitia mkazo wa Huduma bora za jamii ikiwemo Afya bila malipo kwa wananchi wote mwaka 1967
  • Mwaka 1993 utaratibu wa kuchangia huduma kwa kulipa fedha papo kwa papo ulianzishwa na haukuzaa matunda
  • mwaka 1996, Serikali ilianzisha kwa majaribio Mfuko wa Bima ya Afya ya jamii kwa Sekta isiyo rasmi na baada ya mafanikio mwaka 2001 ikatungwa Sheria ya Mfuko wa Afya ya Jamii sura409 kuratibu utaratibu huu
  • Mwaka 1999 ikatungwa sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa ajili ya watumishi wa umma na ikafanyiwa marekebisho mbali mbali ili kuweza kujumuisha makundi mengine ya wanufaika.
  • Vyombo hivi(NHIF & CHF) vimeshajenga msingi wa uzoefu wa uendeshaji, utaalamu wa kutosha na vimechochea uelewa na mwamko wa jamii kuhusu umuhimu wa bima ya afya.
  • Halimashauri na mamlaka za miji 117 zinatekeleza mpango wa afya ya jamii iliyoboreshwa (iCHF) na Tiba kwa Kadi(TIKA.
  • Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeshasajili 99% ya watumishi wa umma,pia imesajiri waheshimiwa wabunge, madiwani, viongozi wa Dini, wanafunzi na umeanza hatua ya kufikia sekta binafsi na sekta isiyo rasmi kama vile wamachinga, wanafunzi, Toto Afya, Wakulima kupitia vyama vya ushirika , Boda Boda Afya , mama Lishe nk
  • Tafiti mbali mbali zimefanywa na serikali kuhusu bima ya afya ikiwemo uwezo na utayari wa uchangiaji(willingness and ability to pay)
  • Uwekezaji katika mifumo ya TEHAMA katika shughuli za uendeshaji wa Bima ya Afya, matibabu, mawasiliano na uimarishaji wa taasisi ya “e-government”.Maandalizi haya ya Teknolojia ni hakikisho la utayari wa kutekeleza mpango wa bima kwa wote kwa urahisi.
  • Uzoefu huu unatoa hakikisho la utayari wa kitaasisi (institutional preparedness) katika kutekeleza sera ya bima ya afya kwa wote.
ii). Kutungwa kwa Mswada wa Bima ya Afya kwa wote
  • Kama ilivyoripotiwa na Waziri mwenye dhamana, Serikali ya Chama cha Mapinduzi ipo katika hatua kubwa ya kukamilisha muswada wa Bima ya Afya kwa wote. Maamuzi haya ni muhimu katika kufanya suala la bima ya Afya kuwa la lazima kwa wote, kuwasaidia wasaio na uwezo kupata bima, kuweka utaratibu wa uendeshaji nk.
  • Ziara ya waheshimiwa wabunge katika nchi ya Rwanda na Ghana kupata uzoefu wa kuelekea Bima ya Afya Kwa wote ni maandalizi mahususi kufikia azma hiyo
  • Kwa vile Chama Cha Mapinduzi kinatarajia kuwa na idadi kubwa ya Wabunge, itakuwa rahisi kutekeleza sera hii kuliko chama kingine chochote.
iii). Utashi wa Kisiasa usio na shaka
  • Ilani ya CCM ya waka 2020 – 2025 ukurasa wa 136 (e) ,na ukurasa wa 180 (L) imesisitiza nia ya serikali “Kuimarisha mfumo wa bima ya afya nchini ikiwemo mifuko ya bima za afya (NHIF na CHF) ili kufikia lengo la Serikali la kuwa na bima ya afya kwa wananchi wote”.
  • Hadi sasa idadi ya usajili wa wananchi katika Bima ya Afya ni miongoni mwa vigezo vinavyotumika kupima utendaji wa watendaji wa Halmashauri na mamlaka za Miji.
  • Utashi huu wa kisiasa unaashiria kwamba umuhimu wa Bima ya Afya umeeleweka vizuri zaidi kwa viongozi wote wa serikali na CCM katika ngazi zote hivyo itakuwa rahisi zaidi kutekelezeka pasipo kuanza kuhamasisha viongozi wapya wa chama kingine cha siasa.
iv). Ongezeko la vituo vya huduma za afya na kupanua wigo wa huduma

