Ukaribu uliopo baina ya kifo na mwanadamu ni zaidi ya umbali wa unyayo wa mguu wake na sori ya kiatu alichovaa,
Tuvichukulie vifo vya wapendwa wetu kama somo kwetu na ukumbusho kuwa hii dunia sio makazi yetu bali ni wapita njia.....mfano wa maisha ya mwanadamu hapa duniani ni sawa na msafiri aliyepo safarini aliyepumzika chini ya mti wenye kivuli huku akivuta muda ili aendelee na safari yake.
Maisha yetu ni mafupi sana kuliko tunavyofikiria na kibaya zaidi kumewekwa siri nzito baina ya kifo na uhai....kwani hakuna yoyote kati yetu hakuna ajuaye siku wala saa ya safari yake ya milele.
Ni upumbavu na ujinga kuihangaikia dunia wakati si mahala pako pa kudumu....hazina unazochuma hapa duniani hazita kusaidia lolote mbele ya muumba wako bali ile mia mbili uliyo mrushia omba omba, yule mwenye njaa uliyempa chakula akashiba na yule mwenye kiu uliyempa maji na akakata kiu yake.
Hutakuta rekodi za watu uliowapa ofa za bia , hutakuta rekodi za vimada uliowahonga magari ,hutakuta rekodi za nyumba nzuri uliokuwa ukiishi bali utakutana na vilio vya watu uliowadhulumu haki zao, utakutana na vilio vya watu uliowaweka misukule ili upate mali....utakutana vilio vya mayatima uliowadhulumu haki zao.
Utakutana na vilio vya watu uliwachukulia wake zao au waume zao isipokuwa nuru ya sadaka zako ulizokuwa ukitoa kwenye nyumba za ibada, Baraka za uliyemchangia pesa ili akapate matibabu na kuokoa maisha yake .
Ninachotaka si kuwaogopesha bali ni kuwakumbusha kufanya mema kwani hakuna ajuae siku wala saa atakayo nyakuliwa.