Imeandikwa na Nashon Kennedy; Tarehe: 21st July 2009 @ 22:00 Imesomwa na watu: 571; Jumla ya maoni: 0
Habari zinazosomwa zaidi:
HIVI karibuni kumekuwapo na minong'ono kutoka kwa wananchi wa maeneo mbalimbali nchini, juu ya kiwango cha dhahabu ambacho kimekuwa kinazalishwa na migodi nchini.
Minong'ono hiyo ilianza mara baada ya kusambaa kwa taarifa, kuwa wananchi wanaoishi kuuzunguka Mgodi wa North Mara Kata ya Kemambo katika vijiji vya Kewanja, Nyamongo na Nyabigena wilayani Tarime, kuwa wameathiriwa na kemikali zinazotokana na shughuli za uchimbaji unaofanywa na mgodi huo.
Wengi wanasema kuwa baadhi ya wamiliki wa migodi mbalimbali iliyopo nchini, wamekuwa wakisafirisha mazao hayo kinyume na utaratibu na kwamba huyatorosha kwenda nje ya nchi bila ya serikali kuwa na taarifa.
Ni kwa mantiki hiyo, Wizara ya Nishati na Madini kupitia kwenye kitengo chake cha Ukaguzi wa Dhahabu iliamua kutoa mafunzo ya siku mbili yaliyowakutanisha madiwani, wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri, wadau wa sekta za madini kutoka katika wilaya za Musoma Vijijini na Tarime ili kuutoa umma wasiwasi juu ya hisia hizo, ambapo mwandishi wa makala haya naye alipata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo.
Akiwasilisha mada maalumu juu ya kuanzishwa kwa kitengo hicho, Paul Masanja ambaye ni Kamishna Msaidizi anayeshughulika na Kitengo hicho, anasema kuwa kitengo hicho kilianzishwa rasmi mara baada ya serikali kuanzisha sera iliyotoa nafasi ya kutoa marekebisho ya baadhi ya sheria za uchimbaji wa madini ili ziweze kwenda na wakati.
Anasema kuanzia mwaka 2002-2003, kulikuwapo na kelele nyingi kutoka kwa wananchi, ambao waliamini na wanaendelea kuamini madini yanayozalishwa kwenye migodi nchini, hutoroshwa na wawekezaji kwenda nje ya nchi.
"Wananchi walianza kusema kuwa hawaoni serikali ikifanya kazi inayojitosheleza juu ya ulindaji wa rasilimali hiyo muhimu kwa taifa na kwa kweli walikuwa na kila sababu ya kuhoji," anaeleza Masanja.
Masanja anaeleza kuwa kutokana na madai hayo ya wananchi, mwaka 2003 iliamua kuingia mkataba na Kampuni ya kigeni ya Alex Stewart iliyopewa jukumu na serikali ya kuhakiki , kukagua hesabu za fedha , ukaguzi wa dhahabu na gharama zinazotumiwa na migodi ya humu nchini na kutoa ushauri serikalini, uliolenga uboreshaji wa uchimbaji wa madini kutoka kwenye migodi hiyo na utunzaji wa mazingira.
Anasema kampuni hiyo ilifanya kazi hadi mwaka 2007 ilipomaliza muda wake na ndipo serikali mara baada ya kupata uzoefu kutoka kwenye kampuni hiyo, iliamua kuanzisha kitengo chake maalumu cha ukaguzi wa dhahabu nchini, yaani Gold Audit Programme(GAP) Agosti 15 mwaka 2007.
Lakini, kutokana na kuwapo kwa mabadiliko ya Sera za Uwekezaji nchini yaliyofanyika miaka ya 1990, Sera ya Madini ya mwaka 1997 na Sheria ya Madini ya mwaka 1988, Serikali iliweka vivutio vya uwekezaji kwenye sekta ya madini ambavyo vilisababisha kukua kwa sekta hiyo hapa nchini.
Anaeleza kuwa jumla ya migodi sita, imeanzishwa chini ya kitengo hicho ambayo hukaguliwa na kitengo hicho.
Anaitaja migodi hiyo kuwa ni pamoja na Bulyanhulu Gold Mine, Tulawaka Gold Mine na North Mara Gold Mine. Migodi hiyo inamilikiwa na Kampuni ya Barrick. Mingine ni Geita Gold Mine, unaomilikiwa na AngloGold Ashanti na Golden Pride Mine , unaomilikiwa na Kampuni ya Resolute Tanzania Limited.