Kuwa na bima ya afya pekee haitoshi bila kuwa na vituo vya kutosha kuhudumia wananchi. Serikali ya chama cha mapinduzi imefanya makubwa katika eneo hili kama ufuatavyo;-
  • Kujenga vituo vipya vingi zaidi kuliko vilivyokuwepo tangu tumepata uhuru.Maajabu hayo ni ujenzi wa zahanati zaidi ya elfu moja, vituo vya afya zaidi ya 487,Hospitali za wilaya zaidi ya 80 na hospitali za kanda 3.
  • Kuimarisha upatikanaji wa dawa kwa kuongeza bajeti ya dawa kutoka billioni 31 hadi 270 billioni.
  • Kuimarisha mifumo ya usambazaji dawa kupitia MSD
  • Kuboresha huduma za Kibingwa kwa kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ya matibabu ya moyo, saratani, upandikizaji wa viungo, radiolojia na upasuaji wa upongo.
  • Ongezeko la wahitimu wa kada za afya utaongeza uwepo wa wahudumu wa kutosha kuhudumia wananchi wengi watakaohudhuria katika matibabu.
  • Uboreshaji wa huduma uliofanywa na serikali ya CCM ndani ya miaka mitano umejenga mazingira mazuri ya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora na hasa atakapokuwa mwanachama wa Bima ya Afya.
v). Utayari wa Vituo vya huduma za Afya kujiunga na Bima ya Afya
  • Vituo vingi vya kutolea huduma vimesajiliwa kutoa huduma za Afya kwa wanachama na wanufaika.Hadi sasa vituo zaidi ya 8,970 ikiwemo vya watu binafsi vinatoa huduma kwa wanachama wa bima ya afya nchi nzima
  • Utayari huu unatokana na sera nzuri za Serikali ya CCM juu ya ushirikiano na sekta binafsi (PPP). Hali hii inatoa hakikisho la mazingira mazuri ya kufanikiwa kwa mpango wa bima ya afya kwa wote
vi). Kuridhia na kutekeleza maazimio ya kikanda na kimataifa kuhusu afya bora na bima ya afya kwa wote.
  • Serikali inaunga mkono tamko la haki za binadamu la mwaka 1948 na katiba ya shirika la afya duniani kuhusu dhana ya huduma za afya kwa wanchi wote.ndio maana mara tu baada ya uhuru Taifa lilitangaza maradhi kama miongoni mwa maadui wakuu watatu.
  • Kuridhia maazimio ya viwango vya Kimataifa katika Mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na. 102 wa mwaka 1952 pamoja na pendekezo Na. 202 la haki za binadamu la mwaka 2012 kuhusu umuhimu wa bima ya afya.
  • Kuridhia azimio la Alma Ata la mwaka 1978 juu ya haja ya kila mwananchi kupata huduma za afya za msingi
  • Kutambua wajibu wa serikali kuboresha afya ya msingi kwa kila mwananchi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
  • Kuridhia lengo namba 3 la malengo endelevu kwa kujiwekea lengo la kuhakikisha upatikanaji wa afya bora kwa wananchi wote ifikapo mwaka 2030.
  • Kuridhia Malengo ya Azimio la Kigali la mwaka 2012 kuhakikisha Afya kwa Wote kupitia Bima ya Afya kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
  • Kuridhia maazimio ya kimataifa na kuyatekeleza kwa vitendo ni kielelezo cha dhamira ya dhati kuhusu haja ya bima ya afya kwa wananchi wote.
HITIMISHO
Naipongeza serikali ya wamu ya tano kwa kuboresha mfumo mzima wa sekta ya afya hususani mazingira ya utoaji wa huduma za afya,kuongeza ajira, kuimarisha mifumo ya TEHAMA, Kuimarisha usimamizi na kupanua wigo wa kugharamia huduma za afya kupitia bajeti na bima ya afya.Hatua zote hizi ni muhimu katika kuelekea azma ya afya bora kwa wote kupitia Bima ya Afya.

Ni dhahiri kuwa Rais John Pombe Magufuli amevunja rekodi katika maboresho ya Sekta ya Afya.Kwa kutambua mchango wake chama cha Madaktari Tanzania kilimpa tuzo maalum kama kielelezo cha shukrani kwake .

Na kwa vile tayari maandlizi ya Mswada wa Bima ya Afya kwa wote umekwisha andaliwa, basi,pasipo shaka tutakapomchagua tena kwa awamu ya pili atakamilisha kazi aliyoianza na kukabiliana na changamoto zilizosalia kwa manufaa yetu sote kama Taifa.

