seedfarm
JF-Expert Member
- Feb 9, 2020
- 260
- 2,655
Jaji Augustino Ramadhani amefariki dunia leo majira ya saa mbili asubuhi katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu
====
Majukumu mbalimbali ya uongozi aliyoshika
Ni mtu aliyetumikia nafasi nyingi kwa nyakati tofauti na kwa mafanikio mazuri.
Jaji Augustino Ramadhani aliyestafu Ujaji Mkuu alipaswa pia kuitwa Brigedia Jenerali kwa kuwa pia alilitumikia Jeshi hadi kufikia ngazi hiyo ya Brigedia Jenerali kabla ya kuitwa katika sekta ya sheria na kutumikia Mahakama hadi kufikia ngazi ya juu kabisa ambayo pia wengi hupenda kuandikwa kwa vyeo walivyowahi kutumikia na baada ya hapo akapewa kazi ya ukasisi.
Mbali na kustaafu ujaji, alipewa kazi ya ukasisi, alitawazwa rasmi kuwa Mchungaji wa Dayosisi ya Kanisa la Anglikana lililopo Mkunazini Zanzibar na hivyo kustahili kuitwa cheo cha Mchungaji Augustino Ramadhani.
Historia na familia yake
Mchungaji Augustino alizaliwa Visiwani Zanzibar, Mtaa wa Kisima Majongoo kwenye familia ya watoto wanne wa Mwalimu Mathew Douglas Ramadhani na Bridget Anna Constance Masoud akiwa ni mtoto wa pili katika familia hiyo, aliishi kwa miaka mitatu Visiwani huko na kisha alikuja Tanzania Bara (Tanganyika) akiwa na umri wa kuanza masomo hadi alipohitimu masomo ya sekondari katika Shule ya Wavulana Tabora na wakati akiwa sekondari ndipo alilpojifunza kupiga kinanda akirithi kipaji cha babu yake Augustino Ramadhani.
Jaji Ramadhani alihitimu elimu ya sekondari mwaka 1965 na kujiunga na elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika fani ya sheria hadi mwaka 1970 alipojiunga katika Jeshi la kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, baadaye aliajiriwa katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) alikofanya kazi za sheria.
Mafanikio zaidi
Aliitwa na aliyekuwa Rais wa pili wa visiwa hivyo, Alhaji Aboud Jumbe mwaka 1978 na kumteua kuwa Naibu Jaji Mkuu kabla ya kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na mwaka huo huo aliitwa tena jeshini kwa ajili ya kushiriki vita ya Kagera, alipelekwa Uganda na kukaa kwa zaidi ya miezi kumi.
Baada ya vita kumalizika alirudi Tanzania kuendelea na kazi katika sekta ya Sheria na mwaka 1980 aliapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar.
Mfumo wa Mahakama Visiwani haukuwa wa kisheria na alifanikiwa kuubadilisha na kuweka mfumo wenye ngazi za Kimahakama kutoka Wilaya, Mkoa hadi Mahakama Kuu.
Hii ilitokana na kutokuwepo na watu waliosomea sheria ili kuajiriwa katika sekta ya sheria.
Alifanikiwa kuondoa mfumo wa mabaraza (Peoples Court) na kuweka mfumo wa mahakama uliofuata ngazi za kimahakama na mahakama ya Rufaa haikuwepo kabisa.
Pia aliapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa mwaka 1989, mwaka 1990 alihamia jijini Dar es Salaam na Mwaka 1993 hadi 2003 aliteuliwa pia kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania Bara na mnamo mwaka 2002-2007 aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar na katika kipindi hicho hicho alikuwa mmoja wa Majaji sita wa Mahakama ya Afrika Mashariki, pia alikuwa ni mmojawapo wa Majaji 11 waliochaguliwa na Marais wa Afrika kwa ajili ya kuitumikia Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na ndipo mwaka 2006 alipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.
Baada ya kustaafu kazi ya Ujaji Mkuu mwaka 2010, Jaji Augustino Ramadhani alikataa kuendelea na kipindi kingine baada ya kufanikiwa kufafanua kifungu kinachokataza Jaji kuendelea na kazi ya Ujaji baada ya umri wake wa kustaafu na kuendelea kwa mkataba wa ajira, ila anaruhusiwa kuongeza kipindi kimoja tu hata kama bado anazo nguvu za kutumikia Taifa.
Mara baada ya kusimikwa kuwa Mchungaji alisema hakuna tofauti kati ya kazi ya Mahakama na kazi ya Uchungaji kwani zote ni kazi za kufanya maamuzi ya watu wanaodai wapatiwe haki na kubainisha kazi za mahakama ukiamua umeamua ila za kanisa zinataka makubaliano na maridhiano japo zote ni kazi za Mungu.
Kazi hii ya uchungaji hakufikiria hata siku moja kwamba ataifanya ingawa alisomea nchini Uingereza na kutunukiwa stashahada. Pia alikuwa akishiriki katika shughuli za madhabahuni hasa wakati wa kuwasimika maaskofu kwa kuwa alikuwa mwanasheria wa kanisa hadi alipoteuliwa kuwa Jaji Mkuu ndipo alipoamua kuacha wadhifa huo ili kuepuka migongano.
Kwa upande mwingine Jaji alisema, lengo lake lilikuwa baada ya kustaafu akafundishe na lengo hilo lilitimia kwani aliwahi kuwa Mkuu wa Chuo cha Tumaini - Iringa (sasa Chuo Kikuu cha Iringa) ambapo alikuwa akifundisha sheria.
Pia aliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.
SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUTOKA KWA RAIS MAGUFULI