Anasema Kitengo hicho kiko chini ya Kamishna wa Madini nchini na kuongeza kuwa ukaguzi unaofanywa na kitengo hicho ni wa kisheria na hufanywa chini ya kifungu cha 100 cha Sheria ya Madini Na. 5 ya mwaka 1998.
"Kifungu hiki humpa mamlaka Kamishna wa Madini au Ofisa aliyeidhinishwa kukagua shughuli za utafutaji, uzalishaji na biashara ya madini inayofanyika ndani ya eneo la leseni hai ya madini, au pengine popote ikiwa ni pamoja na kuchukua sampuli za madini, kuhakiki nyaraka za fedha pamoja na kupata taarifa muhimu za madini zinazotaka kutekelezwa kwa mujibu wa sheria hiyo," anaeleza Masanja.
Masanja anawaeleza wajumbe waliohudhuria kwenye mafunzo hayo, kuwa Dira ya GAP ni kuwa kitovu cha ukaguzi na uhakiki wa shughuli za uzalishaji na biashara ya madini kwenye migodi mikubwa ya dhahabu ya hapa nchini.
"Dhamira ya Kitengo hiki ni kuhakikisha serikali inanufaika na shughuli za migodi mikubwa kupitia ukaguzi wa shughuli za uzalishaji wa biashara ya madini ya dhahabu na kuhakiki gharama za uwekezaji na uendeshaji wa migodi," anaeleza Masanja.
Masanja anaeleza kuwa Muundo wa Kitengo hicho ni wa kisasa, unaotekeleza majukumu yake kisayansi. Kina Mkuu wa Kitengo (kama kiongozi), Idara ya Uhakiki wa Fedha, Idara ya Huduma za Operesheni za migodi na Idara ya Uhakiki wa Uwekezaji na Kodi, Kitengo cha Utoaji wa Huduma za Maabara na Idara ya Takwimu na Uchambuzi.
"Idara hizi zote zilizo chini ya kitengo hiki zinafanya kazi vizuri kwa ushirikiano mzuri na zina jumla ya wataalamu wa Kitanzania 42 katika nyanja za utawala, uhandisi wa migodi, uhasibu, fedha, kemia na uchambuzi wa takwimu," anaeleza Masanja.
Anawatoa Watanzania hofu kuwa dhahabu, ambayo huzalishwa kwenye migodi hiyo ya kuwa haitoroshwi kwenda nje ya nchi, kama ambavyo baadhi ya wananchi kuwa na hisia hizo.
Anasema katika kila mgodi huwa yupo Mkaguzi wa Kitengo wakati wote wa shughuli za uzalishaji na usafirishaji wa madini zinapofanyika. Anasema Mkaguzi huyo huwapo kwenye mgodi mmoja katika kipindi cha wiki sita kwa mfululizo na hutuma taarifa ya ukaguzi makao makuu ya kitengo (wizarani) kila siku.
"Wale wanaodhani dhahabu yetu inatoroshwa kwenda nje ya nchi, sio kweli bali husafirishwa kihalali baada ya taratibu zote za kiserikali kukamilishwa, ikiwa ni pamoja na kuikagua na kulipa kodi serikalini, naomba wananchi wetu walifahamu hilo," anaeleza Masanja.
Masanja anasema kuwa "Sampuli za madini huchukuliwa kutoka migodini na kusafirishwa hadi kwenye Maabara ya Kitengo iliyoko Masaki, Dar es Salaam, kwa uchunguzi ili kujua aina, kiasi na thamani ya madini yaliyomo. Na baada ya uchunguzi huo Sampuli hizo hurudishwa tena mgodini. "
Anasema serikali kwa kushirikiana na migodi hiyo, imeweka utaratibu unaohakikisha kuwa hakuna uzalishaji na usafirishaji wa madini unaofanyika, bila kuwapo Mkaguzi wa Serikali.
Aidha, alibainisha kuwa usafirishaji wa madini ya dhahabu, hufanywa na migodi hiyo mara baada ya kupata vibali vinavyohusika kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA).