Mwandishi:
Dr.Edwin Chitage Manyama (0717233551)Daktari, Mchumi na Mbobezi wa Sera ya hifadhi ya Jamii na Maendeleo-(MD, BA.Economics, Msc.SPP & Development)
 
Hawa watu ahadi zao wala haziaminiki, si ndiyo hawa hawa walitoa ahadi ya kutoa TZS 50Mn kwa kila kijiji nchi nzima! Laptop kwa kila mwalimu nayo je!

Hii elimu ya bure tu inawatoa jasho, na inaendeshwa bora liende tu, ndiyo ije kuwa bima ya afya kwa watu wote. Sera ya kutoa elimu ya msingi bure walidandia treni kwa mbele, na kuiga toka upinzani, matokeo yake tunayaona kwa "poor quality" ya elimu inayotolewa huku wakificha madhaifu yao ktk 'quantity" ya wafaidika.

Mpango wa bima ya afya unahitaji akili pana ya kimkakati. Inahitaji watu makini na wenye mawazo ya kisasa, na wala si hili kundi la watu wabobezi ktk kukimbiza mbio za mwenge.
 
Waliiba sera ya elimu bure kutoka Chadema wakasahau kutoa ajira kwa walimu mpaka waanzilishi wa sera walipotamka sasa wamefungua dirisha la ajira.
Serikali inayoongoza nchi kwa kutegemea kudesa ideas ambazo hawajui plan yake nzima ikoje lazima ifeli tu.

Ukipitia mabandiko kadhaa humu utaona mataga wanavyo ipinga sera ya Cdm ya bima ya afya kwa wote kwa maelezo kuwa haiwezekani na haitatekelezeka, wameona wananchi wanaielewa wameenda kutengeneza vitini kuendana na mdundo.
 
Wapinzani wakisema ndio CCM wanakumbuka kusoma ilani yao
Juzi hapa walikuwa wanaipinga ile ya Chadema, leo wamefukua kwenye ilani yao kuwa inawezekana.

Hawa jamaa ukiwafatilia utajua kuwa hata ilani yao hawaijui kimeandikwa nini na hata mgombea wao hajui na ndio maana ananadi mambo toka kichwani mwake.
 
Bima ya afya gani hiyo mnakata ela nying uduma kiduchu ipo kwa ajili ya panadol na mseto tu

Hizi bima sijui zina maana gani!? Juzi nimempeleka mwanangu hospital kuna dawa wakadai bima haitoi, hapo nikashindwa kabisa kuelewa mantiki ya bima kama baadhi ya dawa inabagua, kwahiyo mtu kama hana hela ya dawa afe na wakati bima kalipia?
 
Hizi bima sijui zina maana gani!? Juzi nimempeleka mwanangu hospital kuna dawa wakadai bima haitoi, hapo nikashindwa kabisa kuelewa mantiki ya bima kama baadhi ya dawa inabagua, kwahiyo mtu kama hana hela ya dawa afe na wakati bima kalipia?

Hiyo bima iliyopo sasa ni wizi tu. Hiyo itakayoletwa na hao watawala utakuwa ufisadi maradufu.
 
Hawa watu ahadi zao wala haziaminiki, si ndiyo hawa hawa walitoa ahadi ya kutoa TZS 50Mn kwa kila kijiji nchi nzima! Laptop kwa kila mwalimu nayo je!

Hii elimu ya bure tu inawatoa jasho, na inaendeshwa bora liende tu, ndiyo ije kuwa bima ya afya kwa watu wote. Sera ya kutoa elimu ya msingi bure walidandia treni kwa mbele, na kuiga toka upinzani, matokeo yake tunayaona kwa "poor quality" ya elimu inayotolewa huku wakificha madhaifu yao ktk 'quantity" ya wafaidika.

Mpango wa bima ya afya unahitaji akili pana ya kimkakati. Inahitaji watu makini na wenye mawazo ya kisasa, na wala si hili kundi la watu wabobezi ktk kukimbiza mbio za mwenge.
Mkuu hakuna elimu bure inyotolewa Tanzania.
 
Hata milioni hamsini kila kijiji na computa kwa kila mwalimu mili ahidi. Viko wapi
 
Iliyoko yenyewe ni wizi mtupu! Mara dawa hii nunua mwenyewe! Maana ya bima ni nini? Hakuna lolote!
 
Back
Top Bottom