Ili soko la filamu lifikie kiwango kizuri, kuna vigezo muhimu viwili ambavyo vinaweza
kutuongoza katika dhana nzima ya mafanikio katika usambazaji filamu:
(1) Maudhui/Mahitaji ya Watazamaji (Content/Audience Connection) na
(2) Jukwaa la Uwasilishaji (Media Delivery Platforms)
Content/Audience Connection:
Kwa miaka kadhaa, sekta ya filamu Tanzania imeshuhudia utofauti mkubwa kati
ya maudhui katika hadithi zetu na kile watazamaji wanachokihitaji, na matokeo yake
yameendelea kuyumbisha mikakati ya soko na sera za usambazaji. Maudhui lazima
yahusishwe moja kwa moja na mahitaji ya watazamaji ili kuwe na nafasi ya mafanikio
kwenye soko.
Maudhui yanayofaa katika kizazi cha leo ni yale yanayokwenda sambamba na watazamaji
ndani ya akili zao na kuihusisha jamii moja kwa moja. Mafanikio yanayotokana na maudhui
yanategemea sana mmenyuko wa watazamaji, na kujenga maudhui yaliyo kwenye mstari
na mwelekeo wa watazamaji na matarajio yao imekuwa vigumu, na sasa inahitajika kwa
watayarishaji/ waandishi wa miongozo ya filamu kujihusisha moja kwa moja na mtazamo
wa watazamaji katika mazingira waliyomo. Kwa matokeo haya, utafiti ni suala la kupewa
umuhimu mkubwa kabla ya kuandaa kazi husika.
Kitu ambacho mtayarishaji/ mwandishi anapaswa kujua kuhusu watazamaji wake ni
muhimu sana kwa mafanikio katika biashara ya usambazaji. Kujenga maudhui bila uelewa
mkubwa na ufafanuzi kwa walengwa, ni kama kufunga safari ya kwenda mahali bila
kufikiria jinsi ya kufika huko. Kama maudhui yako hayakushikamana na aina ya maisha
au matarajio ya watazamaji wako, jua umewapoteza.
Kundi la kwanza la watazamaji wa filamu ni la akina mama wa nyumbani, wafanyakazi
wa ndani, na vijana wasio na ajira. Kundi la pili ni la watazamaji linalotokana na matokeo
ya moja kwa moja ya kituo cha Africa Magic kuonesha filamu kwenye familia za watu
wa tabaka la kati na la juu wenye uelewa mpana kwa maana ya kwenda shule.
Na bila shaka kuna kundi la tatu linalotokana na watazamaji Watanzania walio nje ya nchi
na Waafrika (hasa wanaojua au kukipenda Kiswahili) katika bara la Afrika na maeneo waliko.
Ni muhimu kuelewa kwamba kila moja ya makundi haya ya watazamaji yana muundo na
mawazo ambayo ni tofauti sana na kundi jingine.
Utafiti unaonesha watazamaji wa filamu za Kitanzania wamegawanyika kama ifuatavyo:
Asilimia 67 ya watazamaji wa filamu hizi wanaishi ndani ya Tanzania, asilimia 25 wanatoka
katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, na asilimia 8 wanatoka sehemu zilizobaki za dunia,
hasa ambako Kiswahili kinafundishwa au kupewa umuhimu.
Pia ni asilimia 30 ya wakazi wanaoishi mijini ndiyo huangalia filamu za Kitanzania.
Takwimu hii inatofautishwa kulingana na umri: Asilimia 50 ya watazamaji hawa ni
wenye umri kati ya miaka 10-24, asilimia 30 ni wenye umri kati ya miaka 25-34,
asilimia 15 ni kati ya watu wenye umri wa miaka 35-49 na asilimia 5 tu ya watu
wenye umri zaidi ya miaka 50 ndiyo huangalia filamu hizi. Dar es Salaam ndiyo mji
unaoongoza kuwa na idadi kubwa ya watazamaji wa filamu ikichukua asilimia 31.
Hata hivyo, vijana wadogo ndiyo wenye mazoea ya kwenda kwenye mabanda ya video.
Katika utazamaji filamu hizi, kuna dhana ambayo huendana na mitazamo ya watazamaji
(matamanio, maadili, na mtazamo wa mtu binafsi kulingana na uzoefu wake katika
kuangalia kazi mbalimbali) na vitu hivi huathiri namna watazamaji wanavyohusiana na
dunia inayowazunguka, ikiwa ni pamoja na maudhui.
Media Delivery Platforms:
Maudhui ya jukwaa la uwasilishaji katika dunia ya kisasa ya filamu hayaishii tu
kwenye kazi ya usambazaji, yanakwenda ndani zaidi ya kile hasa soko la filamu lilivyo leo.
Jukwaa litakusaidia kuwasilisha mawazo yako kwa watu katika njia itakayojumuisha
mitazamo yao, na si kupambana nayo.
Ufanisi katika uwasilishaji unachangia utoaji haki ya kuchagua; kuyaleta maudhui kwa
watazamaji katika dunia yao wenyewe. Kulingana na uwezo mkubwa wa soko la Tanzania
kama litawezeshwa (ndani na nje ya bara la Afrika), jukwaa muafaka litamfanikisha kwa
urahisi mtengenezaji wa filamu kuendana na ushindani wa soko.
Mustakabali wa biashara ya usambazaji wa filamu na masoko Tanzania unatokana na
watazamaji vijana. Watoaji filamu wanatakiwa kuandaa kwa uangalifu takwimu (demography)
hii ya watazamaji na kukutana nao katika dunia yao. Dunia hiyo hustawi (flourishes) kwenye
kundi la kweli la teknolojia ya digitali.
Katika hatua hii itakuwa vizuri pia kuuchunguza mfumo wa usambazaji ili kupata ufumbuzi
wa kutangaza na kusambaza (promotion and distribution solutions) ambao umesaidia
kurekebisha tasnia katika nchi nyingine, na kuigwa katika sekta ya filamu Tanzania.
Filamu ni nembo (Film is a brand), kama zilivyo nembo/ bidhaa nyingine, kuzitangaza
na kuzisambaza ni vitu vyenye umuhimu sawa.
Mkakati ambao hatimaye utaweka tabaka la washindi na washindwa ni ubunifu katika kazi
na utafiti. Hii itaongeza mipaka katika utekelezaji wa kampeni ya kuzitangaza kazi.