Si hayo tu, Kitengo pia hujihusisha na shughuli za ukaguzi wa mazingira, ambapo huipitia kwa kina mipango ya utunzaji na ukarabati wa mazingira ya migodi. Hupitia pia bajeti na matumizi halisi ya utunzaji na ukarabati wa utunzaji wa mazingira kwenye migodi mikubwa.
Kuhusu uhakiki wa mahesabu ya fedha unavyofanywa na GAP, Masanja anaeleza kuwa Kitengo hicho huomba taarifa za mahesabu ya fedha ya mgodi unaokusudiwa kukaguliwa na taarifa hiyo huchambuliwa ambao hutoa nafasi ya kuandaa mpango wa ukaguzi.
"Taarifa zinazoonekana kuwa sio za kuridhisha, kitengo huielekeza Menejimenti ya mgodi husika kutoa ufafanuzi wa hoja hizo kabla hazijawasilishwa serikalini na serikali kuchukua hatua husika," anaeleza Masanja.
Kuhusu mafanikio yaliyopatikana mara baada ya kuundwa GAP, Masanja anaeleza kuwa kutokana na kuundwa kwa GAP, serikali inapata takwimu na taarifa sahihi za madini ya dhahabu, fedha na shaba yanayozalishwa nchini na kuuzwa na migodi mikubwa ya dhahabu iliyopo nchini.
Serikali pia inapata mrahaba stahili kutoka katika migodi mikubwa ya dhahabu ; na kujua mapato halisi ya migodi hiyo, kwa lengo la kukokotoa kodi ya mapato inayostahili kulipwa serikalini.
"Uhakiki wa gharama za uwekezaji na uendeshaji wa migodi mikubwa, unaisaidia serikali kutambua gharama zisizostahili za migodi hiyo na hivyo kuondolewa kwenye vitabu vyao vya mahesabu na pia uhakiki wa bajeti kwenye migodi, unahakikisha migodi hiyo inatenga fedha za kutosha na hivyo jukumu la utunzaji wa mazingira linabakia kuwa ni la wamiliki wenyewe na sio serikali," anaeleza Masanja. Anafafanua kuwa shughuli za sasa za ukaguzi wa madini, zinafanyika kwa gharama nafuu, tofauti na zilivyokuwa chini ya Kampuni ya kigeni ya Alex Stewart.
Anataja changamoto kubwa inayokikabili kitengo hicho kuwa ni upungufu wa watumishi na vitendea kazi na baadhi ya watumishi wa migodi, wamekuwa hawatoi ushirikiano wa kutosha wanapohitajika kufanya hivyo kwa wakaguzi wa kitengo.
Kamishna wa Madini nchini, Dk. Dalali Kafumu, anaeleza kuwa serikali imejizatiti kuhakikisha kuwa kitengo hicho kinatekeleza majukumu yake kisayansi na kwa ufanisi zaidi, ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa watumishi wengine wapya na kuboresha mazingira ya wafanyakazi wa kitengo kwa kuwapa marupurupu ya kutosha na vitendea kazi.
Wadau wa sekta ya madini wana maoni gani ?
Wakichangia kwenye mada mbalimbali zilizowasilishwa na wataalamu, walisema ingawa kitengo kilianzishwa siku nyingi, taarifa zake zimechelewa kuwafikia wananchi.
Waliiomba serikali kuhakikisha kuwa elimu zaidi inatolewa kwa umma, juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na kitengo hicho ili wananchi waondokane na fikra mbalimbali, kama vile kwamba madini huwa yanatoroshwa kwenda nje ya nchi bila ya kufuata taratibu.
"Nimefurahi kupata mafunzo haya, naiomba serikali iweke mkazo wa kutoa elimu hii, hasa kwa wachimbaji wadogo ili watambue kuwa shughuli zinazofanywa na kitengo hiki muhimu," anahitimisha John Nyangi, ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Matongo, ambaye naye alihudhuria kwenye mafunzo hayo.
Hiki ndicho Kitengo cha Ukaguzi wa madini cha taifa , ambacho ni muhimu kwa ajili ya ukuzaji wa uchumi wa nchi kupitia sekta ya madini. Ni matumaini yangu kuwa wafanyakazi wa kitengo hiki muhimu, watafanya kazi kwa uwazi, ukweli na uwajibikaji na kutanguliza uzalendo wa nchi